Vijana
Maandhari kutoka Mahali pa Juu
Kama kijana nilipata nafasi nyingi za kufanya ubatizo kwa wafu katika hekalu la San Diego California Ingawaje kila mara nilipata uzoefu mwema, safari moja hasa imekaa akilini mwangu.
Nilikuwa umri wa miaka 16, na dada mdogo alimefika umri wa miaka 12 na alikuwa anafanya safari yake ya kwanza ili kufanya ubatizo kwa wafu. Kwa vile ilikuwa ni safari yake ya kwanza, tuliamua kutembea tembea nje ya hekalu baada ya kumaliza.
Bustani ya hekalu ina sehemu kadha za ulingo kwenye upande mmoja, kwa hivyo tulienda hapo. Kwa sababu hekalu la San Diego lipo karibu na barabara kuu inayotumika sana, unaposimama kwenye ulingo, kwa kweli unatazama chini kwenye baraste.
Kusimama kwenye mahali pa juu pa bustani ya hekalu siku hiyo kulinipatia mtazamo mpya wa maisha. Nilikuwa nikitazama chini kwenye ulimwengu na magari yake yakipita kwa kasi, vituo vya ununuzi vilivyo jaa watu, alama za barabara zilifunikwa na michoro ya grafiti.
Ni wakati huu ndipo wazo liliponijia akilini: “Hautaki kuwa sehemu ya mambo hayo; sio kile maisha yanachohusu.” Kila mara nimekuwa nikifunzwa kwamba madhumuni ya maisha ni kurudi kuishi na Baba yetu wa Mbinguni na kuwa kama Yeye. Sikuhitaji mambo haya ya ulimwengu ili kutimiza hayo madhumuni.
Niligeuka na kutazama hekalu maridadi, na nikawa na shukrani kwa elimu ya injili na mtazamo inayonipatia. Nilijua kwamba katikati ya ulimwengu wa vurugu na udanganyifu, nilikuwa nimepata mahali pa juu pa kusimama.
Siku hiyo hekaluni nilimuahidi Baba yangu wa Mbinguni kwamba kila mara nitasimama upande Wake na sio wa ulimwengu. Bila kujali kile ulimwengu unachotutupia sisi, tunaweza kukishinda kwa kuweka maagano tuliofanya na kusimama mahali patakatifu (ona M&M 87:8).