Ujumbe wa Mwalimu Mtembelezi, Oktoba 2010
Hekalu Takatifu
Katika mahekalu, washiriki wa Kanisa ambao wanastahili wanaweza kushiriki katika maagizo matakatifu zaidi ya ukombozi ambao umefunuliwa mwanadamu.
Katika mahekalu tunaweza kushiriki katika maagizo takatifu zaidi ya ukombozi
Kuna sababu nyingi za mtu kutaka kuingia hekaluni. Hata umbo lake la nje unaonekana kuelezea dhamira zake kamili za kiroho. Hii ni dhahiri zaidi kwenye kuta zake. Juu ya mlango ya hekalu kuna sifa “Utakatifu kwa Bwana.”
Katika mahekalu, washiriki wa Kanisa ambao wanastahili wanaweza kushiriki katika maagizo takatifu zaidi ya ukombozi ambayo yamefunuliwa kwa mwanadamu. Pale, katika sherehe takatifu, mtu anaweza kusafishwa na kutakaswa na kufundishwa na kupata endaumenti na kufunganishwa. Na baada ya kupokea baraka hizi sisi wenyewe, tunaweza kushiriki kwa niaba ya wale waliokufa bila kupata fursa kama hio. Katika mahekalu ibada takatifu zinafanywa kwa waliohai na waliokufa vile vile.
Maagizo na sherehe za hekalu ni rahisi, nzuri, na takatifu
Usomi wa makini wa maandiko unaonyesha kwamba Bwana hakusema mambo yote kwa watu wote. Kulikuwa na masharti fulani yaliyowekwa ambayo yalihitajika kabla ya kupokea habari takatifu. Sherehe za hekalu zimo miongoni mwa mambo haya.
Hatujadili ibada za hekalu nje ya mahekalu. Haikukusudiwa kwamba ufahamu wa sherehe hizi za hekalu zitaruhusiwa tu kwa wachache ambao watahakikisha kwamba wengine hawatapata kufahamu. Ni kinyume sana, kwa hakika. Kwa juhudi kubwa tunahimiza kila nafsi kujistahilisha na kujitayarisha kwa uzoefu wa hekalu. Wale ambao wameenda hekaluni wamefundishwa vyema: Siku moja kila nafsi na kila nafsi aliyewahi kuishi atapata fursa ya kusikia injili na kukubali au kukataa kile ambacho hekalu inatoa. Ikiwa fursa hii imekataliwa, lawama ya kukataa lazima iwe juu ya mtu yule.
Maagizo na sherehe za hekalu ni rahisi. Ni nzuri. Ni takatifu. Zinawekwa siri ili zisipeanwe kwa wale wasiojitayarisha. Upekuzi sio matayarisho. Shauku ya kina sio matayarisho. Matayarisho kwa ibada ujumhuisha hatua za mwanzo: imani, toba, ubatizo, uthibitisho, ustaha, ukomavu na heshima inaostahili mmoja anayekuja akiwa amealikwa kama mgeni katika nyumba ya Bwana.
Wale wanaostahili wanaweza kuingia hekaluni
Wote wanaostahili na kuhitimu katika kila njia wanaweza kuingia hekaluni, pale waweze kutambulishwa kwa kanuni na ibada takatifu.
Mara unapohisi thamana ya baraka za hekalu na kwa utakatifu wa ibada zinazofanywa katika hekalu, utasita kushuku viwango vya juu vilivyowekwa na Bwana ili kuingia katika hekalu takatifu.
Ni lazima umiliki kibali cha sasa ili kuruhusiwa kwenye hekalu. Kibali hiki ni lazima kisahihishwe na maafisa wanaostahili wa Kanisa. Ni wale tu wanaostahili wanaopaswa kuenda hekaluni. Askofu wako au rais wa tawi lako ana jukumu la kufanya uchunguzi katika utakatifu wako wa kibinafsi kabla hujapokea maagizo yako ya hekalu. Haya mahojiano ni ya maana sana, kwani ni fursa ya kuchunguza pamoja na mtumishi wa Bwana aliyetawazwa mwelekeo wa maisha yako. Ikiwa kuna chochote kisicho sahihi katika maisha yako, askofu ataweza kukusaidia kukitatua. Kupitia kwa utaratibu huu, unaweza kuonyesha au kusaidiwa ili kuanzisha utakatifu wako ili kuingia hekaluni kwa idhinisho la Bwana.
