Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Februari 2012
Wahimize Wao Kuomba
Nilipokuwa mtoto mdogo, wazazi wangu walinifunza kwa mfano kuomba. Nilianza kwa kuwa na picha akilini mwangu ya Baba wa Mbinguni kuwa mbali sana. Kama nilivyokomaa, uzoefu wangu wa maombi umebadilika. Picha hii katika akili yangu umekuwa moja ya Baba wa Mbinguni ambaye yu karibu sana, ambaye aliyejawa na nuru angavu, na ambaye ananijua kikamilifu.
Hayo mabadiliko yalikuja nilipopata ushuhuda mkamilifu kwamba ripoti ya Joseph Smith ya uzoefu wake mnamo 1820 katika Manchester, New York, ni kweli:
“Niliona nguzo ya mwanga juu ya kichwa changu, ambao ulikuwa ni mng’aro uliozidi mwangaza wa jua, ambao ulishuka taratibu hadi ukashuka juu yangu.
“Mara ulipoonekana nilijikuta kuwa nimekombolewa kutokana na adui yule aliyenifunga. Wakati mwanga ulipotua juu yangu niliwaona Viumbe wawili, ambao mng’aro na utukufu wao unapita maelezo yote, wakiwa wamesimama juu yangu angani. Mmoja wao akaniambia, akiniita mimi kwa jina na kusema, huku akimwonyesha yule mwingine—Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikize Yeye!” Joseph Smith—Historia ya 1:16–17).
Baba wa Mbinguni alikuwa katika kichaka katika siku hio njema ya majira ya kuchipua. Yeye alimuita Joseph kwa jina. Na akamtambulisha Mwokozi wa ulimwengu aliyefufuka kama “Mwanawe Mpendwa.” Wakati wowote au popote unapoomba, ushuhuda wako wa uhalisi wa uzoefu mtukufu huu unaweza kukubariki.
Baba ambaye kwake tunamwomba ni Mungu mtukufu ambaye aliumba dunia kupitia Mwanawe Mpendwa. Yeye husikia maombi yetu kama Yeye alivyosikia maombi ya Joseph—kwa uwazi kama vile yanatolewa mbele Zake. Yeye anatupenda sisi ya kutosha kwamba alimtoa Mwanawe kama Mwokozi wetu. Kwa hicho kipawa alifanya iwezekane kwetu kupata kutokufa na uzima wa milele. Na Yeye alitupatia sisi, kupitia maombi katika jina la Mwanawe, nafasi ya kuwasiliana naye katika maisha haya kila mara kama tunavyochagua.
Wenye ukuhani katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho wana wakala mtakatifu wa “kutembelea nyumba ya kila mshiriki, na kuwahimiza wao kuomba kwa sauti na kwa faragha” (M&M 20:47; mkazo umeongezewa).
Kuna njia nyingi za kuhimiza mtu kuomba. Kwa mfano, tunaweza kushuhudia kwamba Mungu ametuamuru sisi kuomba kila mara, au tunaweza kuelezea mifano kutoka kwenye maandiko na kutoka kwa uzoefu wetu wenyewe juu ya baraka ambazo zinatokana na maombi ya shukrani, kusihi, na maulizo. Kwa mfano, ninaweza kushuhudia kwamba najua kwamba Baba wa Mbinguni hujibu maombi. Mimi nishapokea maelekezo na faraja kutoka kwa maneno ambayo yamekuja akilini mwangu, na najua kwa Roho kwamba maneno haya yanatoka kwa Mungu.
Nabii Joseph Smith alipata uzoefu kama huu, na vivyo hivyo wewe unaweza. Yeye alipokea jibu la maombi ya moyo:
“Mwanangu, amani iwe katika nafsi yako; taabu yako na mateso yako yatakuwa kwa muda mfupi;
“Na halafu, kama utastahimili vyema, Mungu atakuinua juu” (M&M 121: 7–8).
Huo ulikuwa ufunuo kutoka kwa Baba mwenye upendo kwa mwana mwaminifu akiwa katika dhiki kuu. Kila mtoto wa Mungu anaweza kuwasiliana kwa maombi na Yeye. Hamna kuhimiza kokote kwa kuomba kulikokuwa na athari kuu kwangu kama kuwa na hisia ya upendo na nuru ambayo inakuja na majibu ya maombi ya unyenyekevu.
Tunapata ushuhuda wa amri yoyote ya Mungu kwa kuweka amri hiyo (onaYohana 7:17). Hii ni kweli kwa amri kwamba tuombe kila mara kwa sauti na kwa faragha. Kama mwalimu wako na rafiki yako, mimi ninaahidi kwamba Mungu atajibu maombi yenu na kwamba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, mnaweza kujua wenyewe kwamba majibu yanatoka Kwake.
© 2012 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa USA. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/11. Tafsiri iliidhinishwa: 6/11. Tafsiri ya First Presidency Message, February 2012. Swahili. 10362 743