Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Desemba 2011
Mwenye Shukrani Chaguo la kuwa Mwenye Shukrani
Baba yetu wa Mbinguni anatuamuru kuwa na shukrani katika mambo yote. 1 Wathesalonike 5:18, na anatuhitaji kutoa shukrani kwa ajili ya baraka tunazopokea. (Ona M&M 46:32). Tunafahamu kuwa amri zake zote zinakusudiwa kutufanya kuwa na furaha, na tunajua kuwa kuvunja amri huongoza kwenye mateso.
Kwa hivyo ili kuwa na furaha na kuepuka mateso, ni lazima tuwe na moyo wenye shukrani. Tumeona katika maisha yetu kiunganishi kati ya shukrani na furaha. Sote tungependa kuhisi shukrani, ili hali si rahisi kuwa na shukrani kila wakati katika mambo yote, katika majaribu maishani. Magonjwa, kuvunjika moyo, na kuwapoteza wapendwa huja maishani mwetu wakati mwingine. Huzuni wetu hufanya kuwa vigumu kuona baraka zetu na kufurahia baraka ambazo Mungu ametuwekea kwa siku za usoni.
Ni changamoto kuhesabu baraka zetu kwa sababu tuna mazoea ya kuchukulia mambo mazuri kuwa ya kawaida. Tukipoteza makao, chakula, au joto la familia na marafiki, tunagundua kuwa tungekuwa na shukrani wakati tulipokuwa nao.
Zaidi ya yote, wakati mwingine ni vigumu kwetu kuwa wenye shukrani ya kutosha kwa karama kuu tunazopokea: kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Upatanisho Wake, ahadi ya ufufuo, na nafasi ya kufurahia uzima wa milele na familia zetu, Urejesho wa injili pamoja na ukuhani na funguo zake. Ni kupitia tu kwa usaidizi wa Roho Mtakatifu ambapo tunaanza kuhisi maana ya baraka hizo kwetu na kwa wapendwa wetu. Na hapo tu ndipo tunapoweza kutumainia kuwa wenye shukrani kwa mambo yote bila kumkosea Mungu kwa kukosa shukrani.
Ni lazima tuulize kwa maombi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwamba Mungu atusaidie kuona baraka zetu kwa uwazi licha ya majaribu yetu. Anaweza kutusaidia kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kutambua na kushukuru kwa ajili ya baraka tunazoona kuwa za kawaida. Kilichonisaidia zaidi ni kumwuliza Mungu kwa maombi, “Tafadhali Ungeniongoza kwa mtu ninayeweza kumsaidia kwa niaba Yako?” Ni katika Kumsaidia Mungu kuwabariki wengine ndipo nilipoweza kuona baraka zangu kwa karibu zaidi.
Maombi yangu yalijibiwa wakati mmoja wachumba nisiowajua kabla waliponialika kwenda katika hospitali. Huko nilipata mtoto mdogo aliyeweza kumpima kwenye mkono wangu. Katika majuma machache, alikuwa amefanyiwa upasuaji mara nyingi. Madaktari walikuwa wamewaambia wazazi kuwa upasuaji mgumu zaidi ungehitajika ili kuwezesha moyo na mapafu kuweza kukimu maisha katika huyo mtoto mdogo wa Mungu.
Kwa maombi ya wazazi, nilimpa huyo mtoto baraka za ukuhani. Baraka ilijumuisha ahadi ya maisha marefu. Zaidi ya kupeana baraka, nilipokea baraka mimi mwenyewe kwa moyo wenye shukrani zaidi.
Kwa usaidizi wa Baba yetu, sote tunaweza kuchagua kuhisi shukrani zaidi. Tunaweza kumwuliza atusaidie kuona baraka zetu kwa uwazi zaidi licha ya hali zetu. Kwangu, siku hiyo, nilifurahia zaidi mwujiza wa utenda kazi wa moyo na mapafu yangu mwenyewe. Nilishukuru njiani mwote kuelekea nyumbani kwa baraka kwa watoto wangu na kwamba ningeweza kuona kwa uwazi zaidi miujiza ya wema kutoka kwa Mungu na kutoka kwa watu wema karibu na wao.
Zaidi ya yote, nilihisi shukrani kwa ushahidi wa Upatanisho ukifanya kazi katika maisha ya wazazi hawa na kwa maisha yangu. Nilikuwa nimeona matumaini na upendo halisi wa Kristo uking’aa katika nyuso zao hata katika majaribu yao makali. Na nilihisi ushahidi kuwa unaweza kuhisi ukimwuliza Mungu kukufunulia kuwa Upatanisho unakuwezesha wewe kuhisi matumaini na upendo.
Sote tunaweza kufanya chaguo la kushukuru katika maombi na kumwuliza Mungu maongozi katika kuwahudumia wengine kwa niaba Yake—hasa kwa wakati huu wa mwaka tunaposherehekea kuzaliwa kwa Mwokozi. Mungu Baba alimtoa Mwanawe, na Yesu Kristo akatupa Upatanisho, karama kuu zaidi ya zote na kutoa kote. (ona M&M 14:7).
Kutoa shukrani katika maombi kunaweza kutuwezesha kuona ukuu wa baraka hizi na zingine zote na hivyo kupokea karama ya moyo wenye shukrani zaidi.
© 2011 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa Imechapishwa USA Kiingereza kiliidhinishwa: 6/10. Tafsiri iliidhinishwa: 6/10. Tafsiri ya First Presidency Message, December 2011. Swahili. 09772 743