Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Januari 2016
Furaha kwa Wale Tunaowapenda
Sisi wote tunawatakia furaha wale tanaowapenda, na tunawatakia maumivu kidogo kadri iwezekanavyo. Tanaposoma taarifa kuhusu furaha—na za maumivu—katika Kitabu cha Mormoni, mioyo yetu inachochewa tunapowafikiria wapendwa wetu. Hapa ni taarifa za kweli za nyakati za furaha:
“Na ikawa kwamba hapakuwa na mabishano katika nchi, kwa sababu ya mapenzi ya Mungu ambayo yaliishi katika mioyo ya watu.
“Na hakukuwa na wivu, wala ubishi, wala misukosuko, wala ukahaba, wala uwongo, wala mauaji, wala uzinifu wa aina yoyote; na kwa kweli hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi miongoni mwa watu wote ambao waliumbwa na mkono wa Mungu.”
Kisha tunasoma:
“Na jinsi gani walibarikiwa kwani Bwana aliwabariki kwa matendo yao yote; ndio, hata walibarikiwa na kufanikiwa mpaka miaka mia moja na kumi ikapita; na kizazi cha kwanza kutoka Kristo kilikuwa kimepita, na hakukuwa na ubishi katika nchi yote.” (4 Nefi 1:15–16, 18).
Wanafunzi wapendwa wa Kristo wanaomba na kufanya kazi kwa ajili ya baraka kama hizo kwa wengine na wao wenyewe. Kutoka katika taarifa katika Kitabu cha Mormoni na, kwa wengi wetu, kutoka kwa uzoefu wetu wenyewe, tunajua kwamba kipawa cha furaha kinaweza kupatikana. Tunajua kwamba njia ya kupata furaha imewekwa alama vyema. Sisi pia tunajua kwamba kudumisha furaha si jambo rahisi isipokuwa, kama vile kwa Wanefi baada ya kutembelewa na Mwokozi, upendo wa Mungu unakaa ndani ya mioyo yetu .
Upendo ule ulikuwa ndani ya mioyo ya Wanefi kwa sababu walishika sheria ambayo ilifanya hayo kuwezekana. Muhtasari wa sheria ile unapatikana katika maombi ya sakramenti, ambayo huanza kwa kusihi kwa moyo wa dhati hata kwa Baba yetu wa Mbinguni. Tunaomba kwa moyo uliojaa imani, na kwa upendo wa kina kwa, Mwokozi wetu. Tunaweka sharti kwa dhamira halisi kujichukulia juu yetu jina Lake, kumkumbuka Yeye, na kushika amri Zake zote. Mishowe, tunafanya imani kwamba Roho Mtakatifu, mshiriki wa Uungu, apate kuwa pamoja nasi daima, akishuhudia katika mioyo yetu juu ya Baba na Mwanawe Mpendwa. (Ona M&M 20:77, 79.)
Tukiwa na uenzi wa Roho Mtakatifu, mioyo yetu inaweza kubadilika ili kwamba tutamani na kuukaribisha upendo wa Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo. Njia ya kupata upendo wa Mungu uingie ndani ya mioyo yetu ni rahisi, kama ilivyo njia ya kupoteza hisia za upendo huo katika mioyo yetu. Kwa mfano, mtu anaweza kuchagua kutokuomba kila mara kwa Baba wa Mbinguni ama kutolipa zaka kamili ama kuwacha kusherekea neno la Mungu ama kukosa kuwajali maskini na wenye mahitaji.
Chaguo lolote la kutoshika amri za Bwana linaweza kusababisha Roho ajiondoe kutoka kwa mioyo yetu. Kwa ajili ya kupoteza huku, furaha hififia.
Furaha tunayowatakia wapendwa wetu inategemea chaguo zao. Vile vile tunapompenda mtoto, mchunguzi, ama marafiki zetu, hatuwezi kuwalazimisha kushika amri ili wastahili Roho Mtakatifu kugusa na kubadili mioyo yao.
Kwa hivyo msaada bora tanaoweza kutoa ni ule unaowaongoza wale tunaowapenda kuchunga chaguo zao wenyewe. Alma alifanya hivyo kwa mwaliko ambao unaweza kuutoa:“
Lakini kwamba mtajinyenyekeza mbele ya Bwana, na mliite jina lake takatifu, na kukesha na kusali daima, kwamba msijaribiwe zaidi ya yale ambayo mnaweza kuvumilia, na hivyo mwongozwe na Roho Mtakatifu, katika kuwa wanyenyekevu, wapole, watiifu, wenye subira, wenye upendo na wenye uvumilivu;“Mkimwamini Bwana; mkitumaini kwamba mtapokea uzima wa milele; mkiwa na upendo wa Mungu daima katika mioyo yenu, kwamba muinuliwe katika siku ya mwisho na muingie katika pumziko Lake”
Mimi naomba kwamba wale mnaowapenda waweze kukubali mwaliko wa kuchagua njia ya furaha ya kudumu.
© 2016 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imechapishwa Marekani. Kiingereza kiliidhinishwa: 6/15. Tafsiri iliidhinishwa: 6/15. Tafsiri ya First Presidency Message, January 2016. Swahili 12861 743.