Mikutano ya Ibada ya Ulimwenguni Kote
Sisi ni Waasisi wa Furaha Yetu Wenyewe


2:3

Sisi ni Waasisi wa Furaha Yetu Wenyewe

Akina ndugu na dada wapendwa, usiku wa leo ninahisi heshima kuu na taadhima kuwa na nafasi ya kuwahutubia. Nina uvutiwaji wa kina kwa vijana wazima wa Kanisa, na ninafurahia kuweza kuwa na wakati nanyi jioni ya leo.

Maelfu yenu mko katika hili Tabenakulo zuri. Na hata wengi zaidi ambao siwezi kuwaona wamekusanyika katika maelfu ya nyumba za mikutano kote ulimwenguni. Lakini ninajua kuwa mko makini na mna hamu ya kujifunza. Licha ya umbali unaotutenganisha, ninajua kuwa Roho Mtakatifu anaweza kuwa popote tulipo. Hata zaidi ya matangazo ya setalaiti, ni uwepo wa Roho Mtakatifu unaoleta uunganisho wa kipekee kati yetu sote. Ninaomba kuwa atakuwa nasi, kwamba atatufundisha, kutuelekeza na kutuongoza jioni ya leo.

Maisha yana Maajabu Mengi

Tupo kwenye chumba kizuri kabisa, jengo la ukumbusho la kihistoria linaloipa hadhi imani na utendakazi wa watangulizi walioanzisha Jiji la Salt Lake. Niliingia katika Tabenakulo hili kwa mara ya kwanza nilipokuwa na umri wa miaka 16. Ilikuwa ni ziara yangu ya kwanza Marekani. Baba yangu alikuwa amependekeza kuwa niandamane naye katika mojawapo wa ziara zake kwenda California. Kama kijana aliyelelewa Kusini mwa Ufaransa, niliruka kwa shangwe kwa mwaliko huu. Hatimaye nilikuwa naenda kuona Marekani! Hamasa yangu ilikuwa kuu hata zaidi kwa sababu utaratibu wetu ulijumuisha wikendi katika Jiji la Salt Lake kuhudhuria Mkutano Mkuu.

Ninakumbuka kuwasili kwetu Utah katika gari letu lililokodiwa la Ford Mustang. Kwa masaa mingi tuliotumia njiani, tulipita dhoruba ya barafu, majangwa ya umbali ya upeo wa macho, mabonde ya ajabu yaliyokuwa na rangi ya machungwa na milima ya ajabu. Mandhari ya nchi yalidhihirisha Marekani Magharibi na niliwacha macho wazi nikitumaini kuona wachunga ng’ombe au Wahindi njiani.

Siku iliyofuata, kwa sababu ya wema wa rafiki, tulijikuta tumeketi katika Tabenakulo hili kwenye safu za kwanza ili kuhudhuria vikao vya mkutano mkuu. Nilivutiwa sana. Katika mikutano yote, nilijaribu kushikilia maneno machache ya kiingereza niliyoweza kuelewa. Bado nakumbuka hotuba ya Rais Ezra Taft Benson- si maneno yake hasa, lakini mvuto wa kina iliyoweka moyoni mwangu kama kijana. Nilihisi nilikuwa ninaishi katika ndoto, katika tukio la ajabu.

Wakati huo, ningewezaje kufikiri kile kingetendeka jioni ya leo? Ningeweza kufikiria kutoa hotuba katika Tabenakulo hili hili mbele ya umati kama huu? La hasha!

Maisha yana maajabu mengi, sivyo? Hata miaka mitano iliyopita singeweza kufikiri hili. Kwa wakati huo niliishi Paris pamoja na familia yangu, na maisha yetu yalionekana kuwa yamepangika kabisa. Watoto wetu watano walizaliwa wote katika zahanati moja karibu na nyumba yetu. Kwetu, hatungefikiria maisha tofauti au mahali pengine kama si maeneo hayo yenye amani katika viunga vya Paris, tukizungukwa na watoto wetu na wajukuu watarajiwa. Kisha jioni moja Rais Monson akapiga simu kwetu na maisha yetu yakapinduliwa juu chini.

Tangu wakati huo familia yangu nami tumetambua furaha ya maisha katika Utah--- sehemu za historia ya Kanisa, kukwea milima, kuchoma nyama uani jua linapotua, kufurahia hambaga za kila aina (nzuri zaidi na mbaya zaidi!) michezo ya mpira ya Cougars, ama Utes. Na, kamwe hauwezi kujua, yule mchunga ng’ombe utakayemwona kesho barabarani huenda akawa ni mimi!

Siku Zijazo ni Zisizopimwa

Jukumu langu kama mshiriki wa Uaskofu Simamizi ni la kufurahisha na kuhamasisha. Hata hivyo, uzoefu huu ni tofauti sana na mipango yangu ya ujana. Kama mtoto nilitaka kuwa mwanaakiologia. Bibi yangu alikuwa amechukua jukumu la kuhakikisha kuwa nilipata elimu nzuri. Alinipatia kitabu kuhusu kijana farao aliyejulikana kama Mfalme Tut, na kutoka kwacho nilikuza hamasa ya ustarabu wa kale. Nilitumia wikendi nikiunda michoro ya vita vya kale, na kuta za chumba changu zilifunikuwa na hizi picha. Nilikuwa na ndoto ya kwenda Misri na kushiriki katika machimbuo ya hekalu za Kimisri na makaburi ya farao.

Miongo minne baadaye, mimi bado si mwanaakiologia, na inaelekea kuwa kamwe sitokuwa. Sijawahi kuwa Misri, na kazi yangu ya mwisho kabla ya kuwa kiongozi Mwenye Mamlaka ilikuwa ni katika usambasaji chakula. Hamna uhusiano na mipango yangu ya utotoni!

