UJUMBE WA URAIS WA ENEO
Penda, Tumikia na Hudumia Wengine
Tunapata motisha yetu ya kuwatumikia wengine katika kuelewa lengo la Mungu kwa ajili yetu sisi watoto Wake, ambalo ni kuleta kutokufa na uzima wa milele kupitia Yesu Kristo na Upatanisho Wake.
Katika ufunuo uliotolewa kupitia nabii Joseph Smith mnamo Juni 6, 1831, Bwana alitangaza: “Na tena, nitatoa kwenu utaratibu katika mambo yote” (M&M 52:14).
Utaratibu ni vielelezo, miongozo na njia ambazo mtu anapaswa kufuata ili kufungamana na lengo la Mungu, ambalo ni “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39).
Kote katika huduma yake ya duniani, Mwokozi na Mkombozi wetu Yesu Kristo ameonesha kwetu mfano mkuu kuhusu jinsi ya kupenda, kutumikia na kuwahudumia wengine. Yeye si tu alifundisha hilo bali Aliliishi hilo. Anatualika “tufuate nyayo zake” (1 Petro 2:21), kupenda kama Yeye alivyopenda, kutumikia kama Yeye alivyotumikia na Kuwahudumia wengine.
Rais Spencer W. Kimball (1895–1985) aliwasihi waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kujihusisha katika “matendo rahisi ya upendo na kutumikia”, kwani kuwahudumia wengine kutabariki maisha ya wengine kadhalika na ya kwetu wenyewe.1
Mama kijana aliyekuwa na safari ya ndege ya usiku akiwa na binti wa miaka miwili alikwamishwa na hali mbaya ya hewa uwanja wa ndege wa Chicago bila kuwa na chakula wala nguo safi kwa ajili ya mtoto na bila pesa. Alikuwa mjamzito na alikabiliwa na tishio la mimba kuharibika, hivyo alikuwa chini ya maelekezo ya daktari ya kutobeba mtoto isipokuwa tu ikiwa ilikuwa muhimu. Saa baada ya saa alisimama kutoka mstari mmoja hadi mwingine, akijaribu kupata ndege ya kwenda Michigan. Uwanja wa ndege ulikuwa na kelele, ukifurika abiria wenye uchovu mwingi, wasiwasi, hasira na alisikia marejeleo ya kukosoa kwa mtoto wake aliyekuwa akilia na kwake kwa kumsogeza mtoto sakafuni kwa kutumia mguu wakati mstari uliposonga mbele. Hakuna aliyejitolea kumsaidia mtoto aliyelowa, mwenye njaa na uchovu.
Kisha, mwanamke alisema baadaye, “mtu alikuja kwetu na kwa tabasamu la ukarimu alisema, ‘kuna chochote ninaweza kufanya kukusaidia?’ Kwa pumzi ndefu iliyojaa shukrani nilikubali msaada wake. Alimwinua binti yangu mdogo mwenye huzuni kutoka kwenye sakafu ya baridi na kwa upendo alimbeba wakati akimbembeleza kwa kumpapasa kwa upole kwenye mgongo wake. Aliuliza ikiwa mtoto angeweza kutafuna kipande cha peremende. Mtoto alipotulia, alimbeba na kusema jambo kwa ukarimu kwa wengine waliokuwa kwenye mstari mbele yangu, kuhusu jinsi nilivyohitaji msaada wao. Walionekana kukubali na kisha alikwenda kwenye meza ya tiketi [mbele ya mstari] na kufanya mpango na karani kwa ajili ya mimi kuwekwa kwenye ndege iliyokuwa iondoke punde. Alitembea pamoja nasi mpaka kwenye kiti, ambapo tulizungumza kwa dakika kadhaa, hadi pale alipopata uhakika kwamba ningekuwa salama. Kisha aliondoka zake. Takribani wiki moja baadaye niliona picha ya Mtume Spencer W. Kimball na nilimtambua kuwa alikuwa ndiye yule mtu ambaye sikumfahamu katika uwanja wa ndege.”
Miaka kadhaa baadaye, Rais Kimball alipokea barua iliyosomeka kwa sehemu:
“Mpendwa Rais Kimball:
Mimi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Brigham Young. Nimerudi punde tu kutoka misheni yangu huko Munich, Ujerumani ya Magharibi. Nilikuwa na misheni ya kupendeza na nimejifunza mengi. . . .
