Ujumbe wa Mwalimu Mtembelezi, Mei 2013
“Njooni kwangu”
Kwa maneno Yake na mfano Wake, Kristo ametuonyesha sisi jinsi ya kumjongelea Yeye.
Ninashukrani kuwa nanyi katika mkutano huu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Hili ni Kanisa Lake. Sisi tunajichukulia jina Lake tunapoingia ufalme Wake. Yeye ni Mungu, Muumba, na mkamilifu. Sisi ni wanadamu waliochini ya kifo na dhambi. Lakini katika upendo Wake kwetu na familia zetu, anatualika tuwe karibu Naye. Haya ndio maneno yake: “ Songeni karibu nami na mimi nitasongea karibu nanyi, nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata, ombeni, nanyi mtapewa, bisheni nanyi mtafunguliwa.”1
Katika msimu huu wa Pasaka tunakumbushwa ni kwa nini tunampenda Yeye na juu ya ahadi anayofanya na wafuasi wake waaminifu kuwa marafiki Zake wapendwa. Mwokozi alifanya ahadi hiyo na kutueleza jinsi, katika utumishi wetu Kwake, Yeye huja kwetu. Mfano mmoja ni katika ufunuo kwa Oliver Cowdery alipomtumikia Bwana pamoja na Nabii Joseph Smith katika kutafsiri Kitabu cha Mormoni: “Tazama, wewe ndiwe Oliver, na nimesema nawe kwa sababu ya matakwa yako; kwa hiyo yatunze maneno haya katika moyo wako. Uwe mwaminifu na mwenye juhudi katika kushika amri za Mungu, na mimi nitakuzungushia mikono ya upendo wangu.”2
Nilipitia furaha ya kumjia karibu Mwokozi na kuja Kwake karibu nami kupitia vitendo vidogo vya utiifu kwa amri.
Unaweza kuwa ulikuwa na matukio kama hayo. Inaweza kuwa ulipochagua kuhudhuria mkutano wa sakramenti. Ilikuwa kwangu Sabato nilipokuwa mdogo sana. Siku hizo tulipokea sakramenti wakati wa mkutano wa jioni. Kumbukumbu ya siku moja zaidi ya miaka 65 iliyopita, nilipotii amri kukusanyika na familia yangu na Watakatifu, bado inanivuta karibu zaidi na Mwokozi.
Kulikuwa na giza na baridi nje. Nakumbuka nikihisi mwangaza na joto kanisani jioni hio nikiwa na wazazi wangu. Tulishiriki sakramenti, ikiwa imesimamiwa na wenye Ukuhani ya Haruni, tukifanya agano na Baba wetu wa Milele kuwa daima tutamkumbuka Mwana Wake na kutii amri Zake.
Mwishoni mwa mkutano tuliimba nyimbo “Abide with Me; ’Tis Eventide,” na maneno ndani yake. “Ewe, Mwokozi, kaa usiku huu nami.”3
Nilihisi upendo wa Mwokozi na ukaribu Wake jioni hio. Na nilihisi faraja ya Roho Mtakatifu.
Nilitaka kuamsha tena hisia za upendo wa Mwokozi na ukaribu Wake niliyohisi wakati wa mkutano wa sakramenti katika ujana wangu. Hivyo basi nikatii amri nyingine. Nilipekua maandiko. Ndani yake, nilijua ningeweza kurudi tena kuwa na Roho Mtakatifu akinikubali kuhisi kile wanafunzi wa Bwana walihisi alipokuwa amejibu mwaliko wao kuja nyumbani kwao na kukaa nao.
Nilisoma kuhusu siku ya tatu baada ya Usulubisho Wake na mazishi. Wanawake waaminifu na wengine walikuja nao na kupata jiwe limetolewa kwenye kaburi na mwili Wake haukuwepo. Walikuwa wamekuja kwa sababu ya upendo wao Kwake ili waupake mafuta mwili Wake.
Malaika wawili walisimama hapo na kuwauliza ni kwa nini walikuwa wanaogopa, wakisema:
“Kwa nini mnatafuta aliye hai katika wafu?
