“Yesu Kristo ndiye Chanzo cha ‘Uhai,’ ‘Wema,’ na ‘Tumaini Lililo Kamili Zaidi,’” Liahona, Des. 2024.
Ujumbe wa kila mwezi wa Liahona, Desemba 2024
Yesu Kristo Ndiye Chanzo cha “Uhai,” “Wema,” na “Tumaini Lililo Kamili Zaidi”
Katika msimu huu maalum wa kusherehekea kuzaliwa kwa mtoto huko Bethlehemu, na daima tukumbuke kwamba Yesu Kristo alikuja ulimwenguni kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu.
Mtume Petro na manabii wa Kitabu cha Mormoni Yakobo na Moroni wanasisitiza karama ya kiroho ya tumaini katika Kristo katika njia sawa na hizo.
Kwa mfano, Petro alitangaza, “Heri Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kulingana na rehema yake tele ametuzaa tena katika tumaini hai kwa ufufuko wa Yesu Kristo kutoka kwa wafu” (1 Petro 1:3; msisitizo umeongezwa). Tafadhali tambua matumizi ya neno “hai” kuelezea “tumaini.”
Yakobo alitangaza, “Kwa hivyo, ndugu wapendwa, patanishweni na yeye kwa upatanisho wa Kristo, Mwana wake wa Pekee, na mnaweza kupokea ufufuo, kulingana na nguvu za ufufuo ambazo zimo katika Kristo, na mkabidhiwe kama malimbuko ya Kristo kwa Mungu, mkiwa na imani, na kupokea tumaini jema la utukufu kwake kabla hajajidhihirisha katika mwili” (Yakobo 4:11; msisitizo umeongezwa). Tafadhali tambua matumizi ya neno “wema” kuelezea “tumaini.”
Na Moroni alieleza, “Na ninakumbuka kwamba umesema kwamba umetayarisha nyumba kwa watu, ndiyo, hata miongoni mwa nyumba za Baba yako, ambamo kwake binadamu angekuwa na tumaini kamili; kwa hivyo lazima binadamu atumaini, au hatapokea urithi mahali ambapo umetayarisha” (Etheri 12:32; msisitizo umeongezwa). Tafadhali tambua matumizi ya neno “kamili” kuelezea “tumaini.”
Tumaini katika Kristo ni Nini?
Karama ya kiroho ya tumaini katika Kristo ni matarajio ya furaha ya uzima wa milele kupitia “ustahili, na rehema, na neema za Masiya Mtakatifu” (2 Nefi 2:8) na hamu kubwa ya baraka zilizoahidiwa za haki. Vivumishi “hai,” “wema,” na “kamili zaidi” katika mistari hii vinaonyesha hakikisho linaloongezeka na la kustaajabisha la Ufufuko na uzima wa milele kupitia imani katika Yesu Kristo.
Nabii Mormoni alieleza:
“Na tena, ndugu zangu wapendwa, ninataka kuwazungumzia kuhusu tumaini. Inawezekanaje kwamba mtafikia imani, isipokuwa muwe na tumaini?
“Na ni kitu gani mtakachotumainia? Tazama nawaambia kwamba mtakuwa na tumaini kupitia upatanisho wa Kristo na uwezo wa kufufuka kwake, kuinuliwa kwa maisha ya milele, na hii kwa sababu ya imani yenu kwake kulingana na ile ahadi.
“Kwa hivyo, ikiwa mtu ana imani lazima ahitaji kuwa na tumaini; kwani bila imani hakuwezi kuwepo na tumaini lolote” (Moroni 7:40–42).
Mpango wa Furaha wa Baba
Tumaini katika Kristo ambalo ni hai, jema, na kamilifu zaidi linaanza na ufahamu kwamba Mungu Baba wa Milele yu hai. Yeye ni Baba yetu, na sisi ni watoto Wake wa kiroho. Kiuhalisia sisi ni wana na mabinti wa kiroho wa Mungu na tumerithi sifa takatifu kutoka Kwake.
Baba ni mwanzilishi wa mpango wa furaha (ona Ibrahimu 3:22–28). Kama wana na mabinti wa Mungu wa kiroho, “tulikubali mpango Wake ambao watoto [Wake] wangeweza kupokea mwili na kupata uzoefu wa duniani ili kukua kwa ukamilifu na hatimaye kutambua maisha [yao] matakatifu kama warithi wa maisha ya milele.” Katika maandiko, tunajifunza: “Baba ana mwili wa nyama na mifupa unaoonekana kama wa mwanadamu; Mwana pia” (Mafundisho na Maagano 130:22). Hivyo, kupata miili ni muhimu katika mchakato wa kupiga hatua kuelekea hatma yetu ya kiungu.
Sisi ni viumbe wa aina mbili. Roho zetu, sehemu yetu ya milele, zimevikwa katika miili ya kimwili ambayo iko chini ya hamu na matamanio ya maisha ya duniani. Mpango wa furaha wa Baba umeundwa ili kutoa maelekezo kwa ajili ya watoto Wake, kuwasaidia kurudi nyumbani Kwake salama tukiwa na miili iliyofufuka, iliyoinuliwa, na kupokea baraka za shangwe na furaha ya milele.
