Mikutano ya Ibada ya Ulimwenguni Kote
Chochote Ulicho, Tenda Vyema Nafasi Yako: Epuka Kuvalia Barakoa Ambayo Inaficha Utambulisho


Chochote Ulicho, Tenda Vyema Nafasi Yako: Epuka Kuvalia Barakoa Ambayo Inaficha Utambulisho

Ibada ya MEK kwa Vijana Wazima• March 4, 2012 • Brigham Young University–Idaho

Nafurahia kuwa na fursa ya kuongea nanyi vijana wazima. Nawaletea ninyi upendo na salamu kutoka kwa Urais wa Kwanza na Jamii ya wale Kumi na Wawili. Ni ajabu sana kuwa katika kituo cha mkutano cha BYU-Idaho. Katika macho ya akili yangu naweza kuwaona katika maeneo mengi kote ulimwenguni.

Nilipokuwa wa umri wenu, Rais David  O. McKay alikuwa ndiye nabii. Rais McKay alihudumu kama Rais wa Kanisa kutoka 1951 hadi 1970 ndipo mimi nilifikia miaka 30. Daima kuna kitu cha kipekee sana kuhusu nabii ambaye anahudumu wakati wewe ni kijana mzima. Nilimpenda na kumstahi Rais McKay. Yeye kila mara alieleza tukio la kweli lililotokea wakati alipokuwa akihudumu kama misionari katika Skoti. Yeye alikuwa anahisi kutamani nyumbani baada ya kuwa katika misheni kwa muda mfupi tu na alitumia masaa machache kuzuru Kasri ya Stirling iliyokuwa karibu nao. Wakati yeye na mwenzi wake waliporudi kutoka kuzuru Kasri, walipita jumba ambalo jiwe juu ya mlango wake lilikuwa limechongwa maandishi ya dondoo kwa kawaida inahusishwa Shakespeare ambayo yalisema: Chochote Ulicho, Tenda Vyema Nafasi Yako.

Akikumbuka uzoefu huu katika hotuba yake mnamo 1957, Rais McKay alielezea: “Nilijisemeza mwenyewe, au Roho ndani yako, Wewe ni mshiriki wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Zaidi ya hivyo, wewe ni mwakilishi wa Bwana Yesu Kristo. Ulikubali jukumu la kuwakilisha Kanisa.’ Kisha nikafikiria [kuhusu] kile tulikuwa tumefanya mchana huo. Tulikuwa tumefanya ziara, tulikuwa tumepata mafunzo na maelezo ya historia, ni kweli, na nilikuwa nimechangamshwa na haya …. Hata hivyo, hayo hayakuwa kazi ya umisionari …. Nikakubali ujumbe niliopatiwa katika hilo jiwe, na kutoka wakati huo nilijaribu kutenda nafasi yangu kama sehemu ya wamisionari katika Skoti.”1

Ujumbe huu --- Chochote Ulicho, Tenda Vyema Nafasi Yako --- ulikuwa muhimu sana na ukawa na msukumo kwa Mzee McKay hata akautumia kwa maongozi kwa maisha yake yote. Alitambua kwamba jukumu lolote lile alilonalo, yeye atafanya kwa uwezo wake wote.

Wakati Mzee David B. Haight alipokuwa rais wa misheni katika Skoti, alitafuta yale maandishi kwenye jiwe halisi na alitengeneza nakala ambayo leo hii iko katika kituo cha mafunzo ya umisionari katika Provo, Utah. Wengi wenu mmeshaona dondoo hii na kutafakari umuhimu wa ujumbe wake. Mzee Russell M. Nelson alisisitiza ujumbe huu majuzi katika maadhimisho ya miaka 50 ya Kituo cha Provo cha Mafunzo ya Umisionari.

Nilipotafakari juu ya kile mlicho, hisia zimenijia kwamba kuna uwezekano hamfahamu vyema umuhimu wa kizazi chenu. Jamii kwa jumla imepeana nembo kwa vizazi tofauti ambavyo vi hai leo. Wazee miongoni mwetu Marekani na katika nchi zingine tumepewa nembo ya “Kizazi Kikuu” kwa sababu ya kile walichovumilia katika Mdororo Mkuu wa Kiuchumi duniani kote wa miaka ya 1930 na kisha kufanikiwa katika Vita vya Dunia vya  II na yaliyofuata katika kujenga ulimwengu bora. Idadi fulani ya Ndugu wazee wa Kanisa walishiriki katika matukio haya. Rais Thomas S.Monson alikuwa katika Jeshi la Wanamaji wa Marekani; Rais Boyd K. Packer alihudumu katika Jeshi la Angani la Marekani; Mzee L. Tom Perry alikuwa Mwanamaji wa Marekani. Nitashiriki nanyi baadaye uzoefu fulani waliopata na masomo waliojifunza na kufunza.

