Mlango wa 59
Moroni anamwuliza Pahorani ahifadhi majeshi ya Helamani—Walamani wanakamata mji wa Nefiha—Moroni anakasirikia serikali. Karibia mwaka 62 K.K.
1 Sasa ikawa katika mwaka wa thelathini wa utawala wa waamuzi juu ya watu wa Nefi, baada ya Moroni kupokea na kusoma barua ya Helamani, alifurahi sana kwa sababu ya ustawi, ndiyo, kufaulu kwingi ambako Helamani alikamata nchi ambazo zilikuwa zimepotea.
2 Ndiyo, na aliwajulisha watu wake wote, katika nchi yote karibu na ile sehemu ambayo alikuwa, kwamba wafurahi pia.
3 Na ikawa kwamba mara moja alituma barua kwa Pahorani, akitaka kwamba asababishe watu wajikusanye pamoja kumtia Helamani nguvu, au majeshi ya Helamani, ili aweze kulinda kwa urahisi sehemu hio ya nchi ambayo alikuwa ameipata tena kwa miujiza.
4 Na ikawa wakati Moroni alikuwa ametuma hii barua kwa nchi ya Zarahemla, alianza tena kufikiria kuweka mpango kwamba angeweza kupata tena mabaki ya umiliki na miji ambayo Walamani walikuwa wamechukua kutoka kwao.
5 Na ikawa kwamba wakati Moroni alikuwa anafanya mipango kwenda dhidi ya Walamani kupigana, tazama, watu wa Nefiha, ambao walikusanyika pamoja kutoka mji wa Moroni na mji wa Lehi na mji wa Moriantoni, walishambuliwa na Walamani.
6 Ndiyo, hata wale ambao walikuwa wamelazimishwa kukimbia kutoka nchi ya Manti, na kutoka nchi karibu, walikuwa wamekuja na kujiunga na Walamani katika sehemu hii ya nchi.
7 Na hivyo wakiwa wengi sana, ndiyo, na wakipokea nguvu siku hadi siku, kwa amri ya Amoroni walikuja mbele dhidi ya watu wa Nefiha, na wakaanza kuwaua kwa wingi.
8 Na majeshi yao yalikuwa mengi sana kwamba watu wa Nefiha waliosalia walilazimishwa kukimbia mbele yao; na wakaja hata wakaungana na jeshi la Moroni.
9 Na sasa vile Moroni alidhani kwamba kuwe na watu watumwe kwenye mji wa Nefiha, kwa usaidizi wa wale watu kuulinda mji huo, na akijua kwamba ilikuwa ni rahisi kulinda mji usianguke kwenye mikono ya Walamani kuliko kuuteka kutoka kwao, alidhani kwamba wangelinda mji huo kwa urahisi.
10 Kwa hivyo aliweka majeshi yake yote kwa kuhifadhi zile sehemu ambazo alikuwa ameteka tena.
11 Na sasa, Moroni alipoona kwamba mji wa Nefiha umechukuliwa tena alikuwa na huzuni nyingi sana, na akaanza kuwa na shaka, kwa sababu ya uovu wa watu, ikiwa hawataanguka katika mikono ya ndugu zao.
12 Sasa hii ndiyo ilikuwa fikira ya makapteni wake wote wakuu. Walishuku na kustaajabu pia kwa sababu ya uovu wa watu, na hii ni kwa sababu ya kufaulu kwa Walamani juu yao.
13 Na ikawa kwamba Moroni alikasirishwa na serikali, kwa sababu ya kutojali kwao kuhusu uhuru wa nchi yao.