Mahojiano kwa kibali cha hekalu hufanywa kwa faragha kati ya askofu na mshiriki wa Kanisa mhusika. Hapa mshiriki huulizwa maswali mahususi kuhusu tabia yake ya kibinafsi, utakatifu, na uaminifu kwa Kanisa na maafisa wake. Mtu ni lazima ahakikishe kwamba yeye ni msafi kimaadili na anatii Neno la Hekima, analipa fungu kamili la kumi, anaishi kulingana na mafundisho ya Kanisa, na hana uhusiano au huruma na vikundi potofu. Askofu ameelezwa kwamba uwekaji wa siri katika mambo haya na kila anayehojiwa ni ya muhimu sana.
Majibu yanayo kubalika kwa maswali ya askofu kwa kawaida yataimarisha utakatifu wa mtu ili kupokea kibali cha hekalu. Ikiwa mwombaji hatii amri au kuna kitu kinacho hitaji marekebisho katika maisha yake, itakuwa muhimu kudhihirisha toba kamili kabla ya kutolewa kwa kibali cha hekalu.
Baada ya askofu kufanya mahojiano kama hayo, rais wa kigingi vile vile atakuhoji kabla hujapokea maagizo yako ya hekalu.
Mafundisho katika hekalu ni ya kiishara
Kabla ya kuenda hekaluni kwa mara ya kwanza, au hata baada ya mara nyingi, inaweza kukusaidia kutambua kwamba mafundisho katika hekalu hufanywa njia ya ishara. Bwana, Mwalimu Mkuu, alipeana mengi ya mafundisho Yake kwa njia hii.
Hekalu ni shule kuu. Ni nyumba ya kujifunza. Katika mahekalu mazingira yamehifadhiwa ili yawe ya kufaa kwa mafundisho kwa mambo ambayo ni ya kiroho kamili. Marehemu Mzee John A. Widtsoe wa Jamii ya Wale Mitume Kumi na Wawili alikuwa rais aliye heshimika wa chuo kikuu na msomi mwenye sifa wa ulimwengu. Alikuwa na heshima kuu kwa kazi ya hekalu na alisema kwa wakati moja:
“Maagizo ya hekalu yanajumhisha mpango wote wa wokovu, kama ilivyofundishwa nyakati baada ya nyakati na viongozi wa Kanisa, na yanafafanua mambo yaliyo magumu kueleweka. Hakuna haja ya kupindua au kubadilisha mafundisho ya hekalu katika mpango mkuu wa wokovu. Ujalivu wa kifalsafa wa Endaumenti ni mojawapo ya mapingano makubwa kwa uhalisi wa maagizo ya hekalu. Zaidi, ukamilifu huu wa ukaguzi na ufafanuzi wa mpango wa Injili, unafanya ibada ya hekalu kuwa mojawapo wa mbinu bora zaidi aa kuchangamsha akili kuhusu utaratibu wote wa Injili” (“Temple Worship,” Utah Genealogical and Historical Magazine, Apr. 1921, 58).
Ikiwa utaenda hekaluni na kukumbuka kwamba mafundisho ni ya kiishara, hutawahi kuingia ndani ukiwa na roho halisi na ukose kuondoka ukiwa na ujuzi uliopanuka, ukihisi kuinuliwa kidogo zaidi, na elimu yako ikizidishwa kulingana na mambo ya kiroho. Mpango wa mafundisho ni bora. Una maongozi. Bwana mwenyewe, Mwalimu Mkuu, aliwafundisha wanafunzi Wake kila mara kwa mafumbo—njia ya kuongea ya kuwasilisha mambo kiishara ambayo pengine yanaweza kuwa magumu kueleweka.
Hekalu lenyewe linakuwa ishara. Ikiwa umeona mojawapo ya mahekalu usiku, likiangazwa kikamili, utajua jinsi inavyokuwa sehemu ya kuvutia. Nyumba ya Bwana, ikizingirwa kwa mwangaza, ikisimama nje ya giza, inakuwa ishara ya nguvu na ufunuo wa injili ya Yesu Kristo ikisimama kama mnara katika ulimwengu unaozama zaidi kwenye giza la kiroho.
Unapoingia hekaluni, unabadilisha mavazi yako ya kawaida na mavazi meupe ya hekaluni. Mabadilisho haya ya mavazi hufanyika katika chumba cha mavazi, ambako kila mtu amepewa kijisanduku na sehemu ya mavazi ambayo ni ya faragha. Hekaluni kanuni ya maadili imehifadhiwa kwa makini. Unapoweka mavazi yako ndani ya kijisanduku, unaacha wasiwasi na uwoga na shida hapo pamoja nazo. Unatoka nje ya eneo hili la mavazi ukivalia mavazi meupe, na utahisi umoja na hisia ya usawa, kwani wote walio pamoja nawe wamevalia mavazi sawa.
