2014
Kuharakisha Kazi
June 2014


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Juni 2014

Kuharakisha Kazi

Picha
Rais Thomas S. Monson

Je, unatambua kwamba Kanisa lililorejeshwa lilikuwa na umri wa miaka 98, kabla ya kupata vigingi 100? Lakini chini ya miaka 30 baadaye, Kanisa lilikuwa limeanzisha vigingi vyake vingine 100. Na miaka nane tu baada ya hapo Kanisa lilikuwa na zaidi ya vigingi 300. Leo tuna zaidi ya vigingi 3,000 vilivyoimarika.

Kwa nini ukuaji huu unafanyika katika kiwango cha kasi? Je, ni kwa sababu tunajulikana sana? Je, ni kwa sababu tuna makanisa ya kupendeza?

Mambo haya ni muhimu, lakini sababu ya Kanisa kukua leo ni kwa sababu Bwana alisema ingekuwa. Katika Mafundisho na Maagano, Alisema, “Tazama, nitaiharakisha kazi yangu katika wakati wake.”1

Sisi, kama watoto wa kiroho wa Baba yetu wa Mbinguni, tulitumwa duniani kwa wakati huu ili tupate kushiriki katika kuiharakisha kazi hii kubwa.

Bwana hajawahi, kwa ufahamu wangu, kuonyesha kuwa kazi yake ni ya dunia tu. Badala yake, kazi yake inahusisha maisha ya milele. Naamini Anaiharakisha kazi Yake katika ulimwengu wa roho. Pia naamini kwamba Bwana, kupitia kwa watumishi Wake huko, anatayarisha roho wengi kupokea injili. Kazi yetu ni kuwatafuta wafu wetu na kisha kwenda hekaluni na kufanya ibada takatifu ambazo zitawaletea wale walio upande ule mwingine wa pazia fursa sawa na tulizonazo.

Kila Mtakatifu mwema wa Siku za Mwisho katika ulimwengu wa roho ana kazi nyingi, alisema Rais Brigham Young (1801–77). “Wanafanya nini huko? Wanahubiri, wanahubiri wakati wote, na kutengeneza njia ili tuweze kuharakisha kazi yetu katika kujenga mahekalu hapa na mahali pengine.2

Sasa, kazi ya historia ya familia si rahisi. Kwa wale wenu kutoka Skandinavia, nashiriki shida zenu. Kwa mfano, katika ukoo wangu wa Uswidi, jina la babu yangu lilikuwa Nels Monson; jina la baba yake halikuwa Monson kamwe lakini lilikuwa Mons Okeson. Jina la baba yake Mons lilikuwa Oke Pederson, na jina la baba yake lilikuwa Peter Monson—kurudi kwa Monson tena.

Bwana anatarajia wewe na mimi tufanye kazi yetu ya historia ya familia vizuri. Nadhani jambo la kwanza tunalopaswa kufanya kama tutafanya kazi yetu vizuri ni kuwa na Roho wa Baba yetu wa Mbinguni pamoja nasi. Wakati tunaishi kwa haki kama tunavyojua namna ya kuishi, Yeye atafungua njia ya kutimiza baraka ambazo tunatafuta kwa dhati na kwa bidii.

Tutafanya makosa, lakini hakuna yeyote kati yetu anayeweza kuwa mtaalam katika kazi ya historia ya familia bila kwanza kuwa mwanafunzi. Hivyo, ni lazima tuzame katika kazi hii, na lazima tujitayarishe kufanya kazi nyingi. Hii si kazi rahisi, lakini Bwana ameiweka juu yako, na Ameiweka juu yangu.

Unapofuatilia kazi ya historia ya familia, utajipata ukikwama katika vizuizi, na utajisemeza mwenyewe, “Hakuna kitu kingine nitakachoweza kufanya.” Unapofikia kwa hatua hiyo, piga magoti yako chini na umuulize Bwana akufungulie njia, na Yeye atafungua njia kwako. Nashuhudia kwamba hii ni kweli.

Baba wa Mbinguni anawapenda watoto Wake katika ulimwengu wa roho kama vile Anavyokupenda wewe na mimi. Kuhusu kazi ya kuokoa wafu wetu, Nabii Joseph Smith alisema, “Na sasa kama vile malengo makubwa ya Mungu yanavyoharakisha kwa ufanikishaji wao, na mambo yaliyosemwa na Manabii yanatimizwa, kama vile ufalme wa Mungu unavyoanzishwa duniani, na mpango wa kale wa mambo kurejeshwa, Bwana amedhihirisha kwetu wajibu huu na upendeleo.”3

Kuhusu mababu zetu ambao wamefariki bila ufahamu wa Injili, Rais Joseph F. Smith (1838–1918) alitangaza, “Kupitia kwa juhudi zetu kwa niaba yao minyororo yao ya utumwa itaanguka kutoka kwao, na giza inayowazingira itapotelea mbali, ili kwamba mwanga uweze kuwaangazia na waweze kusikia katika ulimwengu wa roho juu ya kazi ambayo imefanywa kwa ajili yao na watoto wao hapa, na watashangilia pamoja nanyi katika utendaji wako wa kazi hii.” 4

Kuna mamilioni juu ya mamilioni ya watoto wa kiroho wa Baba yetu wa Mbinguni ambao kamwe hawajawahi kusikia jina la Kristo kabla ya kufa na kwenda katika ulimwengu wa roho. Lakini sasa wamefundishwa injili na wanasubiri siku ambapo wewe na mimi tutafanya uchunguzi muhimu kufungua njia ili tuweze kuingia katika nyumba ya Bwana na kuwafanyia kazi ambayo wao wenyewe hawawezi kufanya.

Ndugu zangu na dada zangu, Nashuhudia kwamba Bwana atatubariki tunapokubali na kukabiliana na changamoto hii.

Kufundisha kutoka Ujumbe huu

Fikiria juu ya hadithi nzuri kutoka kwa historia ya familia na ushiriki hadithi hii na wale unaowatembelea. Unaweza kutaka kutumia maswali katika sehemu ya watoto ya Ujumbe wa Urais wa Kwanza (ukurasa 6) ili kuwatia moyo wale unaowatembelea kushiriki hadithi zao. Fikiria kusoma Mafundisho na Maagano 128:15 na kujadili umuhimu wa kufanya ibada za hekalu kwa niaba ya mababu zetu.

Muhtasari

  • Mafundisho na Maagano 88:73.

  • Teachings of Presidents of the Church: Brigham Young (1997), 280.

  • Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2007), 409.

  • Teachings of Presidents of the Church: Joseph F. Smith (1998), 247.

Chapisha