Simama Pahali Patakatifu
Mawasiliano na Baba yetu aliye Mbinguni—pamoja na maombi yetu Kwake na maongozi Yake kwetu—ni muhimu ili tuweze kuepuka dhoruba na majaribu ya maisha.
Ndugu na dada zangu wapendwa, tumesikia jumbe nzuri asubuhi ya leo, na nampongeza kila mmoja ambaye ameshiriki. Tumefurahia hasa kuwepo kwa Mzee Robert D. Hales pamoja nasi tena na akihisi kuwa na nafuu. Tunakupenda, Bob
Kama nilivyotafakari kile nilingesema kusema nanyi asubuhi ya leo nimepata ari ya kushiriki mawazo na hisia kadha ambazo naonelea kuwa muhimu na za kufaa. Ninaomba kwamba niweze kuelekezwa katika maneno yangu.
Nimeishi duniani kwa miaka 84 sasa. Ili kuwapa mtazamo kidogo, nilizaliwa mnamo mwaka ambao Charles Lindbergh aliposafiri bila kutua kutoka New York hadi Paris kwa kutumia ndege ya injini moja, kiti kimoja na seti moja ya bawa. Mengi yamebadilika katika miaka 84 tangu wakati huo. Imekuwa muda mrefu tangu binadamu kuwa mwezini na kurejea. Kwa hakika, sayansi bunifu ya wakati uliopita sasa imekuwa halisi. Na uhalisi huo, kwa msaada wa teknolojia ya wakati wetu, unabadilika kwa kasi hata ni vigumu kushikamana nao—ikiwa tunaweza kamwe. Kwa wale kati yetu wanaokumbuka simu zenye mviringo wa kupiga namba, na mashine ya chapa ya mikono, teknolojia ya leo ni ya kushangaza zaidi sana.
Pia inayogeuka kwa kasi ni dira ya maadili ya jamii. Tabia ambazo wakati mmoja zilionekana kutofaa na zisizo za kimaadili sasa hazivumiliwi tu bali zinaonekana na watu wengi kama zinazokubaliwa.
Hivi majuzi nilisoma katika Wall Street Journal makala yaliyoandikwa na Jonathan Sacks, rabbi mkuu wa Uingereza. Miongoni mwa vitu vingine, aliandika: “Katika takriban kila jamii ya Magharibi mnamo 1960 kulikuwa na mapinduzi ya maadili, kuachwa kwa mfumo wa kitamaduni wa kujizuia. Yote unayohitaji, waliimba Beatles, ni upendo. Mfumo wa maadili wa Uyahudi-Ukristo ulitupwa. Mahali pake, ukaja [usemi]: [Fanya] chochote kinachokufaidi. Amri Kumi ziliandikwa upya kama Mapendekezo Kumi Bunifu.”
Rabbi Sacks anaendelea kuomboleza:
“Tumekuwa tukitumia mtaji wetu wa kimaadili kwa uzembe huo huo ambavyo tunavyotumia mtaji wetu wa kifedha. …
“Kuna sehemu nyingi [za dunia] ambapo dini ni jambo la kale na hakuna sauti ya kusawazisha utamaduni wa nunua, fuja, vaa, punga kwa madaha kwa sababu unastahili. Ujumbe huu ni kwamba uadilifu umepitwa na wakati na dhamiri ni ya wadhaifu na amri kuu ya pekee ni ‘Wewe usipatikane.’”1
Akina ndugu na dada, hii—kwa bahati mbaya—inaeleza kuhusu wingi wa dunia inayotuzunguka Je! tuwe na wasiwasi kwa kukata tamaa na kushangaa jinsi tutakavyonusurika katika dunia kama hii? La. hasha. Kwa hakika, tunayo katika maisha yetu injili ya Yesu Kristo na tunajua uadilifu haujapitwa na wakati, kwamba dhamiri yetu ipo kutuongoza, na kwamba tunawajibikia matendo yetu.
Ingawa dunia imebadilika, sheria za Mungu zinabaki thabiti. Hazijabadilika; hazitabadilika. Amri Kumi ni hizo tu—amri. Nazo si mapendekezo. Zinahitajika kwa kila njia hivi leo kama zilivyokuwa wakati Mungu alipowapa wana wa Israeli. Ikiwa tu tutasikiliza, tunasikia mwangwi wa sauti ya Mungu ikituzungumzia hapa na sasa:
“Usiwe na miungu mingine ila mimi.
“Usijifanyie sanamu ya kuchonga. …
“Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako. …
“Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. …
“Waheshimu baba yako na mama yako. …
“Usiue.
“Usizini.
“Usiibe.
