2021
Kutana na akina dada ambao punde tu wameitwa kama Washauri wa Taasisi wa Eneo
Agosti 2021


SAUTI ZA ENEO

Kutana na akina dada ambao punde tu wameitwa kama Washauri wa Taasisi wa Eneo

“Nafasi hii mpya katika Kanisa inawaruhusu akina dada kushauriana na viongozi wa ukuhani na kutoa mafunzo kwa taasisi zinazoongozwa na akina dada katika vigingi, wilaya, kata na matawi.”

Wanawake saba katika Eneo la Kati mwa Afrika hivi karibuni waliitwa kama Washauri wa Taasisi wa Eneo. Ikiwa unadhani hujawahi kusikia juu ya wito huu hapo kabla, ni kwa sababu hujawahi kusikia!

Ni nafasi mpya ambayo imeongezwa kwenye mfumo wa taasisi wa Kanisa. Inawataka wanawake hawa kushiriki katika mabaraza ya uongozi na kushauri, kutoa mafunzo na kuzisaidia taasisi zinazoongozwa na akina dada katika maeneo yote.

Soma zaidi ili kujifunza kuhusu akina dada saba ambao wameitwa kujaza jukumu jipya kabisa katika eneo.

Dada Njampou Claudelia Nankap alizaliwa Brazzaville, Jamhuri ya Kongo. Alijiunga na Kanisa katika umri wa miaka kumi na alihudumu misheni eneo la jirani la Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. Sasa akiwa na miaka 33, Dada Nankap alikuwa akihudumu kama Rais wa Muungano wa Usaidizi katika kata yake kabla ya wito huu.

Dada Nankap anasema kwamba lengo lake binafsi katika wito wake mpya ni “kumtumikia Bwana kupitia matendo yangu kwa wengine; kuwa rafiki yao na mshauri mwaminifu,” anasema. “Ninaichukulia kama fursa ya kuwa bora na kuwa mfuasi wa kweli wa Kristo pale ninapojiingiza katika kazi hii kuu. Ninahisi kunyenyekezwa zaidi kuliko hapo awali!”

Anapohudumu, Dada Nankap anapata msukumo kwa mfano wa watangulizi wake, hususani baba yake. “Alikuwa mfano wa kweli wa unyenyekevu, kujitolea na uvumilivu: kanuni ambazo ninajua zitanisaidia katika wito wangu,” anasema.

Katika jukumu lake jipya, “ninatazamia kukutana na watoto wengine wa Baba wa Mbinguni ambao yawezekana wanapitia magumu sawa na yangu,” anasema. “Ninatazamia kuona baraka katika maisha yangu na maisha ya wengine: kwa sababu inapendeza sana kuona kile ambacho injili inaweza kuleta kwenye maisha ya mtu. Na pia ninatazamia kufanya kazi na Viongozi Wakuu wenye Mamlaka wa Kanisa. Ni heshima kubwa inayonifanya nihisi kuwa mdogo sana!”

Dada Kabongo Angelique Tarr alizaliwa huko Mwene-Ditu, Kasai-Oriental, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. Ana miaka 58 na alibatizwa zaidi ya miaka thelathini iliyopita akiwa na umri wa miaka 25. Yeye na mume wake ni wazazi wa watoto watano na bibi na babu wa mjukuu mmoja. Kabla ya wito huu, alikuwa akihudumu kama Mshauri wa Muungano wa Usaidizi kwa Vijana wa Kike Waseja katika kata yake.

“Lengo langu katika wito wangu mpya ni—kupitia mfano wangu—kuvisaidia vikundi saidizi vya Muungano wa Usaidizi, Wasichana na Msingi kujenga upendo kwa watu tunaowaongoza na kuwahudumia ili tuwalete kwa Kristo,” anasema.

Mafundisho ya Viongozi Wakuu wenye Mamlaka na ibada za hekaluni, ambapo yeye na familia yake wameunganishwa, vinampa msukumo wa kuendelea kuwa mtu bora zaidi.

