Seminari na Vyuo
Fundisha Mafundisho


“Fundisha Mafundisho,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi: Kwa Ajili ya Wote Wanaofundisha Nyumbani na Kanisani (2022)

“Fundisha Mafundisho,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi

3:33

Fundisha Mafundisho

Ingawa Yesu alikua katika hekima na maarifa katika maisha Yake yote, Yeye hakuwa msomi kama viongozi wengine wa dini wa siku Zake. Lakini bado Yeye alipofundisha, watu walistaajabia, wakisema, “Amepataje huyu kujua elimu, ambaye hakusoma?” Je, kwa nini mafundisho Yake yalikuwa yenye nguvu kubwa? “Mafunzo yangu si yangu mimi,” Mwokozi alieleza, “ila ni yake yeye aliyenipeleka” (Yohana 7:15–16). Mafundisho ni ukweli wa milele—unaopatikana katika maandiko na maneno ya manabii wa siku za mwisho—ambayo hutuonyesha njia ya kuwa kama Baba yetu wa Mbinguni na kurudi Kwake. Bila kujali jinsi ulivyo mzoefu kama mwalimu, unaweza kufundisha kwa uwezo, kama vile Mwokozi alivyofundisha, kwa kufundisha mafundisho ya Baba. Wewe pamoja na wale unaowafundisha mtastaajabia baraka Mungu anazotuma wakati kufundisha na kujifunza kwenu vinapokuwa vimewekwa katika msingi wa neno Lake.

Kufundisha Mafundisho

  • Jifunze mafundisho ya Yesu Kristo kwa ajili yako wewe mwenyewe.

  • Fundisha kutoka katika maandiko na maneno ya manabii wa siku za mwisho.

  • Wasaidie wanafunzi watafute, watambue na waelewe kweli zilizoko katika maandiko.

  • Fokasi kwenye kweli ambazo zinaongoza kwenye uongofu na kujenga imani katika Yesu Kristo.

  • Wasaidie wanafunzi wapate uhusiano binafsi katika mafundisho ya Yesu Kristo.

Mwokozi Alijifunza Mafundisho

Inaonekana wazi kwamba Mwokozi alijifunza kutoka kwenye maandiko katika ujana Wake wakati akizidi kukua “katika hekima … na akimpendeza Mungu” (Luka 2:52). Uelewa wake wa kina juu ya mafundisho ya Baba ulikuwa dhahiri wakati wazazi Wake walipomkuta hekaluni katika umri mdogo akiwafundisha walimu wa Kiyahudi na kujibu maswali yao (ona Tafsiri ya Joseph Smith, Luka 2:46 [katika Luka 2:46, tanbihi c]). Baadaye Shetani alipojitokeza akiwa na majaribu makali nyikani, elimu ya Yesu juu ya mafundisho katika maandiko ilimsaidia kupinga majaribu hayo (ona Luka 4:3–12).

Wewe pia unaweza kutafuta kujifunza mafundisho ya kweli kwa kina zaidi kabla ya kuyafundisha. Unapojiandaa kufundisha na kujifunza na wengine, tafuta kwa makini kile Bwana alichokisema kuhusu ukweli unaoufundisha. Pekua maandiko na maneno ya manabii walio hai kwa ajili ya ufafanuzi na ushauri. Kuishi na kutumia kweli unazojifunza kutamwalika Roho ili akufundishe mafundisho haya kwa njia za kina zaidi na kuthibitisha ukweli wa mafundisho katika mioyo ya wale unaowafundisha.

Maswali ya Kutafakari: Kwa nini ni muhimu kuzielewa kweli za injili wewe mwenyewe? Ni kwa jinsi gani umepata uelewa wa kina zaidi wa kweli za injili? Unahisi ushawishi wa kufanya nini ili kuboresha kujifunza kwako maandiko na maneno ya manabii walio hai?

Kutoka kwenye Maandiko: Mithali 7:1–3; 2 Nefi 4:15–16; Mafundisho na Maagano 11:21; 88:118