Kizazi chenu, kilizaliwa miaka ya 1980 na miaka ya mapema -ya katikati- ya 1990 sasa kinajulikana kama “Kizazi cha Milenia.” Watoamaoni wana shaka kuhusu kile kizazi chenu kitatimiza. Naamini ninyi mna usuli na msingi wa kuwa kizazi bora zaidi, hasa katika kuendeleza mbele mpango wa Baba wa Mbinguni.

Kwa nini niseme hivyo? Kizazi chenu kimepata ufahamu wa mafundisho ya seminari na taasisi kuliko vizazi vilivyopita, na mmepata mafunzo bora kuliko kizazi chochote kuanzia Mafunzo ya Msingi, ukuhani na Msichana. Kwa ziada, takribani 375,000 kati yenu mmehudumu au mtahudumu kama wamisionari. Mnawakilisha zaidi ya theluthi moja ya wamisionari wote ambao wamehudumu katika kipindi hiki. Samuel Smith, mmisionari wa kwanza katika kipindi hiki alitawazwa kuwa mzee na kutengwa kama mmisionari mnamo Aprili 6, 1830, siku ile Kanisa lilipangwa. Kama mkitazama sana wamisionari wote ambao wamehudumu tangu wakati huo, ni yakustajabisha kwamba theluthi moja watakuwa wa umri wenu. Kwa kulinganisha wamisionari 76,000 tu au chini ya asilimia 8 walihudumu katika miaka 12 nilipokuwa katika ya umri wa miaka 18 hadi 30. Kati yenu wale ambao hamjapata nafasi ya kuhudumu misheni, mchango wenu hata hivyo unaweza kuwa muhimu. Karibu nusu ya Urais wa Kwanza na wale Kumi na Wawili hawakupata nafasi ya kuhumu misheni.

Epuka Kutenda Kinyume Kwa Kuvalia Barakoa

Katika kutazama uwezo mwingi wa mema ambayo mulionao, shaka zangu ni nini juu ya maisha yenu yajayo? Ni ushauri gani nitakaowapatia? Kwanza, kutakuwa na shinikizo kuu kwa kila mmoja wenu kutenda kinyume -- hata kuvalia barakoa -- na kuwa mtu ambaye haonyeshi kile mlicho au kile mnataka kuwa.

Majira ya joto yaliyopita Mzee L. Tom Perry pamoja na Michael Otterson,, 2katika nafasi zao katika uhusiano mwema ya umma walikutana na Abraham Foxman katika ofisi yake New York. Bw. Foxman ni mkurugezi wa kitaifa wa Kundi la Linalopiga Kuharibiana Sifa. Kazi yake ni kusitisha kuharibu sifa za watu Wayahudi. Yeye amejihusisha na kazi hii kwa karibu miaka 40. Tukio katika maisha yake lilimpelekea kwa huu msimamo ni la kustajabisha sana. Alizaliwa mwanzoni mwa Vita vya Dunia vya II. Wazazi wake, Joseph na Helen Foxman, wakikabiliwa na maangamizi dhidi ya Wayahudi, walimpeana Abraham kwa msichana Mpolishi, Mkatoliki kabla hawajaingia katika mtaa duni katika Vilna, Lithuania mnamo Septemba, 1941. Abraham alikuwa na umri wa miezi 13. Wazazi wake walinusurika vile vile na Maangamizi Makuu, lakini hawakukutana na Abraham hadi alipokuwa na miaka minne. Inakadiriwa kwamba watoto wa Wayahudi milioni 1.5 waliteketea katika moto wa Wanazi. Abraham alilindwa na msichana Mkatoliki ambaye alimpeleka kanisani kila Jumapili na kuficha utambulisho wake wa Uyahudi. 3Haishangazi kwamba Abraham Foxman ametumia maisha yake kupiga vita upingaji Semiti, chuki, ulokole, na ubaguzi.

Nimefanya kazi pamoja na Bw. Foxman mara nyingi mapema na nastajabia ujasiri wake na azimio lake. Katika mkutano wetu naye katika New York, nilimwuliza ushauri gani angetupatia sisi katika shughuli za majukumu yetu katika uhusiano mwema wa umma wa Kanisa. Alitafakari kwa dakika chache na kisha kuelezea umuhimu wa kuwatia moyo watu wasivalie barakoa. Alielezea kuhusu Ku Klu Klan. Ni kundi ambalo lilikuwa na ushawishi mkubwa sana na lilitisha sana Wamarekani wengi katika sehemu ya kwanza ya karne iliyopita. Kwa mjoho na barakoa za kufanana ambavyo ilikuwa ni vigumu kutambua washiriki, walichoma misalaba kwenye bustani za wale walikuwa wanalenga na kujipatia mamlaka kama walinzi wa maadili mema kama inavyosemeka. Miongoni mwa wale waliolengwa sana walikuwa ni Wamarekani Weusi, lakini Wakatoliki, Wayahudi, na wahamiaji pia walilengwa. Wale waliokuwa wakatili sana kati yao walijihusisha na kupiga kwa mjeledi, dhuluma za kimwili, na hata mauaji. Bw. Foxman alisema kwamba kiasi kidogo cha Ku Klu Klan wangekuwa wadhalimu wa kijeshi katika utawala wa mabavu katika Ulaya ya miaka ya 1930, lakini wengi wao bila barakoa kwa kawaida walikuwa watu wa kawaida wakijumuisha wafanya biashara, na washiriki wa kanisa. Alisema kwamba kwa kuficha utambulisho wao na kuvalia barakoa kuliwawezesha wao kushiriki katika vitendo ambavyo kwa hali ya kawaida wangeepuka.4 Tabia zao ziliathiri vibaya jamii ya Wamarekani.