“Usimshuhudie jirani yako uongo. …
“Usitamani.”2
Mfumo wetu wa kanuni ya maadili ni wa mkataa, hauna mjadala. Haupatikani tu kwa Amri kumi, bali pia katika Mahubiri Mlimani tuliyopewa na Mwokozi alipotembea duniani. Unapatikana kote katika mafundisho Yake. Unapatikana katika maneno ya ufunuo wa kisasa.
Baba yetu wa Mbinguni ni yule yule, jana leo na milele. Nabii Mormoni anatuambia Mungu “habadiliki kutoka milele hadi milele yote.”3 Katika ulimwengu huu ambapo karibu kila kitu kinaonekana kubadilika, uthabiti wake ni kitu ambacho tunaweza kutegemea, nanga ambayo tunaweza kushikilia na kuwa salama, ili tusisombwe kwenye maji ya hatari.
Inaweza kuonekana kwako wakati mwingine kuwa wale walioko duniani wana raha kukushinda wewe. Wengine wenu mnaweza kuhisi kuwa mnafinywa na mfumo wa kanuni za maadili ambayo sisi katika Kanisa tunazingatia. Akina ndugu na dada, nawatangazia hata hivyo kwamba hapana chochote kinachoweza kuleta shangwe maishani mwetu au amani kuliko Roho inayoweza kutujia tunapomfuata Mwokozi na kuweka amri. Kwamba Roho hawezi kuwa kati aina ya matendo ambayo wingi wa ulimwengu hujihusisha. Mtume Paulo alitangaza ukweli huu: “Mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu: maana kwake hayo ni upuuzi wala hawezi kuyafahamu kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.”4 Maneno mwanadamu wa tabia ya asili yanaweza kutuhusu ikiwa tutakubali kuwa hivyo.
Ni lazima tuwe macho katika ulimwengu ambao umesonga mbali sana kutoka kwa kile kilicho cha kiroho. Ni muhimu tukatae chochote kisichopatana na viwango vyetu, kwa njia hiyo tukikataa kupoteza kile tunachotamani zaidi—uzima wa milele katika Ufalme wa Mungu. Mawimbi bado yatapiga milangoni mwetu mara kwa mara, kwani ni sehemu isiyoepukika ya uzoefu wetu katika maisha ya muda. Sisi, hata hivyo tutakuwa tayari kukabiliana nayo, kujifunza kwayo na kuyashinda ikiwa tuna injili kwenye kiini chetu na upendo wa Mwokozi mioyoni mwetu. Nabii Isaya alitangaza, “Na kazi ya haki itakuwa amani; na mazao ya haki yatakuwa utulivu na matumaini daima.”5
Kama njia ya kuwa katika ulimwengu lakini si wa ulimwengu ni muhimu kuwa tunawasiliana na Baba wa Mbinguni kupitia kwa maombi. Anatutaka tufanye hivyo; Atajibu maombi yetu. Mwokozi alitushauri kama ilivyorekodiwa katika 3 Nefi 18,“mjihadhari na kusali siku zote, msije mkaingia majaribuni; kwani Shetani amewataka nyinyi. …
“Kwa hivyo lazima msali siku zote kwa Baba katika jina langu;
“Na chochote mtakachomwomba Baba katika jina langu, ambacho ni haki, mkiamini kwamba mtapata, tazama, kitapeanwa kwenu.”6
Nilipata ushuhuda wangu wa nguvu za maombi nilipokuwa karibu umri wa miaka 12. Nilikuwa nimefanya kazi kwa bidii ili kupata pesa na nilikuwa nimeweza kuweka akiba dola tano. Huu ulikuwa wakati wa Mfadhaiko Mkuu wakati dola tano ilikuwa pesa nyingi—hasa kwa mvulana wa miaka 12. Nilipeana sarafu zangu zote za jumla za dola tano kwa baba yangu, naye akanipa noti badala yake ya dola tano. Najua kulikuwa na kitu maalum nilichokuwa nimepanga kununua kwa dola tano ingawa miaka hii yote baadaye siwezi kukumbuka kilikuwa nini. Nakumbuka tu jisni hizo pesa zilivyokuwa muhimu kwangu.
Kwa wakati huo, hatukuwa na mashine ya kufulia nguo, kwa hivyo mama yangu alikuwa akituma nguo zetu zilizohitaji kufuliwa kwa dobi kila wiki. Baada siku kadha mzigo wa nguo zilizolowa maji ungerudishwa kwetu na Mama angezianika nguo katika kamba ya kuanikia nguo nyuma ya nyumba ili zikauke.
