2000–2009
Ee Kumbukeni, Kumbukeni
Oktoba 2007


2:3

Ee Kumbukeni, Kumbukeni

“Ee Kumbukeni, Kumbukeni,” Manabii wa Kitabu cha Mormoni mara nyingi walisihi.1 Hoja yangu ni kuwasihi mtafute njia za kutambua na kukumbuka ukarimu wa Mungu.

Nilikuwa na shukrani kwa ajili ya kwaya kwenye kipindi chao asubuhi ya leo, ambacho kilikuwa juu ya Mwokozi, na nilishukuru kuona ya kwamba maneno ya mojawapo ya nyimbo walizoimba, “This Is the Christ,” yaliandikwa na Rais James E. Faust. Nilipoketi kando ya Kaka Newell, niliegemea kwa upande wake na kuuliza, “Watoto wako hawajambo?” Alisema, “Wakati Rais Faust alipoketi katika kiti hicho, daima aliuliza hivyo.” Sijashangazwa, kwa sababu Rais Faust daima alikuwa mfano mkamilifu wa mfuasi aliyeelezewa katika Muziki na Neno Simulizi siku ya leo. Daima nilihisi kwamba wakati ningekuwa mkubwa, nilitaka kuwa kama Rais Faust. Yawezekana kwamba bado kuna muda.

Wakati watoto wetu walipokuwa wadogo mno, nilianza kuandika mambo machache kuhusu kile kilichotokea kila siku. Acheni niwaambie jinsi haya yalivyoanza. Nilikuja nyumbani usiku kutoka katika shughuli za Kanisa. Ilikuwa ni baada ya machweo. Baba mkwe wangu, aliyeishi karibu nasi, alinishangaza nilipokuwa nikitembea kuelekea mlango wa mbele wa nyumba yangu. Alikuwa amebeba mzigo wa mabomba mabegani mwake, akitembea kwa kasi akiwa amevalia mavazi yake ya kazi. Nilijua kwamba alikuwa akijenga mfumo wa kusukuma maji kutoka kwenye kijito hadi kwenye shamba letu.

Alitabasamu, akazungumza kwa upole, na kisha akapita kwa haraka nyuma yangu kwenye giza kuendelea na kazi yake. Nilipiga hatua chache kuelekea kwenye nyumba, nikifikiria kile alichokuwa akifanya kwa ajili yetu, na mara nilipofika tu mlangoni, nilisikia akilini mwangu—si kwa sauti yangu mwenyewe—maneno haya: “Mimi sikupi uzoefu huu kwa ajili yako mwenyewe. Uandike.”

Niliingia ndani. Sikwenda kitandani. Ingawa nilikuwa nimechoka, nilitoa karatasi kadhaa na nilianza kuandika. Na nilipofanya hivyo, nilielewa ujumbe niliokuwa nimeusikia katika akili yangu. Nilipaswa kuweka kumbukumbu kwa ajili ya watoto wangu kusoma, siku moja katika siku zijazo, jinsi nilivyoona mkono wa Mungu ukibariki familia yetu. Haikumbidi babu kufanya kile alichokuwa akifanya kwa ajili yetu. Angeacha mtu mwingine afanye au hangefanya kamwe. Lakini alikuwa akituhudumia, familia yake, kama vile wafuasi wa agano la Yesu Kristo wanavyofanya siku zote. Nilijua kwamba hiyo ilikuwa kweli. Na hivyo niliandika, ili kwamba watoto wangu wangeweza kuwa na kumbukumbu siku moja wakati ambapo wangekuwa na haja nayo.

Niliandika mistari michache kila siku kwa miaka mingi. Kamwe sikukosa siku bila kujali jinsi nilivyokuwa nimechoka au mapema jinsi gani ningeanza siku iliyofuata. Kabla sijaandika, nilitafakari swali hili: “Je, nimeona mkono wa Mungu ukinyooka kutugusa, au watoto wetu au familia yetu hivi leo?” “Nilivyoendelea kitu fulani kilianza kutokea. Kadiri ambavyo ningeitazama siku, ningeona ushahidi wa kile Mungu alichofanya kwa mmoja wetu ambacho sikuwa nimetambua katika wakati wa kazi nyingi za siku. Wakati hicho kikitokea, na kilitokea mara nyingi, niligundua kwamba kujaribu kukumbuka kuliruhusu Mungu kunionyesha kile Alichokifanya.