Mwokozi Alitufundisha kutoka kwenye Maandiko

Baada ya kifo cha Mwokozi, wawili kati ya wanafunzi Wake walikuwa wakitembea na kuzungumza wakiwa wamechanganyika na huzuni na mshangao mioyoni mwao. Ingewezaje kuleta maana kwa kile kilichokuwa kimetokea punde? Yesu wa Nazareti, mtu waliyemtumaini kuwa Mkombozi wao, alikuwa amekufa kwa siku tatu sasa. Na kisha kukawa na taarifa kwamba kaburi lake lilikuwa tupu, na malaika wakitangaza kwamba Yeye yu hai! Katika wakati huu muhimu sana katika imani ya wanafunzi hawa, mgeni alijiunga katika safari yao. Aliwafariji kwa “kuwafafanulia katika maandiko yote mambo yaliyomhusu [Mwokozi].” Hatimaye, wasafiri wale wakatambua kwamba mwalimu wao alikuwa Yesu Kristo Mwenyewe na kwamba hakika alikuwa amefufuka. Ni kwa jinsi gani walimtambua Yeye? “Je, mioyo yetu haikuwa inawaka ndani yetu,” walikumbuka baadaye, “wakati alipokuwa anaongea na sisi njiani, na kutufunulia maandiko?” (Luka 24:27, 32).

Mzee D. Todd Christofferson alifundisha, “Dhumuni kuu la maandiko yote ni kuzijaza nafsi zetu kwa imani katika Mungu Baba na Mwanawe Yesu Kristo” (“Baraka ya Maandiko,” Liahona, Mei 2010, 34). Wakati wote wa huduma Yake, Yesu alitumia maandiko kufundisha, kusahihisha, na kuwashawishi wengine. Hakikisha kwamba mafundisho yako hayaendi nje ya maandiko na maneno ya manabii. Kwa uaminifu kabisa unapotegemea maneno ya Mungu katika kufundisha kwako, unaweza kuwatendea wengine kile Mwokozi alichokitenda. Unaweza kuwasaidia wamjue Yeye, kwani sisi sote tunahitaji imani yetu kwa Mwokozi iimarishwe mara kwa mara. Mapenzi yako kwenye maandiko yatathibitika kwa wale unaowafundisha, na ufundishaji wako utamwalika Roho ili kusababisha mioyo yao kuwaka kwa ushuhuda juu ya Baba na Mwana.

Maswali ya Kutafakari: Je, ni kwa jinsi gani wewe umeshawishiwa na mwalimu aliyekuwa akitumia maandiko kukusaidia wewe uje kumjua vyema Mwokozi? Ni nini unapaswa kufanya ili kutegemea zaidi maandiko na maneno ya manabii wakati unapofundisha. Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia wale unaowafundisha walielewe na walipende neno la Mungu?

Kutoka kwenye Maandiko: Luka 4:14–21; Alma 31:5; Helamani 3:29–30;3 Nefi 23

Mwokozi Aliwasaidia Watu Wautafute, Wautambue na Wauelewe Ukweli

Mwanasheria mmoja aliwahi kumuuliza Yesu, “Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?” Katika kujibu, Mwokozi alimwongoza muulizaji kwenye maandiko: “Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje wewe?” Hili lilimwongoza mtu yule siyo tu kwenye jibu lake—“Mpende Bwana Mungu wako … Na jirani yako”—lakini pia kwenye swali la ufuatiliaji: “Na jirani yangu ni nani?” Mwokozi alijibu swali hili kwa mfano kuhusu wanaume watatu ambao walimwona msafiri mwenzao katika uhitaji. Ni mmoja tu katika wale watatu, Msamaria, aliyekuwa akichukiwa na Wayahudi kwa sababu tu ya mahali anakotoka, alisimama akamsaidia. Yesu kisha akamwalika mwanasheria yule kujibu swali lake yeye mwenyewe: “Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?” (ona Luka 10:25–37).

Kwa nini unadhani Mwokozi alifundisha katika njia hii—alijibu maswali kwa mialiko ya kutafuta, kutafakari, na kugundua? Sehemu ya jibu ni kwamba Bwana anathamini jitihada za kutafuta ukweli. “Tafuteni, nanyi mtapata,” Amealika tena na tena (ona, kwa mfano, Mathayo 7:7; Luka 11:9; Mafundisho na Maagano 4:7). Yeye anayazawadia matendo ya imani na subira ya watafutaji.

Kama Mwokozi, unaweza kuwasaidia wale unaowafundisha wautambue na wauelewe ukweli. Maandiko, kwa mfano, yamejaa kweli za injili, lakini wakati mwingine inahitaji jitihada ya dhati kuzipata. Mnapojifunza pamoja kutoka kwenye maandiko, tua kidogo na waulize wale unaowafundisha ni ukweli gani wa injili wameuona. Wasaidie waone jinsi kweli hizi zinavyohusika kwenye mpango wa wokovu wa Baba wa Mbinguni. Wakati mwingine kweli za milele zimeelezwa katika maandiko, na wakati mwingine zimefafanuliwa katika hadithi na maisha ya watu tunaosoma habari zao. Inaweza pia kuwa ya msaada kuchunguza pamoja historia ya mistari unayoisoma, vile vile maana ya mistari hiyo na jinsi inavyotumika kwetu sisi leo.

