Kanuni za Kuhudumu, Desemba 2018
Wasiliana kwamba Unajali
Kuna njia nyingi tunazoweza kuonyesha kuwa tunajali, hasa wakati wa Krismasi. Tunaweza kusema, kutuma ujumbe mfupi wa simu, kutoa, kushiriki, kuomba, kuoka, kuimba, kukumbatia, kucheza, kupanda, au kusafisha. Kwa urahisi ujaribu.
Kuonyesha upendo kwa wengine ni kiini halisi cha kuhudumu. Rais Mkuu wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama alisema: “Kuhudumu kwa kweli kunatimizwa hatua kwa hatua na upendo ukiwa kama motisha. … Upendo ukiwa kama motisha, miujiza itatokea, na tutapata njia za kuwaleta dada zetu na kaka zetu ‘waliopotea’ kwenye mjumuisho-wa pamoja wa injili ya Yesu Kristo.”1
Kuwajulisha wengine kuwa tunajali ni kipengele muhimu katika kuunda mahusiano ya kibinafsi. Lakini watu tofauti hupata ujumbe kwa njia tofauti. Hivyo, tunawezaje kuonyesha ipasavyo upendo wetu kwa wengine kwa njia ambazo wataelewa na kufurahia? Hapa kuna baadhi ya njia za kuonyesha kuwa tunajali, pamoja na mawazo machache kukuanzishia fikira zako mwenyewe.
Sema
Wakati mwingine hakuna mbadala wa kusema jinsi unavyohisi juu ya mtu fulani. Wakati hii inaweza kumaanisha kumwambia mtu kuwa unampenda, pia inajumuisha kushiriki kile kinachokuvutia kwake au kutoa maneno ya dhati ya sifa. Aina hii ya uthibitisho husaidia kuimarisha mahusiano. (Ona Waefeso 4:29.)
-
Tafuta fursa ya kumfanya mtu kujua jinsi unavyovutiwa na mojawapo ya uwezo wake.
-
Tembelea, piga simu, au tuma barua pepe, ujumbe mfupi au kadi ukimwambia mtu kwamba unamfikiria.
Tembelea
Kuchukua nafasi kuzungumza na kumsikiliza mtu ni njia yenye nguvu ya kumwonyesha jinsi unavyomthamini. Iwapo utatembelea nyumbani, kanisani au mahali pengine popote, kuna watu wengi wanaohitaji mtu wa kuzungumza nae. (Ona Mosia 4:26; M&M 20:47.)
-
Kulingana na mahitaji ya mtu binafsi, panga matembezi. Chukua muda kusikiliza kwa dhati na kuelewa hali zake.
-
Ikiwa itakuwa vigumu kutembelea majumbani kwa sababu ya umbali, kawaida za kitamaduni au hali zingine, fikiria kupata muda wa pamoja baada ya mikutano ya Kanisa.
Hudumu kwa Kusudi
Uwe mwenye kujali kuhusu mahitaji ya mtu binafsi au familia. Kutoa huduma yenye maana huonyesha kuwa unajali. Inajumuisha zawadi za thamani za wakati na juhudi za kujali. “Matendo rahisi ya huduma yanaweza kuwa na matokeo makubwa kwa wengine,” alisema Dada Bingham.2
-
Toa huduma inayowaimarisha watu binafsi au familia zao, kama vile kuwaangalia watoto ili wazazi waweze kwenda hekaluni.
-
Tafuta njia za kurahisisha mizigo wakati maisha yanapokuwa magumu, kama vile kusafisha madirisha, kumtembeza mbwa au kusaidia kwenye ua.
Fanyeni Mambo Pamoja
Kuna watu wasioweza kuhusiana kupitia mazungumzo ya kina. Kwa baadhi ya watu, mahusiano yanatengenezwa kwa kutafuta mambo yanayowavutia nyote na kutumia wakati kufanya shughuli hizo pamoja. Bwana amehimiza kuwa “tuwe nao na kuwaimarisha” (M&M 20:53) akina kaka na dada zetu.
