2021
Je, uko Tayari Kutimiza Misheni ambayo Mungu Ameiweka kwa ajili Yako?
Juni 2021


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

Je, uko Tayari Kutimiza Misheni ambayo Mungu Ameiweka kwa ajili Yako?

Ili kutimiza vyema misheni ambayo Mungu anatuita kuitimiza, tunahitaji kuweka kujitegemea kiroho na kimwili kuwa kipaumbele.

Ikiwa Bwana Yesu Kristo angekuomba leo umsaidie Yeye katika njia mahususi, je ungefanya hivyo? Je kuna kitu chochote kiroho au kimwili kinachokuzuia kujibu ombi kutoka Kwake?

Mariamu, mama wa Yesu, aliambiwa na Malaika Gabrieli: “umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yesu. . . . Hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.”1

Wakati Mariamu aliposikia wito kutoka kwa mmoja wa wajumbe wa Mungu, alijibu, “. . . na iwe kwangu kama ulivyosema.”2 Alisikia wito wa Mungu na akaitikia kwa imani.

Yusufu wa Misri, mwana wa Israeli, aliteswa na kaka zake, akauzwa kwa watumwa, akatuhumiwa kwa uongo na kufungwa gerezani, na alibaki gerezani kwa miaka kumi na minne. Hata hivyo, pamoja na yote alibaki mkweli kwenye maagano yake na akawa kifaa chenye nguvu katika mikono ya Mungu kuilinda familia yake na watu wa Misri.

Ni kwa jinsi gani mifano hii halisi ya maisha inahusika kwako? Dhamira moja ya jumla ni kwamba wote Mariamu, mama wa Yesu na Yusufu wa Misri walibaki wakweli kwenye maagano yao na walijiandaa kiroho kuitikia mwaliko wa Mungu wa kutimiza misheni ambayo Yeye aliwatuma kutimiza. Je, tunatunza maagano yetu ili nasi kadhalika tuwe tumejiandaa kiroho?

Rais Russell M. Nelson alieleza:

“Bwana Yesu Kristo anaongoza mambo ya Kanisa Lake, na litafikia malengo yake matakatifu. Changamoto kwako na kwangu ni kuhakikisha kwamba kila mmoja wetu atafikia uwezekano wake mtakatifu.”3

Ili kujiandaa kutimiza misheni ambayo Mungu ametutuma kuitimiza, tunahitaji kuwa wenye kujitegemea kiroho.

Kujitegemea ni uwezo, msimamo na juhudi ya kukimu mahitaji muhimu ya kiroho na ya kimwili ya maisha kwa ajili ya mtu mwenyewe na familia. Pale waumini wanapokuwa wenye kujitegemea, wanakuwa pia wenye kuwatumikia vyema na kuwajali wengine.”4 Kazi inapewa utukufu kama kanuni ongozi katika maisha yao.

Tutakuwa kwenye hata nafasi nzuri zaidi ya kuwa vyombo madhubuti katika mikono ya Mungu ikiwa sisi ni wenye kujitegemea kimwili na kifedha vilevile.

Kuuza ndizi

Mfano wa mtu aliyechukua jukumu binafsi la kuwa mwenye kujitegemea ni Cedrick Tshiambwe. Cedrick alijiunga na Kanisa huko Luputa, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, alipokuwa na umri wa miaka 12 baada ya kusoma na kuomba kuhusu Kitabu cha Mormoni. Alitaka kuhudumu misheni, hivyo alitengeneza mpango wa kuweka akiba ya pesa ili kukidhi baadhi ya gharama za misheni yake. Ili kupata pesa, alinunua ndizi kutoka miji ya jirani ili kuzipeleka Luputa kwa ajili ya kuuza. Akitumia baiskeli yake, aligundua kuwa angeweza kusafirisha takriban mikungu sita kwa mara moja. Kutegemea na siku, aliendesha kadiri alivyoweza kufika mji wa jirani wa Lusuku, umbali wa kilomita 29, ili kununua ndizi. Ilimchukua Cedrick miaka minne, lakini aliweka akiba ya pesa za kutosha kulipia pasi yake ya kusafiria, kununua nguo na maandiko na kuweza kuchangia misheni yake katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo Misheni ya Kinshasa.5

Mzee Joseph Sitati, Rais wa Eneo la Afrika ya Kati, anawahimiza waumini wa Kanisa kujiandaa kimwili na kiroho kwa kiwango wanachoweza kufikia. Kwa ufupi, Bwana hatarajii sisi tuwe na akiba ya kimwili iliyo juu ya uwezo wetu, lakini Yeye anatarajia sisi tufanye kadiri tuwezavyo.