Zaidi ya shukrani ilianza kukua katika moyo wangu. Ushuhuda ulikua. Nikawa na uhakika zaidi kwamba Baba yetu wa Mbinguni husikia na hujibu maombi. Nilihisi shukrani zaidi kwa ulainishaji na utakaso unaokuja kwa sababu ya Upatanisho wa Mwokozi Yesu Kristo. Na nilikuwa katika kujiamini zaidi kwamba Roho Mtakatifu anaweza kuleta mambo yote kwenye kumbukumbu zetu —hata mambo ambayo hatukuona au kuwa nayo makini wakati yalipotokea.

Miaka mingi imepita. Wana wangu ni watu wazima. Na sasa wakati mwingine mmoja wao atanishangaza kwa kusema, “Baba, nilikuwa nikisoma katika nakala yangu ya shajara kuhusu wakati …” na kisha atanielezea kuhusu jinsi kusoma kuhusu kile kilichotokea kitambo mno kulimsaidia kugundua kitu ambacho Mungu alikuwa amefanya katika siku zake.

Hoja yangu ni kwamba ninawasihi mtafute njia za kutambua na kukumbuka ukarimu wa Mungu. Itajenga ushuhuda wetu. Huenda ukakosa kuwa na shajara. Huenda ukakosa kushiriki aina yoyote ya kumbukumbu unayoweka pamoja na wale unaowapenda na kuwahudumia. Lakini wewe na wao mtabarikiwa wakati mnapokumbuka kile ambacho Bwana amefanya. Unakumbuka ule wimbo ambao wakati mwingine huwa tunauimba: “Hesabu baraka zako; moja kwa moja, Nawe utaona ni ajabu kuu.”2

Haitakuwa rahisi kukumbuka. Tukiwa tunaishi namna hii na pazia likiwa limefunika macho yetu, hatuwezi kukumbuka namna ilivyokuwa kuwa na Baba Yetu wa Mbinguni na Mwana Wake Mpendwa, Yesu Kristo, katika maisha kabla ya dunia; wala hatuwezi kuona kwa macho yetu ya kimwili au kwa kutafakari pekee mkono wa Mungu katika maisha yetu. Kuona vitu kama hivi kunahitaji Roho Mtakatifu. Na si rahisi kuwa mstahiki wa wenza wa Roho Mtakatifu katika ulimwengu wenye uovu.

Hii ndiyo sababu kumsahau Mungu kumekuwa tatizo la kudumu miongoni mwa watoto Wake tangu dunia ilipoanza. Fikiria kuhusu nyakati za Musa, wakati Mungu alipotoa mana na katika njia za miujiza na za kuonekana aliwaongoza na kuwalinda watoto Wake. Bado, Nabii aliwaonya watu ambao walikuwa wamebarikiwa sana, kama ambavyo manabii wamewaonya na daima watakavyowaonya: “Jihadhari nafsi yako, ukailinde roho yako kwa bidii, usije ukayasahau mambo yale uliyoyaona kwa macho yako, yakaondoka moyoni mwako siku zote za maisha yako.”3

Na changamoto ya kukumbuka daima imekuwa ngumu zaidi kwa wale wanaobarikiwa zaidi. Wale walio waaminifu kwa Mungu wanalindwa na kufanikishwa. Hii inatokana na kumtumikia Mungu na kutii amri Zake. Lakini pamoja na baraka hizo huja jaribu la kusahau chanzo chake. Ni rahisi kuhisi kwamba baraka zilitolewa si kutoka kwa Mungu mwenye upendo ambaye tunamtegemea bali kupitia uwezo wetu. Manabii wamerudia ombolezi hili tena na tena:

“Na hivyo tunaweza kuona vile uwongo, na pia kutoaminika kwa mioyo ya watoto wa binadamu; ndio, tunaweza kuona kwamba Bwana katika uzuri wake usio na mwisho hubariki na kufanikisha wale ambao huweka imani yao kwake.