Ujanani, kwa jumla, ni wakati mzuri wa kufanya mipango ya kibinafsi. Kila mmoja wetu alikuwa na ndoto za utotoni. Kama kijana, unapaswa bado kuwa na ndoto za siku zako za usoni, kila mmoja wenu! Pengine ni matumaini ya kufaulu katika riadha, au kuunda kazi nzuri ya sanaa, au kupata cheti au nafasi ya kikazi unayotafuta kupata kupitia kwa kazi na uvumilivu. Huenda hata una taswira nzuri sana akilini mwako ya mke au mume wako wa siku za usoni, muonekano wake wa kimwili, sifa zake, rangi ya macho au nywele zake, na watoto wazuri watakaobariki familia yenu.

Ni ngapi kati ya matakwa yenu yatatimia? Maisha yamejaa shaka. Mshangao utatokeza kote katika njia ya maisha. Ni nani anajua kitakachofanyika kesho, utakapokuwa katika miaka michache, na kile utakachokuwa ukifanya? Maisha ni kama ngano ya msisimuo ambao mwelekeo wake ni mgumu kukisia.

Kutakuwa na nyakati muhimu ambazo huenda zikabadilisha mkondo wa maisha yako mara moja. Wakati kama huo unaweza kujumuisha si zaidi ya kutazama, mazungumzo, au hata tukio lisilopangwa. Valerie nami tunakumbuka wakati hasa tulipopendana. Ilikuwa wakati wa mazoezi ya kwaya ya kata ya vijana wazima katika Paris. Hili halikutarajiwa kabisa! Tulikuwa tumejuana tangu utotoni, na lakini hatukuwahi kuwa na hisia za kimapenzi kati yetu. Jioni hiyo, nilikuwa kwenye piano naye alikuwa anaimba katika kwaya. Tulitazamana machoni na jambo likafanyika. Sekunde moja kwa ajili ya milele yote!

Kutakuwa na fursa mpya zitakazojitokeza katika maisha yenu, kama vile tangazo la hivi karibuni la Rais Monson kuhusu umri wa huduma ya misheni. Kufuatia tangazo hili kutoka kwa nabii, kuna pengine maelfu ya vijana na wasichana kanisani wakati huu walio katika mchakato wa kubadilisha mipango yao ya kwenda kuhudumu misheni.1

Wakati mwingine, mabadiliko ya mikondo katika maisha yetu huja kutokana na changamoto na kukatishwa tamaa. Nimejifunza kupitia kwa uzoefu kuwa tunaweza tu kwa kiwango fulani kudhibiti hali za maisha yetu.

Ilhali watu wengi hawapendi kusichojulikana. Shaka ya maisha huleta kukosa uhakika, hofu kuhusu siku za usoni ambazo hujidhihirisha kwa njia tofauti. Wengine husita kufanya ahadi kutokana na hofu ya kushindwa, hata wakati nafasi nzuri zinapojitokeza. Kwa mfano, wanaweza kuchelewesha ndoa, elimu, kaunzisha familia au kujijenga katika kazi dhabiti, wakipendelea ‘kujifurahisha’ au kubaki katika faraja ya nyumba ya wazazi wao.

Falsafa nyingine itakayotuzuia inadhihirishwa na msemo huu: “Kuleni, kunyweni, na mshangilie, kwani kesho tutakufa” (2 Nefi 28:7). Kishazi hiki kinapendekeza kuwa kwa kuwa hatujui kitakachofanyika kesho na sote hatimaye tutakufa, tunapaswa kujifurahisha katika wakati wa sasa. Falsafa hii inapendelea kujiingiza katika raha za papo hapo, bila kujali matokeo yake ya siku za usoni.

Fuata Mapito ya Furaha

Ndugu na dada zangu wapendwa, ujumbe wangu kwenu leo ni kuwa kuna njia tofauti kuliko zile za hofu na shaka au raha za kibinafsi---njia inayoleta amani, kuwa na hakika, na utulivu maishani. Huwezi kudhibiti hali zote za maisha yako. Mambo, mazuri na yenye changamoto usiyotarajia yatakufanyikia . Hata hivyo, ninatangaza kuwa muna udhibiti wa furaha yenu wenyewe. Ninyi ndio waasisi wake.

Bado ninaweza kukumbuka maneno haya yenye hekima yaliyotamkwa na Rais Dieter  F. Uchtdorf katika Mkutano Mkuu uliopita:

“Tunapokuwa wazee, ndipo tunapotazama nyuma na kutambua kuwa hali za nje hazijalishi wala kuamua furaha yetu.

“… Sisi tunaamua furaha yetu”2

Hasha, furaha yako si hasa kwa sababu ya hali ya maisha yako. Ni zaidi matokeo ya ono lako la kiroho na kanuni ambazo unajenga maisha yako. Kanuni hizi zitakuletea furaha licha ya changamoto zisizotarajiwa na mastaajabu ambayo bila shaka utakumbana nayo katika safari yako duniani.

Jioni hii, ninapendekeza kutathmini pamoja nanyi baadhi ya kanuni hizi muhimu.

1.Tambua Thamani Yako ya Kibinafsi

Kanuni ya kwanza ni: Tambua thamani yako ya kibinafsi

Katika msimu huu wa majira ya joto, familia yangu nami tulitumia siku chache tukibarizi katika Provence, eneo mzuri sana la Ufaransa Kusini. Jioni moja, baada ya tu jua kutua na giza kufunika eneo lililokuwa karibu, niliamua kujipa muda wa utulivu kwa kulala katika kiti nje ya nyumba. Kila kitu kilikuwa giza hata nilikuwa na ugumu wa kutofautisha chochote karibu nami. Macho yangu yakaanza kutathmini mbingu. Kwanza kulikuwa na giza totoro. Ghafla, mwanga ukaonekana kwenye mbingu, kama cheche, kisha mbili, kisha tatu. Kwa kuendelea, macho yangu yalipozoea giza, nilijipata nikivutiwa na nyota chungu nzima. Nilichokuwa nikifikiria mbingu ya giza ilibadilika na kuwa Kilimia.

