Tamko Rasmi 2
Kitabu cha Mormoni kinafundisha kwamba “watu wote ni sawa kwa Mungu,” ikijumuisha “weusi na weupe, watumwa na huru, wanaume na wanawake” (2 Nefi 26:33). Katika historia yote ya Kanisa, watu wa kila asili na kabila katika nchi nyingi wamebatizwa na wameishi kama waumini waaminifu wa Kanisa. Katika kipindi cha uhai wa Joseph Smith, wanaume weusi wachache waliokuwa waumini wa Kanisa walikuwa wametawazwa katika ukuhani. Mapema katika historia yake, viongozi wa Kanisa walisimamisha kutunuku ukuhani kwa wanaume weusi wenye asili ya Kiafrika. Kumbukumbu hazitoi taarifa kamili juu ya chanzo cha desturi hii. Viongozi wa Kanisa waliamini kwamba ufunuo kutoka kwa Mungu ulihitajika ili kubadilisha desturi hii na kwa maombi walitafuta mwongozo. Ufunuo ulikuja kwa Rais wa Kanisa Spencer W. Kimball na kuthibitishwa na viongozi wengine wa Kanisa katika Hekalu la Salt Lake 1 Juni 1978. Ufunuo uliondoa masharti yoyote yaliyohusishwa na asili ya mtu ambayo wakati fulani yalitumika kwenye ukuhani.
Kwa Yeyote Anayehusika
Mnamo 30 Septemba 1978, wakati wa Mkutano Mkuu wa 148 wa Nusu Mwaka wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, yafuatayo yalitolewa na Rais N. Eldon Tanner, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza wa Kanisa:
Mwanzoni mwa mwezi Juni ya mwaka huu, Urais wa Kwanza ulitangaza kwamba ufunuo ulikuwa umepokelewa na Rais Spencer W. Kimball wa kutoa ukuhani na baraka za hekaluni kwa wanaume wote walio waumini wa Kanisa. Rais Kimball ameniomba kwamba niueleze mkutano kwamba baada ya kupokea ufunuo huu, ambao ulikuja kwake baada ya tafakari na sala ndani ya vyumba vitakatifu vya hekalu takatifu, aliupeleka kwa washauri wake, ambao waliupokea na kuupitisha. Ndipo baadaye ukafikishwa kwa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, ambao kwa kauli moja waliupitisha, na mwishowe ukapelekwa kwa Viongozi Wakuu wengine wote, ambao nao vile vile waliupitisha kwa kauli moja.
Rais Kimball ameniomba kuwa sasa niisome barua hii:
8 Juni 1978
Kwa viongozi wakuu wote na maofisa wa ukuhani wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ulimwenguni kote:
Ndugu zangu Wapendwa:
Kama vile tunavyoshuhudia kupanuka kwa kazi ya Bwana duniani, tunashukuru kwamba watu wa mataifa mengi wameitikia ujumbe wa injili ya urejesho, na wamejiunga na Kanisa kwa idadi inayoongezeka daima. Hili, matokeo yake, limetusukuma sisi kuwa na hamu ya kutoa kwa kila muumini mwenye kustahili haki na baraka zote ambazo injili hutoa.
Tukiwa tunafahamu ahadi zilizofanywa na manabii na marais wa Kanisa waliotutangulia sisi kwamba kwa wakati fulani, katika mpango wa milele wa Mungu, ndugu zetu wote wenye kustahili wanaweza kupokea ukuhani, na tukiwa tunashuhudia uaminifu wa wale ambao ukuhani umekataliwa, tumeomba kwa dhati na kwa muda mrefu kwa niaba yao hawa, ndugu zetu waaminifu, tukitumia masaa mengi katika Chumba cha Orofani cha Hekalu tukimwambia Bwana atupe mwongozo mtakatifu.
Amesikia sala zetu, na kwa ufunuo amethibitisha kwamba siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa muda mrefu imefika ambapo kila mwanamume, aliye mwaminifu katika Kanisa apate kupokea ukuhani mtakatifu, pamoja na uwezo wa kutumia mamlaka yake matakatifu, na kufurahia pamoja na wapenzi wake kila baraka itiririkayo kutoka huko, pamoja na baraka za hekalu. Kwa hiyo, wanaume wote wenye kustahili walio waumini wa Kanisa wanaweza kutawazwa kwenye ukuhani bila kujali asili au rangi. Viongozi wa ukuhani wanaelekezwa kufuata sera ya kuwatahini kwa uangalifu wote waliopendekezwa kutawazwa au kwenye ukuhani wa Haruni au ukuhani wa Melkizedek ili kuhakikisha kwamba wanatimiza viwango vya ustahili vilivyowekwa.
Tunatamka kwa dhati kwamba Bwana ametujulisha mapenzi yake kwa ajili ya baraka kwa watoto wake wote duniani kote ambao wataisikia sauti ya watumishi wake wenye mamlaka, na kujitayarisha wenyewe kupokea kila baraka ya injili.
Wenu waaminifu,
Spencer W. Kimball
N. Eldon Tanner
Marion G. Romney
Urais wa Kwanza
Kwa kuwa tunamtambua Spencer W. Kimball kama nabii, mwonaji, na mfunuzi, na rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, inapendekezwa kwamba sisi kama kusanyiko la kikatiba kuukubali ufunuo huu kama ndilo neno na mapenzi ya Bwana. Wote wanaokubali tafadhali waonyeshe ishara kwa kunyosha mkono wako wa kulia. Yeyote anayepinga kwa ishara hiyo hiyo.
“Kura ya kuunga mkono hoja ilikubaliwa na wote na kwa kauli moja.”
Jiji la Salt Lake, Utah, 30 Septemba 1978.