“Ndio, na tunaweza kuona kwa ule wakati anaofanikisha watu wake, ndio, kwa kuongeza mavuno yao, wanyama wao na mifugo yao, na kwa dhahabu, na kwa fedha, na katika kila aina ya vitu vya thamani vya kila aina na umbo; kuachilia maisha yao, na kuwaokoa kutoka kwa mikono ya maadui wao; kugusa mioyo ya maadui wao ili wasitangaze vita dhidi yao; ndio, na kwa kifupi, akifanya vitu vyote kwa ustawi na furaha ya watu wake; ndio, na hapo ni wakati ambao wanashupaza mioyo yao, na humsahau Bwana Mungu wao, na kumkanyaga chini ya miguu yao yule Mtakatifu—ndio, na wanafanya hivi kwa sababu ya utulivu wao, na mafanikio yao makubwa sana.”

Na nabii anaendelea kusema “Ndio, jinsi gani kwa haraka wanainuliwa kwa kiburi; ndio, jinsi gani ni wepesi kwa kujisifu, na kufanya kila aina ya yale ambayo ni ya uovu; na jinsi gani wana upole kumkumbuka Bwana Mungu wao, na kusikiliza amri zake, ndio, na jinsi gani ni wapole kutembea kwenye njia za hekima!”4

Kwa huzuni, kufanikiwa si sababu ya pekee ya watu kumsahau Mungu. Inaweza kuwa vigumu pia kumkumbuka Yeye wakati maisha yetu yanapoenda vibaya. Wakati tunapopambana, jinsi wengi wanavyofanya, katika umasikini uliokithiri au wakati maadui zetu wanapotushinda au wakati ugonjwa unapokosa kupona, adui wa nafsi zetu anaweza kutuma ujumbe wake muovu kwamba hakuna Mungu au kwamba ikiwa Yupo Hatujali sisi. Kisha yaweza kuwa vigumu kwa Roho Mtakatifu kuleta katika kumbukumbu baraka za kipindi cha maisha yote ambazo Bwana ametupatia kuanzia utotoni na katikati ya dhiki yetu.

Kuna tiba rahisi ya maradhi ya kumsahau Mungu, baraka Zake, na jumbe Zake kwetu. Yesu Kristo aliwaahidi wanafunzi Wake wakati Alipokuwa karibu kusulubiwa, kufufuka, na kuchukuliwa kutoka kwao apae katika utukufu kwa Baba Yake. Walikuwa na wasiwasi kujua jinsi ambavyo wangeweza kustahimili wakati akiwa hayupo nao tena.

Ahadi ndiyo hii. Ilitimizwa kwa ajili yao wakati ule. Inaweza kutimizwa kwa ajili yetu sote kwa wakati huu:

“Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu.

“Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia. ”5

Cha muhimu katika kukumbuka ambako kunaleta na kudumisha ushuhuda ni kupokea Roho Mtakatifu kama msaidizi. Ni Roho Mtakatifu ambaye anatusaidia kukumbuka kile ambacho Mungu ametutendea. Ni Roho Mtakatifu anayeweza kuwasaidia wale tunaowatumikia waweze kuona kile ambacho Mungu amewatendea.

Baba wa Mbinguni ametoa utaratibu rahisi kwa ajili yetu sisi kupokea Roho Mtakatifu si mara moja lakini daima katika msukosuko wa maisha yetu ya kila siku. Utaratibu huo unarudiwa katika sala ya sakramenti: Tunaahidi kwamba daima tutamkumbuka Mwokozi. Tunaahidi kuchukua jina Lake juu yetu. Tunaahidi kutii amri Zake. Na tunaahidiwa kwamba kama tutafanya hivyo, tutakuwa na Roho Wake pamoja nasi.6 Ahadi hizo zinafanya kazi pamoja katika njia ya ajabu kuimarisha ushuhuda wetu na baada ya muda, kupitia Upatanisho, kubadili asili zetu tunapotimiza sehemu yetu ya ahadi.

Ni Roho Mtakatifu anayeshuhudia ya kwamba Yesu Kristo ni Mwana Mpendwa wa Baba wa Mbinguni anayetupenda na anataka tupate uzima wa milele pamoja Naye katika familia. Hata kwa kuanza kwa ushuhuda huo, tunahisi tamaa ya kumtumikia Yeye na kutii amri Zake. Wakati tunapoendelea kufanya hivyo, tunapokea karama za Roho Mtakatifu kutupatia nguvu katika huduma yetu. Tunakuja kuona mkono wa Bwana wazi wazi, wazi kabisa kwamba baada ya muda hatumkumbuki tu, bali tunakuja kumpenda na, kupitia nguvu za Upatanisho, tunazidi kuwa jinsi alivyo Yeye.

