Hekalu— Mnara kwa Ulimwengu
Baraka muhimu na kuu zinazotokana na ushirika kwa Kanisa na zile baraka tunazopokea katika mahekalu ya Mungu.
Kina ndugu na dada wapendwa, ninaelekeza upendo na salamu zangu kwa kila mmoja wenu na kuomba kwamba Baba yetu wa Mbinguni ataongoza mawazo yangu na kuelekeza maneno yangu ninapowazungumzia siku ya leo.
Naomba nianze kwa kugusia jambo moja au mawili kuhusu jumbe mbili njema tulizopata asubuhi ya leo kutoka kwa Dada Allred na Askofu Burton kuhusu mpango wa ustawi wa Kanisa. Kama ilivyodhihirishwa, mwaka huu ni maadhimisho ya 75 ya mpango huu wa maongozi ambao umewabariki watu wengi. Ilikuwa ni fadhili yangu kuwafahamu kibinafsi baadhi ya wale walioanzisha kazi hii kuu—wanaume wa huruma na mtazamo wa mbele.
Kama vile Askofu na Dada Allred walivyosema, askofu wa kata anapewa jukumu la kuwatunza wale walio na mahitaji ambao wanaishi katika mipaka ya kata yake. Hiyo ilikuwa heshima yangu nilipokuwa nikiongoza kama askofu kijana huko Salt Lake katika kata iliyokuwa na washiriki 1080, wakiwepo wajane 84. Kulikuwa na wengi waliohitaji usaidizi. Ni shukrani ilioje niliyonayo kwa mpango wa ustawi wa Kanisa na kwa usaidizi wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama na jamii za ukuhani.
Ninatangaza kuwa mpango wa ustawi wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho umeongozwa na Mwenyezi Mungu.
Na sasa, ndugu na dada zangu, mkutano huu mkuu unaadhimisha miaka mitatu tangu nilipoidhinishwa kama Rais wa Kanisa. Bila shaka imekuwa miaka yenye kazi nyingi, iliyojaa changamoto nyingi na baraka zisizohesabika, Nafasi niliyopata kuweka wakfu na kuweka wakfu tena mahekalu imekuwa kati ya baraka zenye furaha na utakatifu, na ni kuhusu hekalu ndipo nazungumzia haya leo.
Wakati wa Mkutano Mkuu wa Oktoba mwaka wa 1902, Rais wa Kanisa Joseph F. Smith alidhihirisha katika hotuba yake ya ufunguzi matumaini kwamba siku moja tungekuwa na “mahekalu yakiwa yamejengwa katika sehemu mbalimbali duniani ambapo yanahitajika kwa nafuu kwa watu.”1
Katika miaka 150 ya Kwanza ya mpangilio kwa Kanisa, kutoka 1830 hadi 1980, mahekalu 21 yalijengwa, ikijumhishwa mahekalu ya Kirtland, Ohio na Nauvoo, Illinois. Ukilinganisha na miaka 30 tangu 1980, ambapo mahekalu 115 yalijengwa na kuwekwa wakfu pamoja na kutangazwa kwa mahekalu 3 mapya hapo jana, kuna mahekalu 26 zaidi ambayo yanajengwa au katika hali matayarisho ya ujenzi. Hesabu hizi zitaendelea kuongezeka.
Lengo ambalo Rais Joseph F. Smith alitumainia katika mwaka wa 1902 linaendelea kutimizika. Hamu yetu ni kufanya mahekalu kuweza kufikika kwa washiriki wetu.
Mojawapo ya mahekalu yanayojengwa kwa sasa liko Manaus, Brazil. Miaka mingi iliyopita nilisoma kuhusu kikundi cha zaidi ya washiriki mia moja ambao waliondoka Manaus, iliyoko katikati ya msitu wa mvua wa Amazoni ili kusafiri kwenda katika lililokuwa hekalu la karibu lililoko Sao Paulo, Brazil—karibu maili 2,500 (kilometa 4,000) kutoka Manaus. Washiriki hawa waaminifu walisafiri kwa mashua kwa siku nne, katika Mto Amazoni na vijito vyake. Baada ya kukamilisha usafiri wa majini, waliabiri mabasi yaliyokuwa yamejaa kwa siku zingine tatu za kusafiri—kwa njia zilizokuwa na matuta na chakula kichache sana na bila mahali starehe pa kulala. Baada ya siku saba mchana na usiku, walifika kwenye hekalu huko Sao Paulo, mahali maagizo ya uasili wa milele yalifanywa. Bila shaka safari yao ya kurudi ilikuwa ngumu vivyo hivyo. Hata hivyo, walikuwa wamepokea maagano na baraka za hekalu, ingawa vibeti vyao vilikuwa tupu, wao wenyewe walijazwa na roho wa hekalu na shukrani kwa baraka walizipokea.2 Na sasa, miaka mingi baadaye washiriki wetu huko Manaus wanafurahia wanapoona hekalu lao likijengwa katika kingo za Rio Negro. Hekalu huleta furaha kwa washiriki wetu watakatifu popote yanapojengwa.
