Historia ya Kanisa
“Tunamsaidia Mtu Huyo Afanye Zaidi”


“Tunamsaidia Mtu Huyo Afanye Zaidi”

Olivia Damalie Sserabira, ambaye alihudumu kama rais wa Muungano wa Usaidizi katika Kata ya Mengo, ameelezewa kama gundi ambayo inauunganisha mkusanyiko huo pamoja. Uwezo wake wa kuwaleta watu pamoja unaenda mbali kupita kanisa na unasambaa ulimwenguni kupitia Kituo cha Mafunzo cha Peace and Hope, ambacho ni taasisi isiyo ya faida ambayo yeye aliianzisha.

“Lengo kuu la taasisi hii ya Peace and Hope ni kuboresha maisha ya watu, hususani mtoto wa kike,” Olivia alitamka. “Misheni yetu ni kukuza mipango ya kijamii ambayo inakuza hisani, mshikamano, haki ya kijamii ambavyo baadaye vingeweza kuwa zana za maendeleo katika nchi nzima, au katika Afrika Mashariki yote, au Afrika yote, au ulimwenguni kote.”

Kuanzia mwaka 2006, Olivia alifokasi katika kutoa elimu na mafunzo ya stadi kwa watoto wa familia masikini waliokosa elimu ya msingi. Mnamo 2007, Peace and Hope ilianza kutoa makazi kwa vijana wa kike wasio na makazi na kuwapatia ushauri nasaha pamoja na elimu. Mnamo 2009, Olivia alianzisha programu ya bustani, akizifundisha familia 200 jinsi gani ya kuotesha chakula katika magunia na kulima mboga mboga tofauti za lishe. Chini ya programu ya Olivia, kila familia iliyofundishwa katika bustani ya gunia ilikuwa inawajibika kuwasaidia majirani zao kuanzisha bustani zao wenyewe za gunia. Kanuni hii ya “kuwafunza walimu” ilianzisha mnyororo wa watu kushirikishana ujuzi mpya.

Kituo cha Mafunzo cha Peace and Hope kimeendelea kukua. Wanafunzi wanajifunza kutumia kompyuta, kuoka mikate, na kutengeneza bidhaa za aina mbali mbali, ikijumuisha sabuni, kofia za kamba za migomba, mikufu ya maharage mabovu, masweta, taulo za kike zinazoweza kutumika zaidi ya mara moja, na mikeka. Kituo pia kinafundisha kusoma na kuandika kiingereza, kiswahili na Kifaransa na mafunzo ya ukomavu ambayo huwafundisha wasichana kuhusu afya ya mwanamke na kujikinga na VVU.

Picha
Olivia Sserabira akiwa na wamisionari na wanafunzi

Olivia Sserabira (aliyesimama katikati) akiwa na wamisionari na wanafunzi katika Kituo cha Mafunzo cha Peace and Hope, mwaka 2009.

Olivia hajashtushwa na ukweli kwamba wanafunzi wengi wa kituo hiki huja na rasilimali chache sana za kiuchumi na kielimu. “Tunamsaidia mtu huyo afanye zaidi,” yeye alisema.

“Nilikuja kwenye Kituo cha Mafunzo cha Peace and Hope kwa sababu kuna nyenzo nzuri,” alisema Agnes, mwanafunzi kijana. “Nilikuja hapa kwa sababu niliona kozi ambazo hakika nilizipenda, kama ususi wa nywele, mapishi na kompyuta. Hivyo nilikuja hapa ili niweze kupata ujuzi baada ya kujifunza nafikiri ninaweza kupata kazi.”

Peace and Hope kimeingia ubia na mipango ya kibinadamu ya Kanisa kwenye miradi kama vile mafunzo ya afya na usafi, miradi ya maji safi na elimu ya ukomavu. Peace and Hope huwekeza rasilimali zake katika kuwasaidia wakufunzi kupata kujiamini siyo tu katika ujuzi wa kiteknolojia bali pia katika ujuzi wa kufundisha, kuwawezesha waanzishe mipango mipya miongoni mwa wanawake katika vijiji vya mbali.

Kazi ya Kituo cha Mafunzo cha Peace and Hope imetambuliwa na vyombo vya habari, Umoja wa Wanawake Wafanya Biashara, Wabunge, Spika wa Bunge Rebecca Kadaga, na malkia wa Buganda. Mwaka 2019, Olivia alizungumzia kuhusu Peace and Hope kwenye Mkutano wa Phenomenal Women’s Conference huko Boston Marekani.

Tangu Olivia aanzishe Kituo cha Mafunzo cha Peace and Hope, kimewasaidia makumi elfu ya watu binafsi “kufanya zaidi.” Wengi aliosaidia kuwafundisha sasa wanafundisha na kuwainua wengine.

Chapisha