Unaweza kuuliza, “Lakini ni kwa jinsi gani mchakato huu unaanzishwa ndani ya mtu asiyejua chochote kuhusu Mungu na hana kabisa kumbukumbu ya uzoefu wa kiroho?” Kila mtu amekuwa na uzoefu wa kiroho ambao anaweza kuwa alikosa kuutambua. Kila mtu, punde anapoingia duniani, anapewa Roho wa Kristo. Jinsi roho huyo anavyofanya kazi inaelezewa katika kitabu cha Moroni:

“Kwani tazama, Roho ya Kristo imetolewa kwa kila mtu, ili ajue mema na maovu; kwa hivyo, ninawaonyesha njia ya kuhukumu; kwani kila kitu kinachokaribisha kufanya mema, na kushawishi kuamini katika Kristo, kinasababishwa na uwezo na thawabu ya Kristo; kwa hivyo mngejua na ufahamu kamili kwamba ni cha Mungu.

“Lakini kitu chochote ambacho hushawishi watu kufanya maovu, na kutoamini katika Kristo, na kumkana, na kutomtumikia Mungu, hapo mtajua na ufahamu kamili kwamba ni cha ibilisi; kwani kwa njia hii ndiyo ibilisi hufanya kazi, kwani hamshawishi mtu yeyote kufanya mema, la, sio mmoja; wala malaika wake; wala wale ambao hujiweka chini yake. …

“Kwa hivyo, ninawasihi nyinyi, ndugu, kwamba mtafute kwa bidii katika nuru ya Kristo kwamba mngejua mema na maovu; na ikiwa utashikilia kila kitu kizuri, na usilaumu, hapo utakuwa bila shaka mtoto wa Kristo.”7

Kwa hivyo, hata kabla ya watu kupokea haki ya vipawa vya Roho Mtakatifu, wakati wanapothibitishwa kama washiriki wa Kanisa, na hata kabla ya Roho Mtakatifu kuthibitisha ukweli kwao kabla ya ubatizo, wanao uzoefu wa kiroho. Roho wa Kristo tayari, toka utotoni mwao, amewaalika wao kutenda mema na kuwaonya dhidi ya uovu. Wanazo kumbukumbu za uzoefu huo hata kama hawajatambua chazo chake. Kumbukumbu hiyo itawarejelea pale wamisionari au sisi tunapowafunza neno la Mungu na wanapolisikia. Watakumbuka hisia ya shangwe au huzuni wakati wanapofundishwa kweli za injili. Na kumbukumbu hiyo ya Roho wa Kristo italainisha mioyo yao na kuruhusu Roho Mtakatifu kushuhudia kwao. Hilo litawasababisha kutii amri na kutaka kujichukulia jina la Mwokozi juu yao. Na wakati watakapofanya hivyo, katika maji ya ubatizo, na wanaposikia maneno katika uthibitisho “Pokea Roho Mtakatifu” yatakayozungumzwa na mtumishi wa Mungu mwenye mamlaka, uwezo wa kumkumbuka Mungu daima utaongezeka.

Ninatoa ushuhuda kwenu kwamba hisia nzuri ambazo umekuwa nazo wakati umekuwa ukisikiliza ukweli ukizungumzwa katika mkutano huu zimetoka kwa Roho Mtakatifu. Mwokozi, ambaye aliahidi ya kwamba Roho Mtakatifu angekuja, ni Mwana mpendwa, mtukufu wa Baba yetu wa Mbinguni.

Usiku wa leo, na kesho usiku, unaweza kusali na kutafakari, ukiuliza maswali: Je, Mungu alituma ujumbe ambao ulikuwa mahususi kwa ajili yangu? Je, niliona mkono Wake katika maisha yangu au maisha ya watoto wangu? Nitafanya hivyo. Na kisha nitatafuta njia ya kuhifadhi kumbukumbu hiyo kwa ajili ya ile siku mimi, na wale ninaowapenda, tutakapohitaji kukumbuka ni kiasi gani Mungu anatupenda na kiasi gani tunamhitaji Yeye. Ninashuhudia kwamba Anatupenda na anatubariki sisi, zaidi ya wengi wetu tunavyotambua. Ninajua kuwa hayo ni kweli, na inanipa shangwe kumkumbuka Yeye. Katika jina la Yesu Kristo, amina.