Ushauri wa Bw. Foxman ulikuwa ni tutilie mkazo umuhimu wa watu kuepuka barakoa ambazo zinaficha utambulisho wao halisi.

Katika historia yetu ya Kanisa, Nabii Joseph Smith, Emma, na mapacha wao wa miezi- 11, Joseph na Julia walikuwa katika Hiram, Ohio katika shamba la Johnson. Watoto wote wawili walikuwa wanaugua ukambi. Joseph na mwanawe mchanga walikuwa wanalala katika kitanda ya kukunjwa karibu na mlango wa mbele.

Ndugu Mark L. Staker amerekodi yote yaliyotokea:

Wakati wa usiku kikundi cha watu kilikuja kama kimejipaka rangi nyeusi usoni kiliingia kwa nguvu na kumburuta Nabii nje ambapo walimpiga na kumwagia lami yeye na Sidney Rigdon.

“Wakati Emma alimwona Joseph aliyepigwa na kumwagiwa lami, alizimia. …

“… Ingawaje Nabii alipoteza jino, kupata majeraha mabaya kwenye ubavu wake, kung’olewa nywele, na kuchomwa kwa asidi ya nitriki, yeye alihubiri mahubiri katika ibada kawaida ya Jumapili. Miongoni mwa Watakatifu waliokusanyika hapo karibu wanne wao walikuwa washiriki wa kundi ovu.” 5

Sehemu ya kusikitisha sana ya huu udhalimu ilikuwa ni kwamba Joseph mchanga alipatwa ubaridi wa usiku wakati baba yake alikua anaburutwa nje na akashikwa na homa kali ambayo ilimpelekea, yeye kufa siku chache baadaye.

Cha kushangaza pia kwamba wale walioshiriki katika kifo cha kishahidi cha Nabii Joseph Smith na kakake, Hyrum, walikuwa wamepaka nyuso zao rangi katika hali ya kuficha utambulisho wao halisi.6 Wale wanaoficha utambulisho wao na kuingia katika njama za siri ni wa kuleta shaka sana. Tunajifunza katika Kitabu cha Mormoni kwamba Lusiferi, “huvuruga watoto wa watu kuwa na makundi maovu ya siri na ya mauaji na kila aina ya kazi za siri za giza.” (2 Nefi 9:9; ona pia 3 Nefi 6:27–30).

Sasa mimi, sisemi kwamba yeyote kati yenu atashiriki katika mambo maovu ambayo nimeelezea. Naamini, katika siku zetu, ambapo kuwa umeficha utambulisho wako ni rahisi kanisa, kwamba kuna kanuni muhimu zinazohusiana na kutovalia barakoa na kuwa “mkweli kwa imani…. ambayo kwayo wafia kishahidi waliangamia.”7

Mojawapo wa ulinzi mkuu wenu dhidi ya kufanya chaguzi mbaya ni kutovalia barakoa yoyote ya kujificha. Kama umeshajipata wewe mwenyewe ukitaka kufanya hivyo, tafadhali jua hiyo ni ishara mbaya ya hatari na mojawapo wa vyombo vya adui vya kukufanya wewe kutenda jambo ambalo haufai kutenda. Mojawapo wa sababu tunawashauri wamisionari kuvalia kwa staha na wazee kunyolewa vizuri ni kwamba pasiweze kuwa na swala kama wao ni kina nani na vile wanafaa kutenda. Wengine watauliza: “Hiyo si ni ya juujuu? Sifikirii hivyo. Fikiria vile mavazi na upambaji unavoelezewa katika Kitabu cha Mormoni na nabii Moroni ambaye analinganisha hivyo na kiburi katika kuvalia “nguo nzuri sana.” Anahusisha kiburi kinachoonyeshwa kwa kuvalia “nguo nzuri sana” na “ugomvi, na mabishano, na dhuluma, na aina yote ya maovu” (Mormoni 8:36). Nina wasiwasi hasa kwamba katika siku zetu jinsi ya mavazi na upambaji unaweza kuwa ishara ya uasi au ukosefu wa kushikilia viwango vya maadili, kuathiri vibaya viwango vya maadili vya wengine.

