Jeshi la Malaika la Siku za Mwisho
Habari za jioni, wapendwa kaka zangu na dada zangu. Ninajiona mwenye heri kwa kupata fursa hii ya kuongea na ninyi usiku wa leo tunaposherehekea tukio hili tukufu zaidi katika historia ya mwanadamu—la kuja kwa Mwana wa Mungu ulimwenguni. Kuzaliwa kwa Kristo, maisha yake, na Upatanisho ni zawadi za Mungu kwetu sisi sote.
Tunaposherehekea kuzaliwa kwa Mwokozi katika nyakati hizi za furaha katika mwaka, upendo endelevu wa Mungu unaonekana kupenya mioyo yetu kwa wingi zaidi, ukitusaidia sisi kuigeuza mioyo yetu iwaelekee familia, marafiki na majirani, na unatusaidia sisi kuwa waangalifu zaidi kwa wale ambao yawezekana wanajisikia wapweke, au, wale ambao wanahitaji faraja na amani.
Daima nimekuwa nikishawishika kwamba, katika kuelezea matukio yanayozunguka kuzaliwa kwa Yesu, injili ya Luka inaelezea mifano kadhaa ya faraja na amani ikitolewa kwa wale waliojikuta wao wenyewe katika hali hizo. Mifano ya jinsi hii inaweza kuonekana wakati Baba wa Mbinguni alipowatuma malaika Wake kuwatokea wale wachungaji waliojitenga na jamii wakati wa usiku na kuwatangazia kuzaliwa kwa Mwanawe, na wakati wachungaji walipozungumza kwa zamu na Mariamu na Yusufu, ambao walikuwa walezi wa mtoto yule mchanga mbali na mji wao huko Galilaya.
Safari ndefu ya Yusufu na Mariamu kutoka Nazareti hadi Bethlehemu ili kuandikishwa kwa ajili ya kodi haikuwa tu kwa bahati na nasibu, kwa sababu kwa karne kadhaa, ilikuwa imetabiriwa na manabii wa kale kwamba Mwokozi wa ulimwengu angezaliwa Bethlehemu, katika mji wa Daudi.1 Tunaona kwamba Baba wa Mbinguni alikuwa amejua na kujishughulisha katika kila nyanja iliyozunguka kuzaliwa kwa Mwanawe wa Pekee. “Ikawa, katika kukaa huko, siku zake za kuzaa zikatimia.”2
Ninapofikiria hali hizi za kijamii za wachungaji na wanandoa hawa vijana Mariamu na Yusufu, ninajiuliza jinsi mwonekano wa jeshi la malaika kwa wale wachungaji waliokuwa makondeni na kuwasili kwa wachungaji mahali ambapo Mariamu na Yusufu walikuwepo kulivyoleta katika maisha yao binafsi faraja, amani na shangwe.
Kwa wachungaji, malaika hao yawezekana walileta faraja iliyohitajika kwamba Mungu alikuwa anawakumbuka na aliona thamani ndani yao kama mashahidi wa kwanza waliochaguliwa wa Mwanakondoo mchanga wa Mungu. Kwa Mariamu na Yusufu, wachungaji yawezekana walikuwa wameleta faraja iliyohitajika sana ambayo watu wengine waliijua juu ya muujiza wa kiungu ambao wao walikuwa ni sehemu yake.3
Ni dhahiri, miongoni mwetu kuna wachungaji wa siku za mwisho—wanaume na wanawake ambao hufanya kazi hadi usiku wa manane na mapema alfajiri ili kutafuta maisha. Baadhi ya hawa wachungaji wa siku za mwisho yawezekana ikajumuisha walinzi wa usalama, watumishi wa hospitali na wa sehemu za dharura, wafanyakazi wa maduka muhimu ya saa ishirini na nne na wafanyakazi wa vituo vya kuuzia mafuta ya nishati, na timu za watangazaji wa habari. Wakati mwingine wale wanaofanya kazi zamu za usiku wanaweza kuhisi kutengwa kutoka kuchangamana na jamii ya wale ambao kwa kawaida hufanya kazi wakati wa saa za kawaida. Katika nyongeza ya hayo, pia wako akina Yusufu na Mariamu wa siku za mwisho ambao wamehamia mbali na nchi za nyumbani kwao na ambao wanajaribu kuyazoea maisha mapya wakati wanaposherehekea siku muhimu kama Krismasi, kumbukizi ya siku za kuzaliwa kwao, ndoa, na vifo.
Tunapokaribia Krismasi, najiuliza kama tunaweza kuwa zaidi kama jeshi lile la malaika kwa kuwatembelea wachungaji wa siku za mwisho ili kuwapa habari njema za Kristo, amani, na faraja. Na ninajiuliza kama tunaweza kuwa zaidi kama wale wachungaji kwa kuitikia wito wa kuwatembelea na kuwatumikia akina Yusufu na Mariamu wa siku za mwisho katika maeneo yaliyo jirani na jumuiya zetu ili kutoa hakikisho kwamba Mungu anawapenda na anawalinda na anawajali.
