“Imani katika Yesu Kristo,” Liahona, Apr. 2023.
Ujumbe wa Kila Mwezi wa Liahona, Aprili 2023
Imani katika Yesu Kristo
Kuwa na imani katika Yesu Kristo ni kanuni ya kwanza ya injili (ona Makala ya Imani 1:4). Imani yetu itatusaidia tufanye chaguzi ambazo zitatuongoza kurudi kwa Baba yetu wa Mbinguni. Tunaweza kufanyia kazi ukuaji wa imani yetu maisha yote.
Imani Ni Nini?
Imani ni wazo thabiti au tumaini kwenye jambo fulani. Kuwa na imani kunajumuisha kutumaini na kuamini katika mambo ambayo ni ya kweli, hata wakati hatuyaoni au kuyaelewa kikamilifu (ona Waebrania 11:1; Alma 32:21).
Imani iliyojikita katika Yesu Kristo
Ili ituongoze kwenye wokovu, imani yetu lazima ijikite katika Yesu Kristo kama Mwokozi na Mkombozi wetu. Kuwa na imani katika Kristo humaanisha kuwa mwenye kujiamini katika Yeye. Humaanisha kumtegemea Yeye kikamilifu—kutumaini katika nguvu, akili na upendo Wake. Hujumuisha pia kuamini na kufuata mafundisho Yake.
Kukuza Imani Yetu
Imani ni zawadi kutoka kwa Mungu, lakini lazima tuitafute na tufanye jitihada za kuifanya imara. Tunaweza kukuza imani yetu kwa kusali na kujifunza maandiko na mafundisho ya manabii wa siku za mwisho. Tunaimarisha pia imani yetu wakati tunapoishi kwa haki na kutunza maagano yetu.
Kuishi kwa Imani
Imani ni zaidi ya kuamini tu. Inajumuisha kutenda juu ya imani hiyo. Tunaonesha imani yetu kwa jinsi tunavyoishi. Imani katika Yesu Kristo inatupatia motisha ya kufuata mfano Wake mkamilifu. Imani yetu hutuongoza tutii amri, tutubu dhambi zetu na tufanye na tutunze maagano.
Imani Inaweza Kuongoza kwenye Miujiza
Imani ya kweli huleta miujiza, ambayo inaweza kujumuisha maono, ndoto, uponyaji na vipawa vingine ambavyo huja kutoka kwa Mungu. Maandiko yana hadithi nyingi za watu ambao walipokea miujiza kutoka kwa Bwana kwa sababu ya imani yao Kwake. Ona “Muujiza” katika Mwongozo kwenye Maandiko kwa ajili ya baadhi ya mifano.
Imani Inaweza Kuleta Amani
Kuwa na imani kwa Mungu na mpango Wake wa wokovu kunaweza kutuimarisha wakati wa changamoto zetu. Imani inaweza kutupatia nguvu ya kusonga mbele na kukabiliana na magumu kwa ujasiri. Hata pale wakati ujao unapoonekana kutokuwa wa uhakika, imani yetu katika Mwokozi inaweza kutupatia amani.
Imani katika Yesu Kristo Huongoza kwenye Wokovu.
Kufanyia kazi imani katika Yesu Kristo kutaongoza kwenye wokovu wetu. Kristo ametayarisha njia kwa ajili yetu ili tupokee uzima wa milele. Tunapoishi kwa imani yetu katika Yeye, tunaweza kusamehewa na kurejea kuishi pamoja na Mungu tena.
© 2023 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Limepigwa chapa Marekani. Idhini ya Kingereza: 6/19. Idhini ya kutafsiri: 6/19. Tafsiri ya Monthly Liahona Message, April 2023. Language. 19006 743