Anapohudumu, Dada Tarr anasema anatazamia si tu kuleta upendo kwa watu anaowahudumia, bali pia kuwasaidia akina dada katika Eneo kukua kama mabinti wa Baba yetu wa Mbinguni katika kujitegemea kwao kiroho na kimwili.

Dada Dephine Marie Beatrice Mawang-Luko Muzama alizaliwa Kikwit, Bandundu, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Ana miaka 60 na yeye na mume wake ni wazazi wa watoto wanne. Alibatizwa miaka 22 iliyopita. Kabla ya wito huu, alikuwa akihudumu kama mwalimu wa seminari katika kigingi chake.

Lengo lake katika wito wake mpya ni kumwalika kila mmoja kuja kwa Kristo kwa kuusaidia urais wa eneo katika kutambua malengo yao, kwa kutoa maelekezo, kusimamia taasisi za wanawake za vigingi na wilaya na kwa kuhudumu kama nyenzo kwa taasisi zinazoongozwa na akina dada katika misheni.

Anasema kwamba ushuhuda wake binafsi wa Urejesho wa Injili ya Yesu unampa msukumo wa kuhudumu na kutenda mema, sambamba na usomaji wa kila siku kutoka kwenye Kitabu cha Mormoni na jumbe kutoka kwa Mitume na viongozi wa Kanisa.

Dada Muzama anasema anatazamia kukutana na akina dada katika urais wa vigingi na wilaya katika eneo lake. “Shamba li jeupe tayari kwa mavuno,” anasema (M&M 33:3). “Lazima tuingize mundu zetu kwa nguvu zetu zote.”

Dada Yeweinshet Bezu Biru alizaliwa Aromia Zone Arsi, Ethiopia. Ana miaka 55 na yeye na mume wake ni wazazi wa watoto wawili. Alibatizwa miaka 11 iliyopita. Kabla ya wito huu, Dada Biru alikuwa akihudumu kama Rais wa Muungano wa Usaidizi wa Wilaya katika Wilaya ya Addis Ababa Ethiopia.

Dada Biru ni kipofu na anaendesha taasisi isiyo na faida ambayo huwasaidia vipofu kujifunza jinsi ya kusoma.

Kama mshauri wa taasisi wa eneo “lengo langu ni kujenga ufalme wa Mungu duniani kwa kuwa mwaminifu na mtiifu zaidi,” anasema.

Anapofanya hili, anaendelea kupewa msukumo na mambo yaleyale yaliyompa msukumo kama muongofu mpya Kanisani. “Nilipojiunga, waumini pamoja na wamisionari walinipa msukumo wa kusoma maandiko, kuomba na kusikiliza jumbe za Manabii na Mitume, ambazo hunifanya niwe bora kila siku.”

Dada Biru anatazamia kuwasaidia akina dada katika Kanisa kuongeza uelewa wao wa injili iliyorejeshwa na kuwasaidia kuimarisha shuhuda zao. “Zaidi, ninataka kuona mahekalu zaidi katika eneo ninalohudumu,” anasema.

Dada Vulfrida Chanya Simiyu alizaliwa Taita Taveta, Kenya. Ana miaka 54 na yeye na mume wake ni wazazi wa watoto watatu. Alibatizwa Kanisani miaka nane iliyopita. Kabla ya kupokea wito huu, alikuwa Rais wa Wasichana wa Kigingi katika Kigingi cha Nairobi Kenya West.

Dada Simiyu anasema kwamba misheni yake binafsi kama mshauri wa taasisi wa eneo ni kushauri na kutoa mafunzo kwa viongozi “kuimarisha imani na ushuhuda wao na kukuza miito yao kupitia kuhudumu na kutumikia. Zaidi anatumaini “kuwasaidia kuhisi upendo wa Mwokozi na kushiriki upendo huo kwa wengine.”

Dada Simiyu anasema kwamba anasukumwa na ushuhuda wa Rais Russell M. Nelson. “Upendo wake kwa mwokozi na injili iliyorejeshwa” husaidia kumpa motisha ya kuendelea kuwahudumia wale walio karibu naye.

