Historia ya Kanisa
Maisha Mazuri


Maisha Mazuri

Wakati Gladys Nangoni alipokutana na Joseph Sitati kwenye Chuo cha Nairobi, aligundua kwamba walikuwa wamekulia kwenye eneo moja la kijijini na kusoma shule moja ya msingi. Wote walikuwa na wazazi waliowalea kwenye kufanya kazi kwa bidii na kuwajibika kwa ajili ya wengine. Kama mvulana, Joseph aliamka saa 11:00 asubuhi ili kumsaidia baba yake, kwenye shamba na mifugo ya familia, ambaye alikuwa ni afisa wa kilimo. Gladys, kama mtoto mkubwa kwenye familia yake, alisoma kwa bidii akiufuata nyayo za baba yake, mwalimu wa Kiingereza na hesabu, na hatimaye aliwafundisha ndugu zake.

Gladys aliendelea kusomea elimu, na Joseph alisomea uhandisi. Mnamo 1976, walioana. Gladys alifanya kazi kama mwalimu na kwenye Wizara ya Elimu, na Joseph alifanya kazi kama Mhandisi. Mwishoni mwa 1985, rafiki aliwatambulisha kwenye kundi dogo la Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Nairobi. Wakati mmoja kwenye mkutano, Joseph alimhisi Roho sana. Alimgeukia Gladys. “Huu ni uzoefu mpya kwangu,” alisema. “Watu hawa ni tofauti.” Walibatizwa mwaka uliofuata.

Mnamo 1987, Gladys alianza kupata matatizo ya kiafya, yakimpelekea kufanyiwa upasuaji na uponaji wa taratibu. Alichoka kutokana na mahitaji ya kazi yake na familia yake iliyokuwa ikikua. “Siku nilizokwenda kazini, nilirudi nyumbani na kujilaza,” Gladys anakumbuka, “Sikujisikia vizuri. Nilichoka.”

Joseph alipendekeza kwamba Gladys aache kazi. “Rais Benson alikuwa amesema, ‘akina mama wanaweza kubaki nyumbani,’” Gladys anakumbuka.

“Haikuwa rahisi kuamua,” Gladys anakumbuka. “Nilijua kwamba kama nitabakia nyumbani, ningeleta manufaa sana kwa watoto wangu kwa sababu bado walikuwa wadogo. Lakini pia katika nchi hizo,” anafafanua, “wanaume wengi walikuwa hawawajibiki. Kwangu mimi kuacha tu kazi, ilinifikirisha nini kingetokea kwa watoto wangu.” Alijadili uamuzi wake na ndugu zake, ambao walimsisitiza kuendelea kufanya kazi.

Alijadili uamuzi wake na Joseph. “Tuliamua kama hiki ndicho nabii anachokisema, hiki ndicho kitakachokuwa. Na kitanisadia mimi na kuisaidia familia yangu,” Gladys alisema. “Baada ya kuacha kazi, nilipona haraka sana.”

Gladys na Joseph kwa umakini walipanga bajeti kwa pamoja. Gladys, kama ilivyokuwa kwa baba yake alihakikisha watoto wake wanaelewa vyema Kiingereza na hesabu. Baada ya wapwa wanne kuwa yatima, Gladys na Joseph waliwakuza pamoja na watoto wao wenyewe watano. Ili kuleta uelewano kwenye familia kubwa, walitegemea kwenye kujifunza maandiko asubuhi na mabaraza ya familia.

Baada ya huduma kwenye wilaya, kigingi na ngazi ya misheni, Joseph aliitwa kuwa Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka mnamo 2009. Gladys alisafiri pamoja naye, akitumia ujuzi wake kama mwalimu kwenye majukumu ya kutoa mazungumzo. Mara nyingi alizungumza na vijana, akiongea kutoka kwenye uelewa wake mwenyewe kama mtoto na mzazi: “Hiki ndicho ningetaka mkumbuke: jinsi wazazi wenu kwa bidii walivyofanya kazi kujitolea kwa ajili yenu, jinsi wanavyotaka ninyi muishi maisha mazuri.”