2017
Upendo Kamili Hutupa Hofu Nje
May 2017


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Mei 2017

Upendo Kamili Hutupa Hofu Nje

Acha tuweke kando hofu yetu na badala yake tuishi kwa furaha, unyenyekevu, tumaini, na imani kakamavu kwamba Bwana yu pamoja nasi.

Kina kaka na kina dada, marafiki wangu wapendwa ni fursa na furaha iliyoje kukutana kama Kanisa la ulimwenguni kote tukiungana katika imani yetu na upendo kwa Mungu na watoto Wake.

Nashukuru hasa kwa ajili ya uwepo wa nabii wetu mpendwa, Thomas S. Monson. Rais, daima tutayatia moyoni maneno yako ya maelekezo, ushauri, na hekima. Tunakupenda Rais Monson, na daima tunakuombea.

Miaka iliyopita, nilipokuwa nikihudumu kama rais wa kigingi katika Frankfurt, Ujerumani, dada mpendwa lakini asiye na furaha alinijia mwishoni wa mojawapo wa mikutano yetu ya kigingi.

“Si inasikitisha? alisema. “Lazima kumekuwa na watu wanne au watano waliokuwa wamelala fofofo wakati wa hotuba yako!”

Nikafikiria kwa dakika na kujibu, “Nina hakika kwamba usingizi kanisani ndiyo kati usingizi wenye afya sana.”

Mke wangu wa ajabu, Harriet, alisikia mazungumzo hayo na baadaye kusema kwamba ilikuwa mojawapo wa majibu mazuri ambayo niliyatoa.

Mwamko Mkuu

Miaka michache iliyopita katika Amerika Kaskazini, kundi lililoitwa “Mwamko Mkuu” ambalo lilisambaa kote mikoani. Mojawapo wa madhumuni yake ya msingi yalikuwa ni kuwaamsha watu ambao walikuwa wanaokena kama wamelala kuhusiana na mambo ya kiroho.

Kijana, Joseph Smith alishawishika na mambo aliyoyasikia kutoka kwa wahubiri ambao walikuwa sehemu ya mwamko huu wa kidini. Ndiyo mojawapo wa sababu aliamua kutafuta kwa bidii mapenzi ya Bwana katika sala za faraghani.

Wahubiri hawa walikuwa na elimumwendo, mhemko katika mahubiri ambayo yalijulikana sana kwa msisitizo mkubwa juu ya vitishio vikali vya jehanamu ambavyo viliwangojea wenye dhambi.1 Hotuba zao hazikuwafanya watu wasinzie—bali zingeweza kusababisha ndoto chache za kutisha. Lengo lao na mfumo wao vilionekana kuwaogopesha watu kuja kanisani.

Hofu kama hila

Kihistoria, hofu mara nyingi imetumika kama njia ya kuwafanya watu wachukue uamuzi. Wazazi wameitumia kwa watoto wao, waajiri kwa waajiriwa, na wanasiasa kwa wapiga kura.

Wataalamu wa masoko huelewa nguvu ya hofu na mara nyingi huitumia. Hii ndio maana matangazo huonekana kubeba ujumbe unaodokeza kwamba kama tutakosa kununua chapa sahihi ya nafaka ya kifungua kinywa, au tukikosa mchezo wa video mpya au simu ya kigajani, tutakuwa katika hatari ya kuishi maisha ya taabu na tutakufa peke yetu na pasipo na furaha.

Tunatabasamu katika hili na tunadhani kamwe hatutaangukia katika hila hiyo, lakini wakati mwingine tunafanya hivyo. Kibaya zaidi, wakati mwingine tunatumia njia kama hizo kuwafanya watu watende tunavyotaka.

Ujumbe wangu leo una madhumumni mawili: La kwanza ni kutusihi kutazama kwa makini na kufikiria kiasi ambacho tunatumia hofu kuwahamasisha wengine—ikiwemo sisi wenyewe. La pili ni kupendekeza njia bora zaidi.