Nilikuwa nimeweka noti yangu ya dola tano katika mfuko wa jinzi. Kama unvyoweza kukisia, jinzi yangu ilipelekwa kwa dobi pamoja na pesa zikiwa bado mfukoni. Nilipogundua kilichofanyika, niliugua kwa wasiwasi. Nilijua kuwa mifuko ilikuwa ikiangaliwa kwa kawaida kwenye dobi kabla ya kuoshwa. Ikiwa pesa zangu hazikugunduliwa na kuchukuliwa kwa njia hiyo, nilijua ilikuwa hakika pesa zingeangushwa wakati wa kuoshwa na zingechukuliwa na mfanyikazi kwenye dobi ambaye hangejua arudishie nani pesa hizo hata kama angekuwa na nia hiyo. Nasibu ya kupata dola zangu tano ilionekana mbali sana—jambo ambalo mama yangu mpendwa alihakikisha nilipomwambia kwamba nilikuwa nimeacha pesa mfukoni.
Nilitaka hizo pesa; nilihitaji hizo pesa; nilikuwa nimefanya kazi sana ili kupata pesa hizo. Nilifahamu kulikuwa na kitu kimoja tu ningefanya. Kwa hali ya kufa moyo, nilimgeukia Baba yangu wa Mbinguni na kumsihi aweke pesa zangu salama mfukoni humo hadi kwa njia yoyote hadi nguo zetu zilizoloa zirudi.
Siku mbili ndefu sana baadaye, nilipojua ilikuwa karibu saa ya gari la mizigo kuleta nguo zetu, niliketi karibu na dirisha, nikingoja. Gari lilipoingia kwenye ukingo wa barabara moyo wangu ulikuwa unapiga kwa kasi. Mara wakati nguo zilipofika nyumbani nilichukua jinzi yangu na kukimbia kwa chumba changu. Niliweka mikono yangu iliyokuwa ikitetemeka kwenye mfuko. Wakati sikupata chochote mara moja, nilidhani yote yamepotea. Kisha vidole vyangu vikagusa hiyo noti iliyoloa ya dola tano. Nilipoivuta kutoka mfukoni nilijawa na faraja Nilitoa maombi ya dhati na shukrani kwa Baba yangu wa Mbinguni kwani nilijua alikuwa amejibu ombi langu.
Tangu wakati huo, nimepata kujibiwa maombi yasiyohesabika. Hapana siku iliyopita ambayo sijawasiliana na Baba yangu wa Mbinguni kupitia maombi. Ni uhusiano ambao ninahifadhi kwa upendo mkubwa—mmoja ambao bila ningekuwa nimepotea kabisa. Ikiwa hauna uhusiano kama huo na Baba yako wa Mbinguni, ninakuhimiza kufanya bidii kuelekea shabaha hio. Unapofanya hivyo, utapewa haki ya uongozi na mwelekezo Wake maishani mwako—muhimu kwa kila mmoja wetu ikiwa tutanusurika kiroho katika safari yetu hapa duniani. Mwongozo na mwelekezo kama huo ni karama ambazo anatupatia bila malipo tukiutafuta. Je! ni hazina iliyoje!
Ninanyenyekezwa na kushukuru wakati Baba yangu wa Mbinguni anapowasiliana nami kupitia kwa mwongozo wake. Nimejifunza kuutambua, kuuamini na kuufuata. Mara na mara tena nimekuwa mpokeaji wa mwongozo kama huo. Uzoefu mmoja wa ajabu uliotokea katika mwezi wa Agosti 1987 wakati wa kuwekwa wakfu kwa Hekalu ya Frankfurt Ujerumani. Rais Ezra Taft Benson ambaye alikuwa nasi kwa siku mbili za kwanza ilibidi arejee nyumbani, kwa hivyo ikawa nafasi yangu kusimiamia vikao vilivyobakia.
Siku ya Jumamosi tulikuwa na kikao kwa washiriki wetu wa Kiholanzi waliokuwa katika wilaya ya Hekalu la Frankfurt. Nilikuwa namfahamu mmoja wa viongozi wetu mkakamavu kutoka Uholanzi Ndugu Peter Mourik. Kabla tu baada ya kikao, nilipata msukumo dhahiri kuwa Ndugu Mourik angefaa kuitwa kuzungumzia washiriki wenzake wa Kiholanzi wakati wa kikao hicho, na kwamba kwa kweli, angeitwa kuwa mnenaji wa kwanza. Kwa kuwa sikumwona Hekaluni asubuhi hiyo, nilimpitishia Mzee Carlos E. Asay, Rais wetu wa Eneo, barua ndogo nikiuliza ikiwa Peter Mourik alikuwa amehudhuria katika kikao hicho. Kabla tu ya kusimama kuanzisha kikao, nilipata barua ndogo kutoka kwa Mzee Asay ikinifahamisha kuwa Ndugu Mourik kwa hakika hakuwa amehudhuria, kwamba alikuwa anashughuli kwingine na kuwa alikuwa na mpango wa kuhudhuria kikao cha kuweka wakfu hekaluni siku iliyofuata pamoja na vigingi vya wanajeshi.
