“Shangwe ya kudumu ya kuishi injili,” Liahona, Februari 2024.
Ujumbe wa kila mwezi wa Liahona, Februari 2024.
Shangwe ya Kudumu ya Kuishi Injili
Shangwe ya kudumu huja kwa kubakia katika injili ya Yesu Kristo na kuwasaidia wengine wafanye vivyo hivyo.
Maelezo mafupi ya malengo yetu ya kuishi yanaweza kuonekana katika mafundisho ya kinabii ya Lehi kuhusu mwanzo wa maisha ya mwanadamu duniani. Katika Bustani ya Edeni, Adamu na Hawa walikuwa katika hali ya kutokuwa na hatia. Ikiwa wangebakia katika hali hiyo, “[wasingekuwa] na shangwe, kwani hawakufahamu dhiki; bila kutenda mema, kwani hawakujua dhambi” (2 Nefi 2:23). Hivyo, kama Lehi alivyofafanua, “Adamu alianguka ili wanadamu wawe; na wanadamu wapo, ili wapate shangwe” (2 Nefi 2:25; ona pia Musa 5:10–11).
Kadiri tunavyokua katika ulimwengu ulioanguka, tunajifunza tofauti kati ya mazuri na mabaya kwa yale tunayofundishwa na yale tunayopitia. “Tunaonja uchungu, ili [tupate] kujua kuthamini chema” (Musa 6:55). Shangwe huja pale tunapokataa machungu na kuongeza kuthamini na kushikilia mazuri.
Kutafuta shangwe
Kwa sababu ya upendo Wake mkamilifu kwetu, Baba wa Mbinguni anatamani kutushirikisha katika shangwe yake, kote sasa na milele. Huo umekuwa ni uhamasishaji wake katika kila kitu kuanzia mwanzoni, ikiwa ni pamoja na mpango wake mtukufu wa furaha na dhabihu ya Mwanaye wa Pekee kutukomboa sisi.
Mungu hajaribu kulazimisha shangwe au furaha kwetu sisi, lakini anatufundisha jinsi gani ya kuipata. Anatuambia pia mahala ambapo shangwe haiwezi kupatikana—“uovu [siyo na] kamwe haujawahi kuwa furaha” (Alma 41:10). Ni kupitia amri zake kwamba Baba yetu wa Mbinguni hutufunulia njia ya kuelekea kwenye shangwe.
Rais Russell M. Nelson alielezea njia hii:
“Hapa kuna ukweli mkuu: wakati ulimwengu unasisitiza kwamba nguvu, mali, umaarufu na starehe za kimwili ndizo ziletazo furaha, hazileti! Haziwezi kuleta! Kile kinachozalishwa na vitu hivyo si chochote bali mbadala ulio tupu wa ‘hali ya baraka na yenye furaha ya [yule] anayetii amri za Mungu’ [Mosia 2:41].
“Ukweli ni kwamba ni ya kuchosha zaidi kutafuta furaha mahali ambapo huwezi kamwe kuipata! Hata hivyo, unapojifunga mwenyewe nira kwa Yesu Kristo na kufanya kazi ya kiroho inayohitajika kuushinda ulimwengu, Yeye na ni Yeye pekee, aliye na uweza wa kukuinua juu dhidi ya mvuto wa ulimwengu huu.”1
Hivyo, shangwe ya kudumu inapatikana katika kuzifuata amri za Mungu, na amri za Mungu zinapatikana katika injili ya Yesu Kristo. Lakini ni uchaguzi wetu. Kama katika udhaifu wetu tutashindwa kuzifuata amri, bado tunaweza kurudi nyuma, kukataa machungu na kwa mara nyingine tena kujaribu yaliyo mazuri. Upendo wa Mungu hauvumilii dhambi—hiyo itakuwa rehema ikiikatili haki—lakini kwa Upatanisho Wake, Yesu Kristo anatoa ukombozi kutoka dhambi:
“Amulek … alisema … kwamba kwa hakika Bwana atakuja kuwakomboa watu wake, lakini kwamba haji kuwakomboa katika dhambi zao, bali kuwakomboa kutoka katika dhambi zao.
“Na ana nguvu aliyopewa kutoka kwa Baba kuwakomboa kutoka kwenye dhambi zao kwa sababu ya toba; kwa hivyo amewatuma malaika wake kutangaza habari njema ya hali ya toba, ambayo inaleta uwezo wa Mkombozi, kuwezesha wokovu wa roho zao” (Helamani 5:10–11; msisitizo umeongezwa).
Yesu alisema:
“Kama mtazishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; hata kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
“Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe (Yohana 15:10–11).
Hiki ndicho Lehi alichokihisi katika ndoto yake pale alipolionja tunda la mti wa uzima—ambalo linawakilisha upendo wa Mungu. Alisema, “wakati nilipokula tunda lile lilijaza nafsi yangu na shangwe tele” (1 Nephi 8:12; ona pia11:21–23).
“Lehi pia alieleza njia ya pili ambayo tunaweza kuleta shangwe katika maisha yetu pale aliposema, “Hivyo, nikaanza kutaka jamii yangu na wao pia wale [tunda]” (1 Nefi 8:12).
Kuwasaidia Wengine Wapate Shangwe
Kama watu wa Mfalme Benjamini, “tunajawa na shangwe” pale tunapopokea ondoleo la dhambi zetu na kupata uzoefu wa amani ya nafsi” (Mosia 4:3).) . Tunaihisi tena wakati tunapoangalia nje na kutafuta kuwasaidia wanafamilia na wengine waipokee shangwe na amani ileile.
