2018
Neno la Mungu kwa Watoto Wake.
March 2018


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Machi 2018

Neno la Mungu kwa Watoto Wake

Maandiko yanatueleza kwamba kitu cha kwanza Mungu alichofanya baada ya kumuumba mwanaume na mwanamke ilikuwa ni kuzungumza nao.1 Alikuwa na taarifa muhimu na maelekezo ya thamani kubwa ya kuwapa. Lengo lake halikuwa kuwatwika mzigo au kuwasumbua bali kuwaongoza kuelekea kwenye furaha na utukufu wa milele.

Na huo ulikuwa mwanzo tu. Kutoka siku hiyo hadi leo, Mungu ameendelea kuwasiliana na watoto Wake. Maneno Yake yamekuwa yakihifadhiwa, kuthaminiwa, na kusomwa na wafuasi wa kila kizazi. Yanaheshimiwa na wale ambao hutafuta kujua mapenzi ya Mungu, na wanatoa ushahidi juu ya ukweli kwamba “Bwana Mungu hatafanya neno lolote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.”2

Huu umekuwa ndiyo utaratibu tangu mwanzo wa nyakati, na utaratibu unaoendelea leo. Sio tu hadithi nzuri ya Biblia; ni njia iliyoanzishwa na Mungu ya kuwasilisha ujumbe muhimu kwa watoto Wake. Yeye huinua watu kutoka katikati yetu, huwaita kuwa manabii, na huwapa maneno ya kusema, ambayo tunaalikwa “kuyapokea, kama vile kutoka kwenye kinywa [Chake] mwenyewe.”3 Ametangaza, Iwe kwa sauti yangu mwenyewe au kwa sauti ya watumishi wangu, yote ni sawa.4

Huu ni mojawapo ya ujumbe wa kupendeza, wenye kutia moyo, na wenye matumaini ya Urejesho—Mungu hajanyamaza! Yeye anawapenda watoto Wake. Yeye hakutuacha sisi tutangetange gizani.

Mara mbili kila mwaka, Aprili na Oktoba, tunapata nafasi ya kusikia sauti ya Bwana kupitia watumishi Wake katika mikutano yetu mikuu ya kupendeza.

Ninakupeni ushahidi wangu binafsi kwamba muda mrefu kabla mzungumzaji katika mkutano mkuu hajaanza kutembea umbali mrefu kuelekea kwenye mimbari, anakuwa tayari amewekeza nguvu nyingi, sala, na kujifunza kama mwitikio wa uteuzi wa kuzungumza. Kila ujumbe wa mkutano huwakilisha masaa yasiyo na idadi ya maandalizi na ya kusihi kwa dhati ya moyo ili kuelewa kile ambacho Bwana hutamani Watakatifu Wake wasikie.

Nini chawezatokea kama sisi wasikilizaji tungelinganisha maandalizi ya mzungumzaji na ya kwetu wenyewe? Je ni kwa namna gani mtazamo wetu juu ya mkutano mkuu ungekuwa tofauti kama tungeliuona mkutano kama fursa ya kupokea ujumbe kutoka kwa Bwana Mwenyewe? Kupitia maneno na muziki wa mkutano mkuu, tunaweza kutegemea kupokea majibu binafsi kwa maswali yo yote au matatizo tunayoweza kuwa tunapitia.

Kama umewahi kujiuliza kama Baba wa Mbinguni kweli ataongea nawe, nitakukumbusha juu ya maneno rahisi lakini yenye maana sana ambayo watoto wetu wa madarasa ya Msingi huimba: “[Wewe ni] mwana wa Mungu, na amekuleta [wewe] hapa.” Lengo lake ni kukusaidia “kurudi kuishi pamoja naye siku moja.”

Endapo utamsogelea Baba wa Mbinguni kama mtoto Wake, unaweza kumuomba kwa moyo wa dhati, “Niongoze, kaa nami, unifundishe, unionyeshe njia. Nifundishe yale yote ninayopaswa kufanya.” Ataongea nawe kupitia Roho Wake Mtakatifu, na kisha ni juu yako “kufanya mapenzi yake.” Ninaahidi kwamba kama utafanya hivi, baraka nyingi zinakusubiri.”5

Muongozo wa Bwana unahitajika leo kama vile ambavyo imekuwa katika historia ya ulimwengu. Tunapojiandaa kusikia neno la Bwana, na kwa bidii tumtafute Roho wa kweli ili kwamba Bwana anapozungumza kupitia watumishi Wake, tuweze kuelewa, kujengwa, na kufurahi pamoja.6

Ninashuhudia kwamba “kwa kufanya mambo haya milango ya jahanamu haita[tushinda]; ndiyo, na Bwana Mungu atazitawanya nguvu za giza kutoka mbele [yetu], naye atasababisha mbingu zitetemeke kwa ajili [yetu], na kwa ajili ya utukufu wa jina lake.”7