-
Nenda kwenye matembezi, panga usiku wa michezo au panga wakati maalum wa kufanya mazoezi pamoja.
-
Toeni huduma pamoja katika mradi wa jamii au wa Kanisa.
Toa Zawadi
Wakati mwingine muda au nafasi za mwingiliano ni chache. Katika tamaduni nyingi, kupeana zawadi ni ishara ya kujali na huruma. Hata zawadi ndogo, ya mara moja inaweza kuonyesha hamu yako ya kujenga uhusiano bora. (Ona Mithali 21:14.)
-
Wapelekee kitoweo wanachokipenda.
-
Shiriki nukuu, andiko, au ujumbe mwingine unaohisi kuwa watafaidika kutokana nao.
Kazi ya Upendo
Unapokuja kuwafahamu wale unaowahudumia na unapotafuta mwongozo wa kiungu juu yao, utajifunza kwa njia maalum zaidi jinsi ya kuonyesha upendo wako na kuwajali wao kibinafsi.
Kimberly Seyboldt wa Oregon, Marekani, anasimulia hadithi ya kutafuta mwongozo wa kiungu na kutoa zawadi ili kuonyesha upendo:
“Ninapokuta kuwa maisha yananisukuma chini, ninaamka na kutengeneza mkate wa Zucchini, kawaida karibu mikate minane. Kiungo changu maalum ni sala ya kimya ninayotoa ninapooka ili nijue anayehitaji mikate hiyo. Nimeweza kuwajua vyema zaidi majirani zangu wa karibu kwani mkate wa zucchini umekuwa mwaliko wangu kwenye nyumba zao na maisha yao.
“Siku moja wakati wa majira ya joto, nilisimama karibu na familia iliyokua ikiuza forosadi kando ya barabara. Sikuhitaji forosadi zaidi, lakini kijana mdogo, mwembamba kwenye kibanda alifurahia kuniona, akifikiri nilikuwa mteja wake aliyefuata. Nilinunua baadhi ya forosadi, lakini pia nilikuwa na zawadi kwa ajili yake. Nilimpa yule kijana mikate miwili. Alimgeukia baba yake kwa ajili ya idhini, kisha akasema, ‘Tazama, Baba, sasa tuna kitu cha kula leo.’ Nilijawa na shukrani kwa nafasi hii ya kuonyesha upendo kwa njia rahisi.”
Mzee Jeffrey R. Holland wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alisihi “kwamba kila mwanaume na mwanamke—na wavulana wetu wakubwa na wasichana—[watakuwa] … wenye msimamo wa kina zaidi kwa dhati kulindana wao wenyewe, wakihamasishwa tu na upendo msafi wa Kristo kufanya hivyo. … Sote na tufanye kazi bega kwa bega pamoja na Bwana shamba la mizabibu, tukimpa Mungu na Baba yetu sote mkono wa usaidizi katika hii kazi Yake kuu sana ya kujibu maombi, kuleta faraja, kufuta machozi, na kuimarisha magoti yaliyolegea.3
Yesu Kristo Anajali
Baada ya Yesu kumfufua Lazaro kutoka kwa wafu, “Yesu alilia.
“Kisha walisema Wayahudi, Tazama alivyompenda!” (Yohana 11:35 –36).
“Nina huruma juu yenu,” Kristo Aliwaambia Wanefi. Kisha akawaita wagonjwa wao na waliosumbuka, na vilema wao na vipofu wao, na “akawaponya” (ona 3 Nefi 17:7–9).
Mwokozi alionyesha mfano kwetu pale Yeye alipowajali wengine. Yeye alitufundisha:
“Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.
“Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.
“Na ya pili yafanana nayo, Mpende jirani yako kama nafsi yako” (Mathayo 22:37–39).
Nani anahitaji kujali kwako? Unawezaje kuwaonyesha kwamba unajali?
© 2018 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa huko Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/17. Idhini ya kutafsiri: 6/17. Tafsiri ya Ministering Principles, December 2018. Swahili. 15056 743