2018
Mambo Matatu ya Kukumbuka
February 2018


Vijana

Mambo Matatu ya Kukumbuka

Neno kumbuka linaonekana mara nyingi katika Kitabu cha Mormoni. Nefi aliwahimiza ndugu zake kukumbuka jinsi Mungu alivyowaokoa mababu zao. Mfalme Benyamini aliwaomba watu wake wakumbuke ukuu wa Mungu. Na Moroni aliwaagiza wasomaji wake wakumbuke jinsi Bwana amekuwa na huruma.

Kumkumbuka Mwokozi ni muhimu—hata tunaagana kumkumbuka kila wakati tunapopokea sakramenti. Rais Eyring anatualika tukumbuke mambo haya matatu wakati wa sakramenti.

  1. Mkumbuke Yesu Kristo: Soma maandiko kuhusu jinsi Mwokozi alivyohudumu na kuonyesha upendo kwa wengine. Unahisi vipi kuhusu upendo Wake? Ni namna gani unaweza kuhudumu na kuonyesha upendo kwa wengine jinsi Mwokozi alivyofanya?

  2. Kumbuka kile unachohitaji kuboresha: Tafakari kuhusu wiki yako iliyopita kwa moyo wenye kutaka kutubu. Chagua kitu kimoja ambacho unaweza kubadili, na uandike jinsi utakavyofanya maboresho hayo. Weka lengo lako mahali ambapo utaweza kuliona kila mara.

  3. Kumbuka maendeleo unayoyafanya: Muombe Mungu akuonyeshe maendeleo mazuri unayofanya. Weka kumbukumbu ya jinsi unavyohisi.

Sisi sio wakamilifu, lakini Mwokozi anafahamu hivyo. Ndio maana anatuomba tumkumbuke. Kumkumbuka kunatupatia matumaini na hutusaidia kutaka kufanya vizuri zaidi. Hata wakati ambapo tunashindwa kumkumbuka, Rais Eyring anasema, “Daima anakukumbuka.”