Nilifikiria: “Hii kidogo ni kama uhusiano wetu wa kibinafsi na Mungu. Ni watu wangapi wanaoamini kuwa Yeye yuko mbali au hata hayuko? Watu hao hupata kuwa maisha ni yenye giza na meusi. Huwa hawachukui muda au kufanya juhudi kutathmini mbingu ili kuona kuwa Yeye yupo, karibu sana nasi.”

Akili yangu ikaendelea kutanga. Nilitafakari kuhusu ukuu wa ulimwengu uliojidhihirisha mbele ya macho yangu na kwa kutokuwa kwangu muhimu kimwili, na nikajiuliza “ Mimi ni nini mbele ya ukuu na uzuri huu?” Andiko lilinijia akilini mwangu. Ni andiko nzuri, mojawapo ya Zaburi za Daudi ambaye ushairi wake umenihamasisha kila mara.

“Nikiziangalia mbingu zako, kazi ya vidole vyako, mwezi na nyota, uliziziratibisha;

”Mtu ni kitu gani, hata umkumbuke ? na binadamu hata umwangalie”(Zaburi 8:3–4).

Mara inafuata kifungu hiki cha kufariji:

“Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu, umemvika taji ya utukufu na heshima.” (Zaburi 8:5).

Hii ndiyo kweli kinza na mwujiza wa uumbaji. Ulimwengu ni mkuu na usio na mwisho, ilhali, wakati huo huo, kila mmoja wetu ana thamani ya kipekee, yenye utukufu na usiyo na kikomo machoni mwa Muumba wetu. Uwepo wangu wa kimwili ni mdogo mno, ilhali thamani yangu ya kibinafsi ni ya umuhimu usiopimika kwa Baba yangu wa Mbinguni

Rais Uchtdorf alitangaza:

“ Popote ulipo, katika hali yoyote, hujasahaulika. Hata siku zao zikionekana kuwa giza vipi, hata unavyojihisi kuwa hauna thamani, hata unavyofikiria kuwa umezuiliwa vipi, Baba yako wa Mbinguni hajakusahau. Kwa hakika, Anakupenda na upendo usio na kikomo.

“… Unajulikana na kukumbukwa na Kiumbe wa kifahari, mwenye nguvu, na utukufu ulimwenguni kote. Unapendwa na Mfalme wa anga na wakati usio na mwisho!”3

Kufahamu kuwa Mungu anatujua na kutupenda kibinafsi ni kama mwanga unaoangaza maisha yetu na kuyapa maana. Ninakumbuka msichana mmoja aliye kuja kuniona baada ya mkutano niliokuwa nao katika Roma, Italia. Sauti yake ilijawa na mhemko, na alinizungumzia kuhusu dada yake aliyekuwa akipitia wakati mgumu na wa wasiwasi. Kisha akaniuliza swali hili: “Nitamsaidiaje kujua kuwa Baba yake wa Mbinguni anampenda?”

Je! Si hilo ndilo swali la msingi? Tunawezaje kujua kuwa Mungu anatupenda? Mara nyingi hisia tuliyo nayo ya thamani yetu ya kibinafsi huwa na misingi yake katika upendo na mvuto tunaopata kutokana na wale walio karibu nasi. Na hali wakati mwingine upendo huu hukosekana. Upendo wa wanadamu mara kwa mara si mkamilifu, au una uchoyo.

Hata hivyo, upendo wa Mungu ni mkamilifu, wa dhati na bila choyo. Yule niliye, niwe na marafiki au la, niwe maarufu au la, na hata nikihisi kukataliwa na wengine, nina hakika kamili kuwa Baba yangu wa Mbinguni ananipenda. Anajua mahitaji yangu; anaelewa haja zangu; ana hamu ya kunibariki. Na dhihirisho kuu la upendo wake kwangu ni kuwa “ jinsi hii aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee” (Yohana 3:16). Hakuondoa kikombe cha uchungu cha Mwokozi na kwa kweli alikuwa katika machungu mwenyewe alipomwona Mwanawe akiteseka katika Bustani la Gethsemane na msalabani. Kristo alilipia dhambi za watu wote na sehemu ya Upatanisho mkuu huo uliandaliwa kwangu na umewekwa kwa ajili yangu. Karama hii isiyo na kifani ambayo Baba alishiriki na Mwanawe, inahakikisha katika nafsi yangu thamani ya kibinafsi niliyo nayo Kwao.

Ndugu na dada zangu, fikiria kile kingemaanisha kwako kama ungejiona kama Mungu anavyokuona. Kama ungejiona kwa wema sawa, upendo, na imani ambayo Mungu anakuona? Fikiria athari ambayo ingekuwa nayo katika maisha yako kuelewa unachoweza kuwa kama vile Mungu anavyoelewa. Kama ungejiona kupitia kwa macho yake, ingekuwa na athari gani maishani mwako?

Ninashuhudia kuwa Yeye yupo. Mtafute! Tafuta na usome. Omba na uulize. Ninakuahidi kuwa Mungu atatuma ishara dhahiri ya kuweko Kwake, na upendo Wake kwako. Inaweza kuwa kupitia jibu kwa ombi, inaweza kuwa ushawishi mpole wa Roho Mtakatifu akikufariji, inaweza kuwa hamasisho wa ghafla au nguvu mpya ambayo unajua haikutoka kwako, inaweza kuwa kupitia kwa mwanafamilia, rafiki, au kiongozi wa ukuhani ambaye anakuwa katika mahali panapofaa ili kubariki maisha yako. Kwa njia moja au nyingine, unapomkaribia, atakujilisha kuwa Yeye yupo.

1. Kuwa Yule Uliye

Na sasa, kanuni ya pili ya upendo: Kuwa Yule Uliye

Kishazi hiki “ Kuwa yule uliye,” kinadhaniwa kuwa cha Pindar, mmoja wa washairi maarufu wa Kigiriki4. Inasikika kama ukweli kinza. Nitakuwaje yule niliye tayari?

