2021
Kuhudumu: Njia ya kujenga Kanisa katika mioyo ya watakatifu
Oktoba 2021


UJUMBE WA KIONGOZI WA UKUHANI

Kuhudumu: Njia ya kujenga Kanisa katika mioyo ya watakatifu

Huduma kama ya Mwokozi huja kutoka kwenye upendo wa dhati kwa Mwokozi na upendo kwa wale ambao ametupatia sisi fursa ya kuwasaidia.

Mpango wa Baba yetu wa Mbinguni unatarajia kwamba sisi tuje duniani, kujaribiwa na kujaribu kufuzu kurudi na kuishi katika uwepo Wake. Kila mwanadamu anayeishi au aliyepata kuishi duniani atapata fursa ya kupokea wokovu au uzima wa milele, ambao humaanisha “kuwa kama Mungu”, na kuishi milele kama familia katika uwepo Wake.

Bila msaada kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni, ingekuwa vigumu kwetu sisi kufikia kutokufa na uzima wa milele, hii ndiyo sababu Akamtuma Mwanaye wa pekee ili atukomboe kupitia dhabihu Yake ya upatanisho. Katika Yohana 3:16, tunasoma: “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Tangu enzi za Agano la Kale, Baba yetu wa Mbinguni amewaita manabii kuwaongoza watu Wake, kama ilivyo katika Amosi 3:7, inayosomeka: “Hakika Bwana MUNGU hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.” Kupitia manabii, Anafikisha ujumbe wake kwa watoto Wake.

Tunaye nabii aliye hai leo ambaye sote tunamkubali. Mnamo Aprili 2018, Bwana alimfunulia nabii Wake kile Alichokitaka kwa ajili ya watu Wake na Rais Russell M. Nelson alizungumza kuhusu utekelezaji wa kuhudumu kwa maneno haya: “Sasa tunaenda kutangaza njia mpya na takatifu zaidi ya kuwajali ndugu zetu na kuwatumikia.”1 Tunajua kwamba kuna tofauti mbili kuu kati ya kuhudumu na mafundisho ya nyumbani au mafundisho ya kutembeleana nyumbani na kwamba tulizoea kufanya katika kipindi cha nyuma, yafuatayo:

  1. Upendo wa dhati kwa kila mmoja na

  2. Kuvuviwa

Upendo wa dhati kwa kila mmoja

“Upendo ni kipimo cha imani yetu, himizo la utiifu wetu na kipimo halisi cha ufuasi wetu,” alisema Mzee Dieter F. Uchtdorf katika mahubiri ya Mkutano Mkuu wa 2009.2

Na kutumikia ni kuwasaidia wale wanaohitaji msaada. Huduma kama ya Kristo hutoka katika upendo wa dhati kwa Mwokozi na katika upendo kwa ajili ya hao aliotupatia fursa ya kuwasaidia.

Kazi hii ya kuwatumikia wengine huongozwa na kanuni kuu mbili: Kumpenda Mungu na kumpenda jirani yetu, kama ilivyo katika Mathayo 22:37–39: “Akamwambia, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.

“Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza.

“Na ya pili yafanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako.”

Utiifu kwa amri hizi huturuhusu sisi kupata amani na shangwe zaidi katika ulimwengu huu. Kama tutampenda na kumtumikia Bwana, na kumpenda na kumtumikia jirani yetu, tutapata shangwe zaidi ambayo huja kwetu katika hali kamilifu.

“Kumpenda Mungu na jirani yetu ni msingi wa kimafundisho wa kuhudumu, wa kujifunza kunakolenga nyumbani kunakokubaliwa na Kanisa, wa kazi ya wokovu katika pande zote mbili za pazia. Haya yamejikita juu ya amri takatifu ya kumpenda Mungu na jirani yetu,” alisema M. Russell Ballard, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili3.

Upendo ni zaidi ya hisia tu; tunaposema tunawapenda kaka na dada zetu, inamaanisha kwamba tunataka kuwasaidia. Mathayo 20:26–27 inasomeka kama ifuatavyo: “Bali mtu yeyote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu;

“Na mtu yeyote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu.”

Baada ya kuuliza swali, “Ni kwa jinsi gani tunakuwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo?” Mzee Dieter F. Uchtdorf alisema kwamba Mwokozi alilijibu swali hili yeye mwenyewe aliposema: “Kama wanipenda, zishike amri zangu”.4 Hiki ni kiini cha kile inachomaanisha kuwa mfuasi wa kweli wa Bwana.

Wale wanaompokea Bwana Yesu Kristo hutembea pamoja Naye na kushika amri Zake. Katika Mosia 15:14, tunasoma: “Na hawa ndiyo wameitangaza amani, walioleta habari njema ya mambo mazuri, ambao wametangaza wokovu; na kuiambia Sayuni: Mungu wako anatawala!” Kuhudumia huleta amani, shangwe na habari njema kwa wale wanaohisi upweke na kutengwa. Tunahitaji kuwafundisha watoto wetu upendo kwa familia, kwa kaka na dada zetu na kwa majirani zetu.

