Ndoa, Pesa, na Imani
Mwandishi anaishi Mkoa wa Ashanti, Ghana.
Mimi na mchumba wangu tulikuwa na muda mchache kabla ya harusi yetu, na hata pesa pungufu, lakini tulikuwa na kitu fulani cha muhimu zaidi: imani.
Nilihudhuria mkutano wa vijana waseja huko Kumasi, Ghana, siyo kwa sababu nilihitaji rafiki wa kike—nilikuwa tayari kwenye uchumba—lakini kwa sababu nilijisikia kuhitaji motisha zaidi na kwamba mkutano ule ungekuwa mahala sahihi pa kuipata. Kweli, maombi yangu yalijibiwa kwenye mkutano baada ya Dada Call, mmisionari mkubwa aliyepangiwa kushughulika na vijana waseja, aliongelea kuhusu umuhimu wa ndoa ya hekaluni.
Kuelekea mwisho wa majadiliano, muonekano wake ghafla ulibadilika na akasema, “huhitaji pesa kufunga ndoa—yote unayohitaji ni imani.” Nilihisi kama alikuwa akiongea na mimi moja kwa moja, lakini sikudhani ingeweza kweli kutumika kwangu kwa sababu tulitakiwa kununua vitu kadhaa katika maandalizi ya harusi. Nilijiambia, “Je, ni kwa jinsi gani Ninaweza nisihitaji pesa bali imani tu?”
Nilifikiri kuhusu hili tena na tena kwa wiki nzima. Katika mchakato, Nilijiuliza mwenyewe, “Je, Mungu ana ukomo katika yale Anayoweza kufanya?” Mwanzo, nilifikiri hapana, lakini wazo la pili Nilifikiri ndiyo. Lakini punde likaja swali la-kufuatilia, “Anawezaje kuwa na ukomo kama Yeye ana nguvu-zote?” Roho alinifundisha jibu: baraka za Mungu hutegemea utiifu wetu Kwake. Hana ukomo katika uwezo Wake kutubariki sisi, lakini lazima tualike baraka hizo kwa kufanyia kazi imani kwa kufanya yale Anayotaka sisi tufanye.
Baadaye, Nilimpigia simu mchumba wangu, Priscilla, kujadili mipango yetu ya ndoa. Licha ya kutokuwa na pesa, tuliamua kuchagua tarehe ya harusi yetu, lakini hatungeweza kuamua juu ya tarehe fulani hasa. Tulikubaliana kwamba amuulize askofu wake tarehe zipi zilikuwa wazi kwenye kalenda ya kata na kigingi. Kati ya tarehe mbili alizotoa, tulichagua Septemba 27, 2014—ambayo ilimaanisha kwamba tulikuwa na wiki saba tu kufikia siku ya harusi yetu!
Priscilla aliuliza, “Obim [ikimaanisha “moyo wangu” katika lugha ya Igbo], je, una pesa? Muda ni mfupi.”
Nilijibu, “Hapana, lakini ninayo imani.”
Alicheka na kusema, “Ni Sawa. Acha tufunge na kuomba.” Akifafanua 1 Nefi 3:7, aliendelea, “Bwana atafungua njia kwa ajili yetu kwa sababu Ametuamuru tufunge ndoa.”
Ndani ya wiki ile Nililipwa kwa ajili ya kazi Niliyofanya miezi iliyopita. Kisha Priscilla aliniambia kwamba alitaka kuanzisha biashara kupata pesa zaidi. Kwa pesa nilizokuwa nimepata, alinunua mikoba iliyotumika ya wanawake na kuiuza tena. Baada ya kununua baadhi ya vitu katika orodha yake ya vitu vilivyohitajika, alibakiwa na zaidi ya mara mbili ya pesa nilizompa.
Wakati huu, hakukua na kazi zilizokuja upande wangu. Kila kazi niliyoahidiwa haikutokea. Tulikuwa na wiki mbili zimebaki na kulikuwa bado na vitu tulivyohitaji kununua. Mchumba wangu alipendekeza kwamba tarehe isogezwe mbele. Yote Niliyosema ilikuwa, “Muujiza upo njiani.”
Siku mbili tu kabla ya harusi yetu, muujiza ulitokea: Nililipwa kwa kazi Niliyokuwa nimefanya zaidi ya wiki mbili kabla. Nilikuwa pia najifunza kwamba kwa imani na kufanya kazi kwa bidii, Bwana angetubariki kufanikisha malengo yetu ya haki.
Tulienda benki kupata pesa taslimu ya hundi na kutoka hapo kwenda sokoni kufanya manunuzi ya masalia ya vitu vilivyohitajika katikati ya mvua kubwa, ambayo tuliona kama idhini ya mbingu kwa tendo letu la imani.
Chini ya saa 24 baadaye, tulifunga ndoa. Tulipotakiwa kuweka nadhiri, hisia hazikuwa sawa na chochote nilichowahi kuhisi maishani mwangu. Nilihisi kukamilishwa mno kwamba Niliamini Ningeweza kufanya mambo yote kupitia imani tokea pale na kuendelea. Baadaye tuliunganishwa katika Hekalu la Accra Ghana.
Japo unaweza kuhitaji kiasi cha pesa kujiandaa kwa ajili ya ndoa, kitu muhimu unachohitaji ni imani.