Tenda Kulingana na Imani Yako ya Kweli

Ushauri wa pili nitakotoa ni: Tenda kulingana na imani yako ya kweli kwa kutumia wakati wako kwa yale mambo yanayojenga na kukuza silika yako na kukusaidia kuwa zaidi kama Kristo. Natumaini hakuna wenu atakayechukulia maisha kimsingi kama “starehe na michezo” bali kama wakati wa kujitayarisha kukutana na Mungu”(Alma 34:32).

Mfano wa ajabu wa kutenda nafasi yako na kutumia wakati vyema unaonyeshwa kwa tukio katika maisha ya Mzee L.  Tom Perry alipokuwa Marini, alikuwa sehemu ya jeshi la Marekani lililosimamia Japani mwisho wa Vita vya Dunia vya II. Mzee Perry alishiriki haya wakati aliandika ushuhuda maalumu wake wa Mwokozi, ambao unaonyeshwa katika kituo cha wageni chetu:

Taarifa ya Mzee Perry:

“Kulikuwa na uzoefu katika maisha yangu ambao kila mara umenikumbusha furaha inayotokana na kuuliza swali ‘Mwokozi angefanya nini katika hali hii?’

“Nilikuwa mmojawapo wa kundi la kwanza la Marini kushuka ufuoni katika Japani baada ya kuwekwa sahihi kwa mkataba wa amani baada Vita vya Dunia vya 11. Tulipokuwa tunaingia mji wa Nagasaki ulioharibiwa, ilikuwa ni mojawapo wa uzoefu wa kuhuzunisha katika maisha yangu. Sehemu kubwa ya mji ilikuwa imehangamizwa kabisa. Kati ya wale waliokuwa wamekufa walikuwa bado hawajazikwa. Kama majeshi simamizi, tulitengeneza makao makuu yetu na tukaanza kazi.

Hali ilikuwa mbaya sana, na wachache wetu walikuwa wanataka kufanya mengi. Tulimwendea kasisi wa diviseni yetu na kuomba ruhusa ya kusaidia kujenga makanisa ya Wakristo. Lakini kwa sababu ya vizuizi vya kiserikali wakati wa vita, haya makanisa yalikuwa yemewacha kutumika. Machache yao yalikuwa yameharibiwa vibaya. Kikundi chetu kilijitolea kurekebisha na kupaka kuta za makanisa haya wakati wa mapumziko yetu ili kwamba yaweze kuwa tayari kwa kutumika kwa ibada za kikristo tena.

“Hatukuwa na ufasaha wa lugha. Yale yote tungeweza kufanya ilikuwa ni kazi ya mkono ya kurekebisha majengo. Tuliwapata watumishi ambao walikuwa hawawezi kuhudumu wakati wa miaka ya vita na tukawatia moyo kurudi katika nimbari yao. Tulipata uzoefu wa ajabu sana na watu hawa walipokuwa walipata uzoefu wa uhuru tena kushiriki imani yao ya Kikristo.

“Tukio lilitokea tulipokuwa tukiondoka Nagasaki kurudi nyumbani ambalo nitalikumbuka daima. Tulipokuwa tukiabiri gari moshi ambao ingetupeleka hadi kwenye meli zetu kurudi nyumbani, tulidhiakiwa na kundi lingine la Marini. Walikuwa wamekuwa na marafiki wa kike pamoja nao wakiwapa kwaheri. Walituchekelea na kuonyesha kwamba sisi tulikosa burudani ya kuwa katika Japani. Tulikuwa tumepoteza wakati tukifanya kazi na kuweka plasta kuta.

“Walipokuwa katika kilele chao ya kutudhiaki, kwenye mwinuko karibu na stesheni ya gari moshi walikuja karibu Wakikristo Wajapani 200 wema kutoka kwa makanisa ambayo tulikuwa tumerekebisha, wakiimba ‘Mbele, Majeshi Wakristo.’ Walikuja na kutuzawadia. Kisha wakapanga foleni kandoni mwa mtambo wa reli. Na gari moshi lilipokuwa likiondoka, tulinyosha mkono yetu na kushika vidole vyao tulipokuwa tunaondoka. Hatukuweza kuongea: mihemko yetu ilikuwa ya nguvu sana. Lakini tulikuwa na shukrani kwamba tuliweza kusaidia kwa njia kidogo katika kurejesha tena Ukristo katika taifa baada ya vita.