Hadithi za dhabihu zilizofanywa ili kupokea baraka zinazopatikana tu hekaluni pa Mungu haziachi kunigusa na kuniletea hali ya shukrani kwa mara nyingine tena kwa ajili ya hekalu.
Hebu nishiriki nanyi hadithi ya Tihi na Taraina Mou Tham, na watoto wao 10. Familia nzima ilijiunga na Kanisa miaka ya mapema 1960 wakati wamisionari walipokuja kwenye kisiwa chao, kilichoko zaidi ya maili 100 (Km 160) kusini mwa Tahiti. Punde wakaanza kuwa na hamu ya baraka za kufunganishwa milele kwa familia katika hekalu.
Wakati huo, hekalu lililokuwa karibu kwa familia ya Mou Tham lilikuwa hekalu la Hamilton New Zealand ambalo lilikuwa karibu maili 2,500 (Km 4,000) kusini mashariki ambalo linafikiwa tu kwa safari ya gharama kubwa ya ndege. Familia kubwa ya Mou Tham ilipata riziki duni kwa shida sana katika shamba ndogo, hawakuwa na fedha za nauli ya ndege wala hawakuwa na nafasi ya ajira katika kisiwa chao cha Pacific. Kwa hivyo Ndugu Mou Tham na mwanawe Gerard walifanya uamuzi mgumu wa kuungana na mwana mwingine aliyekuwa akifanya kazi katika migodi ya nikeli ya New Caledonia, maili 3,000 (Km 4,800) kuelekea magharibi. Mwajiri aliwapa waajiri wake usafiri kwenda kwenye migodi lakini hakutoa usafiri wa kurejea nyumbani
Waume watatu wa Mou walifanya kazi kwa miaka minne katika migodi ya nikeli ya hali ya joto jingi, wakilima na kupakiza mawe mazito yenye madini. Ndugu Mou Tham alirejea kutembelea nyumbani mara moja kila mwaka, akiwaacha wanawe huko New Caledonia.
Baada ya miaka minne ya kazi ya sulubu, ndugu Mou Tham na wanawe waliweza kuweka akiba pesa za kutosha kupeleka familia hekaluni huko New Zealand. Wote wa familia walienda, ispokuwa binti mmoja. Walifunganishwa kwa wakati na milele, uzoefu wenye furaha na usioelezeka.
Ndugu Mou Tham alirejea kutoka hekaluni kwenda moja kwa moja hadi New Caledonia, ambako alifanya kazi kwa miaka miwili zaidi ili kulipia nauli ya binti mmoja aliyekuwa amekosa kwenda hekaluni nao—binti aliyekuwa ameolewa na mtoto na mmewe.
Katika miaka yao ya baadaye, Ndugu na dada Mou Tham walitamani kuhudumu hekaluni. Kwa wakati huo, hekalu la Papeete Tahiti lilikuwa limejengwa na kuwekwa wakfu, na Ndugu na Dada Mou Tham walihudumu misheni mbili huko.3
Ndugu na dada zangu, mahekalu ni zaidi ya mawe na simiti. Yamejaa imani na mfungo. Yamejengwa kwa majaribu na ushuhuda. Yametakaswa kwa kujitolea na huduma.
Hekalu la kwanza kujengwa katika kipindi hiki cha maongozi lilikuwa ni hekalu la Kirtland, Ohio. Watakatifu walikuwa masikini lakini Bwana aliamuru kuwa hekalu lijengwe, kwa hivyo wakalijenga. Mzee Heber C. Kimball aliandika haya kuhusu uzoefu huo, “Bwana tu anajua zile hali za umasikini mateso na matatizo tuliyopitia ili kuitimiza.”4 Kisha, baada ya yote yaliyokamilishwa kwa shida, watakatifu walilazimishwa kuondoka Ohio na kuacha hekalu lao walilopenda Hatimaye walipata kimbilio—na ingawa ilikuwa kwa muda—katika kingo za mto Misissippi katika jimbo la Illinois. Waliyaita makao yao Nauvoo, na kwa kuwa radhi kutoa yote waliyokuwa nayo tena na imani yao ikiwa imara, walijenga hekalu lingine kwa Mungu wao. Mateso yalizidi, hata hivyo, na hekalu likiwa halijakamilika kabisa, walifukuzwa tena kutoka nyumba zao kutafuta kimbilio jangwani.
