2022
‘Kutoa dhabihu zako kwa Aliye Juu Sana’
Agosti 2022


UJUMBE WA URAIS WA ENEO

‘Kutoa dhabihu zako kwa Aliye Juu Sana’

Ni ishara ipi tunamwonesha Bwana kwamba tunaitakasa siku Yake takatifu?

Miaka mingi iliyopita wakati nikiwa mvulana mdogo kipindi cha muongo wa miaka ya 1960, ningehudhuria kanisani pamoja na familia yangu kila Jumapili. Wakati huo, tungehudhuria shule ya Jumapili asubuhi na mkutano wa sakramenti baadaye mchana. Nakumbuka kuhudhuria shule ya Jumapili ya watoto, nikiwa nimeketi kwenye chumba cha Msingi pamoja na watoto wengine wakati tukiimba nyimbo za Msingi kama vile, “Jesus Once was a Little Child,” “I Wonder When He Comes Again,” na “I am a Child of God.” Jumapili moja ya kipekee, nilipokuwa nikiimba pamoja na watoto wengine, nilihisi hisia nzuri zikijaza moyo wangu. Zilitoka moyoni mwangu hadi kwenye kifua changu na kisha zikajaza mwili wangu wote. Zilikuwa hisia ambazo zilileta amani ndani ya nafsi yangu. Katika wasaa ule, nilihisi uzoefu wangu wa kwanza wa Roho Mtakatifu akishuhudia kwangu kwamba Mungu Baba yu hai na kwamba alinifahamu. Ulikuwa uzoefu rahisi, lakini ulikuwa wa kupendeza kwangu, uzoefu ninaoukumbuka dhahiri zaidi ya miaka hamsini baadaye.

Tunaposhiriki katika shughuli za siku ya Sabato ambazo zinatuleta karibu na Mungu, tunafungua mlango kwa Baba wa Mbinguni mwenye upendo kuwasiliana nasi—kutujulisha kwamba Yeye anatujua sisi pamoja na mahitaji yetu. Yeye amesema, “Sogeeni karibu nami na mimi nitasogea karibu na nyinyi; nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata; ombeni, nanyi mtapewa; bisheni, nanyi mtafunguliwa”1.

Tunapoitakasa siku ya Sabato, tunafungua pia mlango kwa ajili ya Baba wa Mbinguni kubariki maisha yetu. Katika injili ya Luka, tunajifunza juu ya uzoefu wa mwanamke aliyekuwa na “pepo wa udhaifu muda wa miaka kumi na minane, naye amepindana, hawezi kujinyosha kabisa”2. Hata pamoja na udhaifu wake, alimwabudu Mungu kwa kuhudhuria kanisani (katika tukio hili, sinagogi) siku ya sabato. Katika macho ya akili yangu, ninamfikiria akihangaika kutembea kuingia ndani ya sinagogi. Siku moja ya kipekee, wakati mwanamke huyu mwaminifu alipohudhuria kanisani, Yesu aliingia na kumwona na “alimwita na akamwambia, Mama, umefunguliwa katika udhaifu wako.

Akaweka mikono yake juu yake, naye akanyoka mara hiyo, akamtukuza Mungu”.3

Hakuteseka tena kwa ugonjwa wake wa mwili. Alikuwa akimwabudu Mungu kwa uaminifu na aliponywa kulingana na muda wa Baba yake wa Mbinguni mwenye upendo. Je angeweza kuponywa kama asingehudhuria kanisani siku ile? Je, wewe na mimi tunaweza kuponywa kwa kuhudhuria kanisani? Maandiko yanafundisha kwamba Mungu anao uwezo wa kuponya kimwili na kiroho. Kwa Mungu, yote yanawezekana4—lakini ni kulingana na mapenzi Yake na muda Wake.

Wakati Mungu alipoumba dunia hii ya kupendeza, mwishoni mwa juhudi Zake, Alipumzika kutoka kazi Zake. Aliifanya siku ya saba kuwa siku iliyotukuka, takatifu; siku ambapo mawazo yetu na moyo wetu wa ibada vinapaswa kumgeukia Yeye. Yeye ametuamuru tuitakase sabato. “Kwani amini hii ndiyo siku iliyoteuliwa kwako kupumzika kutokana na kazi zako, na utoe dhabihu zako za shukrani kwa Aliye Juu Sana”5. Rais Nelson alitualika kuzingatia ni ishara ipi tunamwonesha Bwana kwamba tunaitakasa siku ya Sabato6. Ni kipi tunafanya siku ya Sabato kumwonesha Mungu kwamba tunatii amri Yake kuhusu siku ya Sabato?

Njia mojawapo ya kuonesha uaminifu wetu kwa Mungu ni kumwabudu Yeye.Katika hali yake ya uhalisia, neno la Kiebrania “avodha” humaanisha “kazi, kuabudu na huduma” na lilirejelea dhabihu iliyotolewa ndani ya hekalu huko Yerusalemu. Tunapomwabudu Mungu, tunamtumikia na kuifanya kazi Yake, ikiwa ni pamoja na kukuza miito yetu. Tunapohudhuria kanisani na kupokea sakramenti kwa kustahili, tunamwabudu Mungu. Tunapowahudumia wale wanaotuzunguka, ikiwa ni pamoja na wana familia wetu, kuwasaidia kuwa wafuasi wazuri zaidi wa Yesu Kristo, tunamtumikia Mungu. “Mnapowatumikia wanadamu wenzenu mnamtumikia tu Mungu wenu”7. Kwa wale wanaoitakasa siku ya Sabato kwa kumwabudu Mungu, Yeye anatoa ahadi yenye nguvu na ya wazi—na Mungu daima anatimiza ahadi Zake. Anatuambia “kadiri mtakavyofanya hivi, vyote viijazavyo dunia ni mali yenu,” kwamba “tutalindwa na dunia pasipo mawaa,” kwamba “shangwe yetu iweze kuwa timilifu,” na kwamba tutapokea “amani katika ulimwengu huu, na uzima wa milele katika ulimwengu ujao8.

Katika Mkutano Mkuu wa Oktoba, Rais Nelson alitoa ushauri ufuatao: “Hakuna kinachomwalika Roho zaidi ya kuweka fokasi yako kwa Yesu Kristo. Zungumzeni kuhusu Kristo, furahini katika Kristo, sherehekeeni maneno ya Kristo na msonge mbele mkiwa na imani imara kwa Kristo. Fanya sabato yako kuwa ya furaha pale unapomwabudu Yeye, unapopokea sakramenti na kuitakasa siku yake”9.

Wakati ukisoma haya, ni misukumo ipi imekujia kuhusu ishara ipi utakayomwonesha Mungu? Ninakualika ufanyie kazi misukumo hiyo. Unapoitakasa siku ya Sabato kulingana na maelekezo ya Mungu, baraka za kimwili na kiroho zitatiririka kwenye maisha yako.

Muhtasari

  1. Mafundisho na Maagano 88:63.

  2. Ona Luka 13:11.

  3. Luka 13:12–13.

  4. Ona Matayo 19:26; Marko 10:27.

  5. Mafundisho na Maagano 59:10.

  6. Ona Russell M. Nelson, “Sabato ni ya Furaha,” Mkutano Mkuu wa April 2015.

  7. Mosia 2:17.

  8. Ona Mafundisho na Maagano 59:9, 13, 16, 23.

  9. Russell M. Nelson, “Tenga Muda kwa ajili ya Bwana,” Liahona, Novemba 2021, 120–121.

Chapisha