Najua kwamba Mungu yu hai, Najua kwamba sisi sote ni watoto Wake na anatupenda sisi. Najua kwamba Yeye alituma Mwanawe ulimwenguni kuwa dhabihu ya upatanisho kwa wanadamu wote. Na wale ambao watakubali injili Yake na kumfuata watapokea uzima wa milele, kipawa kikuu kati ya vipawa vyote vya Mungu. Najua kwamba Yeye alisimamia Urejesho wa injili tena hapa ulimwenguni kupitia huduma ya Nabii Joseph Smith. Najua kwamba tu shangwe na furaha ya milele tutakayopata katika uzoefu wa maisha ya duniani itakuja kwa kumfuata Mwokozi, kutii sheria Zake, hata Yesu Kristo, amina.”8

Fikiria umuhimu wa askari wengine wanaotumia wakati wao wakirekebisha makanisa ya Kikristo ukilinganisha na askari wengine wanajihusisha katika vitendo vya upuuzi, upumbavu, au uovu. Tafadhali tafakari na uwe makini katika kuchagua jinsi ya kutumia wakati wako.

Kutazama video kunanikumbusha mojawapo wa kumbukumbu zangu za mapema wakati nilikuwa umri wa miaka mitano. Rais wa kigingi wetu alikuwa babake Mzee Perry. Mwishoni wa Vita vya Dunia vya Pili, aliwaita askari warejea wote wakae jukwani katika kanisa wakati mkutano wa sakramenti. Walikuja kama wamevalia mavazi bora ya kijeshi, na kila mmoja alitoa ushuhuda mfupi. Rais Perry alitokwa na majonzi wakati wanawe wawili, Mzee Perry na kaka yake mdogo Ted, walipokuwa walitoa ushuhuda wao. Kama kijana mdogo, ilikuwa ya kuinua na kuvutia kwangu. Sikumbuki walisema nini, lakini nakumbuka vile nilivyohisi.

Kama vile unaweza kuona kutoka kwa mfano wa Mzee Perry katika video hii, siongei juu ya kuvalia dini yako kama shirt au kuwa na imani kijuujuu. Hiyo inaweza kuwa ya kuaibisha kwako na Kanisa. Naongea juu ya ninyi kuwa kile mnafaa kuwa. Tulipokuwa tunashughulikia mwongozo wa, Hubiri Injili Yangu,tulihisi kwamba ungekuwa mwongozo wa kufaa maishani mwote kwa wamisionari wetu, na washiriki, hasa katika sura ya 6, “Nawezaje Kukuza Sifa Kama Kristo?” Mnapojaribu kutenda katika nafasi zenu na kutambua sifa zile mnataka kukuza, “mngeorodhesha na kujifunza ….mafungu ya maandiko ambayo yanafunza kuhusu hizo sifa,” “weka shabaha na fanya mipango kutumia hizi sifa katika maisha yenu” na “ombeni kwa Bwana awasaidie kukuza hizi sifa.”9 Katika kifanya hivyo, sharti usivalie barakoa na kuficha utambulisho wenu.

Wengine wenu mnaweza kuwa mmeingia katika tabia ambazo zimepita starehe na michezo. Hizo zinaweza kuhusiana na picha za ngono au aina zingine za uovu ni kutenda kinyume na wajibu wenu tofauti na kile kihalisi mnataka kuwa au mnafaa kuwa. Cha kushangaza ni kwamba karibu kila mmoja anayehusika na picha za ngono huchukua utambulisho bandia na kuficha kushiriki kwake. Wanaficha tabia zao ambazo wanajua ni za kulaumika na kuangamiza kwa wale wanaowapenda. Picha za ngono ni tauni ambayo ina madhara kwa hadhi ya kimaadili ya mtu mbele za Mungu, lakini inaweza pia kuvunja ndoa na familia na ina athari mbaya kwa jamii. Uraibu wa intaneti na picha za ngono yote yanavuruga familia.10 Mnaposonga mbele hata kwenye ndoa, sharti msivalie barakoa yoyote ambayo inaficha tabia zisizo nzuri ambazo zitakuwa na madhara kwa ndoa yenu.

Kwa wale ambao wameingia katika mtego wa hii tabia angamizi, tafadhali mjue kwamba mnaweza kutubu, na mnaweza kuponywa. Toba itahitaji kutangulia uponyaji. Uponyaji unaweza kuchukua muda mrefu. Askofu wako anaweza kukushauri jinsi unaweza kupokea usaidizi unaohitaji ili uponywe. Tumewauliza maaskofu kuwaelekeza kwa wale wanaoweza kuwasaidia vyema.