“Hayupo hapa, amefufuka: kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa aliko Galilaya,
“Akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mkononi mwa wenye dhambi, na kusulubiwa, na kufufuka siku ya tatu”4
Katika injili ya Marko anaongezea maelekezo kutoka kwa malaika mmoja: “ Lakini endeni zenu, mwaambie wanafunzi Wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia.”5
Mitume na wanafunzi walikuwa wamekusanyika Yerusalemu. Kama vile sisi tungekuwa, walikuwa na wanaogopa na wakishangaa walipozungumza pamoja kuhusu kile kifo na habari ya ufufuo Wake ilimaanisha.
Wanafunzi wawili walitembea jioni hio kutoka Yerusalemu njiani kuelekea Emau. Kristo aliyefufuka alitokea utusitusi njiani na kutembea nao. Bwana aliyefufuka alikuwa amekuja kwao.
Kitabu cha Luka kinaturuhusu kutembea nao jioni hio:
“Ikawa katika kuzungumza na kuulizana kwao, Yesu mwenyewe alikaribia, akaandamana nao.
“Macho yao yakafumbwa wasimtambue.”
“Akawaambia, Ni maneno gani haya mnayosemezana hivi mnapotembea? Wakisimama wamekunja nyuso zao.
Akijibu mmoja wao, jina lake Kleopa, akamwambia, Je! Wewe peke yako mgeni katika Yerusalemu, hata huyajui yaliotukia humo siku hizi?6
Walimwambia kuhusu huzuni wao kwamba Yesu alikuwa amekufa wakati walikuwa wameamini kuwa Yeye angekuwa Mkombozi wa Israeli.
Lazima kuwe kulikuwa na upendo katika sauti ya Bwana aliyefufuka alipozungumza na wanafunzi hawa wawili wenye huzuni na kuomboleza:
“Akawaambia, Enyi msiofahamu, wenye mioyo mizito ya kuamini yote waliyoyasema manabii:
Je! Haikumpasa Kristo kupata mateso haya na kuingia katika utukufu wake?
“Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomuhusu yeye mwenyewe.7
Kisha kukaja wakati ambao umefurahisha moyo wangu tangu nilipokuwa kijana mdogo:
“Wakakaribia kule kijiji walichokuwa wakienda, naye alifanya kama anataka kuendelea mbele.
“Wakamshawishi wakisema, Kaa pamoja nasi, kwa kuwa kumekuchwa, na mchana unakwisha. Akaingia ndani kukaa nao.”8
Mwokozi alikubali usiku huo mwaliko kuingi nyumbani kwa wanafunzi Wake karibu na kijiji cha Emau
Aliketi mezani nao. Akachukua mkate, akaubariki, akaumega,na kuwapa. Macho yao yakafumbuliwa ili basi wakamjua Yeye. Kisha akapotea kutoka uwepo wao. Luka alituandikia hisia za wanafunzi hao waliobarikiwa: “Wakaambiana, Je! Mioyo yetu halikuwaka ndani yetu hapo alipokuwa akisema nasi njiani, na kutufunulia maandiko?”9
Wakati huo huo, wanafunzi hao wawili walikimbia kurudi Yerusalemu na kuwaambia Mitume wale kumi na moja kile kilochokuwa kimewatendekea. Katika muda huo Mwokozi akatokea tena.
Alirejelea unabii wa misheni Wake kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watoto wote wa Baba Yake na kuvunja pingu za kifo.
“Akawaambia, Ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu:
“Na kwamba mataifa yote yatahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu.
“Nanyi ndiyo mashahidi wa haya.”10
Maneno ya Mwokozi ni ya kweli kwetu kama vile yalivyokuwa kwa wanafunzi wake siku hizo. Sisi ni mashahidi wa mambo haya. Na jukumu tukufu ambalo tulikubali tulipobatizwa katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho liliwekwa wazi kwa ajili yetu na nabii Alma karne nyingi zilizopita katika maji ya Mormoni:
“Na ikawa kwamba aliwaambia: tazameni, hapa kuna maji ya Mormoni (kwani hivi ndivyo yaliitwa) na sasa, kwa vile mnatamani kujiunga na zizi la Mungu, na kuitwa watu wake, na mko radhi kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine, ili iwe miepesi;
Ndio, na mko tayari kuomboleza na wale wanaoomboleza; ndio, na kufariji wale ambao wanahitaji kufarijiwa, na kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote mlipo, hata hadi kifo, ili muweze kukombolewa na Mungu, na kuhesabiwa pamoja na wale wa ufufuko wa kwanza, ili mpokee uzima wa milele—
Sasa ninawaambia, ikiwa hilo ndilo pendo la mioyo yenu, ni nini mnacho dhidi ya kubatizwa kwa jina la Bwana, kama ushahidi mbele yake kwamba mmeingia kwenye agano na yeye, kwamba mtamtumikia na kushika amri zake, ili awateremshie Roho yake juu yenu zaidi?