Mapambano na kujitolea kulianza tena walipofanya kazi kwa miaka 40 kujenga Hekalu la Salt Lake, ambalo linasimama kwa utukufu kwenye eneo kusini tu kwa wale wetu sisi tulio hapa katika Jumba la Mikutano.
Kiwango fulani cha kujitolea kumehusishwa na ujenzi na kuhudhuria hekalu. Wasiohesabika ni wale waliofanya kazi na kushughulika ili kujipatia na familia zao baraka ambazo zinapatikana katika mahekalu ya Mungu.
Kwa nini wengi wako radhi kutoa sana ili kupokea baraka za hekalu? Kwa wale wanaoelewa baraka za milele zinazotokana na Hekalu wanajua kuwa hakuna kujitolea kulioko kukuu, hakuna gharama iliyo ghali wala mapambano yaliyo magumu ili kupokea baraka hizo. Hakuna kamwe maili nyingi sana za kusafiri, vizuizi vingi vya kushinda na shida nyingi ya kuvumilia. Wanaelewa kuwa maagizo ya wokovu yanayopokelewa katika hekalu siku moja yatatuwezesha kurejea kwa Baba yetu wa Mbinguni katika uhusiano wa kifamilia ya milele na kuimarishwa na baraka na nguvu kutoka juu zinastahili kila kujitolea na kila bidii.
Hivi leo wengi wetu hatuhitaji kupitia matatizo makubwa ili kuhudhuria hekalu. Asilimia themanini na tano ya ushirika wa Kanisa sasa huishi katika umbali wa maili 200 (Km 320) kutoka hekaluni, na kwa wengi wetu umbali huwa mdogo zaidi.
Ikiwa umehudhuria hekaluni kwa ajili yako, na ikiwa unaishi karibu na hekalu, kujitolea kwako kutakuwa ni kuweka wakati katika maisha yenu yenye shughuli nyingi ili kuhudhuria hekalu. Kuna mengi ya kufanywa katika mahekalu yetu kwa niaba ya wale wanaongojea upande ule wa pazia. Tunapowafanyia kazi, tutajua kwamba tumetimiza kile wasichoweza kujifanyia. Rais Joseph F. Smith katika tangazo kuu alisema, “kupitia kwa bidii yetu kwa niaba yao minyororo ya utumwa itaanguka kutoka kwao na giza iliyowazunguka itaondoka na mwangaza utaangaza kwao na watasikia katika dunia ya roho kuhusu kazi walizofanyiwa na watoto wao hapa na watafurahia nanyi katika kutenda kazi hizi.”5 Kina ndugu na dada zangu, kazi ni yetu kuifanya.
Katika familia yangu, baadhi ya uzoefu mtakatifu na wa thamani ulitokea tulipounganishwa pamoja katika hekalu na kufanya maagizo ya ufunganishaji kwa mababu zetu waliofariki.
Ikiwa hujaenda hekaluni au ikiwa umeenda lakini kwa wakati huu hustahili sifu ya hekaluni, hapana lengo lililo muhimu kwako kuliko kujitahidi kuwa wa kustahili kwenda hekaluni. Kujitolea kwako kunaweza kuwa kunaleta maisha yako katika uwiano na yale yanayohitajika ili kupokea sifu ya hekalu, labda kwa kuacha tabia za zamani ambazo zinaweza kukuzuia. Inaweza kuwa ni kuwa na imani na nidhamu ya kulipa fungu la kumi. Kwa vyovyote, hitimu kuingia katika hekalu la Mungu. Pata sifu ya hekalu na kuichukulia kuwa mali ya thamani, kwani ndio.
Hadi utakapoingia katika nyumba ya Bwana na kupokea baraka zote zinazokungojea huko, bado hujapokea kila kitu ambacho Kanisa hupeana. Baraka muhimu na tukufu zinazotokana na ushirika kwa Kanisa ni zile baraka tunazopokea katika mahekalu ya Mungu.
Na sasa, marafiki zangu wadogo mko kwenye miaka ya ujana, kila wakati, muwe na hekalu katika maono yenu. Usitende chochote kitakachokuzuia kuingia malango yake na kushiriki baraka takatifu na za milele huko. Ninawapongeza wale wenu ambao huenda hekaluni mara kwa mara kufanya ubatizo kwa ajili ya wafu, wakiamka masaa ya asubuhi sana ili kushiriki ubatizo kabla ya shule kuanza. Siwezi kufikiria njia bora zaidi ya kuanza siku.
