2022
Makaribisho ya Urais Mpya wa Eneo
Agosti 2022


Habari za Eneo

Makaribisho ya Urais Mpya wa Eneo

Mnamo Agosti, Eneo la Kati la Afrika liliukaribisha Urais mpya wa Eneo. Viongozi hawa wa ukuhani husimamia nchi zilizopo eneo la kati la Afrika. Wanawajibika kwa Urais wa Sabini.

Matthew L. Carpenter ndiye Rais wa Eneo la Kati la Afrika. Alizaliwa huko Jijini Salt Lake, Utah, mnamo tarehe 21 Oktoba 1959. Alimuoa Michelle (Shelly) Kay Brown mnamo 1982. Wao ni wazazi wa watoto watano.

Alitunukiwa shahada ya sayansi katika utawala wa biashara kutoka Chuo Kikuu cha Brigham Young mnamo 1983. Mnamo 1987 alipokea shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara kutoka Kitivo cha Biashara cha Harvard.

Amehudumu katika miito kadhaa ya Kanisa, ikiwemo kuwa mmisionari katika Misheni ya Switzerland Geneva, mmisionari wa kata, kiongozi wa skauti, rais wa kigingi wa Wavulana, mshauri kwenye uaskofu, mshauri katika urais wa kigingi wa misheni, kiongozi wa kata wa wamisionari, mshauri mkuu, askofu na rais wa kigingi.

Kabla ya wito huu, Mzee Carpenter alikuwa akihudumu kama Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Eneo la Kati la Afrika. Kabla ya kupokea miito kwenye urais wa Eneo la Kati la Afrika amehudumu kama Sabini wa Eneo katika Eneo la Kati la Amerika ya Kaskazini, Msaidizi wa Urais wa Eneo la Utah, kama mshauri katika Urais wa Eneo la Kati la Amerika ya Kaskazini na katika kamati anuai kwenye Makao Makuu ya Kanisa.

Wakati wa taaluma yake ya kazi, amefanya kazi kama afisa mkuu wa maswala ya fedha, rais na afisa mkuu mtendaji wa taasisi anuai za kibiashara zinazohusika na fedha.

Thierry K. Mutombo ndiye Mshauri wa Kwanza katika Eneo la Kati la Afrika. Alizaliwa Kinshasa, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, tarehe 31 Januari 1976. Amemuoa Tshayi Nathalie Sinda mnamo 2002. Wao ni wazazi wa watoto sita.

Alihitimu katika maswala ya utawala wa biashara kutoka Chuo Kikuu cha Cepromad mnamo 2010 na mnamo 2012 alipata shahada ya kwanza katika utawala wa rasilimali watu kutoka chuo kikuu hicho hicho.

Amehudumu katika miito kadhaa ya Kanisa, ikiwemo kuwa mmisionari katika Misheni ya Côte d’Ivoire Abidjan, kiongozi wa wamisionari wa kata, mwalimu wa kata wa Shule ya Jumapili, katibu mtendaji wa kigingi, mshauri katika urais wa kigingi, rais wa kigingi na rais wa Misheni ya Maryland Baltimore.

Wakati anaitwa kwenye wito wake, alikuwa akihudumu kama Mshauri wa Pili katika Urais wa Eneo la Kati la Afrika.

Aliwahi kumiliki biashara ya usafirishaji kutoka mwaka 2000 mpaka 2005. Amewahi kuajiriwa na Kanisa kama msimamizi katika Kitengo cha Utawala wa Nyenzo na meneja wa Kitengo cha Rasilimali Watu huko Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo. Hivi karibuni alifanya kazi kama meneja wa Kitengo cha Historia ya Familia huko Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.

Ian S. Ardern ndiye Mshauri wa Pili katika Urais wa Eneo la Kati la Afrika. Alizaliwa huko Te Aroha, New Zealand, tarehe 28 Februari 1954. Alimuoa Paula Ann Judd mnamo Januari 1976. Wao ni wazazi wa watoto wanne.

Alipata shahada ya kwanza kwenye masuala ya elimu mnamo 1982 na shahada ya uzamili kwenye masuala ya elimu kutoka Chuo Kikuu cha Waikato huko New Zealand mnamo 1994.

Amehudumu katika miito kadhaa ya Kanisa, ikiwemo kuwa mmisionari huko Ufarasa na Ubelgiji, rais wa kigingi wa Wavulana, mshauri mkuu, mshauri katika uaskofu, askofu, mshauri katika urais wa kigingi, rais wa Misheni ya Fiji Suva, sabini wa Eneo na Rais wa Eneo la Pacific.

Mnamo 1981 alijiunga na Mfumo wa Elimu wa Kanisa kama mwalimu na baadaye alikuwa mkuu wa chuo wa Chuo cha Kanisa cha New Zealand. Mnamo 2004 alikuwa mkurugenzi wa Mfumo wa Elimu wa Kanisa katika Eneo la Pacific na baadaye alifanya kazi kama mkurugenzi wa chuo na mratibu wa seminari kwa ajili ya Mfumo wa Elimu wa Kanisa huko New Zealand.