“Na sasa wakati watu waliposikia haya maneno, walipiga makofi kwa shangwe, na wakasema kwa nguvu: Hili ndilo pendo la mioyo yetu.”11
Sisi tuko chini ya agano kuwainua wanaohitaji na kuwa mashahidi wa Mwokozi almradi tunaishi
Tutaweza tu kufanya hivyo bila kushindwa tunapohisi upendo kwa Mwokozi na upendo Wake kwetu. Tunapokuwa waaminifu kwa ahadi tulizofanya, tutahisi upendo wetu Kwake. Ukiongezeka kwa sababu tutahisi nguvu Zake na kuja Kwake karibu nasi katika huduma Yake.
Rais Thomas S. Monson ametukumbusha mara kwa mara kuhusu ahadi ya Bwana kwa wanafunzi Wake waaminifu: “ Na yeyote awapokeaye ninyi, hapo nitakuwepo pia, kwani nitakwenda mbele ya uso wenu. Nitakuwa mkononi mwenu wa kulia na wa kushoto, na Roho wangu atakuwa mioyoni mwenu, na malaika wangu watawazingira, ili kuwabeba juu.”12
Kuna njia nyingine wewe na mimi tumemhisi Yeye akija karibu nasi. Tunapotoa huduma ya kujitolea Kwake, Yeye huja karibu na wale tunaowapenda katika familia zetu. Kila wakati nimeitwa katika huduma ya Bwana kuhamisha ama kuacha familia yangu, mimi nikaona kuwa Bwana alikuwa akibariki mke wangu na watoto. Aliwatayarisha watumishi wapendwa na fursa ya kuvuta familia yangu karibu Naye.
Umehisi baraka hio hio katika maisha yako. Wengi wenu mnao wapendwa wanaopotea kutoka kwenye njia ya maisha ya milele. Mnashangaa kile zaidi mnachoweza kufanya ili kuwarejesha. Mnaweza kumtegemea Bwana kuenda karibu nao mnapomtumikia Yeye kwa amani.
Unakumbuka ahadi ya Bwana kwake Joseph Smith na Sidney Rigdon walipokuwa mbali na familia zao katika kazi Yake: “Marafiki zangu Sidney na Joseph, familia zenu ni njema, wako mikononi mwangu, na nitawafanyia nionavyo kuwa ni vyema; kwani ndani yangu kuna uwezo wote.”13
Kama Alma na Mfalme Mosia, baadhi yenu watumishi waaminifu ambao mmetumikia Bwana kwa muda mrefu na vyema sana mmekuwa na watoto waliopotea licha ya dhabihu ya wazazi wao kwa ajili ya Bwana. Walifanya yote wawezayo, hata na usaidizi kutoka kwa marafiki wenye upendo na waaminifu.
Alma na Watakatifu waiomba kwa ajili ya mwanawe na wana wa Mfalme Mosia Malaika akaja. Maombi yenu na maombi ya wale wanaofanya imani yataleta watumishi wa Bwana kusaidia wanafamilia wenu. Watawasaidia kuchagua njia ya kuelekea nyumbani kwa Mungu, hata wanaposhambuliwa na Shetani na wafuasi wake, ambao lengo lao ni kuangamiza familia katika maisha haya na katika milele.