Mimi na familia yangu tumeguswa katika matukio mengi tofauti kwa hisia za faraja na amani ambazo jeshi la malaika wa siku za mwisho linaweza kuleta. Usiku wa leo ningependa kuangazia juu ya moja ya matukio hayo. Mwaka 2003, tulihama kutoka nchi ya nyumbani kwetu na kuhamia Utah. Majira yale ya baridi, tulipata moja ya dhoruba kubwa ya theluji ambayo haijapata kutokea Utah kwa miaka mingi. Hatukuwahi kuona kitu chochote kama hicho katika maisha yetu, kwani tumekulia kwenye minazi na fuko zenye mchanga. Nyumba yetu ilikuwa kwenye kona kilimani huko Bountiful ambayo ilikuwa na njia ndefu pembeni ya waendao kwa miguu. Theluji ilipoanza, mke wangu kwa ujasiri alianza kuipuliza theluji barabarani na njia za pembeni za waendea kwa miguu kwa sababu nilikuwa nimeteleza kwenye barafu na nikavunjika kiwiko cha mkono siku chache kabla nilipokuwa napita barabarani ili kumtembelea mmoja wa majirani zetu. Ajali hiyo iliishia katika upasuaji na kufungiwa bandeji ngumu kubwa mkononi kwa miezi kadhaa. Alipoanza kupuliza theluji kwenye eneo hilo kwa mara ya kwanza katika maisha yake, mke wangu alikuwa hana wazo kwamba ingembidi kubadilisha mwelekeo wa chuti baada ya kusafisha upande mmoja wa barabara. Hivyo basi, alipokuwa akienda upande mwingine ili kusafisha, kumbe huko ndiko upande ile chuti inakoelekeza theluji hiyo. Nyuma na mbele alienda, pasipo mafanikio. Ni vurugu gani hii! Kwa sababu ya kuwa kwenye baridi kwa muda mrefu, alipata maambukizi ya sikio mara mbili na alikaribia kuwa kiziwi kabisa kwa miezi miwili. Wakati huo huo mvulana wangu wa umri wa miaka kumi na sita alijiumiza mgongo wake wakati akiondoa theluji na alilazimika kulala kitandani ili majeraha yake yapate kupona. Tukawa hivyo, mmoja kitandani, mmoja kiziwi, mmoja kafungwa bandeji kubwa ngumu, na sote tunapigwa na baridi. Nina hakika tulionekana vituko kwa majirani zetu. Katika mojawapo ya hizo asubuhi za baridi kali mapema, karibia saa 11:00 alfajiri, niliamshwa na sauti ya kipuliza theluji nje ya dirisha langu. Nilichungulia dirishani na nikamwona jirani yangu kutoka ng’ambo ya barabara ya mtaa, Kaka Blaine Williams. Akiwa na umri yapata miaka sabini, alikuwa ameacha nyumba yake yenye joto na faraja na utulivu na kimya kimya alikuwa amekuja na kusafisha barabara na njia za pembeni, akijua kwamba hatungeweza kufanya hivyo sisi wenyewe. Na vivyo hivyo alivyokuja kimya kimya na kwa njia rahisi, rafiki mwingine, Kaka Daniel Almeida, alifika nyumbani kwetu ili anipe lifti kwenda jijini Salt Lake kazini, kwani nisingeweza kuendesha gari kutokana na bandeji ile kubwa niliyofungwa. Wao walikuwa hapo kimya kimya na kwa ukarimu kwa ajili yangu kila asubuhi hadi familia yangu ilipokuwa imepona. Wakati huo wa majira ya baridi ya Krismasi ya mwaka 2003, hawa akina kaka malaika walikuwa wametumwa kwetu, kama vile wale malaika watumishi walivyotumwa kwa wale wachungaji wanyenyekevu wa siku za kale. Hawa akina kaka wawili walifuata mfano wa Mwokozi na wakafikiria mahitaji yetu kabla ya kufikiria yao wenyewe.
Wapendwa kaka zangu na dada zangu, Maisha ya Mwokozi yalikuwa mfano mkamilifu wa upendo na ukarimu kwa wanadamu. Daima alijisahau Yeye Mwenyewe kwa niaba ya wengine. Matendo Yake yasiyo na uchoyo yalidhihirika katika yote aliyofanya kila siku katika maisha Yake na hayakuishia kwenye majira maalumu au sikukuu. Tunapoigeuzia mioyo yetu nje kama Mwokozi alivyofanya, ninawaahidi kuwa, tunaweza kupata uzoefu mzuri zaidi wa maana ya Krismasi. Tunapofanya hivyo, ninaweza kuwahakikishia kwamba tutapata fursa zisizo na kikomo za kujitolea kimya kimya na kwa ukarimu kwa watu wanaotuhitaji sisi. Hii itatusaidia sisi kuja kumjua Mwokozi vyema zaidi na kujionea wenyewe amani duniani na mapenzi mema kwa watu, ambayo kwa kiwango kikubwa, hupima upendo, amani, na nguvu iliyofanywa upya ambayo tunaweza kuihisi na kuishiriki na wengine. Tunapofuata nyayo za Mwokozi, daima tusikilize sauti za miyembeo ya miguu iliyovaa ndala na kuutegemeza mkono imara wa fundi Seremala. Tunapomtafuta Mwokozi katika yote tunayofanya, Krismasi haitakuwa tu ni siku au majira bali itakuwa ni hali ya moyo na akili, na shangwe na upendo unaohisiwa wakati wa Krismasi na daima utakuwa karibu. Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo, yule mtoto mchanga aliyezaliwa Bethlehemu, kwa hakika ndiye Mwokozi na Mkombozi wa Ulimwengu.
Heri ya Krismasi kwenu nyote. Ninasema mambo haya katika jina la Yesu Kristo, amina.