Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Februari 2018
Daima Mmkumbuke Yeye
Je, waweza kuvuta taswira pamoja nami nabii Moroni akiandika maneno ya mwisho ya Kitabu cha Mormoni kwenye mabamba ya dhahabu? Alikuwa peke yake. Alikuwa ameshuhudia nchi yake, watu wake, na familia yake ikiangamia. Nchi ilikuwa “daima ni mviringo” wa vita (Mormoni 8:8). Lakini bado alikuwa na matumaini, kwani alikuwa ameona siku zetu! Na katika vitu vyote ambavyo angeweza kuandika juu yake, alitualika tukumbuke (ona Moroni 10:3).
Raisi Spencer W. Kimball (1895–1985), alipenda kufundisha ya kwamba neno ambalo lilikuwa muhimu zaidi katika kamusi lingeweza kuwa ni kumbuka. Kwa sababu tumefanya maagano na Mungu, alisema, “mahitaji yetu muhimu zaidi ni kuyakumbuka”.1
Unaweza kulipata neno kumbuka kote katika maandiko. Wakati ambapo Nefi aliwaonya ndugu zake, mara nyingi aliwaalika wakumbuke maneno ya Bwana na wakumbuke jinsi ambavyo Mungu alikuwa amewaokoa babu zao (ona 1 Nefi 15:11, 25; 17:40).
Katika hotuba yake kuu ya buriani, Mfalme Benyamini alitumia neno kumbuka mara saba. Alitumai ya kwamba watu wake wangekumbuka “ukuu wa Mungu … na wema wake na subira yake” kwao (Mosia 4:11; ona pia 2:41; 4:28, 30; 5:11–12).
Wakati Mwokozi alipoanzisha sakramenti, Aliwaalika wanafunzi Wake wapokee zile ishara “kwa ukumbusho” wa dhabihu Yake (Luka 22:19). Katika kila sala ya sakramenti ambayo mimi na wewe husikiliza, neno daima linatangulia neno kumbuka (ona M&M 20:77, 79).
Ujumbe wangu ni mwaliko, hata ombi, la kukumbuka. Haya ni mapendekezo matatu kuhusu kile ambacho unaweza kukumbuka kila wiki wakati unapopokea ishara takatifu za sakramenti. Ninatumaini yatakusaidia kama yalivyokuwa kwangu.
Mkumbuke Yesu Kristo
Kwanza, mkumbuke Mwokozi. Kumbuka alikuwa nani alipokuwa duniani, jinsi alivyozungumza na wengine, na jinsi alivyoonyesha ukarimu katika matendo Yake. Kumbuka alishinda na kina nani na yale aliyofundisha. Mwokozi “akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema ” (Matendo ya Mitume 10:38). Aliwatembelea wagonjwa. Alikuwa amejitolea kutimiza mapenzi ya Baba Yake.
Zaidi ya yote, tunaweza kukumbuka gharama kubwa ambayo Alilipa, kutokana na upendo Wake kwetu, kutoa doa la dhambi zetu. Tunapomkumbuka, nia yetu kumfuata itakua. Tutataka kuwa wakarimu zaidi kidogo, wenye kusamehe zaidi, na wenye kutaka sana kutafuta kujua mapenzi ya Mungu na kuyatimiza.
Kumbuka Kile Unachohitaji Kukifanya Vyema Zaidi
Ni vigumu kufikiria kuhusu Mwokozi—Usafi na Ukamilifu Wake—bila ya kufikiria pia kuhusu jinsi tulivyo na dosari na tusio wakamilifu tukijilinganisha Naye. Tumefanya maagano kushika amri Zake, lakini mara nyingi tunashindwa kufikia kiwango hiki cha juu. Lakini Mwokozi alijua hili lingetokea, ndiyo maana alitupa ibada ya sakramenti.
Sakramenti ina mizizi katika agizo la Agano la Kale la kutoa dhabihu, ambalo lilijumuisha ungamo la dhambi (ona Mambo ya Walawi 5:5). Hatutoi dhabihu ya wanyama tena, lakini bado tunaweza kuacha dhambi zetu. Maandiko huita dhabihu hii ya “moyo uliyopondeka na roho iliyovunjika” (3 Nefi 9:20). Njoo kwenye sakramenti na moyo wenye kutubu (ona M&M 59:12; Moroni 6:2). Unapofanya hivyo, utapokea msamaha wa dhambi na hautapotea kutoka kwenye njia inayokurejesha kwa Mungu.
Kumbuka Maendeleo Unayofanya
Unapochunguza maisha yako wakati wa ibada ya sakramenti, ninatumai ya kwamba mawazo yako hayatalenga tu kwenye vitu ambavyo hukufanya vyema lakini pia kwenye vitu ambavyo umeweza kufanya vyema—nyakati ambazo umeweza kuhisi ya kwamba Baba wa Mbinguni na Mwokozi walikuwa wamefurahishwa nawe. Waweza hata kuchukua nafasi wakati wa sakramenti kumuuliza Mungu akusaidie uone mambo haya. Ikiwa utafanya hivyo, ninakuahidi utahisi kitu fulani. Utahisi matumaini.
Wakati nimefanya hivi, Roho amenithibitishia ya kwamba wakati bado niko mbali na ukamilifu, hali yangu ya leo ni bora kuliko ilivyokuwa jana. Na hili linanipa ujasiri kwamba, kwa sababu ya Mwokozi, ninaweza hata kuwa bora zaidi kesho.
Daima ni muda mrefu, na humaanisha juhudi zenye fokasi nyingi. Unafahamu kutokana na uzoefu jinsi ilivyo vigumu kufikiria moyoni kuhusu jambo moja kila wakati. Lakini bila kujali ni vizuri kiasi gani unavyoweka ahadi yako ya daima kumkumbuka, Yeye hukukumbuka daima.
Mwokozi anafahamu changamoto zako. Anafahamu jinsi gani ilivyo kuwa na shida za maisha zikiwa zinakulemea. Anajua jinsi unavyohitaji kwa haraka baraka ambayo hutokana na kumkumbuka daima na kumtii Yeye—“ili [wewe] uweze daima kupata Roho wake kuwa pamoja [nawe]” (M&M 20:77; imetiliwa mkazo).
Basi, Anakukaribisha tena kwenye meza ya sakramenti kila wiki, kwa mara nyingine akikupa nafasi ya kutoa ushuhuda mbele Yake kwamba daima utamkumbuka.
© 2018 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Imepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/17. Idhini ya kutafsiri: 6/17. Tafsiri ya First Presidency Message, February 2018. Swahili. 15046 743