Hamu
Ili kufikia hatima yetu ya milele, tutatamani na kufanyia kazi viwango vinavyohitajika ili kuwa viumbe wa milele.
Nimechagua kuongea kuhusu umuhimu wa hamu. Natumaini kila mmoja wetu atachunguza moyo wake ili kujua kile tunachotamani hasa na jinsi tunavyotoa kipaumbele kwa hamu zetu zilizo muhimu sana.
Hamu huamua vipaumbele vyetu, vipaumbele vinajenga chaguzi zetu, na chaguzi huamua matendo yetu. Hamu tunazozifanyia kazi huamua badiliko letu, kufanikiwa kwetu na kuwa tukitakacho.
Kwanza nitaongelea baadhi ya hamu za kawaida. Kama binadamu tuna baadhi ya mahitaji ya kimwili ya msingi. Hamu ya kutimiza mahitaji haya hulazimisha chaguzi zetu na huamua matendo yetu. Mifano mitatu itaonyesha jinsi sisi wakati mwingine tunavyoshinda hamu hizi kwa hamu zingine ambazo tunaweza kufikiria kuwa muhimu zaidi.
Kwanza, chakula. Tuna hitaji la kimsingi la chakula, lakini kwa muda fulani hiyo hamu inaweza kushindwa na hamu kubwa ya kufunga.
Pili, makazi. Kama mvulana wa miaka 12 nilishinda hamu ya makazi kwa sababu ya hamu kuu ya kutimiza mahitaji ya Uskauti ya kulala usiku msituni. Nilikuwa mmoja wa wavulana kadhaa ambao waliacha faraja ya mahema na kupata njia ya kujenga makazi na kutengeneza kitanda cha kawaida kutokana na vifaa vya asili ambavyo tungeweza kuvipata.
Tatu, usingizi. Hata hii hamu ya msingi inaweza kushindwa kwa muda na hata hamu iliyo muhimu zaidi. Kama askari kijana katika Utah National Guard, nilijifunza mfano wa hili kutoka kwa ofisa wa mapambano mwenye uzoefu.
Katika miezi ya mwanzoni ya Vita vya Korea, kikosi cha mizinga cha Richfiled Utah National Guard kilienda vitani. Kikosi hiki, kikiongozwa na Kapteni Ray Cox, kilikuwa na karibia wanaume wamormoni 40. Baada ya mafunzo ya ziada na kuongezwa nguvu na wanajeshi wa ziada kutoka sehemu zingine, kilitumwa Korea, ambapo walipata uzoefu wa mapambano makali ya vita hiyo. Katika mapambano fulani iliwabidi wakinzane na shambulio la adui la moja kwa moja la mamia ya jeshi la nchi kavu, aina hii ya shambulio ambalo lilishinda na kuangamiza kikosi cha mizinga.
Hii ina uhusiano gani na kushinda hamu ya usingizi? Wakati wa usiku fulani muhimu sana, wakati jeshi la nchi kavu lilisonga upande wa mbele na sehemu za nyuma za eneo lilishikiliwa na kikosi cha mizinga, kapteni alikuwa na simu katika hema lake na aliamuru walinzi wake wengi wa eneo hilo kumpigia simu yeye binafsi kila baada ya saa moja usiku kucha. Hii iliwafanya walinzi wawe macho, lakini pia ilimaanisha kwamba Kapteni Cox alipata usumbufu mwingi katika usingizi wake. “Unawezaje kufanya hilo?” Nilimwuliza. Jibu lake linaonyesha nguvu za kushinda hamu.
“Nilijua kwamba ikiwa ningerudi nyumbani, ningekutana na wazazi wa wavulana hao katika mitaa katika mji wetu mdogo, na nisingependa kukutana na yeyote kati yao kama mwana wao asingeweza kurudi nyumbani kwa sababu ya chohote nilichokosea kufanya kama kamanda wake.”1
Ni mfano ulioje wa nguvu ya kushinda hamu ya vipaumbele na ya matendo! Ni mfano ulioje kwa ajili yetu sote ambao tuna jukumu la ustawi wa wengine—kama wazazi, viongozi wa Kanisa na walimu!