Picha za ngono na uasherati, kando, kuna tabia zengine zenye kudhuru ambazo ni sumu kwa jamii na zinachimba maadili kimsingi. Ni kawaida leo kuficha utambulisho wa mtu wakati anapoandika ya kuleta chuki, utunu, mawasiliano ya ulokole fiche katika mtandao. Wengine wanataja hivi kama kuwa kwa hasira. Mashirika mengine yanajaribu kuchuja maoni. Kwa mfano,New York Times hairuhusu maoni ambayo yana mshambulizi ya kibinafsi, machafu, matusi, ulaghai, yasiyoshimana, na UPAYUKAJI.  …

The Times pia inahimiza utumiaji wa majina halisi kwa sababu, ‘Tumegundua kwamba watu wanaotumia majina yao huendeleza mazungumzo yanayoelimisha, na ya staha.’”11

Mtume Paulo aliandika:

“Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema.

“Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu” (1 Wakorintho 15:33–34).

Ni wazi kwamba mazungumzo maovu si tu jambo la tabia mbaya, bali kama yanapotumiwa na wale ambao ni Watakatifu wa Siku za Mwisho, yanaweza kuwaathiri vibaya wale ambao hawana elimu juu ya Mungu au ushuhuda wa Mwokozi.

Matumizi yoyote ya Intaneti kudhulumu, kuvunja sifa, au kumfanya kuonekana vibaya ni ya kulaumiwa. Kile tunaona katika jamii ni kwamba kama watu wanavalia barakoa ya kujficha, kuna uwezekano mkubwa wa kujihusisha katika tabia, ambazo ni angamizi sana kwa mhadhara wa raia. Pia inavunja kanuni za kimsingi alizofunza Mwokozi.

Mojawapo wa jumbe za kimsingi za injili ya Yesu Kristo ambazo mmejifunza kutoka ujana wenu, ni, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”(Yohana 3:16; ona pia M&M 34:3). Mwokozi alieleza kwamba Yeye hakuja kuhukumu ulimwengu, bali kuokoa ulimwengu. Kisha akaelezea maana ya hukumu:

“Nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.

“Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa.

Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.”(Yohana 3:19–21; ona mistari ya 17–21).

Matendo ya haki hayahitaji kuvalia barakoa kuficha utambulisho. Naipenda hii taarifa halisi kutoka katika maisha ya Rais Thomas S Monson. Hakufikia miaka 18 mpaka mwisho wa Vita vya Dunia vya II. Kwa kweli vita katika Ulaya vilikuwa vimeisha, lakini vita katika Pasifiki viliendelea.

Yeye alijiunga na Jeshi la Wanamaji la Marekani na alipelekwa San Diego. Mnakumbuka taarifa katika mkutano mkuu uliopita. Katika Jumapili yake ya kwanza sajenti wa gawaribe alipigisha foleni kila mmoja kwenda kanisani. Aliwapeleka Wakatoliki sehemu moja, Wayahudi sehemu ingine, na akajaribu kuwapeleka waliobakia kwenye mkutano wa Kiprotestanti. Rais Monson alijua kwamba hakuwa Mkatoliki, Muyahudi, au Mprotestanti; yeye alikuwa Mmormoni. Yeye alikuwa na ujasiri wa kusimama hapo na alifurahia kujua kwamba kulikuwepo na washiriki waaminifu wengine waliosimama nyuma yake. Ingekuwa rahisi kwenda na kundi kubwa kwenye mkutano wa Kiprotestanti. Aliazimia kutambulika kwa kile aliachokuwa na kutenda nafasi yake vilivyo.12

Weka Shabala Zifaazo

Ushauri wangu wa tatu unahusiana na shabaha fulani unazofaa kuzifikiria. Karibu ya wakati ule ule kwamba Mzee Perry alikuwa Japani katika Marini, Rais Boyd K. Packer alihudumu katika Japani katika Jeshi la Angani mwisho wa Vita vya Dunia vya II.

Katika hutoba yake katika maadhimisho ya miaka 100 ya seminari ya Januari 22 mwaka huu, yeye alielezea kwamba hii ilikuwa miaka ukuaji mkuu katika maisha yake. 13 Katika mwaka wa 2004, niliambatana na Rais Packer na wengine hadi Japani. Alipata nafasi ya kurejelea nyayo zake na kutafakari juu ya uzoefu na maamuzi aliyofanya wakati huo. Alikariri machache juu ya hayo katika ujumbe wake kwa seminari. Kwa ruhusa yake nitashiriki nanyi mawazo na hisia zingine.

Rais Packer anaelezea juu ya uzoefu ambao ulitokea katika kisiwa kandoni mwa pwani ya Okinawa. Anachukulia haya kama kukwea kwake jangwani. Matayarisho yake ya kibinafsi na kukutana na washiriki wengine kulifanya imani kuwa ya kina katika mafundisho ya injili. Kile alichukuwa anakosa ilikuwa ni uthibitisho---elimu halisi ya kile alichopata tayari kuhisi kilikuwa ni kweli.