Wajibu wa Ukombozi wa Yesu Kristo katika Mpango wa Baba
Yesu Kristo ndiye Mwana Pekee wa Baba wa Milele. Alikuja ulimwenguni kufanya mapenzi ya Baba Yake (ona 3 Nefi 27:13). Yesu Kristo ndiye mpakwa mafuta wa Baba kuwa mwakilishi Wake binafsi katika mambo yote yahusuyo wokovu wa wanadamu. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu kwa sababu alishinda vyote, kifo na dhambi.
Alma alitoa unabii kwa watu wa Gideoni kuhusu kazi ya kuokoa ya Masiya:
“Na atakwenda, na kuteseka maumivu na masumbuko na majaribio ya kila aina; na hii kwamba neno litimizwe ambalo linasema atabeba maumivu na magonjwa ya watu wake.
Na atajichukulia kifo, ili afungue kamba za kifo ambazo zinafunga watu wake; na atajichukulia unyonge wao, ili moyo wake ujae rehema, kulingana na mwili, ili ajue kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao.
Sasa Roho anajua vitu vyote; walakini Mwana wa Mungu anateseka katika mwili ili achukue dhambi za watu wake, kwamba aondoe uvunjaji wao wa sheria kulingana na nguvu za ukombozi wake” (Alma 7:11–13).
Kanuni ya kwanza ya injili ni imani katika Bwana Yesu Kristo. Imani ya kweli inafokasi ndani ya Mwokozi na kwa Mwokozi na inatuwezesha kumwamini Yeye na kuwa na ujasiri kamili katika nguvu Zake za kutuokoa kutokana na kifo, kutusafisha kutokana na dhambi, na kutubariki kwa nguvu zaidi ya zetu wenyewe.
Moroni alishuhudia, “Na kwa sababu ya ukombozi wa binadamu, ambao ulifika kupitia kwa Yesu Kristo, wanarudishwa kwenye uwepo wa Bwana; ndiyo, hii ndiyo njia ambayo kwake watu wote wanakombolewa, kwa sababu kifo cha Kristo husababisha kutimizwa kwa ufufuko, ambao husababisha kutimizwa kwa ukombozi kutoka kwa usingizi wa milele, usingizi ambao watu wote wataamshwa kwa uwezo wa Mungu wakati tarumbeta itakapolia; na watatoka nje, wote wadogo na wakubwa, na wote watasimama mbele ya hukumu yake, wakikombolewa na kufunguliwa kutoka kwenye kamba hii ya kifo cha milele, kifo ambacho ni kifo cha mwili” (Mormoni 9:13).
Ninashuhudia kwamba Mwokozi alivunja kamba za kifo. Alifufuka, Yu hai, na Yeye ndiye chanzo pekee cha uhai, wema, na tumaini kamili zaidi.
Nanga ya Nafsi
Nabii Etheri alishuhudia, “Kwa hivyo, yeyote aaminiye katika Mungu angeweza kwa hakika kutumaini ulimwengu bora, ndiyo, hata mahali katika mkono wa kulia wa Mungu, tumaini ambalo huja kutokana na imani, hutengeneza nanga kwa nafsi za watu, ambayo ingewafanya kuwa imara na thabiti, wakizidi sana kutenda kazi njema, wakiongozwa kumtukuza Mungu” (Etheri 12:4; msisitizo umeongezwa).
Katika msimu huu maalum wa kusherehekea kuzaliwa kwa mtoto huko Bethlehemu, na daima tukumbuke kwamba Yesu Kristo alikuja ulimwenguni kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu. Anatupa karama za kiroho zenye thamani kuu za maisha, nuru, kufanywa upya, upendo, amani, mtazamo, shangwe, na tumaini.
Ninawaalika mtafute ipasavyo karama ya kiroho ya tumaini katika Mwokozi kwa kujifunza mafundisho na shuhuda za manabii wa kale na wa sasa kuhusu dhabihu Yake ya upatanisho na Ufufuko Wake halisi. Mnapofanya hivyo, ninaahidi kwamba ushuhuda wenu wa uungu wa Mkombozi utaimarishwa, uongofu wenu Kwake utaimarishwa, tamanio na azimio lenu la kusimama kama ushahidi jasiri juu Yake vitaongezeka, na utabarikiwa kwa nanga ya nafsi yako—hata uhai, wema, na tumaini lililo kamili zaidi.
Pamoja na Mitume ambao wametoa ushuhuda juu Yake katika nyakati zote, kwa shangwe ninatangaza ushahidi wangu kwamba Yesu Kristo ni Mwana aliye hai wa Mungu aliye hai. Yeye ni Mkombozi wetu aliyefufuka akiwa na mwili uliotukuka, unaoonekana wa nyama na mifupa. Na kwa sababu ya ukombozi na upatanisho kwa Mungu ambao Bwana huuwezesha wanadamu wote, tunaweza kupokea hakikisho la kiroho na tumaini hai, jema, na kamili zaidi kwamba “katika Kristo wote watahuishwa” (1 Wakorintho 15:22).
© 2024 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Limepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly Liahona Message, December 2024. Swahili. 19296 743