Muziki
Dibaji ya Uraisi wa Kwanza


Dibaji ya Uraisi wa Kwanza

Miezi mitatu baada ya Kanisa kuundwa, Bwana, kupitia Nabii Joseph Smith, alimuelekeza mke wa Joseph, Emma, kuchagua nyimbo takatifu za dini kwa ajili ya Kanisa: “Kwani nafsi yangu hufurahia katika nyimbo za moyoni; ndiyo, wimbo wa mwenye haki ni sala kwangu Mimi, nayo itajibiwa kwa baraka juu ya vichwa vyao” (M&M 25:12).

Sasa, miaka 150 baada ya kitabu cha nyimbo za dini cha kwanza kuchapishwa na Kanisa, tunafuraha ya kutoa toleo hili la masahihisho. Nyimbo nyingi za dini zilizokuwepo kwenye toleo la kwanza na matoleo mengine yaliyofuata yamejumuishwa, kama ilivyo kwa baadhi ya nyimbo zingine mpya za dini. Zote zimechaguliwa kukidhi mahitaji tofauti tofauti ya waumini wa Kanisa la dunia nzima la leo.

Muziki kwenye Mikutano Yetu ya Kanisa

Muziki unaovutia ni sehemu muhimu ya mikutano yetu ya kanisa. Nyimbo za dini zinakaribisha Roho wa Bwana, hutengeneza hali ya uchaji, hutujumuisha kama waumini, na hutupatia njia ya kutuwezesha kutoa sifa kwa Bwana.

Baadhi ya hotuba mashuhuri zinahubiriwa kwa uimbaji wa nyimbo za dini. Nyimbo za dini hutugusa hisia kufanya toba na matendo mema, hujenga shuhuda na imani, hufariji wachovu, huwaliwaza wenye huzuni, na hututia moyo kuvumilia mpaka mwisho.

Tunatumaini kuona kuongezeka kwa uimbaji wa nyimbo za dini kwenye ushirika wetu. Tunawahamasisha waumini wote, iwe unamwelekeo wa kimuziki ama hauna, kujiunga nasi katika uimbaji wa nyimbo za dini. Tunatumaini kuwa viongozi, walimu, na waumini ambao wataitwa kutoa neno watageukia mara kwa mara kitabu cha nyimbo za dini kupata hotuba zenye nguvu na za kuvutia katika ushairi.

Watakatifu wa Siku za Mwisho wanatamaduni ya muda mrefu ya uimbaji katika kwaya. Kila kata na tawi katika Kanisa wanapaswa wawe na kwaya inayoimba mara kwa mara. Tunawahamasisha kwaya kutumia kitabu cha nyimbo za dini kama nyezo yao ya msingi.

Muziki Nyumbani Mwetu

Muziki una nguvu zisizo na mipaka kwa ajili ya kugusa hisia ya familia kuelekea kwenye mambo ya kiroho zaidi na kupenda injili. Watakatifu wa Siku za Mwisho wanapaswa kujaza nyumba zao na sauti ya nyimbo stahili.

Chetu ni kitabu cha nyimbo za dini kwa ajili ya nyumbani pamoja na nyumba ya mkutano. Tunatumaini kuwa kitabu cha nyimbo za dini kitachukua nafasi kubwa baina ya maandiko matakatifu na vitabu vingine vya dini nyumbani mwetu. Nyimbo za dini zinaweza kuwaletea familia roho mzuri na amani na huweza kuchochea upendo na umoja miongoni mwa wanafamilia.

Wafundishe watoto wenu kupenda nyimbo za dini. Ziimbeni siku ya Sabato, jioni ya familia, wakati wa masomo ya maandiko matakatifu, wakati wa sala. Ziimbe wakati mnafanya kazi, mnapocheza, na mnaposafiri pamoja. Imba nyimbo za dini kama nyimbo ya kubembelezea watoto kujenga imani na ushuhuda kwao.

Muziki katika Maisha Yetu Binafsi

Pamoja na kutubariki kama waumini wa Kanisa na wanafamilia, nyimbo za dini zinaweza kutufaa sisi binafsi. Nyimbo za dini zinainua nafsi zetu, zinatupa ujasiri, na kutugusa kufanya matendo ya haki. Zinaweza kujaza nafsi zetu na mawazo ya kiungu na kutuletea roho ya amani.

Nyimbo za dini pia zinaweza kutusaidia kuhimili matamanio ya mwovu. Tunawahamasisha kukariri nyimbo mnazozipenda za dini na kujifunza maandiko matakatifu yanayohusiana nazo. Kisha, kama mawazo yasiostahili yakiingia akilini, jiimbie wimbo wa dini, kuzuia yale maovu kwa yaliomema.

Wakina kaka na dada, acha tutumie nyimbo za dini kumkaribisha Roho wa Bwana katika ushirika wetu, majumbani mwetu, na maisha yetu binafsi. Acha tuzikariri na kuzitafakari, tuzighani na tuziimbe, na tushiriki chakula chake cha kiroho. Jua kwamba wimbo wa mwenye haki ni sala kwake Baba yetu wa Mbinguni, “nayo itajibiwa kwa baraka juu ya vichwa [vyenu].”

Uraisi wa Kwanza