Unakumbuka maneno yaliyozungumzwa na malaika kwa Alma Mdogo na wana wa Mosia katika uasi wao: “Na tena malaika akasema: Tazama Bwana amesikia sala za watu wake, na pia sala za mtumishi wake, Alma ambaye ni baba yako; kwani ameomba kwa imani kubwa kukuhusu ili upate kuelimika kwa ukweli; kwa hivyo ni kwa sababu hii nimekuja kukusadikisha kuhusu uwezo na mamlaka ya Mungu, kwamba sala za watumishi wake zijibiwe kulingana na imani yao.”14
Ahadi yangu kwenu mnaoomba na kumtumikia Bwana haiwezi kuwa kwamba mtapata kila baraka mnayotaka kwenu wenyewe na familia zenu. Lakini ninaweza kuahidi kuwa Mwokozi atakuja karibu nanyi na kuwabariki na familia yenu na kile kilicho bora. Mtakuwa na faraja ya upendo Wake na kuhisi jibu ya kuja Kwake karibu mnaponyosha mikono yenu katika kuwatumikia wengine. Mnapofunga majeraha ya wale wanaohitaji na kutoa uwezo wa kusafisha wa Upatanisho kwa wale wanaohuzunika katika dhambi, Nguvu ya Bwana itakuhimili. Mikono Yake imenyoshwa pamoja na yako kusaidia na kubariki watoto wa Baba yetu wa Mbinguni, ikijumuisha wale walio katika familia yako.
Kuna urejesho wetu nyumbani wa ajabu ulioandaliwa kwa ajili yetu. Kisha tutaona ahadi iliyotimizwa ya Bwana tunayempenda. Ni Yeye anayetukaribisha katika uzima wa milele pamoja Naye na Baba yetu wa Mbinguni. Yesu Kristo aliielezea hivi:
“Tafuta kuanzisha na kustawisha Sayuni yangu. Shika amri zangu katika mambo yote.
“Na, kama unashika amri zangu na kuvumilia hadi mwisho utapata uzima wa milele, kipawa ambacho ni kikuu katika vipawa vyote vya Mungu.”15
“Kwani wale waishio watairithi nchi, na wale wanaokufa watapata kupumzika kutoka kwa kazi zao zote, na matendo yao yatafuatana nao; na watapokea taji katika nyumba ya Baba yangu, ambayo nimeitayarisha kwa ajili yao.”16
Ninashuhudia kuwa tunaweza kwa Roho kufuata mwaliko wa Baba wa Mbinguni: “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!”17
Kwa maneno Yake na mfano Wake, Kristo ametuonyesha jinsi ya kujongea karibu Naye. Kila mtoto wa Baba wa Mbinguni aliyechagua kuingia kupitia mlango ya ubatizo katika Kanisa Lake atakuwa na fursa ya kufundishwa injili Yake na kusikiliza kutoka kwa watumishi Wake walioitwa mwaliko Wake “Njooni kwangu.”18
Kila mtumishi Wake wa agano katika ufalme Wake duniani, na katika dunia ya roho, atapokea maelekezo yake wanapobariki na kuwatumikia wengine kwa ajili Yake. Kisha wao watahisi upendo Wake, na wapate furaha katika kuvutiwa karibu Naye.
Mimi ni shahidi wa Ufufuo wa Bwana kwa hakika kama nilikuwa hapo jioni na wanafunzi wale wawili katika nyumba kwenye njia ya Emau. Najua kuwa Yeye anaishi kwa hakika kama alivyo Joseph Smith alipomuona Baba na Mwana katika nuru ya asubuhi angavu katika kichaka cha miti kule Palmyra.
Hili ndilo Kanisa la kweli la Yesu Kristo. Ni tu kwenye funguo za ukuhani ambazo Rais Thomas S. Monson anazo ndiko uwezo kwetu wa kuunganishwa katika familia ili kuishi milele pamoja na Baba wetu wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo. Sisi tutasimama kwenye Siku ya Hukumu mbele ya Mwokozi, ana kwa ana. Itakuwa ni wakati wa furaha kwa wale waliokuja karibu Naye katika huduma Yake katika maisha haya. Itakuwa shangwe kusikia maneno: “Vema, mtumwa mwema na mwaminifu.”19 Ninashuhudia hayo kama shahidi wa Mwokozi aliyefufuka na Mkombozi wetu katika jina la Yesu Kristo, amina.
© 2013 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa USA. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/12. Tafsiri iliidhinishwa: 6/12. Tafsiri ya Visiting Teaching Message, May 2013. Swahili. 10665 743