Tatizo la Hofu

Kwanza, ngoja tuzungumze tatizo la hofu Kwani, nani kati yetu hajawahi kushurutishwa na hofu kula vizuri, kufunga mkanda wa usalama, kufanya mazoezi zaidi, kutunza fedha, au hata kutubu dhambi?

Ni kweli hofu inaweza kuwa na ushawishi wa nguvu katika matendo na tabia zetu. Lakini uwezo huu huwa wa muda na hauna kina. Hofu mara chache ina nguvu ya kubadilisha mioyo yetu, na kamwe haitatubadili kuwa watu ambao hupenda mema na watiifu kwa Baba yetu wa Mbinguni.

Watu ambao wana hofu wanaweza kusema na kutenda vitu sahihi, lakini hawahisi vitu sahihi. Mara nyingi huhisi hawana msaada na ni wenye kuchukia na hata hasira. Baada ya muda hisia hizi hupelekea kutoamini, kutojali hata uasi.

Kwa bahati mbaya, huu mwenendo potovu katika maisha na uongozi hauko tu katika dunia ya kiliumwengu. Hunihuzunisha sana ninaposikia waumini wa Kanisa ambao hutumia mamlaka yasiyo haki—iwe nyumbani kwao, miito ya Kanisa, kazini au kwenye uhusiano wa kila siku na wengine.

Mara nyingi, watu wanaweza kushutumu uonevu kwa wengine, lakini hawauoni ndani yao. Wakidai kushikiliwa kwa sheria zao za udhalimu, wakati wengine hawafuati sheria hizo zisizo na mpangilio, watu hao huwarudi kimaneno, kihisia na wakati mwingine hata kimwili.

Bwana amesema kwamba “wakati … tunatumia uthibiti au utawala au ulazimishaji juu ya nafsi za wanadamu, katika kiwango chochote kisicho cha haki, … mbingu hujitoa zenyewe [na] Roho wa Bwana husikitika.”2

Nyakati zinaweza kutokea ambapo tunajaribiwa kuhalalisha vitendo vyetu kwa kuamini kuwa matokeo huhalalisha njia iliyotumika. Hata tunaweza kudhani kuwa kudhibiti, kutawala kwa hila, na ukali itakuwa kwa ajili ya mazuri ya wengine. Sivyo, kwa kuwa Bwana ameweka wazi kwamba, “tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, imani, upole, [na] kiasi.”3

Njia bora

Ninavyozidi kumjua Baba yangu wa Mbinguni, ndivyo ninavyoona jinsi Yeye huwapa mwongozo na kuwaongoza watoto Wake. Yeye akasiriki, halipizi kisasi, wala hana chuki.4 Lengo Lake hasa—na kazi yake—ni kutufundisha, kutuinua, na kutuongoza katika ukamilifu Wake.5

Mungu alijielezea kwa Musa kama “mwenye rehema na hisani, mvumilivu na mwingi wa neema na ukweli.”6

Upendo wa Baba Yetu wa Mbinguni kwetu sisi, watoto Wake, hupita sana uwezo wa uelewa.7

Je, hii humaanisha kuwa Mungu huruhusu au hatilii maanani tabia ambazo ni kinyume na amri Zake? La, Hasha!

Lakini anataka kubadili zaidi kuliko tabia tu. Anataka kubadili asili yetu hasa. Anataka kubadili mioyo yetu.

Anataka tufikie na kushikilia kwa nguvu fimbo ya chuma, kupambana na hofu zetu, na kishujaa kupiga hatua mbele na juu katika njia iliyosonga na nyembamba. Anataka hivi kwetu kwa sababu Anatupenda na kwa sababu hii ndio njia ya kuelekea kwenye furaha.

Kwa hivyo, Mungu huwahamasisha watoto wake namna gani kumfuata katika siku zetu?

Mungu Alimtuma Mwanawe!