Je, wewe ni mwenye kujitegemea kiroho na kimwili sasa? Ikiwa Mungu angekuomba kutimiza misheni ambayo Yeye anayo kwa ajili yako, je, uko tayari? Hakika, Yeye anakuita sasa ili kujiandaa kwa Ujio wa Pili wa Yesu Kristo na kukusanya Israeli iliyotawanyika. Ili kutimiza vyema misheni ambayo Mungu anatuita kuitimiza, tunahitaji kufanyia kazi suala la kuwa wenye kujitegemea kiroho na kimwili sasa.

Rais Marion G. Romney alieleza, “Tunawezaje kutoa ikiwa hakuna chochote hapo? Chakula kwa ajili ya mwenye njaa hakiwezi kutoka kwenye rafu zilizo tupu. Pesa kwa ajili ya kumsaidia mhitaji haziwezi kutoka kwenye pochi iliyo tupu.”6

Wapi pa kuelekea kutokea hapa?

Hivyo, ikiwa sisi bado si wenye kujitegemea, au tunamtunza mtu ambaye si mwenye kujitegemea, je tunafanyaje?

Mzee Dieter F. Uchtdorf alifundisha yafuatayo:

“Hakuna jibu moja linalotosheleza majibu yote katika ustawi wa Kanisa. Ni programu ya msaada binafsi ambapo watu wanawajibika kuwa wenye kujitegemea wao wenyewe. Rasilimali zetu zinajumuisha sala binafsi, uwezo na talanta zetu wenyewe tulizopewa na Mungu, rasilimali zinazopatikana kwetu kupitia familia zetu wenyewe na ndugu na jamaa wengine wa familia, rasilimali mbalimbali za jamii na hakika msaada wa uangalizi wa akidi za ukuhani na Muungano wa usaidizi. Hii itatuongoza kupitia mpangilio wenye uvuvio wa kujitegemea.”7

Kuna watu wengi wema na mashirika ulimwenguni ambayo yanajaribu kukidhi shinikizo la mahitaji ya maskini na wenye uhitaji. Tunashukuru kwa hili, lakini njia ya Bwana ya kuwatunza wenye uhitaji ni tofauti na njia ya ulimwengu. Bwana amesema, “Lakini haina budi kufanyika katika njia yangu mwenyewe.”8 Yeye havutiwi tu na mahitaji yetu ya sasa; bali pia Ana shauku kuhusu maendeleo yetu ya milele. Kwa sababu hii, njia ya Bwana inajumuisha amri za kuwa wenye kujitegemea na kuwahudumia jirani zetu katika kuongezea kwenye kuwajali maskini.

Tunaweza kujaribiwa kuwategemea wengine watuondoe katika hali ngumu tulizonazo. Wakati tunaweza kuwaomba wengine watuongoze, lazima sisi tufanye sehemu yetu ili kubadili njia yetu. Rais Russell M. Nelson ameeleza, “Bwana anapenda juhudi.”9 Mungu ametuleta kwenye dunia hii ili kujaribiwa na kuthibitisha ili kuona kama “tutafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru.”10 Wakati tunaweza kwa hakika kunufaika kutokana na utaalamu na uzoefu wa wengine, tunakua na kujifunza zaidi pale tunapokamilisha kazi kupitia juhudi zetu wenyewe.

Hii haina maana kwamba hatupaswi kumshirikisha Mungu katika safari yetu ya kujitegemea. Mungu ndiye mtoaji wa vipawa vyote vizuri, na Yeye anapenda na anatamani kuwabariki watoto wake wote. Lakini Yeye anatarajia kwamba tufanye sehemu yetu. Na tufanye maandalizi yetu ya kimwili na kiroho kuwa kipaumbele.

Ninatoa ushahidi kwamba tunapofanya sehemu yetu kuwa wenye kujitegemea kimwili na kiroho, ikiwa tutaomba kwa imani, Mungu ataleta utofauti kwa nguvu zake zisizolinganishwa. Katika jina la Yesu Kristo, Amina.

Matthew L. Carpenter aliitwa kama Sabini mwenye Mamlaka mnamo Machi 2018. Amemuoa Michelle (Shelly) Kay Brown; wao ni wazazi wa watoto watano.

Muhtasari

  1. Luka 1:30–31, 35.

  2. Luka 1:38.

  3. Russell M. Nelson, “Utamaduni Mpya,” Liahona, Nov. 2020, 118.

  4. Manuel 2 : Administration de l’Église [2010], 6.1.1. ; General Handbook: Serving in The Church of Jesus Christ of Latter-day Saints, 22.0, ChurchofJesusChrist.org

  5. Tazama Church News, Machi 16, 2016.

  6. Marion G. Romney, “The Celestial Nature of Self-reliance,” Ensign, Nov. 1982.

  7. Dieter F. Uchtdorf, “Pourvoir aux besoins à la façon du Seigneur,” Liahona, Nov. 2011, 55.

  8. Tazama Mafundisho na Maagano 104:16.

  9. Joy D. Jones, “Wito Mahususi wenya Uadilifu,” Liahona, Mei 2020, 16.

  10. Ibrahimu 3:25.