Kama kijana mdogo, Alma alitafuta furaha katika kila kitu kilichopingana na injili ya Yesu Kristo. Baada ya kukaripiwa na malaika, alitembea njia ndefu kutoka “uchungu” hadi “wema” kwa toba “inayokaribia kifo” (Mosia 27:28) na rehema tele ya Mwokozi. Miaka mingi baadaye, Alma kwa ari alitangaza kwa mwana wake Helamani:
“Na Ee, ni shangwe gani, na ni mwangaza gani wa ajabu niliouona; ndiyo, nafsi yangu ilijazwa na shangwe ya ajabu kama vile ulivyokuwa uchungu wangu! …
“Ndiyo, na tangu wakati huo hata hadi sasa, nimefanya kazi bila kukoma, kwamba nilete nafsi za watu kutubu; kwamba ningewaleta wapate kuonja shangwe kuu ambayo niliiona. …
“Ndiyo, na sasa tazama, Ee mwana wangu, Bwana hunipa shangwe kuu kwa matokeo ya kazi yangu;
“Kwani kwa sababu ya neno ambalo amenipatia, tazama, wengi wamezaliwa kwa Mungu, na wameonja vile nilivyoonja” (Alma 36:20, 24–26).
Katika hali nyingine, Alma alishuhudia:
“Huu ni utukufu wangu, kwamba labda niwe chombo kwenye mikono ya Mungu kuleta roho moja kwa toba; na hii ndiyo shangwe yangu.
“Na tazama, ninapoona wengi wa ndugu zangu wametubu kweli, na kumkubali Bwana Mungu wao, ndipo nafsi yangu hujaa na shangwe” (Alma 29:9–10).
Alma aliendelea kutangaza shangwe isiyo na kifani aliyokuwa akiihisi wakati wengine walipofanikiwa kuzileta nafsi kwa Kristo.
“Lakini mimi siwezi kuwa na shangwe kwa mafanikio yangu mwenyewe, lakini shangwe yangu imejaa zaidi kwa sababu ya kufanikiwa kwa ndugu zangu [watoto wa Mosia], ambao wamekuwa kwenye nchi ya Nefi.
“Tazama, wamefanya kazi sana, na wameleta matunda mengi; na zawadi yao itakuwa kubwa kiasi gani!
“Sasa, ninapofikiria mafanikio ya hawa ndugu zangu roho yangu inabebwa, hata kama imetenganishwa kutoka kwa mwili, vile ilivyokuwa, kwani shangwe yangu ni kubwa sana” (Alma 29:14–16).
Tunaweza kuipata shangwe ile ile kadiri tunavyowapenda wengine kwa “upendo msafi wa Kristo” (Moroni 7:47; ona pia mstari wa 48), shiriki nao ukweli uliorejeshwa, na waalike wakusanyike na watu wa agano.
Shangwe Katikati ya Mateso
Tusiogope kwamba majaribu na changamoto ambazo hatuna budi kukumbana nazo katika maisha ya kimwili yatazuia au kuharibu shangwe yetu. Alma alikuwa mmoja wa wale ambao huduma yake isiyo na ubinafsi kwa wengine ilimgharimu sana. Alifungwa gerezani, aliteseka kwa kipindi kirefu cha njaa na kiu, kipigo, vitisho kwenye maisha yake na kudhihakiwa mara kwa mara na kukataliwa. Na bado, yote “yalimezwa katika shangwe ya Kristo” (Alma 31:38). Labda mateso ya Alma yalitengeneza shangwe iliyofuatia ambayo ni kubwa zaidi.
Rais Nelson anatukumbusha kwamba shangwe ilikuwa na sehemu kubwa katika mateso ya Mwokozi—“Kwa shangwe ambayo ilikuwa imewekwa mbele yake [Yeye], aliustahimili msalaba” (Waebrania 12:2).
“Fikiria hilo! Ili Yeye aweze kuvumilia uzoefu wa kuteseka kwa kina ambao haujawahi kamwe duniani kuvumilika, Mwokozi wetu alifokasi kwenye shangwe!
“Na nini ilikuwa shangwe ambayo iliwekwa mbele Yake? Hakika inajumuisha shangwe ya kusafisha, kuponya, na kutuimarisha; shangwe ya kulipia dhambi za wote watakaotubu; shangwe ya kutuwezesha wewe na mimi kurudi nyumbani—safi na wenye kustahili—ili kuishi na Wazazi wetu wa Mbinguni na familia.
“Kama tunafokasi katika shangwe itakayokuja kwetu, au kwa wale tuwapendao, nini tunachoweza kuvumilia ambacho sasa kinaonekana kushindikana, kichungu, cha kutisha, kisicho haki, au hakiwezekani?”2
Shangwe ya kudumu huja kwa kubakia katika injili ya Yesu Kristo na kuwasaidia wengine wafanye vivyo hivyo. Shangwe ya kudumu huja pale tunapokaa kwenye upendo wa Mungu, tukitii amri zake na kupokea rehema ya Mwokozi. Katika njia ya injli, kuna shangwe katika safari vile vile kuna shangwe mwishoni. Injili ya Yesu Kristo ni njia ya shangwe ya kila siku.
© 2024 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Limepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly Liahona Message, February 2024. Language. 19276 743