Ndoa ya hekalu ni agizo muhimu la hekalu
Wale wenu wanaotazamia ndoa ya hekalu wangetaka kujua kile kitakachotokea. Hatutaji maneno ya agizo ya ufunganishaji (ndoa) nje ya hekalu, bali tunaweza kuelezea chumba cha ufunganishaji kuwa kimerembeshwa kwa mapambo yake, tulivu na shwari kiroho, na kufanywa takatifu kwa kazi wakfu ambayo inafanywa humo ndani.
Kabla ya wachumba kuelekea kwenye altare kwa agizo la kufunganishwa, ni fursa ya msimamizi kupeana, na wachumba vijana kupokea, ushauri mwingine. Haya ni miongoni mwa mawazo ambayo wachumba vijana wanaweza kusikia wakati huo.
“Leo ni siku yenu ya harusi. Mmejumuika katika hisia ya ndoa yenu. Mahekalu yalijengwa kama madhabahu ya maagizo kama haya. Hatupo ulimwenguni. Mambo ya ulimwenguni hayahitajiki hapa na hayapaswi kuwa na ushawishi kwa kile tunachofanya hapa. Tumekuja kutoka ulimwenguni hadi ndani ya hekalu la Bwana. Hii inakuwa mojawapo ya siku muhimu sana ya maisha yenu.
“Mlizaliwa, kualikwa duniani, na wazazi waliotayarisha tabenakulo la dunia ili roho yenu iweze kuishi humo. Kila mmoja wenu amebatizwa. Ubatizo, agizo takatifu, ni ishara ya utakasaji, ishara ya kifo na ufufuko, ishara ya kuinuka katika upya wa uzima. Inajumhuisha toba na msamaha wa dhambi. Sakramenti ya Jioni ya Bwana ni uwekaji upya wa agano la ubatizo, na tunaweza, ikiwa tutaiishi, kuhifadhi msamaha wa dhambi zetu.
“Wewe, bwana harusi, ulitawazwa kwa ukuhani. Kwanza uliweka juu yenu Ukuhani wa Haruni na pengine umeendelea kupitia kwa afisi zote zilizomo—shemasi, mwalimu, na kuhani. Halafu siku iliwadia ulipopatikana kustahili Ukuhani wa Melkizedeki. Ukuhani huo, ukuhani wa mkuu, imeelezwa kama ukuhani kwa mfano mtukufu wa Mungu, au Ukuhani Mtakatifu kwa mfano wa Mwana wa Mungu(ona Alma 13:18; Helamani 8:18; Mafundisho na Maagano 107:2–4) Ulipatiwa ofisi katika ukuhani. Wewe sasa ni mzee.
“Kila mmoja wenu amepokea endaumenti yake. Katika endaumenti hio ulipokea manufaa ya uwezo wa kimilele. Lakini mambo haya yote, kwa njia moja, yalikuwa mwanzo na msingi kwa kuja kwenu kwa altare ili kufunganishwa kama mume na mke kwa muda na kwa milele yote. Sasa mnakuwa familia, mko huru kutenda katika uumbaji wa maisha, kupata fursa kupitia kwa maombi na kujitolea ili kuwaleta watoto ulimwenguni na kuwalea na kuwasaidia kwa usalama kwa maisha yao ya duniani; ili kuwaona wakija siku moja, jinsi mlivyokuja, ili kushiriki katika maagizo haya matakatifu ya hekalu.
“Mnakuja kwa hiari na mmeonekana kustahili. Kukubali kila mmoja katika agano la ndoa ni jukumu kubwa, moja ambalo linakuja pamoja na baraka zisizokuwa na kipimo.”
Nguvu ya ufunganisho huunganisha duniani na pia mbinguni
Ikiwa tunaweza kuelewa historia vile vile na mafundisho ya kazi ya hekalu, ni lazima tuelewe nguvu za ufunganisho ni nini. Ni lazima tuwaze kuelewa, angalau kwa kadri fulani, kwa nini funguo za mamlaka ya kutekeleza nguvu za ufunganisho ni muhimu.
“Wakati Yesu alipoenda katika pwani za Kaisaria-Filipi, aliwauliza wanafunzi wake akisema, Watu hunena mimi Mwana wa Adamu kuwa ni nani? …
“Naye Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.
“Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Baryona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni.
“Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda.
“Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni” (Mathayo 16:13, 16–19).