Kwenu wazazi wa watoto wadogo, hebu nishiriki nanyi wasia wa hekima kutoka kwa Rais Spencer W. Kimball. Alisema, “Ingekuwa jambo bora ikiwa … wazazi wangekuwa na picha ya hekalu katika kila chumba ili [watoto wao] kutoka wakiwa wachanga wangeweza kutazama picha hiyo kila siku hadi itakapokuwa sehemu ya [maisha yao]. Wanapotimu umri ambao wanahitaji kufanya maamuzi muhimu [kuhusu kwenda hekaluni]’ itakuwa tayari imefanyika.6
Watoto wetu huimba katika mafundisho ya Msingi:
Ninawaomba muwafundishe watoto wenu kuhusu umuhimu wa hekalu.
Dunia inaweza kuwa yenye changamoto na mahali pagumu kuishi. Tunazungukwa wakati wote na yale yanayoturudisha chini. Wewe na mimi tunapoenda katika nyumba takatifu za Mungu, tunapokumbuka maagano tunayofanya naye, tutaweza hata zaidi kubeba kila mateso na kushinda kila majaribio. Katika mahali hapa pa takatifu tutapata amani; tutafanywa upya na kuimarishwa
Na sasa kina ndugu na dada zangu, hebu niseme kuhusu hekalu moja kabla ya kuhitimisha. Katika wakati usio mrefu ujao, wakati mahekalu mapya yanapojengwa ulimwenguni, moja litasimama katika mji uliojengwa miaka 2500 iliyopita. Nazungumza kuhusu hekalu ambalo sasa linajenjwa jijini Roma huko Italia.
Kila hekalu ni nyumba ya Mungu likitimiza majukumu na kwa baraka na maagizo yale yale. Helalu la Roma Italia, kwa njia ya kipekee limejenjwa katika mojawapo ya sehemu ya kihistoria, katika jiji ambapo mitume wa Kale Petro na Paulo walihubiri na kila mmoja wao kuuawa.
Oktoba iliyopita, tulipokutana katika sehemu ya kichungaji pembeni mwa mji wa Roma, ilikuwa nafasi yangu kutoa maombi ya kuweka wakfu tulipojitayarisha kuweka jiwe la msingi. Nilihisi ushawishi kumwalika Seneta wa Kiitaliani Lucio Malan na naibu wa meya wa jiji la Roma Giusseppe Ciardi kuwa kati ya wa kwanza kutupa kijiko cha mchanga Kila mmoja wao alikuwa sehemu ya uamuzi wa kuturuhusu kujenga hekalu katika jiji lao.
Mawingu yalikuwa yametanda lakini kulikuwa na joto, na ingawa kulionekana kama kungenyesha, hakuna zaidi ya tone au mawili yaliyoanguka. Wakati kwaya ya ajabu ilipoimba katika lugha ya Kiitaliani “The Spirit of God,” mtu alihisi kama mbingu na ulimwengu ziliungana katika wimbo mtukufu wa sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Machozi hayangeweza kuzuiwa.
Katika nyakati zijazo, watakatifu katika jiji hili la milele watapokea maagizo yenye asili ya milele katika nyumba takatifu ya Mungu.
Ninadhihirisha shukrani yangu kuu kwa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya hekalu linalojengwa sasa huko Roma na kwa ajili ya mahekalu yetu yote popote yalipo. Kila moja linasimama kama mnara kwa ulimwengu, dhihirisho la ushuhuda wetu kwa Mungu, Baba yetu wa Milele, yu hai na kwamba anataka kutubariki na kwa kweli kuwabariki wana na binti zake kwa vizazi vyote. Kila moja wa mahekalu yetu ni dhihirisho la ushuhuda wetu kwamba maisha baada ya kaburi ni yakini kama vile maisha hapa ulimwenguni. Nashuhudia hivyo.
Kina ndugu na dada zangu wapendwa hebu na tujitolee kwa vyovyote ili kuhudhuria hekalu na kupata roho wa hekaluni katika mioyo yetu na nyumbani mwetu. Acha tufuate nyayo za Bwana na Mwokozi wetu, Yesu Kristo, aliyetoa dhabihu kamilifu kwa ajili yetu, ili tuweze kupata uzima wa millele na kuinuliwa katika ufalme wa Baba yetu wa Mbinguni. Haya ni maombi yangu ya dhati, na ninayatoa katika jina la Mwokozi wetu Yesu Kristo Bwana, Amina.
© 2011 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa USA Kiingereza kiliidhinishwa: 6/10. Tafsiri iliidhinishwa: 6/10. Tafsiri ya First Presidency Message, May 2011. Swahili. 09765 743