Jioni ya Nyumbani Ni Nini? Liahona, Agosti 2022.
Ujumbe wa Kila Mwezi wa Gazeti la Liahona Agosti 2022
Jioni ya Nyumbani Ni Nini?
Jioni ya nyumbani ni wakati uliotengwa katika wiki kwa ajili ya familia kukusanyika pamoja. Wakati huu, mnaweza “kujifunza injili, kuimarisha shuhuda, kujenga umoja na kufurahiana” (Kitabu cha Maelezo Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 2.2.4, ChurchofJesusChrist.org). Jioni ya nyumbani huonekana kwa njia fulani tofauti kwa kila familia. Lakini lengo ni kutumia wakati huu ili kuwa karibu pamoja na kumsogelea zaidi Mwokozi.
Maandalizi
Fikiria shughuli ambayo familia yako hufurahia na mada ya injili ambayo ungependa kuijadili na kujifunza juu yake kwa pamoja. Pia, chagua siku na muda kila wiki ambapo wanafamilia wengi au wote wanaweza kukutana. Kanisa linawahimiza waumini kufanya jioni ya nyumbani usiku wa Jumatatu. Lakini wanafamilia wanaweza kukutana wakati unaofaa kwao.
Sala
Familia nyingi huanza na kumalizia jioni ya nyumbani kwa sala. Hii humwalika Roho Mtakatifu katika nyumba yao. Jioni ya nyumbani ni wakati muafaka kwa ajili ya watoto na watu wazima kujifunza kusali katika kundi dogo.
Muziki
Familia nyingi pia zinakuwa na wimbo wa kufungua na kufunga. Kwa kawaida wanachagua wimbo kutoka katika kitabu cha nyimbo za dini au kitabu cha nyimbo za watoto. Kanisa lina rekodi za piano za nyimbo katika music.ChurchofJesusChrist.org. Mnaweza pia kutazama video za Kwaya ya Tabernacle katika Temple Square. Kuimba wakati wa jioni ya nyumbani huwasaidia waumini kujifunza nyimbo ambazo zinaimbwa kanisani.
Somo
Kanisa lina nyenzo nyingi ambazo zinaweza kusaidia katika jioni ya nyumbani. Ungeweza kuchukua dakika chache kusoma na kujadili makala kutoka katika Liahona, Rafiki, au Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana. Huu unaweza pia kuwa wakati wa kutazama na kujadili video za Kanisa. Au mngeweza kusoma hotuba kutoka katika mkutano mkuu, kusoma maandiko, au kujadili usomaji wa wiki hii katika Njoo, Unifuate.
Ushiriki wa Familia
Watoto wanaweza kushiriki katika jioni ya nyumbani. Wanaweza kusaidia kupanga shughuli, kusali, au kuchagua na kuongoza nyimbo. Wanaweza hata kufundisha masomo. Kabla ya jioni ya nyumbani, unaweza kumsaidia mtoto wako kusoma hadithi katika gazeti la Rafiki au hadithi zao pendwa za maandiko. Mtoto kisha anaweza kusimulia hadithi hiyo kwa familia kama somo. Watoto wengi pia wanapenda kuigiza hadithi za maandiko katika jioni ya nyumbani. Waache watoto wakubwa kupanga somo au kuchagua hotuba ya mkutano mkuu ambayo wangependa kusoma. Kisha waache wao waongoze mjadala.
Shughuli
Familia nyingi zinafurahia kufanya shughuli kama sehemu ya jioni ya nyumbani. Shughuli za ndani ya nyumba zinaweza kujumuisha kucheza michezo, kutengeneza vitu, au kupika pamoja.
Kwa ajili ya shughuli za nje mngeweza kutembea, kwenda kwa matembezi ya masafa kama familia, au kucheza mchezo wa nje pamoja. Tafuta shughuli ambayo wanafamilia wote wanaweza kufanya, na kufurahia pamoja. Epuka nyakati za kushindana ambazo zinaweza kumfukuza Roho.
Huduma
Jioni ya nyumbani ni wakati mzuri sana kwa ajili familia kuwahuhumia wengine. Mngeweza kuwasaidia baadhi ya majirani wakongwe, kutoa chakula kwenye makazi ya wasio na malazi, kuwaandikia barua wamisionari, au kuzoa taka, kama mfano.
© 2022 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Limepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kiingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly Liahona Message, August 2022. Swahili. 18316 743