2016
Baada ya Upendo, Kisha Nini?
Septemba 2016


Ujumbe wa Urais wa Kwanza Septemba 2016

Baada ya Upendo, Kisha Nini?

Nabii wetu mpendwa, Rais Thomas S. Monson, amefundisha kwamba “upendo ni asili kubwa ya injili.”1

Upendo ni muhimu hata kwamba Yesu aliuita “amri ya kwanza na iliyo kuu” na alisema kwamba kila sehemu ya sheria na maneno ya manabii hutegemea juu yake.2

Upendo ni nia kuu kwa yote tunayoyafanya katika Kanisa. Kila mpango, kila mkutano, kila tendo tunalohusika nalo kama wafuasi wa Yesu Kristo lazima litokane na tabia hii—kwani bila hisani, “upendo mkuu wa Kristo,” sisi si kitu.

Mara tunapoelewa haya kwa akili na moyo wetu, mara tunapotangaza upendo wetu kwa Mungu na kwa wenzetu—nini kinafuata?

Je, kuwa na huruma na upendo kwa wengine kunatosha? Je, kutangaza upendo wetu kwa Mungu na jirani zetu kunakidhi wajibu wetu kwa Mungu?

Mithali ya Wana Wawili

Hekaluni huko Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walimjia Yesu kumtega katika maneno yake. Mwokozi, hata hivyo, akageuza meza juu yao kwa kuwaambia hadithi.

“Kuna mtu alikuwa na wana wawili,” Alianza. Baba akamwendea wa kwanza na kumwambia aende kufanyakazi katika shamba la mizabibu. Lakini mwana alikataa. Baadaye yule mwana “akatubu, na akaenda.”

Baba kisha akamwendea mwana wa pili na kumwambia aende kufanyakazi katika shamba la mizabibu. Mwana wa pili alimhakikishia kwamba angekwenda, lakini hakwenda kamwe.

Mwokozi akawageukia makuhani na wazee na kuwauliza, “Ni nani kati ya wana hawa wawili alitenda mapenzi ya baba yake?”

Walikubali kwamba mwana wa kwanza—yule aliyesema asingekwenda lakini baadaye alitubu na kwenda kufanyakazi kwenye shamba la mizabibu.4

Mwokozi alitumia hadithi hii kusisitiza kanuni muhimu—ni wale wanaotii amri ndio kweli wanaompenda Mungu.

Pengine, ndiyo maana Yesu aliwaambia watu wasikilize na kufuata maneno ya Mafarisayo na walimu lakini wasifuate mfano wao.5 Walimu hawa wa dini hawakufuata mwongozo. Walipenda kuongea kuhusu dini, lakini kwa masikitiko walikosa uasili wake.

Matendo na Wokovu wetu

Katika masomo ya mwisho ya Mwokozi kwa wanafunzi Wake, Aliongea nao kuhusu Hukumu ya Mwisho. Waovu na wema watatenganishwa. Wema wataurithi uzima wa milele, waovu watapelekwa kwenye adhabu ya milele.

Ni nini ilikuwa tofauti kati ya makundi mawili?

Wale walioonyesha upendo wao kupitia matendo waliokolewa. Wale ambao hawakuonyesha upendo walilaaniwa.6 Uongofu wa kweli kwa injili ya Yesu Kristo na thamani zake, na kanuni zake zitashuhudiwa na matendo yetu katika maisha yetu ya kila siku.

Mwishoni, kutangaza tu upendo kwa Mungu na wenzetu hakutatuwezesha sisi kutukuka. Kwani, kama Yesu alivyofundisha, “sio kila anayesema kwangu, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; lakini yule anayefanya mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.”7

Nini Kinafuata baada ya Upendo?

Jibu kwa swali “Baada ya upendo, kisha nini?” inaweza kuwa rahisi na moja kwa moja. Kama kweli tunampenda Mwokozi, tunaitoa mioyo yetu Kwake na kisha kutembea katika njia ya ufuasi. Tunapompenda Mungu, tutajitahidi kutii amri zake.8

Kama kweli tunawapenda wenzetu, tunajitoa sisi wenyewe kuwasaidia, maskini na wenye shida, wagonjwa na wanaoteseka.”9 Kwani wale watendao matendo ya huruma na huduma isiyo ya kibinafsi,10 hao ndio wafuasi wa Yesu Kristo.

Hiki ndicho kinachofuata baada ya Upendo.

Hiki ndicho kiini cha injili ya Yesu Kristo.

Kufundisha kutoka kwenye Ujumbe Huu

Rais Uchtdorf anaelezea wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo ni wale wanaoonyesha upendo Kwake na kwa wengine kupitia matendo yao. Anatufundisha kwamba “kama kweli tunampenda Mwokozi, tunaitoa mioyo yetu Kwake na kisha kutembea katika njia ya ufuasi.” Fikiria kuwauliza wale unaowafundisha ni katika njia gani upendo umewatia moyo wa kutembea katika njia ya ufuasi. Unaweza kushiriki uzoefu wako pamoja nao pia. Unaweza kufikiria kuwaalika kuomba kwa ajili ya hisani zaidi na nguvu ya kuonyesha upendo.

Chapisha