Habari za Eneo Husika
Pathway Ulimwenguni kote = Elimu kwa Ajili ya Kazi Nzuri
Elimu ya juu, ya gharama nafuu inatengeneza njia kwa ajili ya maisha mazuri kwa Waafrika wengi.
BYU Pathway Ulimwenguni kote ilitambulishwa miaka michahce iliyopita kwenye nchi za Afrika na inabariki maisha ya wengi kwenye bara la Afrika. Tayari imehudumia karibu wanafunzi 2,000, waumini na wasio waumini vilevile. Wamisionari waliorejea nyumbani wanathibitishwa mapema kwa ajili ya BYU–Pathway na wanapewa punguzo la 25% pale wanapojiunga. Wanafunzi wote pia ni wastahiki wa Udhamini wa Heber J. Grant, ambao unaweza kupunguza ada yao kwa hadi 50%. Kwa nyongeza, wanafunzi wasiozungumza Kingereza wana fursa ya kujifunza Kingereza kupitia EnglishConnect na kisha kujiandikisha kwenye PathwayConnect. Wanafunzi wengi wanakiri kupata ajira, kupandishwa cheo au kukuza biashara zao za sasa wakati wakiendelea na shahada ya kwanza.
Annet Nankumba wa Kata ya Upperhill Nairobi, Kenya, kwa mara ya kwanza alijua kuhusu BYU–Pathway kutoka kwa Rais wake wa Misheni huko Cote d’Ivoire. Kutokana na viwango vyake vya chini katika shule ya sekondari, Annet alikuwa na hofu kuhusu kujiunga na elimu ya chuo. Miezi michache baada ya kurejea kutoka misheni yake, aliamua kujiandikisha kwenye PathwayConnect na kuanza safari yake kuelekea shahada ya kwanza. Hii itamfanya kuwa mhitimu wa kwanza wa chuo kwenye familia yake. “PathwayConnect imekuwa baraka kubwa kwangu. Moja ya kozi zangu za mwanzo, ilinifunza kuhusu kuwa na mtazamo wa ukuaji. Tofauti na hapo kabla, sasa ninaona kushindwa kama fursa ya kukua,” alisem.
Annet anaendelea kueleza, “Mtu mwenye mtazamo usiobadilika huogopa kushindwa, hukata tamaa mapema wakati mambo yanapokuwa magumu na hujiona wao kama hawana akili nyingi. Ili kufokasi kwenye njia yangu ya elimu, ninapaswa kuwa chanya na kumtumaini Baba yangu wa Mbinguni ambaye atanisaidia kupita changamoto”. Annet anasema amejifunza pia usimamizi mzuri wa fedha, ambao unamsaidia katika biashara yake ndogo. “Nimejifunza kuweka kipaumbele kwenye ulipaji wa zaka na sasa ninahisi mwongozo zaidi wa Mwokozi wangu katika maisha yangu. Ninapata msukumo kwa ibada fupi za kila wiki na chuo cha madarasa ya kanisa; yote haya husaidia kuongeza imani yangu katika Mwokozi. Ninajua kwamba ninaweza kufanya mambo magumu!”
Phineas Nyambita pamoja na mkewe, Caroline, wote ni wanafunzi wa BYU–Pathway. Phineas ni mmisionari aliyerejea na anahudumu kama rais wa tawi katika tawi lake huko Dar es Salaam, Tanzania. Phineas, akisomea Shahada ya kwanza ya Teknolojia, alisema, “ninaifurahia programu kwa sababu ninafanya kazi kutwa nzima na kuhudhuria madarasa yangu. Kuwa mume na baba, kiongozi wa kanisa na kuongeza jukumu lingine kama mwanafunzi inaweza kuonekana ya kuchosha. Lakini nimeona kwamba inawezekana kwa mafanikio makubwa.” Akizungumza na vijana wakubwa katika Tawi la Chang’ombe na popote pale, Phinias anatoa ushauri huu: “Ninajua kwamba Bwana anatutaka tuwe na mafanikio katika maisha haya.
“Hata hivyo, kuwa mwenye mafanikio hakuwezi kuja ikiwa hatutendi kwa imani. Tunaweza kuwa na mengi ya kufanya kama akina baba, akina mama, viongozi na vijana wakubwa. Tunaweza kuwa wenye mafanikio kwa kuwa na imani na hamu ya kujifunza jinsi ya kuweka vipaumbele. BYU–Pathway itawasaidia wale wote wanaotaka kuendeleza elimu yao ili waweze kujenga msingi wa kuwa wenye mafanikio kupitia fursa ambazo zitakuja hapo baadaye.”
Caroline ana cheti cha PathwayConnect na ilimbidi apumzike masomo yake ili kuruhusu uzazi wa mtoto wao wa pili miezi michahce iliyopita. “Nitaendelea tena Septemba hii; nimekwishajiandikisha tayari” alisema. Akitazama nyuma kwenye safari yake kupitia PathwayConnect, Caroline anasema, “Safari haikuwa rahisi kwa sababu tuna mambo mengi ambayo tunahitaji kuyakamilisha kama akina mama. Hata hivyo, kwa imani na masomo kutoka BYU–PathwayConnect, nilisonga mbele na kukamilisha PathwayConnect. Ibada fupi za kila wiki zilikuwa msukumo wa kunifanya nisonge mbele. Kukutana na wanafunzi wenzangu wakati wa mikusanyiko ya kila wiki na kupata kusikia uzoefu wao ilinijenga na kunitia hamasa. Nilimwomba Baba yangu wa Mbinguni kwa ajili ya usaidizi na nguvu ili kwamba niweze kukamilisha masomo yangu.”
Kutafuta shahada ya Pathway wakati mwingine ni mchakato mrefu, wa uvumilivu. Daddy Kampoy David anashiriki uzoefu huu. “Nina familia changa na kazi ya kila siku. Ninahudumu kama mshauri wa kwanza katika Kata ya Bandalungwa, Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, na ninafundisha katika programu ya EnglishConnect. Muda wangu wa kusoma ni mchache sana. Nilianza shahada yangu mnamo 2020 na ninategemea kumaliza mnamo 2024. Ninaamka saa 11:00 kwa ajili ya kusoma, ninaitunza familia, ninafanya kazi siku nzima na kujisomea masaa kadhaa kabla ya kurejea nyumbani usiku. Kabla ya mtihani, ninachukua siku chache za mapumziko kwa ajili ya kusoma. Ninajua shahada hii itanisaidia kukua mimi mwenyewe na kuleta maisha yenye uhakika zaidi kwa familia yangu. Ninajua hii si bure!”
Rais Russell M. Nelson ametoa mwaliko na ahadi hii: “BYU Pathway Ulimwenguni kote inaleta mbinu ya uvumbuzi kwenye elimu. Ninamhimiza kila mtu, bila kujali umri, aendelee kusoma. Tafuta njia yoyote itakayokuwa na thamani kwako na kwa familia yako. Utabarikiwa pale unapofanya hili. Utabarikiwa kielimu, kiweledi na kiroho pale unapotafuta kukuza elimu yako.”1
BYU–Pathway iko wazi kwa ajili ya kila mmoja. Ikiwa unataka kuendeleza elimu yako, tafadhali tembelea www.byupathway.org.