Niliposimama katika mimbari kukaribisha watu na kutoa muhtasari wa mpango, nilipokea msukumo dhahiri tena kuwa nitangaze Peter Mourik kama mnenaji wa kwanza. Hii ikiwa kinyume na hisia zangu kwani nilikuwa nimefahamu kutoka kwa Mzee Asay kuwa Ndugu Mourik kwa hakika hakuwepo kwenye hekalu. Nikiamini msukumo huo, hata hivyo, nilitangaza toleo la kwaya na maombi na kueleza kuwa mnenaji wa kwanza angekuwa Ndugu Peter Mourik.
Niliporejea kwenye kiti changu, nilitupa macho kwa upande wa Mzee Asay na niliona katika uso wake sura ya wasiwasi. Baadaye aliniambia nilipotangaza Ndugu Mourik kama mnenaji wa kwanza, hakuamini masikio yake. Alijua kuwa nilipokea barua yake, na hata nikaisoma, na hakuelewa kwa nini nilitangaza Ndugu Mourik kama mnenaji nikijua hakuwa popote hekaluni.
Wakati hayo yote yalipokuwa takitendeka, Peter Mourik alikuwa katika mkutano katika ofisi za eneo huko Porthstrasse. Wakati mkutano wake ukiendelea ghafula alimgeukia Mzee Thomas A. Hawkes Jr ambaye alikuwa mwakilishi wa eneo na kumwuliza “Itamchukua muda gani kunifikisha hekaluni?”
Mzee Hawkes, ambaye alijulikana kuendesha kwa kasi gari lake ndogo la spoti, akajibu, “Ninaweza kukufikisha kwa dakika 10! Lakini kwa nini unahitaji kuwa hekaluni?”
Ndugu Mourik alikubali kuwa hakujua kwa nini alihitaji kwenda hekaluni lakini alijua alilazimika kufika huko. Wawili hao walielekea hekaluni mara moja.
Wakati wa wimbo mzuri wa kwaya nilitupa macho huku na kule, nikifikiri kwa wakati wowote ningemwona Peter Mourik. Sikumwona. La ajabu hata hivyo, sikuhisi wasiwasi wowote. Nilikuwa na hakikisho dhahiri kuwa yote yangekuwa sawa.
Ndugu Mourik aliingia kwenye mlango wa mbele wa hekalu wakati maombi ya kufungua yalipokuwa yakiitimishwa, akiwa bado hajafahamu kwa nini alikuwa pale. Alipotembea kwa kasi ukumbini aliona picha yangu kwenye runinga na akanisikia nikisema, “Na sasa tutasikia kutoka kwa Ndugu Peter Mourik.”
Kwa mshangao wa Mzee Asay, Peter Mourik mara moja akaingia chumbani na kuchukua nafasi yake katika jukwaa.
Baada kikao hicho, ndugu Mourik nami tulijadili kile kilichokuwa kimetendeka kabla ya fursa yake kuongea. Nimetafakari msukumo huo uliokuja siku hiyo, sio tu kwangu bali pia kwa Ndugu Peter Mourik. Huo uzoefu wa ajabu imenipa ushuhuda dhahiri kuhusu umuhimu wa kustahili kupokea msukumo kama huo, kisha kuuamini—na kuufuata—unapokuja. Ninajua bila tashwishi kwamba Bwana alitaka kwa wale waliokuwa katika kikao hicho cha kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Frankfurt kusikiliza ushuhuda wa nguvu na wa kugusa wa mtumishi Wake Ndugu Peter Mourik.
Akina ndugu na dada zangu, mawasiliano na Baba yetu wa Mbinguni—pamoja na maombi yetu kwake na ufunuo wake kwetu—ni muhimu kwetu kuweza kustahimili mawimbi na mateso ya maisha. Bwana anatualika, “Sogeeni karibu nami na mimi nitasogea karibu na nyinyi; nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata.”7 Tunapofanya hivyo, tutahisi Roho Wake maishani mwetu, akitupa hamu na ujasiri kusimama kwa nguvu na imara katika haki— “kusimama… katika mahali pa takatifu, na wala msiondoshwe.”8
Upepo wa mabadiliko unapovuma ukituzunguka, na mfumo wa jamii kuendelea kuvunjika mbele ya macho yetu, acha tukumbuke ahadi za thamani za Bwana kwa wale wanaomwamini: “Usiogope; kwa maana mimi ni pamoja nawe: usifadhaike kwa maana mimi ni Mungu wako: nitakutia nguvu naam nitakusaidia, naam nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.”9
Ni ahadi gani hii! Na baraka namna hiyo iwe yetu, naomba katika jina takatifu la Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo, amina.
© 2011 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa USA. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/10. Tafsiri iliidhinishwa: 6/10. Tafsiri ya First Presidency Message, November 2011. Swahili. 09771 743