Kuvuviwa

Tunajenga Kanisa katika mioyo ya kaka na dada zetu pale tunapohudumu vyema. Siku moja, wakati nikihudumu kama Rais wa Kigingi cha Lubumbashi, Roho wa Bwana alinipa msukumo wa kumpa pete rafiki wa kata ya Lubumbash Second. Nilikuwa na misukumo hii siku nzima na hatimaye niliamua kumpigia nilipofika kazini. Hiki ndicho kilichotokea: Alipiga kelele, “Rais, nashangaa kwamba umenipigia wakati huu! Punde tu nilikuwa na mjadala na mchungaji wa Kiprotestanti ambaye ameonekana kunishawishi! Simu yako imeniimarisha; huu ni uthibitisho kwamba tuko katika Kanisa la kweli la Bwana.” Nilimjibu: “Kaka yangu, sisi ni waumini wa Kanisa la Bwana; hili ni Kanisa lake, tunahitajika kusimama imara bila kujali magumu yote tunayoweza kupitia maishani. Sisi ni wa Kanisa la Bwana, hakuna hata mmoja atakayetutenganisha sisi na upendo wake, na hakuna anayeweza kubadili hilo.”

Simu hii ilimsaidia kaka yangu kusimama imara akiwa na imani zaidi kwa Bwana, kwa kuwa alikuwa muumini wa Kanisa kwa miaka miwili.

Katika M&M 42:14, tunasoma: “Na msipompokea Roho msifundishe.” Ni sawa kwamba tunapaswa kumtafuta Roho, kwa sababu kuhudumu ni kuwa sawa na Roho wa Bwana. Kama kaka na dada wahudumiaji, sote na tuishi katika hali ya kuweza kuhisi Roho wa Bwana katika kila kitu tukifanyacho ili kwamba tuweze kuvuviwa.

Alma na kaka zake walisaidia kuwarudisha wazoramu kwa Bwana, na kuwahudumia. Kwa kuwa Alma Alitambua kwamba kazi haikuwa nyepesi, aliwaita kaka zake na kutoa sala ifuatayo: “Ee Bwana, utukubalie sisi kwamba tuwe na mafanikio kwa kuwaleta kwako tena katika Kristo.

“Tazama, Ee Bwana, roho zao ni za thamani, na wengi wao ni ndugu zetu; kwa hivyo, tupatie, Ee Bwana, uwezo na hekima kwamba tuwalete hawa, ndugu zetu, tena kwako” (Alma 31:34–35).

Kupitia sala, tunapokea msaada kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni, na tutakuwa na nguvu ya kutosha kutimiza kile ambacho Bwana anakitarajia kutoka kwetu, watoto Wake.

Ningependa kuhitimisha mahubiri yangu kwa fungu linalopatikana katika 2 Nefi 32:8–9, linalosomeka kama ifuatavyo: “Na sasa, ndugu zangu wapendwa, naona kwamba bado mnatafakari mioyoni mwenu; na inanihuzunisha kwamba lazima nizungumze kuhusu kitu hiki. Kwani ikiwa mtasikiliza Roho ambaye anawafundisha wanadamu kusali, mtajua kwamba lazima msali, kwani roho mchafu hawafundishi mwanadamu kusali, lakini humfundisha kwamba lazima asisali.

“Lakini tazameni, nawaambia kwamba lazima msali kila wakati, na msife moyo; na kwamba msifanye lolote kwa Bwana bila kumuomba Baba kwa jina la Kristo, kwamba awatakasie matendo yenu, kwamba matendo yenu yawe ni kwa ajili ya ustawi wa nafsi yako.”

Tunajua kwamba kuhudumu kunafanywa kwa kuvuviwa; kwa hivyo, kama wazazi, tunaalikwa kuwafunza watoto wetu jinsi Bwana anavyojibu wakati tunapofanya vitu Anavyotuhitaji sisi tufanye. Katika M&M 82:10, tunasoma, “Mimi, Bwana, ninafungwa wakati ninyi mnapofanya ninayosema; lakini msipofanya ninayosema, ninyi hamna ahadi.”

Akina kaka na akina dada, ninajua kwamba Russell M. Nelson ni nabii wa Mungu, Bwana amemlinda ili awe chombo katika mikono Yake kwa wakati huu. Mnamo Aprili 2018, Bwana alifunua kwa nabii ufunuo juu ya kuhudumu, na mnamo Oktoba 2018 funuo zingine mbili kuhusu Njoo, Unifuate na mabadiliko ya muda wa ibada ya Jumapili inayofokasi nyumbani zilikuja. Kwa wakati huo hatukujua kwamba ulimwengu huu utaharibiwa na janga la ulimwengu, kwamba milango ya kumbi zetu za mikutano ingefungwa na kwamba kila baba angeandaa sakramenti nyumbani. Tunatoa shukrani kwa Bwana kwa kuliongoza Kanisa Lake leo duniani kupitia nabii aliye hai, Russell M. Nelson.

Pungwe S. Kongolo aliitwa kama Sabini wa Eneo mnamo Aprili 2018. Amemuoa Séraphine Mugo Ngwezya. Wao ni wazazi wa watoto wawili. Mzee na Dada Kangolo wanaishi Lubumbashi, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Ministering,” Liahona, May 2018, 100.

  2. Dieter F. Uchtdorf, “The Love of God,” Liahona, Nov. 2009, 24.

  3. M. Russell Ballard, “The True, Pure, and Simple Gospel of Jesus Christ,” Liahona, May 2019, 29.

  4. See Dieter F. Uchtdorf, “The Love of God,” 21.