Alimtuma Mwanawe wa Pekee, Yesu Kristo, kutuonyesha njia sahihi.

Mungu hutuhamasisha kupitia ushawishi, uvumilivu, utu wema, upole na upendo usiyo na unafiki.8 Mungu yuko upande wetu. Anatupenda, na tunapojikwaa, Anataka tusimame, na kujaribu tena na kuwa imara zaidi.

Yeye ni mnasihi wetu.

Yeye ni mkuu wetu na tumaini letu la kuvutia.

Yeye anatamani kutusisimua kwa imani.

Yeye ana imani tutajifunza kutokana na kiujikwaa kwetu na kufanya chaguo sahihi.

“Hii ndiyo njia bora!9

Je, Maovu ya Ulimwengu?

Njia mojawapo ambayo Shetani anataka tuwatawale wenzetu kwa hila ni kwa kuendelea kukaa katika uovu na hata kutia chumvi uovu duniani.

Hakika ulimwengu wetu umekuwa, na utaendelea, kutokuwa mkamilifu. Zaidi pia, watu wengi wasio na hatia wanateseka kwa sababu ya hali halisi na pia kukosekana kwa utu. Ubovu na uovu katika siku zetu ni wa kipekee na unatisha.

Lakini licha ya haya yote, nisingebadilisha kuishi katika kipindi hiki na kipindi kingine chochote katika historia ya ulimwengu. Tumebarikiwa kupita kiasi kuishi katika siku ya mafanikio yasiyo kifani, kuelimika na faida. Zaidi ya yote, tumebarikiwa kuwa na utimilifu wa injili ya Yesu Kristo, ambayo hutupatia mtazamo wa kipekee juu ya hatari za kiulimwengu na kutuonyesha jinsi ya kuepuka hatari hizi au kupambana nazo.

Nifikiriapo juu ya baraka hizi, ninataka kupiga magoti na kutoa sifa kwa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya upendo Wake usio na mwisho kwa watoto Wake.

Siamini Mungu anataka Watoto Wake kuwa na hofu au kuendelea na maovu ya ulimwengu huu. “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi.”10

Yeye ametupa sababu nyingi za kufurahia. Tunahitaji kuzitafuta na kuzitambua. Mara nyingi Bwana anatukumbusha “usiogope,” na “jipeni moyo,”11 na “msiogope, wanakondoo”12

Bwana Atatupigania Vita Vyetu

Kina ndugu na dada, sisi tu “wanakondoo” wa Bwana. Sisi ni Watakatifu wa siku za mwisho. Asili ya jina letu ni msismamo wa kutarajia kurudi kwa Mwokozi na kuandaa wenyewe na ulimwengu kumpokea Yeye. Kwa hiyo, acha tumtumikie Mungu na kuwapenda wanadamu wenzetu. Acha tufanye hilo kwa imani halisi, kwa unyenyekevu, bila kupuuza dini ingine yoyote au makundi mengine. Kina kaka na kina dada, tunaamriwa kujifunza neno la Mungu na kufuata sauti ya Roho, kwamba tuweze “kujua ishara za nyakati, na ishara za kuja kwa Mwana wa Mtu.”13

Sisi, kwa hiyo, si mbumbumbu kuhusu changamoto za kiulimwengu au hatufahamu ugumu wa nyakati zetu. Lakini hii haimaanishi kwamba tujitwike mzigo wa hofu au kuwatwika wengine na hofu ya kila mara. Badala ya kufikiria ukubwa wa changamoto zetu, haingekuwa vizuri kuzingatia ukubwa usio na mwisho, uzuri, na uhakika wa nguvu za Mungu wetu, kumwamini Yeye, na kujiandaa kwa moyo wa furaha kwa ujio wa Yesu Kristo?