Niruhusu nidhihirishe kanuni hii kupitia hadithi. Hivi majuzi nilitazama filamu inayoitwa Age of Reason. Filamu hii inasimulia hadithi ya Marguerite, mfanyikazi mfanisi wa benki ambaye aliyeishi maisha yenye shughuli nyingi, zilizojaa safari na mikutano katika pembe zote za dunia. Ingawa ameolewa, anasema hana wakati wa kupata mtoto.

Anapotimia umri wa miaka 40, anapokea barua ya kifumbo iliyosema” Kwangu, Hivi leo nina umri wa miaka saba na ninakuandikia barua hii kukusaidia kukumbuka ahadi ulizofanya katika umri wa mantiki, na pia ili ukumbuke kile ninachotaka uwe.” Marguerite kwa ghafla akaelewa mwandishi wa barua si mwingine bali yeye mwenyewe alipokuwa na umri wa miaka saba. Kinachofuata ni kurasa kadha ambapo msichana huyu mdogo anaeleza kinaganaga malengo ya maisha yake.

Marguerite anagundua kuwa mtu ambaye amekuwa hana mshabaha kamwe na kile alichotaka kuwa alipokuwa msichana mdogo. Anapoamua kukomboa mtu huyo aliyetazamia akiwa msichana, maisha yake yaliyopangwa kwa ufasaha yanabadilishwa kabisa juu chini. Anajipatanisha na familia yake na kuamua kuzingatia maisha yake yote kuwahudumia watu wasiojiweza. 5

Marafiki zangu wapendwa, kama ungepokea barua hivi leo kutoka maisha yako ya awali, ingesema nini? Ni yapi yangekuwa katika barua ambayo ungeweza kuwa ulijiandikia katika siku ya ubatizo wako ulipokuwa wa umri wa miaka minane? Nitaendelea hata kitambo zaidi. Kama ingewezekana kwako kupokea barua kutoka kwa maisha yako kabla ya hapa duniani, ingesema nini? Barua kama hiyo kutoka kwa ulimwengu uliosahaulika lakini ulio halisi ingekuwa na athari gani ikiwa ungeipokea leo?

Hii barua inaweza kusema kitu kama: “Kwangu Mimi mpendwa, ninakuandikia ili ukumbuke yule ninataka kuwa. Nilishangilia kwa furaha kwa nafasi ya kuja ulimwenguni. Ninajua kuwa maisha duniani in njia muhimu ya kuniwezesha kukua hadi upeo wa uwezo wangu kamili na kuishi milele na Baba yangu wa Mbinguni. Ninatumaini kuwa utakumbuka kuwa hamu yangu kuu ni kuwa mfuasi wa Mwokozi wetu Yesu Kristo. Ninaidhinisha mpango wake na nikiwa duniani ninataka kumsaidia katika kazi Yake ya Wokovu. Tafadhali kumbuka pia kuwa ninataka kuwa sehemu ya familia itakayokuwa pamoja milele yote”

Wazo hili la mwisho linanikumbusha wimbo mzuri sana unaopatikana katika Kitabu cha Nyimbo cha Kanisa cha Kifaransa – moja ambayo haumo katika vitabu vya nyimbo vya nchi zingine zote. Unaitwa, “Souviens-toi,” inayomaanisha “kumbuka,” na imewekwa katika muziki kutoka kwa New World Symphony by Antonín Dvořák. Ni wimbo wa mzazi akimzungumzia mtoto mchanga aliyezaliwa .

Niruhusu kuwasomea aya ya tatu:

“Kumbuka, mwanangu, katika macheo ya wakati,

Tulikuwa marafiki tukicheza kwenye upepo.

Kisha siku moja, kwa shangwe, tulichagua

Kukubali mpango mkuu wa uzima kutoka kwa Bwana.

Jioni hiyo, mwanangu, tuliahidi,

Kwa upendo, kwa imani, kuunganishwa tena”.6

“Kumbuka, Mwanangu” Mojawapo wa matukio makuu ya maisha haya ni yale ya kupata kujua sisi ni kina nani hasa, tulikotoka wapi, na kisha kuishi kwa upatanifu kulingana na utambulisho wetu na madhumuni ya kuwepo kwetu.

Brigham Young said: “Somo kuu unaloweza kujifunza ni kujijua mwenyewe…. Umekuja hapa kujifunza haya… hakuna anayeweza kujifahamu kabisa, bila kuelewa zaidi ya mambo ya Mungu; wala hakuna kiumbe kinachoweza kujifunza na kuelewa mambo ya Mungu bila ya kujijua: ni sharti ajijue mwenyewe, au hawezi kamwe kumjua Mungu”7

Hivi majuzi, binti zangu walinionyesha kuwa mfano ufaao wa kanuni hii unapatikana katika filamu ya The Lion King. Kizazi chenu kilikuwa kwa sauti na taswira za filamu hii. Pengine mnakumbuka lile onyesho ambapo Simba anapata tembeleo kutoka kwa babake, Mufasa, mfalme aliyekufa. Baada ya babake kufa, Simba alitoroka mbali kutoka kwa ufalme kwa sababu alihisi hatia kuhusiana na kifo cha babake. Alitaka kuepukana na jukumu lake kama mrithi wa ufalme.

Baba yake anamjia na kumwonya: “Umesahau wewe ni nani na kwa hivyo umenisahau. Jiangalie ndani yako, Simba. Wewe ni zaidi ya kile umekuwa. Ni lazima uchuke nafasi yako katika duara ya maisha.” Kisha mwaliko huu unarudiwa mara nyingi: Nina hakika unaweza kurudia tena na mimi “ Kumbuka wewe ni nani. Kumbuka wewe ni nani.”

Simba akiwa anatingiswa kabisa kutokana na matokeo hayo, anaamua kukubali kudura yake. Anamwambia kwa siri rafiki yake, nyani wa kuiga kwamba “inaonekana kama upepo unabadilika.”

Yule nyani anajibu,“Mabadiliko ni mazuri.”