Dada Simiyu anasema kwamba anatazamia kuwapa ushauri akina dada wa “kuhudumu kwa nguvu na uimara katika wito wao, kuwaleta wengi kwa Kristo na kwenye injili iliyorejeshwa.” Anatazamia kuhudumu chini ya maelekezo ya urais wa eneo “kadiri wanavyonielekeza kwenye mahitaji ya viongozi wa taasisi wa kigingi” na “kutoa majibu yanayostahili kama nitakavyoongozwa na Roho.”

Dada Epiphanie Christel Mabiala alizaliwa Pointe Noire, Jamhuri ya Kongo. Ana miaka 50 na yeye na mume wake ni wazazi wa watoto watatu. Alibatizwa katika umri wa miaka 23 na alihudumu misheni katika Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. Kabla ya wito huu, alikuwa akihudumu kama Rais wa Muungano wa Usaidizi wa Kigingi cha Makelekele katika Kigingi cha Jamhuri ya Kongo.

Lengo lake binafsi katika jukumu lake jipya ni “kutambua vikwazo vinavyowazuia viongozi wa kigingi na wilaya kutimiza miito yao.” Anatamani “kuwaleta mabinti wa Mungu kwa Kristo na kuwapa mafunzo ya kuwa viongozi ambao watawasaidia waumini kubaki kwenye njia ya agano.”

Dada Mabiala anasema anasukumwa na hamu ya “kutunza maagano aliyofanya na Bwana na kuwafunza viongozi akina dada katika njia ya Mwokozi.”

Anatazamia kuwaunga mkono na kuwaidhinisha urais wa eneo. Anatumaini kwa usahihi kutimiza wito wake kwa kutathmini na kuchunguza mitindo katika jamii na sababu zinazopelekea mitindo hiyo na kisha kutafuta mada husika za mafunzo ambazo huangazia mipangilio hii ya kijamii.

Dada Stella Marys Ajilong alizaliwa Soroti, Uganda. Sasa akiwa na miaka 57, alijiunga na Kanisa takriban miongo mitatu iliyopita akiwa na umri wa miaka 31. Kabla ya wito huu, Dada Ajilong alikuwa akihudumu kama Rais wa Msingi wa Kigingi wa Kampala Uganda North. Kabla ya hapo, alihudumu kama Rais wa Muungano wa Usaidizi wa Kigingi kwa takriban miaka 20. Yeye ni mzazi mmoja wa watoto wawili. Dada Ajilong alistaafu kazi kwenye kampuni ya bima baada ya miaka 34 ya utumishi. Kwa sasa anaongoza taasisi isiyo ya faida ambayo hutoa makazi ambapo akina mama na akina baba walezi huwakuza watoto yatima kama watoto wao wenyewe katika shamba na mazingira ya kifamilia; na kutoa elimu na ujuzi mwingine ili waweze kuwa watu wazima wa baadaye wenye kujitegemea.

“Kwa mtazamo wangu, lengo langu kama Mshauri wa Taasisi wa Eneo ni kuwasaidia viongozi wa taasisi kujifunza majukumu yao ili kwamba kupitia mfano wao, mafundisho na huduma, akina dada, Wasichana na watoto wa Msingi waweze kuwa na hamu ya kusonga karibu na Baba wa Mbinguni,” anasema Dada Ajilong.

Anapoendelea kuhudumu kama mama, katika wito wake na katika kazi yake ya hisani, anahisi “tamanio la baraka za Upatanisho katika maisha haya na katika maisha yajayo,” anasema. “Hicho ndicho kinachonipa mimi msukumo wa kufanya vizuri zaidi.”

Dada Ajilong anapohudumu katika jukumu lake jipya, anatazamia “mwongozo kutoka kwa Baba wa Mbinguni kupitia ufunuo na misukumo, kuwasaidia wengine kwamba kupitia huduma yetu tuweze kuona ukuaji Kanisani kwa namba na ushuhuda na pengine kuwa mtu bora mimi mwenyewe.”