Kama watu Wake wa maagano, hatuhitaji kuduwazwa na hofu kwa sababu ya kile ambacho kinaweza kutokea. Badala yake tunaweza kusonga mbele kwa imani, ujasiri, nia ya dhati na tumaini katika Mungu tunapokaribia changamoto na nafasi zilizo mbele yetu.14

Hatutembei katika njia ya ufuasi peke yetu. “Bwana Mungu wako … anayekwenda pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha.”15

“Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”16

Tukitokewa na tishio, acha tupate ujasiri wetu, imani ya kutosha na tuwe na imani katika ahadi kwamba “hakuna silaha ambayo itafanyika dhidi itafanikiwa.17

Tunaishi nyakati za hatari na ghasia? Bila shaka!

Mungu Mwenyewe amesema “Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu.”18

Je, tunaweza kutumia imani kuamini na kutenda ipasavyo? Je, tunaweza kuishi kulingana na ahadi zetu na maagano matakatifu? Je, tunaweza kushika amri za Mungu hata katika hali zenye changamoto? Bila shaka tunaweza!

Tunaweza kwa sababu Mungu ameahidi, “Mambo yote yatafanyika kwa pamoja kwa faida yenu, kama ninyi mnatembea wima.”19 Kwa hiyo, acha tuweke kando hofu yetu na tuishi kwa furaha, unyenyekevu, tumaini, na imani kakamavu kwamba Bwana yu pamoja nasi.

Upendo Kamili Hutupa Hofu Nje

Rafiki zangu wapendwa, kaka zangu na dada zangu wapendwa katika Kristo, kama tutajikuta tunaishi katika hofu au woga, au kama tutajikuta kuwa maneno yetu wenyewe, mtazamo wetu na matendo yetu yanasababisha hofu kwa wengine, Mimi naomba kwa nguvu zote za nafsi yangu kwamba tuweze kukombolewa kutoka kwa hofu hii kwa tiba teule ya kiungu: “pendo lililo kamili huitupa nje hofu.”20

Upendo kamili wa Kristo hushinda majaribu ya kudhuru, kuonea au kukandamiza.

Upendo kamili wa Kristo huruhusu unyenyekevu, heshima na ujasiri mkuu kama wafuasi wa Mwokozi wetu mpendwa. Upendo kamili wa Kristo hutupatia kujiamini kusonga mbele kupita hofu zetu na kuweka uaminifu wetu wote katika nguvu na uzuri wa Baba yetu wa Mbinguni, Mwanawe, Yesu Kristo.

Nyumbani kwetu, sehemu zetu za biashara, miito yetu katika Kanisa, katika mioyo yetu, acha tubadilishe hofu kwa upendo kamili wa Kristo. Tutabadlisha hofu kwa imani!

Upendo Wake utatuwezesha kutambua, kuamini na kuwa na imani katika uzuri wa Baba yetu wa Mbinguni, mpango Wake mtakatifu, injili Yake na amri Zake.21 Kumpenda Mungu na wanadamu wenzetu kutageuza utiifu wetu katika amri za Mungu kuwa baraka bali si mzigo. Upendo wa Kristo utatusaidia kuwa wakarimu zaidi, wenye kusamehe zaidi, wenye kujali zaidi, na wenye kujitolea zaidi katika kazi Yake.

Tunapojaza mioyo yetu na upendo wa Kristo, tutaamshwa na upya wa kiroho na tutatembea kwa furaha, kwa kujiamini, kuwa macho, na kuwa hai katika nuru na utukufu wa Mwokozi wetu mpendwa, Yesu Kristo.

Ninashuhudia, pamoja na Mtume Yohana, “Hakuna hofu katika upendo wa [Kristo].”22 Akina kaka na kina dada wapendwa wangu, rafiki wapendwa, Mungu anawajua vyema! Yeye anawapenda kweli. Yeye anajua siku za usoni zetu. Yeye anawataka “msiogope, ila muamini tu”23 na “kukaa katika upendo wake [kamili].”24 Haya ndiyo maombi yangu na baraka zangu katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. George Whitehead and Jonathan Edwards ni mifano miwili mikubwa ya wahubiri wa namna hii.