Kama hitimisho la kielelezo hiki, mapema asubuhi kufuatia usiku wa bila usingizi, Kapteni Cox aliongoza watu wake kufanya shambulizi kwenye kambi ya adui. Waliteka maabusu 800 na walikuwa na majeruhi wawili tu. Cox alituzwa kwa ushupavu, na kikosi chake kilipata tuzo ya Kitengo cha Rais cha Nukuu kwa ushujaa wake wa ajabu. Na, kama wavulana jasiri wa Helamani (ona Alma 57:25–26), wote walirudi nyumbani.2
Kitabu cha Mormoni kina mafundisho mengi juu ya umuhimu wa hamu.
Baada ya saa nyingi za kumsihi Bwana, Enoshi aliambiwa kwamba dhambi zake zimesamehewa. Ndipo yeye “alianza kushughulika na ustawi wa ndugu [zake]” (Enoshi 1:9). Yeye aliandika, “Na … baada ya kuomba na kumtumikia kwa bidii, Bwana akaniambia: Kwa sababu ya imani yako, nitakutendea kulingana na mahitaji yako” (mstari wa 12). Tazama mambo matatu muhimu ambayo yalitangulia ahadi zilizoahidiwa: hamu, kazi na imani.
Katika hotuba yake juu ya imani, Alma anafundisha kwamba imani inaweza kuanza na “kuacha hamu hii ifanye kazi ndani [yetu]” (Alma 32:27).
Fundisho kuu lingine la hamu, hasa juu ya kile kinachopaswa kuwa hamu yetu kuu, hutokea katika uzoefu wa mfalme Mlamani akifunzwa na mmisionari Haruni. Wakati mafundisho ya Haruni yalipomvutia, mfalme aliuliza, “Nitafanya nini ili nizaliwe kwa Mungu” na “nipate uzima wa milele?” (Alma 22:15). Haruni alijibu: “Ikiwa unatamani kitu hiki, ikiwa utamsujudia Mungu, ndio, ikiwa utatubu dhambi zako zote, na umsujudie Mungu, na umlingane kwa imani, ukiamini kwamba utapokea, ndipo utakapopokea matumaini ambayo unatamani (mstari wa 16).
Mfalme alifanya hivyo na katika sala kuu alitamka, “Nitaacha dhambi zangu zote ili nikujue wewe, … na niokolewe siku ya mwisho” (mstari wa 18). Kwa dhamira hiyo na utambulisho huo wa hamu kuu, maombi yake yalijibiwa kimiujiza.
Nabii Alma alikuwa na hamu kubwa ya kusihi toba kwa watu wote, lakini alikuja kuelewa kwamba hakupaswa kutamani nguvu za kuzidi ambazo zingehitajika kwa sababu, alihitimisha, “Mungu wa haki, kwani najua kwamba hutoa kwa watu kulingana na kutaka kwao, kama itakuwa kwenye kifo ama kwenye uhai” (Alma 29:4). Vivyo hivyo, katika ufunuo wa kisasa Bwana ametangaza kwamba Yeye “atawahukumu watu wote kulingana na matendo yao, kulingana na tamaa za mioyo yao” (M&M 137:9).
Je, sisi kweli tumejiandaa ili Mwamuzi wetu wa Milele aweke huu umuhimu mkubwa kwa kile tunachotamani?
Maandiko mengi yanasema juu ya kile tunachotamani yakimaanisha kile tunachotafuta. “Yule anitafutaye mapema ataniona, na wala hatasahaulika” (M&M 88:83). “Takeni sana karama zilizo kuu” (M&M 46:8). “Kwani atafutaye kwa bidii atapata” (1 Nefi 10:19). “Njoo karibu yangu nami nitakuja karibu yako; nitafuteni kwa bidii nanyi mtaniona; ombeni nanyi mtapata, bisheni, nanyi mtafunguliwa” (M&M 88:63).