Na Simba anajibu: “ Lakini si rahisi. Ninajua kile ninapaswa kufanya . Lakini kurejea kunamaanisha ni lazima nikabiliane na maisha yangu ya awali. Nimekuwa nikiyakimbia kwa muda mrefu.”

“Unaenda wapi?” Yule nyani anamwuliza.

“Ninarudi!” alia Simba. 8

Sote tunaweza kuchukua---au kurejesha---nafasi yetu katika duara ya maisha. Kuwa yule ambaye wewe ndiwe kwa halisi. Furaha yako na uwezo wako wa kupata uwiano katika maisha yako utatendeka unapopata, fahamu, na kukubali utambulisho wako wa kweli kama mtoto wa Baba yetu wa Mbinguni na kisha kuishi kulingana na maarifa haya.

1. Amini katika Ahadi za Mungu

Na sasa ninashiriki nanyi kanuni ya tatu ya furaha: Amini ahadi za Mungu

Ninayapenda maneno haya ya kutia motisha ya Rais Thomas S. Monson: “Siku za usoni zinaangaza kama imani yenu” 9 Kufaulu kwetu na furaha maishani kunategemea kwa kiwango kikubwa imani tulio nao kuwa Bwana atatuongoza maishani ili kutimiza kudura yetu.

Nimeona kuwa waume na wake wanaotimiza mambo makubwa maishani wana imani kuu katika maisha yao ya usoni kutoka miaka ya awali ya ujana wao. Mfano ni Winston Churchill, Kiongozi maarufu wa Uingereza. Kama kijana alikuwa na imani isiyotingika katika siku zake za usoni. Akihudumu katika kikosi cha askari-farasi kule India akiwa na umri wa miaka 23, alimwandikia mama yake, “Nina imani katika nyota yangu, kwamba ninakusudiwa kufanya jambo kwa ulimwengu” 10 Ni wazo la kinabii jinsi gani! Kimsingi aliona kuwa angekuwa mtu muhimu katika historia ya nchi yake na akawa mtu aliyeongoza Uingereza katika ushindi wakati wa Vita Vikuu vya Dunia II.

Ninaamini kuwa kila mmoja wenu vijana wa Kanisa la Yesu Kristo muna zaidi ya nyota mbinguni kuwaongoza. Mungu anawalinda na ameweka ahadi kwenu.

Andiko kutoka kitabu cha Malaki limo katika msingi wa Urejesho wa injili, na lilirejelewa na malaika Moroni katika kila ya matembezi yake kwa kijana Joseph Smith. Malaika alisema akinukuu kutoka kwa nabii Eliya: “Naye atapanda katika mioyo ya watoto ahadi zilizofanywa kwa baba, na mioyo ya watoto itawageukia baba zao.” (Joseph Smith—Historia 1:39).

Ndugu na dada zangu wadogo, kwa ajili ya Urejesho, ninyi ni watoto wa ahadi. Mtapokea kama urithi ahadi zilizofanywa kwa baba zenu. Ahadi hizi kutoka kwa Bwana zinawafanya muwe sehemu ya kizazi cha kifalme.

Wengi wenu ambao ninawazungumzia mnahesabu watangulizi waadilifu kati ya wahenga wenu, nafsi kuu waliosaidia kujenga Kanisa la urejesho kupitia kwa kujitolea kwao na ujasiri. Vizazi vya Watakatifu wajasiri wamewatangulia. Wengine wanaonisikiliza leo ni watangulizi wa familia zao na katika nchi zao. Ninyi ndio kiunganisho cha kwanza katika kile kitakachokuwa mfululizo wa milele. Chochote kiwe hadithi yenu ama urithi wenu, kama washiriki wa Kanisa nyinyi mmeunganishwa katika familia ya kiroho. Nasaba yenu ya Kiroho inawafanya kila mmoja wenu muwe uzao wa kina baba, kama ilivyotabiriwa na manabii, na warithi wa ahadi za Mungu kwao.

Soma tena baraka yako ya baba mkuu. Katika baraka hii, Bwana anahakikisha kuwa umefungishwa katika mojawapo ya makabila ya Israeli, na kwa sababu ya hili, kupitia kwa uaminifu wako, unakuwa mrithi wa baraka nyingi zilizoahidiwa Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Mungu alimuahidi Ibrahimu kuwa “kwani kadiri wengi watakavyoipokea Injili hii wataitwa kwa jina [lake], nao watahesabiwa kuwa uzao [wake], na watainua na kukubariki, kama baba yao” (Ibrahimu 2:10). Katika kusoma baraka yako ya baba mkuu, weka nathari yako kwa ahadi za Bwana alizokufanyia binafsi. Tafakari kila moja yao. Zina maana gani kwako?

Ahadi hizi ni dhahiri na kama tutafanya sehemu yetu, Mungu atafanya Yake. Ninapenda sana maneno yaliyotamkwa na Alma siku alipatiana rekodi hizo takatifu kwa mwanawe Helamani:

“Kumbuka, kumbuka, mwana wangu Helamani. …

“… Kama utatii amri za Mungu, na ufanye vitu hivi ambavyo ni vitakatifu kulingana na yale ambayo Bwana amekuamuru ufanye… tazama, hakuna nguvu za ardhini au jahanamu, zinazoweza kuvichukua kutoka kwako, kwani Mungu ni mwenye uwezo kwa kutimiza maneno yake yote.

“Kwani atatimza ahadi zake zote ambazo atakuahidi, kwani ametimiza ahadi zake ambazo amewaahidi babu zetu.” (Alma 37:13, 16–17).

Kutimizwa kwa ahadi za Bwana kila mara kunafunganishwa kwa utiifu wa sheria husika. Bwana alisema: “ Mimi, Bwana, ninafungwa wakati ninyi mnapofanya ninayosema; lakini msipofanya ninayosema, ninyi hamna ahadi.” (M&M 82:10).