Mwandika wasifu wa Rais Packer kisha anaandika kile kilichotokea: “Kinyume cha amani ya uthibitisho aliotafuta, alikumbana ana kwa ana na jinamizi la vita dhidi ya wasio na hatia. Akitafuta faragha na wakati wa kutafakari, alikwea, siku moja, kuinuka juu ya bahari. Hapo alipata kijumba cha mkulima mdogo, shamba la viazi vitamu lililoachiliwa karibu na hapo. Na kilicholala kati ya mti uliyonyauka aliona miili ya mama na watoto wake wawili waliouawa. Picha hii ilimfanya kujawa ni huzuni mkubwa ukichanganika na hisia za upendo kwa familia yake mwenyewe na familia zingine zote.” 14

Baadaye alienda ndani ya handaki la muda ambapo alifikiria, akatafakari, na kuomba. Rais Packer katika kutazama nyumba juu ya tukio hili alielezea kile ninachoweza kukiita uzoefu wa uthibitisho wa kiroho. Alihisi maongozi ya kile anachofaa kufanya na maisha yake. Yeye, kwa kweli, hakujua kwamba angeitwa katika wito wa juu na mtakatifu anaoshikilia sasa. Maoni yake yalikuwa kwamba alitaka kuwa mwalimu, wa kutia mkazo mafundisho ya Mwokozi. Alifanya maamuzi kwamba ataishi maisha ya wema.

Ilimjia katika njia ya nguvu kwamba atapata mke mwema na pamoja watalea familia kubwa. Huyu mwanajeshi kijana alitambua uchaguzi wake wa ajira ungekuwa na mapato kidogo na mwenzi wake mpendwa angekuwa na kipaumbele hicho hicho na angekuwa tayari kuishi bila vitu fulani. Kwa wengine wenu wale wamekuwa na uhusiano wa karibu na Dada Donna Packer, alikuwa, na ni mwenzi kamili kwa Rais Packer. Hawakuwa na senti nyingi kuzidi, lakini hawakuhisi kupungukiwa kwa njia yoyote. Walilea watoto 10 na wakajitolea ilipohitajika. Sasa wana wajukuu 60 na vitukuu 79.

Naweza kukumbuka hisia laini nilizopata nilipojua kwamba alisikia aibu kama Kiongozi mwenye Mamlaka mpya kuambatana na mmoja wa Ndugu wakuu kwenye mkutano wa viongozi wa Kanisa kwa sababu hakuwa na mashati meupe ya kutosha ya kuvalia.

Nashiriki hii taarifa halisi nanyi kwa sababu mara nyingi shabaha zetu zinalenga wiwango vya dunia. Mambo muhimu kwa kweli ni rahisi sana kwa washiriki ambao wamepokea maagizo ya kuokoa. Kuweni wema. Jenga familia. Tafuta njia inayofaa ya kukidhi maisha. Hudumu kama unavyoitwa. Jitayarishe kukutana na Mungu.

Mwokozi alifunza kwamba, “uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo. ”(Luka 12:15). Kisha akatumia mithali:

“Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana:

“Na akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema, Nifanyeje, maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu?

“Na akasema, Nitafanya hivi: nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu.

“Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.

“Lakini Mungu akamwambia, Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?

“Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.”(Luka 12:16–21).

Jengeni Nchi Yenu na Jamii Pale Mnapoishi

Katika ziada kwa sifa, viwango, na maamuzi ya kibinafsi, kama mtakuwa kizazi mnachohitajika kuwa, mtajenga nchi yenu na jamii pale mnapoishi. Kizazi chenu, kama Kizazi Kikuu sana, kitahitajika kulinda wema na uhuru wa dini. Urithi wa Kiyahudi-Kikristo tuliorithi sio tu thamani, bali pia ni muhimu kwa mpango wa Baba yetu wa Mbinguni. Tunahitaji kuuhifadhi kwa vizazi vijavo. Tunahitaji kujiunga wa watu wema, ikijumuisha wale wa imani zote--- hasa wale wanaohisi kuwajibika kwa Mungu kwa tabia zao. Kuna watu ambao wanafahamu kwa nini tunaongea haya jioni hii “chochote ulicho, tenda vyema nafasi yako. “Ufanisi wa kuzidisha viwango na uhuru wa Kiyahudi-Kikristo utawatambulisha kizazi chenu kama kizazi kikuu sana kinavyohitajika kuwa.

Pamoja na changamoto zilizopo dunia leo, Urais wa Kwanza na Jamii ya wale Kumi na Wawili wangependelea hasa kwamba ninyi mshiriki vilivyo katika shughuli za kisiasa katika nchi mnayoishi. Kanisa halipendelei upande wowote katika ugombeaji wa kisiasa na wala haliungi mkono wagombea viti au vyama. Tunatarajia, hata hivyo, kwamba washiriki wetu watashiriki kikamilifu kuwaunga mkono wagombea viti na vyama wanavyochagua wenyewe kulingana na kanuni zile zitakazo linda serikali nzuri. Mafundisho yetu ni wazi: wale walio “waaminifu” na “wenye hekima” yapaswa watafutwe kwa bidii”(M&M 98:10). “wakati mwovu atawalapo watu huomboleza” (M&M 98:9) Hii inamaanisha kwamba kila mtu anafaa kihisi kuwa na wajibu wa kupiga kura.

