Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Mei 2016
Chaguzi
Na tuweze daima kuchagua yaliyo magumu ya haki, badala ya yaliyo rahisi ya makosa.
Ndugu na dada, kabla ya kuanza ujumbe wangu rasmi leo hii, ningependa kutangaza mahekalu manne mapya ambayo, katika miezi na miaka ijayo, yatajengwa katika maeneo yafuatayo: Quito, Ecuador; Harare, Zimbabwe; Belém, Brazil; na la pili katika Lima, Peru
Wakati nilipopewa mwito kuwa mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili mwaka wa 1963, kulikuwepo na mahekalu 12 yaliyokuwa yakitumika katika Kanisa zima. Pamoja na kuwekwa wakfu kwa Hekalu la Provo City Center wiki mbili zilizopita, kunayo mahekalu 150 yanayotumika kote duniani. Ni shukrani iliyoje tuliyonayo kwa baraka tunazopokea katika nyumba hizi takatifu.
Sasa, ndugu na dada, ningependa kutoa shukrani kwa nafasi ya kushiriki mawazo kadhaa nanyi asubuhi ya leo.
Nimekuwa nikifikiria hivi majuzi kuhusu chaguzi. Imeshasemwa kwamba mlango wa historia hufunguliwa juu bawaba ndogo, na hivyo pia ndivyo maisha yetu. Chaguzi tunazofanya huamua hatima yetu.
Tulipoondoka katika maisha kabla ya hapa duniani na kuingia katika maisha ya duniani, tulikuja na zawadi ya uhuru wa kujiamulia. Lengo letu ni kupata utukufu wa selestia, na uchaguzi tunaofanya utaweza, pakubwa, kuamua ikiwa tutafikia lengo letu au la.
Wengi wenu mnafahamu Alice katika riwaya ya Lewis Carroll ya Alice’s Adventures in Wonderland. Mtakumbuka kwamba anafika kwenye njia panda yenye njia mbili mbele yake, kila moja ikinyooka kwenda mbele lakini kwenye mielekeo tofauti. Huku akitafakari upande gani wa kuelekea, anakabiliwa na yule paka Cheshire, ambaye Alice anamuuliza, “Njia ipi nitafuata?
Yule paka anajibu, “Inategemea na wapi unapotaka kwenda. Kama hujui mahali unapotaka kwenda, haijalishi njia utakayochagua.”1
Tofauti na Alice, tunajua tunapotaka kwenda, na ndiyo inajalisha njia ambayo tutachagua, kwa vile njia tunayofuata maishani humu inaelekea hadi hatima yetu katika maisha yajayo.
Na tuweze kuchagua kujenga imani ndani yetu, imani kubwa na yenye nguvu ambayo itakuwa kinga yetu yenye ufanisi zaidi dhidi ya mipango ya adui—imani ya kweli, aina ya imani ambayo itatuimarisha na itasaidia hamu yetu ya kuchagua haki. Bila imani kama hii, hatuendi popote. Tukiwa nayo, tunaweza kutimiza malengo yetu.
Ingawa ni lazima tuchague kwa busara, kuna wakati ambapo tutafanya uchaguzi usio wa busara. Zawadi ya kutubu, iliyotolewa na Mwokozi wetu, inatuwezesha kurekebisha mwelekeo wetu, ili tuweze kurudi katika njia ambayo itatuongoza hata kwenye ule utukufu selestia tunaoutafuta.
Natuweze kuendelea kuwa na ujasiri wa kupinga yanayokubaliwa na wengi. Natuweze daima kuchagua yaliyo magumu ya haki, badala ya yaliyo rahisi ya makosa.
Tunapotafakari uamuzi tunaofanya maishani mwetu kila siku—kama ni kufanya uchaguzi huu au ule mwingine—ikiwa tutamchagua Kristo, tutakuwa tumefanya uchaguzi sahihi.
Kwamba hili na liweze kuwa hivyo ni sala yangu ya dhati na ya unyenyekevu katika jina la Yesu Kristo, Bwana na Mwokozi wetu, amina.
© 2016 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa Marekani. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/15. Tafsiri iliidhinishwa: 6/15. Tafsiri ya First Presidency Message, May 2016. Swahilli. 12865 743