Maswali ya Kutafakari: Je, unatambuaje kweli za milele katika maandiko au maneno ya manabii? Ni kwa jinsi gani kweli hizo zinayabariki maisha yako? Je, ni zipi baadhi ya njia ambazo kupitia kwazo unaweza kuwasaidia wanafunzi wazitambue na wazielewe kweli ambazo zitakuwa na maana kwao na kuwaleta karibu zaidi na Mungu?

Kutoka kwenye Maandiko: Yohana 5:39; 1 Nefi 15:14; Mafundisho na Maagano 42:12

wanafunzi wakijifunza

Tunaweza kuwasaidia wale tunaowafundisha watafute na watambue ukweli wao wenyewe

Mwokozi Alifundisha Kweli Ambazo Ziliongoza kwenye Uongofu na Kujenga Imani

Siku moja ya Sabato, Mwokozi na wanafunzi Wake, wakiwa wanaona njaa, walipita kwenye shamba na kuanza kula nafaka. Mafarisayo, daima wakiwa na hamu ya kusisitiza pointi muhimu kwenye sheria ya Musa, walionyesha kwamba kukusanya nafaka ilikuwa ni aina ya kazi, ambayo ilikatazwa siku ya Sabato (ona Marko 2:23–24). Kwa kutumia kirai kutoka kwa nabii Yakobo katika Kitabu cha Mormoni, Mafarisayo “waliangalia zaidi ya lengo” (Yakobo 4:14). Kwa maneno mengine, walikuwa wamefokasi zaidi juu ya tafsiri ya mazoea ya amri kiasi kwamba walikosa dhumuni la kiungu la amri hizo—kutusogeza karibu zaidi na Mungu. Kwa hakika, Mafarisayo hata hawakutambua kwamba Mtu aliyetoa amri hiyo ya kuheshimu Sabato alikuwa amesimama mbele yao.

Mwokozi alichukua fursa hii kushuhudia juu ya utambulisho Wake wa kiungu na kufundisha kwa nini Sabato ni muhimu. Ilifanyika kwa ajili yetu sisi kama siku ya kumwabudu Bwana wa Sabato, Yesu Kristo Mwenyewe (ona Marko 2:27–28). Kweli za jinsi hiyo zinatusaidia tuelewe kwamba amri za Mungu ni zaidi ya tabia ya nje tu. Zimekusudiwa zitusaidie tubadili mioyo yetu na kuwa waongofu kamili.

Kwa uangalifu fikiria mafundisho na kanuni unazoamua kufokasi juu yake. Wakati ziko kweli nyingi katika maandiko ambazo zinaweza kujadiliwa, ni vyema kufokasi juu ya kweli za injili ambazo zinatuongoza kwenye uongofu na kujenga imani katika Yesu Kristo. Kweli rahisi, na za msingi Mwokozi alizozifundisha na kuzitolea mfano zina nguvu kubwa ya kubadilisha maisha yetu—kweli kuhusu Upatanisho Wake, mpango wa wokovu, amri za upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani yetu, na kadhalika. Mwalike Roho atoe ushuhuda juu ya kweli hizi, akisaidia zizame kwa kina ndani ya mioyo ya wale unaowafundisha.

Maswali ya Kutafakari: Ni zipi baadhi ya kweli za injili ambazo zimekusaidia uwe mwongofu zaidi kwa Yesu Kristo na kuwa na imani kubwa zaidi Kwake? Je, mwalimu alikusaidiaje ufokasi juu ya kweli muhimu zaidi za injili? Je! Unaweza kufundisha nini ambacho kitawasaidia wengine waongoke zaidi kwa Yesu Kristo?

Kutoka kwenye Maandiko: 2 Nefi 25:26; 3 Nefi 11:34–41; Mafundisho na Maagano 19:31–32; 68:25–28; 133:57; Musa 6:57–62

Mwokozi Aliwasaidia Watu Watafute Uhusiano Binafsi katika Mafundisho Yake

“Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao,” Mafarisayo walinung’unika kuhusu Yesu—wakimaanisha kwamba hiyo haikuwa tabia sahihi kwa mwalimu wa kiroho (Luka 15:2). Yesu aliona kwamba hii ilikuwa fursa ya kufundisha kweli muhimu. Ni kwa jinsi gani Yeye angefanya hivyo? Ni kwa jinsi gani Yeye angewasaidia Mafarisayo waone kwamba ilikuwa ni mioyo yao—na sio Wake—ambayo haikuwa safi na ilihitaji uponyaji? Ni kwa jinsi gani Yeye alitumia mafundisho Yake kuwaonyesha kwamba mawazo yao na tabia zao zilihitaji mabadiliko?