Katika yale majimbo katika Marekani ambako kuna kongamano la kuchagua wagombezi mnafaa kujifahamisha na maswala na wagombezi na kishiriki kikamilifu. Kwa mfano, kongamano kwa vyama tofauti tofauti katika Utah na Idaho yatafanyika kuanzia wiki hii na kuendelea mpaka katikati ya Aprili. Kama utahudhuria, utakubaliwa kushiriki. Tunatumaini kwamba mtaangalia masaa ya kongamano kwa chama mnachopendelea and kisha mtahisi wajibu huu na kuhudhuria. Tunatumaini hii itakakuwa hivyo kwa raia wote, washiriki na wasiokuwa washiriki vile vile katika majimbo yote na nchi zote kule chaguzi zinafanyika. Gharama ya uhuru imekuwa juu sana na matokeo ya kutoshiriki ni makuu sana kwa raia wowote kuhisi wanaweza kupuuza majukumu yao.

Tafadhali jua kwamba tuna imani kuu kwenu. Uongozi wa Kanisa kwa haki wanaamini kwamba ninyi mnaweza kujenga ufalme kushinda vizazi vilivyopita. Sio tu kwa kuwa mna upendo na imani yetu tu, bali pia maombi na baraka zetu. Tunajua ufanisi wa kizazi chenu ni muhimu kwa kuendelea kuendeleza Kanisa na ukuaji wa ufalme. Tunaomba kwamba mtatenda vyema sehemu yenu: mnapoepuka kuvalia barakoa, mkitenda kulingana na utambulisho wenu halisi, wekeni shabaha zinazofaa, na mjenge nchi na jamii mnayoishi.

Ninahitimisha kwa ushuhuda wangu wa kibinafsi wa Urejesho wa injili kupitia wakala wa Nabii Joseph Smith. Joseph Smith alimwona Mungu Baba na Yesu Kristo. Baba yetu aliye Mbinguni ni baba wenye upendo, wenye mpango ambao utabariki kila mmoja wa watoto Wake. Yesu Kristo ni Mwokozi wetu na Upatanisho Wake ni tukio la upandaji mbegu katika historia yote. Roho Mtakatifu hutuhudumia sisi na kutoa ushuhuda juu ya Baba na Mwana. Kwa vitu hivi nashuhudia kama mmoja wa mashahidi wa Mwokozi, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. David O. McKay, katika Francis M. Gibbons, David O. McKay: Apostle to the World, Prophet of God (1986), 45; ona pia “Pres. McKay Speaks to Pioneer Stake Youth,” Church News, Sept. 21, 1957, 4.

  2. Michael Otterson ni Mkrugenzi Mkuu wa idara ya Kanisa ya Uhusiano Mwema wa Umma.

  3. Ona Joseph Foxman, In the Shadow of Death (2011), 10.

  4. Mkutano na Abraham Foxman katika ofisi yake katika New York City, New York Juni 14, 2011.

  5. Mark L. Staker, “Remembering Hiram, Ohio,” Ensign, Oct. 2002, 35, 37.

  6. OnaTeachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 24.

  7. “True to the Faith,” Hymns, no. 254.

  8. L. Tom Perry, transcribed from Special Witnesses of Christ (DVD, 2003).

  9. Preach My Gospel: A Guide to Missionary Service [2004], 123; see pages 115–26.

  10. Ona Elizabeth Stuart, “Internet Addiction Harming Marriage,” Deseret News, July 20, 2011, http://www.deseretnews.com/article/700164510/Internet-addiction-harming-marriage.html.

  11. Mark Brent, in “The Public Forum,” The Salt Lake Tribune, July 27, 2011, A16.

  12. Ona Thomas S. Monson, “Dare to Stand Alone,” Ensign, Nov. 2011, 61–62; see also Heidi Swinton, To the Rescue: The Biography of Thomas S. Monson (2010), 96–97.

  13. Ona Boyd K. Packer, “How to Survive in Enemy Territory,” Commemorating 100 Years of Seminary broadcast, Jan. 22, 2012, http://seminary.lds.org/history/centennial/eng/how-to-survive-in-enemy-territory/.

  14. Lucile C. Tate, Boyd K. Packer: A Watchman on the Tower (1995), 58–59.

© 2012 by Intellectual Reserve, Inc. All rights reserved. English approval: 2/12. Translation approval: 2/12. Translation of What E’er Thou Art, Act Well Thy Part: Avoid Wearing Masks That Hide Identity. Language. PD50039044 xxx

Chapisha