Kitabu cha Mormoni kinafundisha kwamba “watu wote ni sawa kwa Mungu,” ikijumuisha “weusi na weupe, watumwa na huru, wanaume na wanawake” (2 Nefi 26:33). Katika historia yote ya Kanisa, watu wa kila asili na kabila katika nchi nyingi wamebatizwa na wameishi kama waumini waaminifu wa Kanisa. Katika kipindi cha uhai wa Joseph Smith, wanaume weusi wachache waliokuwa waumini wa Kanisa walikuwa wametawazwa katika ukuhani. Mapema katika historia yake, viongozi wa Kanisa walisimamisha kutunuku ukuhani kwa wanaume weusi wenye asili ya Kiafrika. Kumbukumbu hazitoi taarifa kamili juu ya chanzo cha desturi hii. Viongozi wa Kanisa waliamini kwamba ufunuo kutoka kwa Mungu ulihitajika ili kubadilisha desturi hii na kwa maombi walitafuta mwongozo. Ufunuo ulikuja kwa Rais wa Kanisa Spencer W. Kimball na kuthibitishwa na viongozi wengine wa Kanisa katika Hekalu la Salt Lake 1 Juni 1978. Ufunuo uliondoa masharti yoyote yaliyohusishwa na asili ya mtu ambayo wakati fulani yalitumika kwenye ukuhani.