Kurekebisha hamu zetu ili kuweka kipaumbele cha juu kwa vitu vya milele si rahisi. Sisi sote tunajaribiwa kutamani vitu vinne vya ulimwengu, mali, umaarufu, ufahari, na nguvu. Tunaweza kutamani vitu hivi, lakini hatupaswi kuviwekea vipaumbele vyetu.
Wale ambao hamu kuu ni kupata mali wanaangukia katika mtego wa kutafuta mali. Wanashindwa kutii onyo “Usitafute utajiri wala vitu visivyo vya maana vya ulimwengu huu” (Alma 39:14; ona pia Yakobo 2:18).
Wale ambao wanatamani umaarufu au nguvu wanapaswa kufuata mfano wa jasiri Kapteni Moroni, ambaye huduma yake haikuwa kwa ajili ya “ukubwa” au kwa ajili ya “heshima ya ulimwengu” (Alma 60:36).
Tunakuzaje hamu? Wachache watakuwa na tatizo kama lile lililomtia Aron Ralston motisha,3 lakini uzoefu wake unatoa somo la thamani kuhusu kukuza hamu. Wakati Ralston akipanda korongo huko kusini mwa Utah, mwamba wa ratili 800 (kilo 360) ulihama ghafla na kunasa mkono wake. Kwa siku tano za upweke aling’ang’ana kujikwamua. Wakati akiwa karibu kukata tamaa na kukubali kifo, aliona ono la mtoto wa miaka mitatu akimkimbilia na kumnyanyua kwa mkono wake wa kushoto. Akielewa hili kama ono la mwanawe wa siku za usoni na hakikisho la kwamba bado angeweza kuwa hai, Ralston alijipa ujarisi na kuchukua hatua kali ya kuokoa maisha yake kabla nguvu hazijamwishia. Alivunja mifupa miwili ya mkono wake wa kulia uliokwama na kisha kutumia kisu kuukata mkono huo. Yeye kisha akajikokota kupanda mwendo wa maili tano (kilometa 8) kutafuta msaada.4 Ni mfano ulioje wa nguvu za hamu iliyozidi kipimo! Tunapokuwa na ono la kile tunachoweza kuwa, hamu yetu na nguvu zetu za kutenda huongezeka maradufu.
Wengi wetu kamwe hatutakabiliana na tatizo kali kama hilo, lakini sisi sote tunakabiliana na mitego ambayo itazuia kusonga kuelekea hatima yetu ya milele. Ikiwa matamanio yetu ya haki yana uzito wa kutosha, yatatupatia motisha ya kujikata na kujichonga ili tuwe huru kutokana na uraibu na mashinikizo mengine ya dhambi na vipaumbele vinavyozuia maendeleo yetu ya milele.
Tunapaswa kukumbuka kwamba matamanio ya haki hayawezi kuwa ya juu juu, ya kushitukiza, au ya muda tu. Yanapaswa kusikika moyoni, yasiyoyumba na ya kudumu. Tukiwa na hamu ya dhati, tutatafuta hali ile iliyoelezwa na Nabii Joseph Smith, ambayo ni “tunashinda uovu wa [maisha yetu] na kupoteza kila hamu ya dhambi.”5 Huo ni uamuzi wa kibinafsi kabisa. Kama Mzee Neal A. Maxwell alivyosema:
“Wakati watu wanaelezewa kama ‘wamepoteza hamu yao ya dhambi,’ ni wao, na wao pekee, ambao kwa kusudi waliamua kupoteza hizo hamu mbaya kwa kuwa tayari ‘kuacha dhambi [zao] zote’ ili kumjua Mungu.”
