Kanuni za Kuhudumu, June 2018
Vitu Vitano Wasikilizaji Wazuri Hufanya
Kusikiliza kwa ukweli kutakusaidia kujua jinsi ya kutatua mahitaji ya kiroho na kimwili ya wengine kama ambavyo Mwokozi angefanya.
Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisema: “Pengine kilicho muhimu zaidi ya kusema ni kusikiliza. … Kama tukisikiliza kwa upendo, hatutakuwa na haja ya kushangaa nini cha kusema. Tutapewa—na Roho.”1
Kusikiliza ni ujuzi tunaweza kujifunza. Kusikiliza kunaonesha upendo wetu kwa wengine, husaidia kujenga mahusiano, na kunamwalika Roho kutubariki na karama ya utambuzi ili kutusaidia kuyaelewa mahitaji ya wengine.2 Hapa kuna njia tano tunazoweza kuboresha jinsi ya kusikiliza.
1. Wape Muda
Watu wengi wanahitaji muda kukusanya mawazo yao kabla ya kusema. Wape muda wa kufikiri vyote kabla na baada ya kusema kitu fulani (ona Yakobo 1:19). Sio tu kwa sababu wamemaliza kusema inamaanisha wamesema kila kitu walichotaka. Usiogope ukimya (ona Ayubu 2:11–3:1 na Alma 18:14–16).
2. Zingatia
Tunafikiri haraka kuliko wengine wanavyosema. Jizuie ushawishi wa kufikia uamuzi bila kutafakari au kufikiri kabla ya kile utakachosema wakati watakapomaliza (ona Mithali 18:13). Badala yake, sikiliza kwa makini ili uelewe. Jibu lako litakuwa zuri zaidi kwa sababu litakuwa limejulishwa na uelewa mkubwa mno.
3. Eleza kwa uwazi
Usiogope kuuliza maswali ambayo yataeleza kwa uwazi kitu ambacho hukukielewa (ona Marko 9:32). Kueleza kwa uwazi kunapunguza kutoelewana na kunaonesha shauku yako katika kile kinachosemwa.
4. Tafakari
Fafanua kile ulichosikia na jinsi unavyoelewa wengine wanavyohisi. Wasaidie kujua kama wameeleweka na wape nafasi ya kujieleza kwa uwazi.
5. Tafuta Hoja Inayokubaliwa na Wote
Unaweza usikubali kila kitu kilichosemwa, lakini ukakubali kile unachoweza bila kutafsiri vibaya hisia zako mwenyewe. Kuwa marithia kunaweza kusaidia kutuliza wasiwasi na kujilinda (ona Mathayo 5:26).
Rais Russell M. Nelson alifundisha kwamba hatuna budi “kujifunza kusikiliza, na kusikiliza ili kujifunza kutoka kwa wengine.”3 Unaposikiliza kwa dhamira ya kujifunza kuhusu wengine, utakuwa katika nafasi mzuri mno kuelewa mahitaji yao na kusikia vishawishi kuhusu jinsi unavyoweza kuwalinda hao wanaokuzunguka kama vile Mwokozi angefanya.
Kusikiliza Ni Kupenda
Hadithi kutoka kwa Mzee Holland inaonesha nguvu ya kusikiliza:
“Rafiki yangu Troy Russell alilitoa polepole gari lake la pickup kutoka kwenye gereji yake. … Alihisi tairi lake la nyuma likizunguka kwenye tuta. Alitoka nje na kugundua kwamba mtoto wake mpendwa wa kiume wa umri–wa miaka–tisa, Austen, amelala kifudifudi kwenye barabarani. … Austen alikuwa amefariki.
“Kutoweza kulala, kutoweza kupata amani, Troy alikuwa asiyefarijika. … Lakini katika ufa ule wa mateso alikuja … John Manning. …
“Kwa hakika mimi sijui katika ratiba ipi John na mwenza wake mdogo walitembelea nyumba ya Russell, … Kile ninachokijua ni kwamba majira ya kuchipua yaliyopita Kaka Manning alikuja na kumnyakua Troy Russell kutoka kwenye janga lile la barabarani kama vile alikuwa akimnyakua mtoto Austin mwenyewe. Kama vile … kaka katika injili alitakiwa awe, John kikawaida alichukuwa ulinzi wa kikuhani na ulinzi wa Troy Russell. Alianza kwa kusema, ‘Troy, Austin anakutaka wewe usimame kwa miguu yako—pamoja na kuwa kwenye uwanja wa mpira wa kikapu—kwa hiyo nitakuwa hapa kila asubuhi saa 11:15. Uwe tayari. …’
“Sikupenda kwenda,’ Troy alinieleza baadaye, ‘ kwa sababu daima nimekuwa nikimchukua Austin pamoja nami. … Lakini John alisisitiza, basi nikaenda. Kutoka siku ile ya kwanza wakati huo, tuliongea—au pengine mimi niliongea na John alisikiliza. Mwanzoni ilikuwa vigumu, lakini kadiri nilivyoendelea nilijiona nimepata nguvu zangu katika umbo la [John Manning], aliyenipenda na kunisikiliza hadi jua hatimaye likachomoza tena juu ya maisha yangu.’”4
© 2018 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/17. Idhini ya kutafsiri: 6/17. Tafsiri ya Ministering Principles, June 2018. Swahili. 15055 743