Kwa upande mwingine, ahadi hizi hazihakikishi kuwa kila kitu kinachofanyika maishani mwetu kitakuwa ni kulingana na matarajio na hamu zenu. Badala yake, ahadi za Mungu zinahakikisha kuwa kile kitakachofanyika kwetu ni kulingana na mapenzi yake. Wakati mwingine majaribu yasiyotarajiwa yatajitokeza ambayo ni sharti tushinde; wakati mwingine baraka zitachelewa kwa muda. Lakini wakati utafika ambapo tutajua kuwa majaribu haya na kuchelewa huku kulikuwa kwa wema wetu na maendeleo yetu ya milele. Tunaweza kuomba nini zaidi?

Kitu kikubwa tunachoweza kutamani maishani ni kulinganisha mapenzi yetu na mapenzi ya Bwana, kukubali agenda yake kwa maisha yetu. Anajua kila kitu kutoka mwanzo, na ana mtazamo ambao hatuna, na anatupenda kwa upendo usio na kifani.

Niruhusu nidhihirishe kanuni hii kwa uzoefu wa kibinafsi. Nilipokuwa kijana niliamua kujitayarisha kwa mtihani wa kuingia shule bora zaidi ya somo la biashara nchini Ufaransa. Matayarisho haya, yaliyochukua mwaka mmoja, yalikuwa ya changamoto sana na yalihitaji kazi ya kibinafsi kila siku. Mwanzoni mwa mwaka, niliamua kuwa hata uzito wa kazi uwe vipi, kamwe sitakubali masomo yangu yanizuie kuhudhuria mikutano yangu ya Jumapili au kushiriki katika darasa la chuo mara moja kila wiki. Hata nilikubali kuhudumu kama karani wa kata ya vijana wazima, ambayo ilimaanisha masaa kadha ya kazi kila wiki. Nilikuwa na hakika kuwa Bwana angetambua uaminifu wangu na angenisaidia kutimiza malengo yangu.

Kufikia mwisho wa mwaka, wakati mitihani ilipokaribia, nilihisi kama nilikuwa nimefanya yote ambayo ningeweza. Nikawa wa dhati zaidi katika maombi yangu na kufunga. Nilipofika kwa mitihani ya shule maarufu zaidi, nilikuwa na hakika kamili kuwa Bwana angejibu haja zangu. Kwa bahati mbaya matukio yalitokea kwa njia tofauti na vile nilivyokuwa nimetumaini. Mtihani wa mahojiano wa somo langu ninalolielewa zaidi yalikuwa balaa isiyotarajiwa---nilipata alama iliyonizuia kuingia shule hii iliyotamaniwa sana. Nilijawa na dhiki kabisa. Bwana angewezaje kuniacha wakati nilikuwa nimevumilia katika uaminifu wangu?

Nilipojipeleka katika mtihani wa mahojiano kwa shule ya pili katika orodha yangu, nilijawa na shaka na kutokuwa na hakika. Katika shule hili, mtihani uliokadiriwa kuwa muhimu zaidi yalikuwa mahojiano ya dakika 45 na yaliongozwa na mkurugenzi wa shule. Mwanzo wa mahojiano yalikuwa ya kawaida… hadi nilipoulizwa swali lililoonekana kutokuwa na maana sana.: “tunajua ulisoma sana kujitayarisha kwa mtihani huu. Lakini tuna haja ya kujua kuhusu shughuli zako nje ya masomo yako.” Moyo wangu uliruka mdundo! Kwa mwaka mmoja nilikuwa nimefanya vitu viwili tu: kusoma, na kwenda kanisani! Kwa hivyo nilijua ilikuwa wakati wa ukweli. Nilihofia kuwa waamuzi wangetafasiri ushirika wangu kanisani kwa njia mbaya. Lakini, kwa sekunde moja, nilifanya uamuzi kuwa mwaminifu kwa kanuni zangu.

Nilisema, “Mimi ni mshiriki wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.” Kisha kwa dakika 15 hivi, nilielezea shughuli zangu katika Kanisa: mikutano ya Sabato, madarasa ya chuo, majukumu yangu kama karani wa kata.

Nilipomaliza, mkurugenzi wa shule alizungumza: “Unajua, nina furaha umesema hivyo. Nilipokuwa kijana, nilisomea Marekani. Mmoja wa marafiki zangu wa dhati alikuwa Mmormoni. Alikuwa kijana mwema aliyekuwa na sifa kuu za ubinadamu. “Ninafikiria Wamormoni ni watu wazuri sana.”

Nafuu iliyoje! Siku hiyo nilipata alama nzuri iwezekanavyo, iliyoniwezesha kuingia katika shule hiyo kwa nafasi ya heshima.

Nilimshukuru Bwana kwa wema wake. Hata hivyo, kwa wakati huo, singeweza kukubali kuanguka kwangu kuingia katika shule iliyosifika zaidi. Kwa muda mrefu niliweka hisia moyoni mwangu wa kuanguka na hata kukoseshwa haki. Ilinichukua miaka kadha kuelewa baraka ya kimiujiza ambayo kuanguka kwangu kuingia shule ya ndoto zangu ilikuwa. Katika shule ya pili nilikutana na watu muhimu. Faida za kuhusiana nao zilidhihirika kote katika upeo wa kazi yangu na hata leo ni muhimu katika maisha yangu na maisha ya familia yangu. Ninajua sasa kuwa, hata katika umri huu mdogo, Bwana alikuwa anaongoza hatua zangu na ubashiri wa jukumu ambalo angeniuliza kutimiza baadaye maishani mwangu.

Ndugu na dada zangu, baada ya kufanya yote unayoweza, ikiwa vitu havitakuwa vile ulitumaini au kutarajia, kuwa tayari kukubali mapenzi ya Baba yako wa Mbinguni. Tunajua kuwa hatatuweka katika kitu chochote ambacho hatimaye hakitakuwa chema kwetu. Sikiliza sauti hiyo ya kutuliza inayonong’oneza masikioni mwetu, “mwili wote wako mikononi mwangu; tulieni na jueni kuwa Mimi ni Mungu,” (M&M 101:16).