Nilikuwa nimeketi kwenye mkutano wa ukuhani wiki iliyopita wakati hadithi iliposimuliwa ya huduma ya upendo ambayo uliitoa miaka ishirini na moja iliyopita katika uwanja wa ndege wa Chicago. Hadithi ilisimulia jinsi ulivyokutana na mama mjamzito kijana akiwa na mtoto aliyepiga kelele, akiwa katika huzuni, akingojea tiketi yake katika mstari mrefu. Alikuwa na tishio la mimba kuharibika na hivyo hakuweza kumwinua mtoto wake ili kumsaidia. Alikuwa amepitia uharibifu wa mimba kwa awamu nne, jambo ambalo lilitoa sababu za ziada kwenye maagizo ya daktari ya kutoinama wala kunyanyua kitu.
Ulimfariji mtoto aliyekuwa akilia na kuelezea mtanziko kwa abiria wengine waliokuwa kwenye mstari. Tendo hili la upendo liliondoa mzigo na hofu kutoka kwa mama yangu. Nilizaliwa miezi kadhaa baadaye huko Flint, Michigan.
Ninataka tu kukushukuru kwa upendo wako. Asante kwa mfano wako wa huduma.”2
Mzee Joseph B. Wirthlin wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha: “Upendo ni mwanzo, kati na mwisho wa njia ya ufuasi. Unafariji, unashauri, unaponya na kuhimiza. . . .
Upendo ni amri kuu—zingine zote zinaning’inia juu yake. Upendo ni fokasi yetu kama wafuasi wa Kristo aliye hai”3.
Watu waliomfuata Alma nyikani walijinyenyekeza baada ya kupokea neno la Mungu lililofundishwa na nabii Alma. Walifanya agano—licha ya hali zao, changamoto zao na mazingira yao—kuitwa watu wa Mungu, kubebeana mizigo, kuomboleza pamoja na wale wanaoomboleza, kuwafariji wale wanaohitaji kufarijiwa na daima kusimama kama mashahidi wa Mungu. Maisha yao yalibadilika: walikuwa waongofu kwa Bwana na kuungana na kanisa Lake na inasema kwamba viongozi wa Kanisa katika siku ya Alma, “waliwalinda watu wao, na kuwalisha vitu vilivyohusu haki” (ona Mosia 23:18).
Kote katika maisha yangu, nimegundua kwamba wakati mtu anapoelewa baraka za nguvu ya maagano yaliyofanywa kupitia ubatizo, bila kujali amekuwa muumini wa Kanisa kwa muda gani, yeye huchukulia miito na majukumu yake kanisani kwa shauku na shangwe kuu.
Agano Jipya halina kumbukumbu ya matukio yote yaliyotukia kipindi cha Mlo wa Mwisho wa Kristo na mitume wake. Baadhi ya matukio muhimu yaliyotukia wakati wa Mlo, ni wakati Mwokozi Yesu Kristo alipoinuka na kujifunga Yeye mwenyewe kama mtumishi na kupiga magoti ili kuosha miguu ya mitume (ona Yohana 13:3–17). Ni mfano wa kupendeza ulioje tunaojifunza kutoka kwa Mwokozi wa jinsi ya kuwahudumia wengine. Yeye anatualika kuweka dhamiri na kujitolea maisha yetu kama waumini wa Kanisa kuwatumikia akina kaka na akina dada wenzetu, hata wale ambao si waumini wa Kanisa.
Mwokozi alifundisha: Yeye aliye mkuu kati yenu, na awe mtumwa wenu. (Ona Matayo 23:11, Luka 22:26.)
“Amri mpya nawapeni, alisema, pendaneni, kama nilivyowapenda ninyi, nanyi pia pendaneni.
Kwa hili watu wote watajua kwamba ninyi ni wafuasi wangu, ikiwa mmependana ninyi kwa ninyi” (Yohana 13:34–35).
Ninawaalikeni, kaka zangu na dada zangu wapendwa, kupenda, kutumikia na kuwahudumia wengine kama vile ambavyo Mwokozi angefanya na ninaahidi kwamba maisha yetu wenyewe yatajazwa na nuru na shangwe pale tunapofuata mfano wa Mwokozi.
Thierry K. Mutombo aliidhinishwa kama Sabini Mkuu mwenye Mamlaka mnamo Aprili 2020.Amemuoa Tshayi Nathalie Sinda; wao ni wazazi wa watoto sita.