Yeye alilifanya hili kwa kuzungumza nao juu ya kondoo ambaye alipotea kutoka kundini na juu ya sarafu iliyopotea. Alizungumza juu ya mwana muasi aliyetafuta msamaha na juu ya kaka mkubwa ambaye alikataa kumpokea au kula naye. Kila moja ya mifano hii ilikuwa na kweli ambazo zilihusika na jinsi Mafarisayo walivyokuwa wakiwaangalia watu wengine, akiwafundisha kwamba kila nafsi ina thamani kubwa (ona Luka 15). Mwokozi hakuwaambia Mafarisayo—au yeyote kati yetu—nani wa kujitambulisha naye katika mifano Yake. Wakati mwingine tunakuwa yule baba mwenye wasiwasi. Wakati mwingine sisi ni yule kaka mwenye wivu. Mara nyingi sisi ni yule kondoo aliyepotea au mwana mpumbavu. Lakini vyovyote vile hali yetu iwavyo, kupitia mifano Yake, Mwokozi anatualika tutafute uhusiano katika mafundisho Yake—ili kugundua kile Yeye anachotaka sisi tujifunze na kile tunachohitaji kubadilisha katika mawazo yetu na tabia zetu.

Unaweza kugundua kwamba baadhi ya wanafunzi hawaoni kwa nini baadhi ya kweli zina maana kwao. Unapozingatia mahitaji ya wale unaowafundisha, fikiria kuhusu jinsi kweli katika maandiko zinavyoweza kuwa za maana na zenye matumizi katika hali zao. Njia mojawapo ambayo kupitia hiyo unaweza kuwasaidia wanafunzi waone uhusiano wa kweli wanazozigundua ni kwa kuwauliza maswali kama “Ni kwa jinsi gani hili linaweza kukusaidia kwenye kile unachokipitia sasa?” “Kwa nini ni muhimu kwako kujua hili?” “Je! ni tofauti gani hili linaweza kuleta katika maisha yako? Wasikilize wale unaowafundisha. Waruhusu waulize maswali. Wahimize wafanye muunganiko kati ya mafundisho ya Mwokozi na maisha yao wenyewe. Ungeweza pia kushiriki jinsi wewe ulivyopata uhusiano kwenye maisha yako mwenyewe katika yale unayoyafundisha. Kufanya hili kunaweza kumwalika Roho ili awafundishe wanafunzi mmoja mmoja jinsi mafundisho yanavyoweza kuleta tofauti katika maisha yao.

Maswali ya Kutafakari: Ni kitu gani hufanya kweli za injili ziwe zenye maana na muhimu kwetu? Je, ni nini kinakusaidia wewe upate uhusiano binafsi wakati unapojifunza injili? Je, unafanya nini ili kufokasi kwenye kweli ambazo zinahusika kwa wale unaowafundisha?

Kutoka kwenye Maandiko: 1 Nefi 19:23; 2 Nefi 32:3; Mafundisho na Maagano 43:7–9

Baadhi ya Njia za Kutumia Kile Unachojifunza

  • Tathmini kile unachokifundisha ili kuhakikisha kwamba unafundisha mafundisho ya kweli. Maswali yafuatayo yanaweza kusaidia:

    • Je, kile ninachopanga kufundisha kinatokana na maandiko na maneno ya manabii wa siku za mwisho?

    • Je, manabii wengi wamefundisha hili? Je, viongozi wa sasa wa Kanisa wanafundisha nini kuhusu hili?

    • Je, hili litawasaidiaje wengine wajenge imani katika Yesu Kristo, kutubu, na kupiga hatua kwenye njia ya agano?

    • Je, hili linaoana na misukumo ya Roho Mtakatifu, au ninahisi kutotulia kiroho kuhusu hili?

  • Kila siku jifunze neno la Mungu ili kujifunza mafundisho ya kweli wewe mwenyewe.

  • Waombe wanafunzi wasome maandiko na maneno ya manabii wa sasa wakati unapofundisha.

  • Wafundishe wanafunzi jinsi ya kutumia tanbihi, Mwongozo wa Maandiko, na nyenzo nyinginezo pale wanapojifunza maandiko.

  • Waalike wanafunzi watafute kweli katika vifungu vya maandiko au hadithi.

  • Toa ushuhuda juu ya jinsi wewe ulivyojua kuwa mafundisho ni ya kweli.

  • Tumia hadithi au isitiari ili kuwasaidia wanafunzi wapate uelewa wa kina wa kweli za injili.