Petro ndiye aliyekuwa na funguo. Petro ndiye aliyekuwa na nguvu ya ufunganisho, yale mamlaka ambayo yana nguvu za kuunganisha au kufunganisha duniani au kufungua duniani na itakuwa vivyo hivyo hata mbinguni. Funguo hizo ni za Rais wa Kanisa—kwa nabii, mwonaji, na mfunuaji. Hizo nguvu takatifu za ufunganisho zimo Kanisani sasa. Hakuna kitu kinachochukuliwa kwa fikra takatifu na wale wanaojua umuhimu wa mamlaka haya. Hakuna kitu kinachowekwa kwa karibu vile. Kwa kulinganisha kuna watu wachache ambao wamekabidhiwa nguvu hizi za ufunganisho. Hakuna anayeweza kuzipata ila kutoka kwa nabii, mwonaji, na mfunuaji na Rais wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Nabii Joseph Smith alisema kwamba aliulizwa kila mara swali “‘Je, hatuwezi kuokolewa bila kupitia maagizo hayo yote, nk?’ Ningejibu, La, sio ujalivu wa uwokovu. Yesu alisema, ‘Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; maana naenda kuwaandalia mahali.’ [Ona Yohana 14:2.] Nyumba kama ilivyotumika hapa inapaswa kutafsiriwa ufalme; na mtu yeyote ambaye ameinuliwa kwa makao makubwa ni lazima azingatie amri ya selestia, na amri yote pia” (in History of the Church, 6:184).
Kazi ya Hekalu ni chimbuko la nguvu za kiroho
Mahekalu ni sehemu muhimu ya nguvu za kiroho za Kanisa. Ni lazima tutarajie kwamba adui atajaribu kutuingilia kama Kanisa na sisi binafsi tunavyotafuta kushiriki katika kazi hii takatifu na yenye kuvutia. Kazi ya hekalu huleta pingamizi nyingi kwani ndio asili ya nguvu nyingi za kiroho kwa Watakatifu wa Siku za Mwisho na kwa Kanisa nzima.
Kwenye uwekaji wakfu jiwe la msingi la Hekalu la Logan Utah, Rais George Q. Cannon, wakati huo wa Urais wa Kwanza, alitoa taarifa hii:
“Kila jiwe la msingi ambalo limewekwa kwa ajili ya Hekalu, na kila Hekalu lililokamilishwa kulingana na utaratibu ambao Bwana amefunua kwa Ukuhani Wake Mtakatifu, upunguza nguvu za Shetani duniani, na kuongeza nguvu za Mungu na Umungu, kusongeza mbingu kwa nguvu za ajabu kwa niaba yetu, kuleta kutuita juu yetu baraka za Miungu wa Milele, na wale wanaoishi uweponi mwao” (katika “The Logan Temple,” Millennial Star, Nov. 12, 1877, 743).
Wakati washiriki wa Kanisa wanapofadhaika au wakati maamuzi magumu yanaingia akilini mwao, ni jambo la kawaida kwao kwenda hekaluni. Ni mahali pazuri pa kupeleka haja zetu. Hekaluni tunaweza kupokea maono ya kiroho. Pale, wakati wa huduma ya hekalu, tuko “nje ya ulimwengu.”
Mara nyingine mawazo yetu husumbuliwa na matatizo na kuna mambo mengi yanayohitaji usikivu mara moja ambapo hatuwezi tu kufikiria wazi na kuona wazi. Kwenye hekalu vumbi la vurugu huonekana kutulia, ukungu na mawingu huonekana kuondoka, na tunaweza “kuona” mambo ambayo hatukuweza kuyaona mbeleni na kupata njia kupitia kwa shida zetu ambayo hatukujua mbeleni.
Bwana atatubariki tunavyofanya kazi ya maagizo takatifu ya mahekalu. Baraka hapo hazitakomea tu kwa huduma zetu za hekalu. Tutabarikiwa katika shughuli zetu zote.
Kazi zetu katika hekalu zinatukinga kwa ngao na ulinzi
Hakuna kazi iliyo na ulinzi zaidi kwa Kanisa hili kuliko kazi ya hekalu na utafiti wa historia ya familia unaisaidia. Hakuna inayoinua zaidi kiroho. Hakuna kazi inayotupatia nguvu zaidi. Hakuna kazi inayohitaji kanuni za juu za utakatifu.
Kazi zetu katika hekalu zinatukinga kwa ngao na ulinzi, kwote kibinafsi na kama watu.
Kwa hivyo njoo hekaluni—njoo na udai baraka zako. Hii ni kazi takatifu.
© 2010 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Ilichapishwa USA. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/09. Tafsiri iliidhinishwa: 6/09. Tafsiri ya Visiting Teaching Message, October 2010. Swahili. 09370 743