Hivi majuzi niliona filamu ya kugusa iliyofuatilia historia ya kampuni za mikokoteni za Willie na Martin. Mnamo Mei 1856, vikundi viwili vilivyofuatana vikiwa na zaidi ya Watakatifu elfu moja viliondoka Uingereza kuhamia Utah. Walipofika miezi sita baadaye, katika Salt Lake Valley katika mwisho wa safari yao yenye mashaka, zaidi ya 200 kati yao walikuwa hawajulikani waliko. Wengi wao walikuwa wamekufa kutokana na maradhi, njaa na kuchoka njiani wakielekea mahali walipoita “Sayuni.”

Mmoja wa watangulizi aliyeonyeshwa katika filamu alinivutia sana. Alijaza kampuni yake kwa vichekesho na shauku. Alikuwa, hata hivyo, si wa kawaida sana wa watangulizi. Mtu mdogo na, aliyekuwa mwenye ulemavu sana, alikuwa mwujiza mwenyewe! Nilijifunza huyu mtangulizi shujaa alikuwa Robert Pierce wa Cheltenham, Uingereza .

Mmoja wa wasafiri wenzi wake alimweleza kama “mmoja wa vilemavu kupita kiasi zaidi niliwahi kuona kama msafiri. Miguu yake ilikuwa imelemaa, na mwili wake umekunjana vibaya, lakini alikuwa mwenye nguvu katika imani. Aliweza kujisukuma kwa upesi wa kushangaza kwa kutumia magongo.” 11

Siku moja, Robert Pierce alifuata njia isiyo sahihi na kupotea kwa kampuni. Wanaume kadha walitoka kwenda kumtafuta, na hatimaye kumpata katika hali isiyofurahisha. Ninanukuu maneno yao:

“Kwa hofu yetu tuliona karibu na mti mbwa mwitu wawili wakizungukazunguka na tai nusu dazani wakizunguka mtini wakingoja aache kulia kwake na kuashiria kwa magongo yake ili kumshambulia na kumrarua katika hali yake ya kufinyiliwa chini ya mizizi ya mti ule. …

Tulifika kwa wakati kumwokoa kutoka kwa hatima yake, tukamtoa na kumweka kwenye mkokoteni tuliokuwa tumeleta, tukamweka katika hali ya kurudi kwenda kambini.”

Na sasa, umaizi katika sifa ya ucheshi ya Robert: “ Jinsi gani, jamaa huyu maskini alituomba kuwacha atembee kama alivyosema alikuwa ameahidi tulipoanza safari yetu kuwa tungetembea kila futi ya njia hadi Jiji la Salt Lake.”

Kisha, sehemu ya huzuni ya hadithi: “Hata hivyo, tulimwokoa kusafiri siku chache tu baadaye, wakati katika mwisho wa siku ya sita ya kutembea, shida zake ulimwenguni zilifikia kikomo na alizikwa katika ufuo wa Mto wa Elkhorn” 12

Dada Jolene Allphin, aliyekusanya hadithi ya Robert Pierce, alisema kumhusu “Kwa kweli ni ajabu kwamba Robert Pierce alikuwa tayari amesafiri maili 600 kwa magongo yake kabla ya kushindwa na matatizo ya njia. Tamaa ya moyo wake ilikuwa kuwakusanya watakatifu katika Sayuni na kutokuwa mzigo kwa wasafiri wowote wenzake …Robert hakutaka usaidizi wowote au kufanyiwa tofauti na wengine.” 13

Ndugu and dada, nilijiuliza swali lifuatalo: kwa nini Mungu, ambaye alikuwa ameokoa kimiujiza maisha ya mtu huyu wa imani kuu kutoka kwa mbwa mwitu na tai, akakubali afariki katika upande wa barabara siku chache tu baadaye.

Kufa kwake kulikuwa kwa utulivu mkubwa. Katika filamu, anasema kwa kifupi kabla ya mwisho:

“Wamisionari waliniambia mimi ni muhimu na siku moja nitakuwa bora zaidi!  …

“Kila mara nilitamani mwili wenye nguvu. Sasa, nitaupata. Mkifika Sayuni, nifikirieni”14

Kuhusiana na Robert pierce, ninafikiri maneno ya waraka wa Paulo kwa Waebrania:

“Hawa wote wakafa katika imani, wasijazipokea zile ahadi, bali wakaziona tokea mbali na kuzishangilia, na kukiri kwamba walikuwa wageni, na wasafiri juu ya nchi.

“… hao wasemao maneno kama hayo waonyesha wazi kwamba wanatafuta nchi. …

“Lakini sasa waitamani nchi iliyo bora, yaani, ya mbinguni” (Waebrania 11:13–14, 16).

Mwishowe, Robert Pierce alitambua kuwa kudura yake hatimaye ilikuwa Ufalme wa Mungu wala haikuwa Bonde la Salt Lake.

Ndivyo ilivyo kwetu sote. Ahadi za Bwana zinatuhakikishia kudura yetu. Mpangilio kwa kila mmoja wetu ni tofauti kulingana na ubashiri wa Mungu. Hali zetu zinaweza kubadilika, matukio yasiyotarajiwa yanaweza kutokea, changamoto zinaweza kutokea, lakini ahadi za Mungu kwetu zimehakikishwa kupitia kwa uaminifu wetu.

