2016
Baba Yetu, Mnasihi Wetu
Juni 2016


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Juni 2016

Baba Yetu, Mnasihi Wetu

Je, umewahi kufungua sanduku la vifaa, ukatoa karatasi la maelekezo ya kuviunganisha, na ukafikiria, “Hii haileti maana hata kidogo?”

Wakati mwingine, bila kujali dhamira yetu ya dhati na kujiamini, tunavitoa vifaa na kujiuliza, “Hivi ni vya nini?” au “Vinawezaje kuunganishwa?”

Kukata tamaa hukua tulipokuwa tunaliangalia sanduku na kuona kanusho lililo sema, “Kuunganisha kunahitaji mwenye miaka 8 na zaidi.” Kwa sababu bado hatujui kutatua, hakutupi msukumo wa kujiamini au kujistahi.

Wakati mwingine tuna uzoefu kama huo katika injili. Tunapoangalia sehemu zake, tunaweza kukuna vichwa vyetu na kushangaa kifaa hicho ni cha nini. Au tunapokichunguza kifaa kingine, tunaweza kuona kwamba hata baada ya kujitahidi kwa nguvu ili kuelewa zaidi, hatuwezi kujua kwa nini kile kifaa kilijumuishwa.

Baba Yetu wa Mbinguni ni Mnasihi Wetu

Kwa bahati, Baba yetu wa Mbinguni ametupa maelekezo ya kuyajenga maisha yetu na kujiweka pamoja sisi wenyewe. Maelekezo hayo yanafanya kazi bila kujali umri wetu au hali ya mambo. Ametupa injili na Kanisa la Yesu Kristo. Ametupa mpango wa ukombozi, mpango wa wokovu, hata mpango wa furaha. Hajatuacha peke yetu pamoja na mashaka na changamoto zote za maisha, akisema, “Haya basi. Kila la heri. Tambua mwenyewe.”

Kama tutakuwa wavumilivu na kuangalia kwa moyo mnyenyekevu na akili zilizofunguka, tutagundua kwamba Mungu ametupa nyenzo nyingi ili kuweza kuyaelewa maelekezo Yake kwa ajili ya furaha yetu katika maisha:

  • Ametupa zawadi isiyo na gharama ya Roho Mtakatifu, ambaye anaweza kuwa wa kwetu binafsi, mwalimu wa mbinguni wakati tunajifunza neno la Mungu na kujaribu kuyaweka mawazo na matendo yetu kulingana na maneno Yake.

  • Ametupa masaa 24 kila siku kwa siku 7 ili kumfikia Yeye kwa njia ya sala za imani na maombi yenye dhamira ya kweli.

  • Ametupa mitume na manabii wa kisasa, ambao wanafunua neno la Mungu katika siku zetu na wanayo mamlaka kuunganisha au kufunganisha duniani na mbinguni.

  • Amelirejesha Kanisa Lake—jumuiya ya waaminio ambao wanafanya kazi pamoja ili kusaidiana huku wakifanya kazi yao ya wokovu kwa woga, kutetemeka, na kwa furaha isiyo na kifani.

  • Ametupa maandiko matakatifu—neno Lake lililoandikwa kwetu.

  • Ametupa zana nyingi za teknolojia ya kisasa ili kutusaidia kutembea katika ufuasi. Vifaa hivi vingi vinaweza kupatikana kwenye LDS.org.

Kwa nini Baba yetu wa Mbinguni ametupa msaada mwingi? Kwa sababu Anatupenda. Na kwa sababu, kama Alivyojisemea Mwenyewe, “Hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu.”2

Kwa maneno mengine, Baba wa Mbinguni ni Mungu wetu, na Mungu ndiye mnasihi wetu.

Baba yetu wa Mbinguni anajua vizuri mahitaji ya watoto Wake kuliko mtu mwingine yeyote. Ni kazi na utukufu Wake kutusaidia sisi katika kila kona, akitupa rasilimali za ajabu za kimwili na kiroho ili kutusaidia kwenye njia ya kurudi Kwake.

Kila Baba ni Mnasihi

Katika sehemu nzingine za ulimwengu, akina baba wanaheshimika na familia na jamii katika mwezi Juni. Mara zote ni vizuri kuwaheshimu na kuwastahi wazazi wetu. Akina baba wanafanya mambo mengi mazuri kwa ajili ya familia zao na wana sifa nyingi nzuri. Majukumu muhimu mawili ambayo akina baba wanayo katika maisha ya watoto wao ni yale ya kuwa mfano mzuri na mshauri. Akina baba wanafanya mengi zaidi ya kuwaambia watoto wao yaliyo mema na mabaya; wanafanya mengi zaidi ya kuwapa vitabu na kutarajia kuyatambua maisha kivyao wenyewe.

Akina baba wanawashauri watoto wenye thamani na kuwaonyesha kwa mfano mzuri jinsi maisha ya uaminifu yanavyotakiwa kuishiwa. Akina baba hawawaachi watoto wao pekee lakini huwakimbilia wanapohitaji msaada, na kuwasaidia kuinuka wanapojikwaa. Na wakati mwingine busara inatumika, akina baba wanawaacha watoto wao wapate shida, wakijua kwamba hii inaweza kuwa njia nzuri ya wao kujifunza.

Sisi Wote ni Wanasihi

Wakati akina baba wa duniani wakifanya haya kwa ajili ya watoto wao wenyewe, roho wa unasihi ni kitu tunachohitaji kukifanya kwa watoto wote wa Mungu, bila kujali umri, mahali, au hali ya mambo. Kumbuka, watoto wa Mungu ni kaka na dada zetu; sisi wote ni familia moja ya milele.

Kwa maana hii, acha wote tuwe wanasihi—tukitamani kuwafikia na kusaidiana ili tuwe watu wazuri zaidi. Kwa sababu sisi ni watoto wa Mungu, tuna nafasi ya kuwa kama Yeye. Kumpenda Mungu na jamaa zetu, kutii amri za Mungu, na kufuata mfano wa Kristo ni njia iliyonyooka, nyembamba, na yenye furaha ya kurudi kwenye uwepo wa wazazi wetu wa mbinguni.

Kama Mungu wa ulimwengu wote anatujali sana na kuwa ni mnasihi wetu, huenda na sisi pia tunaweza kuwafikia jamaa zetu, bila kujali rangi zao, asili, hali ya kijamii, lugha, au dini. Acha tuwe wanasihi wenye maongozi na kuyabariki maisha ya wengine—siyo watoto wetu pekee lakini pia watoto wote wa Mungu ulimwenguni kote.

Kufundisha kutoka kwenye Ujumbe Huu

Unaweza kuanza kwa kuwauliza wale unaowafundisha kufikiria kwa dakika chache wakati Baba wa Mbinguni alipowanasihi. Kisha ungeweza kuwaomba kufikiria kufanana kati ya kipindi kile na kipindi ambacho walihisi walinasihiwa na baba yao wa duniani. Waalike waandike mfanano wa jinsi walivyonasihiwa. Unaweza kuwapa changamoto ya kujaribu kuigiza vitu walivyoviandika katika juhudi za kuwa mfano bora kwa wengine.