“Kwa hivyo, kile tunachotamani siku zote, kwa muda mrefu, ndio kile hatimaye tutakachokuwa na ndicho tutakachopokea katika umilele.”6
Kama ilivyo muhimu kwenye kupoteza hamu yote ya kutenda dhambi, uzima wa milele unahitaji zaidi. Ili kufikia hatima yetu ya milele, tutatamani na kufanyia kazi viwango vinavyohitajika ili kuwa viumbe wa milele. Kwa mfano, viumbe wa milele wanawasamehe wote ambao wamewakosea. Wanaweka ustawi wa wengine mbele ya ustawi wao wenyewe. Na wanawapenda watoto wote wa Mungu. Kama hili linaonekana kuwa gumu sana—na hakika siyo rahisi kwa yeyote kati yetu—basi tunapaswa kuanza na hamu ya viwango vya aina hiyo na tumwombe mpendwa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya msaada wa hisia zetu. Kitabu cha Mormoni hutufundisha kwamba tunapaswa “kuomba kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba [sisi] tujazwe, na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo” (Moroni 7:48).
Ninafunga na mfano wa mwisho wa hamu ambayo inafaa kuwa muhimu kwa wanaume na wanawake wote—wale ambao kwa sasa wameoana na ambao bado. Wote wanapaswa kutamani na kuwa na bidii kushughulikia kuwa na ndoa ya milele. Wale ambao tayari wana ndoa ya hekaluni wanapaswa kufanya yote wawezayo ili kuihifadhi. Wale ambao hawako kwenye ndoa wanapaswa kutamani ndoa ya hekaluni na kutia bidiii ya kuipata. Vijana wakubwa kwa wadogo wanapaswa kukinzana na kilicho sahihi kisiasa lakini kisicho dhana sahihi ya milele ambacho kinabeza umuhimu wa kuoana na kuwa na watoto.7
Wanaume waseja, tafadhali fikirieni changamoto iliyopo katika hii barua iliyoandikwa na dada mseja. Alisihi “mabinti wa haki wa Mungu ambao kwa dhati wanatafuta msaidizi mwenye kustahili vya kutosha, hali wanaume wanaonekana kupofushwa na kuchanganyikiwa kama ni wajibu wao au la kutafuta hawa mabinti wazuri, wateule wa Baba yetu wa Mbinguni na kuwachumbia na kuwa radhi kufanya na kuweka maagano matakatifu katika nyumba ya Bwana.” Alihitimisha, “Kuna wanaume WSM waseja wengi ambao wanafurahia kujifurahisha, na kufanya miadi na kuburudika, lakini hawana hamu kabisa ya kuonyesha dhamira ya aina yoyote kwa mwanamke.”8
Nina hakika kwamba baadhi ya wavulana wanaotafuta kwa bidii wangependa niongezee kwamba kuna baadhi ya wasichana ambao wanatamani ndoa ya kustahili ila swala la watoto linakuwa la mbali sana kushinda hamu yao ya ajira au sifa zingine za ulimwemgu. Wote wanaume na wanawake wanahitaji hamu za haki ambazo zitawaongoza hadi kwenye uzima wa milele.
Acha tukumbuke kwamba hamu huamuru vipaumbele vyetu, vipaumbele vinajenga chaguzi zetu na chaguzi huamua matendo yetu. Cha kuongezea, ni matendo yetu na hamu zetu ambavyo hutujenga sisi kuwa kitu fulani, aidha tuwe ni rafiki wa dhati, mwalimu mwenye kipawa au mtu anayefaa tuzo ya uzima wa milele.
Mimi nashuhudia juu ya Yesu Kristo, ambaye upendo Wake, mafundisho Yake, na Upatanisho Wake hufanya yote yawezekane. Ninaomba kwamba juu ya mengine yote tutatamani kuwa kama Yeye ili kwamba siku moja tuweze kurejea katika uwepo Wake na kupokea utimilifu wa furaha Yake. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.