  2. Mafundisho na Maagano 121:37.

  3. Wagalatia 5:22–23

  4. Wakati fulani, Mwokozi alitaka kuingia kijiji cha Wasamaria, lakini watu walimkataa Yesu na hawangetaka kumpokea katika kijiji chao. Wawili kati ya wafuasi Wake, walikerwa sana na hiki na wakauliza, “Bwana wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize?” Yesu alijibu kwa onyo hili: “Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo. “Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa.” (Luka 9:51–56, Toleo la New King James [1982]).

  5. Ona Musa 1:39; ona pia Waefeso 3:19.

  6. Kutoka 34:6.

  7. Ona Waefeso 3:19;

  8. Ona Mafundisho na Maagano 121:41. Hakika Mungu hutarajia sisi, watoto Wake wa hapa duniani, kutendeana hivyo, Yeye—mtu mkamilifu akiwa na maadili ya kila aina—angekuwa mfano wa tabia hiyo.

  9. Baraza kuu la Mbinguni ni tukio mahususi la kuonyesha tabia ya Mungu. Pale, Baba Yetu wa Mbinguni alielezea mpango wake kwa ajili ya ukuaji wetu wa milele. Mambo muhimu ya mpango huo yalijumuisha uhuru wa kuchagua, utifu, na ukombozi kupitia Upatanisho wa Kristo. Lusiferi, hata hivyo alipendekeza namna tofauti. Angehakikisha kuwa wote wangetii—na hakuna ambaye angepotea Njia pekee ya kufikia hili ni kwa kupitia udhalimu na ukandamizaji. Lakini Baba yetuwa Mbinguni mwenye upendo hangeruhusu mpango kama huo. Alithamini uhuru wa kuchagua wa watoto Wake Alijua lazima tutatenda makosa kwa namna fulani katika kujifunza kikweli. Na ndio maana alimtoa Mwokozi, ambaye dhabihu yake ya milele ingeweza kututakasa dhambi na kuturuhusu kuingia katika ufalme wa Mungu.

    Wakati Baba yetu wa Mbinguni aliona wengi wa watoto Wake wakishawishiwa na Lusiferi, je, aliwalazimisha kufuata mpango Wake? Je, aliwatisha au kuwaogopesha wale ambao walichagua chaguo hilo la kutisha? La. Mungu wetu mwenye nguvu hakika angeweza kuzuia uasi huu. Angelazimisha mapenzi Yake juu ya waasi na kuwafanya wakubali. Lakini badala yake, aliwaruhusu watoto Wake wachague wao wenyewe.

  10. 2 Timotheo 1:7.

  11. Ona, kwa mfano, Yoshua 1:9; Isaya 41:13; Luka 12:32; Yohana 16:33; 1 Petro 3:14; Mafundisho na Maagano 6:36; 50:41; 61:36; 78:18.

  12. Luka 12:32.

  13. Mafundisho na Maagano 68:11.

  14. Ushauri wa Musa kwa watu wake bado unafaa: “Usiogope. … Mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo”(Kutoka 14:13, Toleo la New King James).

  15. Kumbukumbu la Torati 31:6.

  16. Kutoka 14:14, Toleo la New King James.

  17. Isaya 54:17.

  18. Yohana 16:33.

  19. Mafundisho na Maagano 90:24; ona pia 2 Wakorintho 2:14; Mafundisho na Maagano 105:14.

  20. 1 Yohana 4:18.

  21. Na tukumbuke kuwa Mwokozi hakuja “ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye.” (Yohana 3:17). Kwa kweli, “hafanyi chochote ila tu kwa manufaa ya ulimwengu; kwani anapenda ulimwengu, hata kwamba anatoa maisha yake ili awavute wanadamu wote kwake. (2 Nefi 26:24).

  22. 1 Yohana 4:18; ona pia 1 Yohana 4:16.

  23. Marko 5:36.

  24. Yohana 15:10.