Dada Anne C. Pingree alieleza vizuri kuwa muktasari kinachomaanisha kuwa na imani katika ahadi za Mungu. Alianza kwa kumnukuu Mzee Bruce R . McConkie ifuatavyo:

‘“ Imani katika hali yake ya ukamilifu na safi huhitaji hakikisho lisilotikisika na …amini kamilifu kuwa [Mungu] atasikia kilio chetu na kutupa maombezi yetu’ kwa wakati Wake unaofaa. Kuamini kuwa sisi pia tunaweza ‘kusimama imara katika imani’ leo na kesho”

Kisha akaendelea:

“Haijalishi tunapoishi au hali zetu za kibinafsi. Kila siku, kuishi kwetu kwa haki kunaweza kudhihirisha imani katika Yesu Kristo inayoona kupita maumivu ya moyoni duniani, kuvunjika moyo, na ahadi zisizotimizwa. Ni kitu kitukufu kuwa na imani inayotuwezehsa kutazamia siku hiyo “wakati yote yaliyoahidiwa, watakatifu watapewa’” 15

Ndugu na dada, hali ya maisha yangu hivi leo ni, dhahiri, tofauti na kile nilichokuwa nimepanga nikiwa na umri wenu. Hata hivyo siamini kama nimewahi kufurahi kuliko sasa. Kama mtu angenipa nilipokuwa na umri wa miaka 20 masimulizi ya maisha yangu hadi sasa, nafikiri ningweka sahihi kwenye mstari bila kusita!

Siku Zenu za Usoni ni Angavu kama Imani Yenu

Ninataka kuzungumza kwa niaba ya Valerie nami. Ninapotafakari mkondo wa maisha yetu ndipo ninapoamini zaidi kuwa kilicholeta tofauti ni kuwa katika ujana wetu tulishiriki ono sawa la uzima wa milele. Tulitaka kuanzisha familia ya milele. Tulijua kwa nini tulikuwa ulimwenguni na madhumuni yetu ya milele. Tulijua kuwa Mungu alitupenda na kuwa tulikuwa na thamani kubwa machoni Mwake. Tulikuwa na hakika kuwa angejibu maombi yetu kwa njia Yake na kwa wakati ulioonekana bora Kwake. Sijui kama tulikuwa tayari kukubali matakwa Yake katika vitu vyote, kwa sababu hilo lilikuwa jambo tulilojifunza---na tunaendelea kujifunza. Lakini tulitaka kufanya kadiri ya uwezo wetu kumfuata na kujitenga kwa ajili Yake.

Ninashuhudia, pamoja na Rais Monson, kuwa, “siku zenu za usoni zinaangaza kama imani yenu” Furaha yenu inategemea sana kanuni utakayochagua kufuata kuliko hali za nje za maisha yenu. Kuwa mwaminifu kwa kanuni hizi. Mungu anakujua na anakupenda. Ukiishi katika uwiano na mpango Wake wa milele na ukiwa na imani katika ahadi Zake, basi siku zenu za usoni zitaangaza!

Mna ndoto na malengo? Hivyo ni vyema! Fanya kazi na moyo wako wote ili kuyatimiza. Kisha, mwachie Bwana kufanya kilichobaki. Atakuongoza pale ambapo huwezi kujiongoza; atakufanya uwe kile hauwezijifanya mwenyewe kuwa.

Katika nyakati zote, kubali mpenzi Yake. Kuwa tayari kwenda anapokuuliza kwenda, na kufanya kile anachokuuliza kufanya. Kuwa waume ama wake ambao Yeye anawalea kuwa.

Ninaomba kuwa mtahisi upendo wa Baba yetu wa Mbinguni katika maisha yenu, kwamba mtajua jinsi ya kujiamini kama anavyowaamini. Ninaomba kuwa daima mtakuwa waaminifu, nyakati zote na katika kila mahali. Ninadhihirisha upendo wangu na kuvutiwa kwangu na heshima ya kina kwa mifano na nguvu mlio kwa ulimwengu mzima.

Ninashuhudia kuwa maisha haya ni wakati wa ajabu wa milele. Tuko hapa kwa lengo tukufu, lile la kujitayarisha kukutana na Mungu. Mwanawe Yesu Kristo anaishi, na Upatanisho Wake ni karama isiyo na kifani ya upendo unaofungua lango kwa furaha ya milele. Kanisa la Yesu Kristo linadumu tena ulimwenguni katika hali kamilifu, na Nabii wa Mungu yu kichwani mwake. Ni shangwe ya ajabu na taadhima kuwa wa Kanisa hili. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Thomas S. Monson, “Welcome to Conference,” Ensign or Liahona, Nov. 2012, 4–5.

  2. Dieter F. Uchtdorf, “Of Regrets and Resolutions,” Ensign or Liahona, Nov. 2012, 23.

  3. Dieter F. Uchtdorf, “Forget Me Not,” Ensign or Liahona, Nov. 2011, 122–23.

  4. Ona Pindar (ca. 522–443 B.C.), Pyth. 2.72.

  5. L‘âge de raison or With Love … from the Age of Reason, directed by Yann Samuell (France, 2010; USA, 2011), motion picture.

  6. “Souviens-toi,” Cantiques (1993), no. 179.

  7. Discourses of Brigham Young, sel. John A. Widtsoe (1954), 269.

  8. The Lion King, directed by Rob Minkoff and Roger Allers (1994; Walt Disney Studios Home Entertainment, 2011), DVD.

  9. Thomas S. Monson, “Be of Good Cheer,” Ensign or Liahona, May 2009, 92.

  10. Winston Churchill, imedondolewa katika John Charmley, Churchill: The End of Glory, A Political Biography (1993), 20.

  11. John William Southwell, imedondolewa katika Jolene S. Allphin, Tell My Story, Too, 8th ed. (2012), 287.

  12. Southwell, katika Tell My Story, Too, 287.

  13. Allphin, Tell My Story, Too, 288.

  14. 17 Miracles, directed by T. C. Christensen (2011; EXCEL Entertainment and Remember Films, 2011), DVD.

  15. Anne C. Pingree, “Seeing the Promises Afar Off,” Ensign or Liahona, Nov. 2003, 14–15.

© 2012 by Intellectual Reserve, Inc. All rights reserved. Kiingereza kiliidhinishwa: 5/12. Tafsiri iliidhinishwa: 5/12. Tafsiri ya We Are the Architects of Our Own Happiness. Language. Swahili PD50039056 743