2023
Ujenzi wa Madarasa Unatengeneza Nafasi kwa ajili ya Kristo
Desemba 2023


Makala

Ujenzi wa Madarasa Unatengeneza Nafasi kwa ajili ya Kristo

Ni kwa kiasi kidogo tu tulijua kwamba ujenzi wa madarasa kupitia miradi ya kibinadamu iliyolenga kwa Kristo ingetengeneza nafasi ndani ya mioyo ya watoto wengi kwa kutumia madarasa haya kuelimisha akili zao. Wakati wa chakula cha usiku cha shukrani kilichoandaliwa na mmoja wa wakurugenzi wa manispaa jijini Dar es salaam, Tanzania, kiongozi mwenye ushawishi alitoa mwaliko wa kushangaza kwa Kanisa. Alisema, “Kanisa limefanya kazi ya kupendeza katika ujenzi na ukarabati wa madarasa na vyoo katika manispaa yetu. Sasa tunawaalikeni mje na mtusaidie katika kupambana na mmomonyoko wa maadili kwa kizazi kinachoinukia suala ambalo sasa linakita mizizi.”

Maadili mema hutufunza wema, ikiwa ni pamoja na uaminifu, ukweli, ukarimu, uadilifu, usaidizi, huruma, upendo, heshima kwa wengine, bidii ya kazi, ushirikiano na msamaha. Viongozi wetu wanaelewa kikamilifu kwamba vijana ndiyo tegemeo la siku zijazo na ni nguvu kazi ya kila taifa. Kwa uelewa huo wa kinabii, moja ya vipaumbele vinne kwa Eneo la Afrika ya Kati ni kuimarisha imani kwa kizazi kinachoinukia. Kwa hivyo mwaliko huu ulipofika Kanisani, viongozi wa maeneo husika walipata motisha kubwa na kwa haraka walichukua hatua wakiweka msisitizo kwenye kujifunza mafundisho ya injili.

Kwa haraka waliitikia mwaliko kwa kupanga baadhi ya nyenzo kupitia CES programu ya [Mfumo wa Elimu wa Kanisa] pamoja na walimu, ambao sasa wanafundisha madarasa ya dini katika shule hizi za umma. Inastaajabisha kuona kwamba zaidi ya asilimia themanini ya wale wanaohudhuria madarasa haya ya dini si wa imani yetu. Kadiri ambavyo mpaka sasa habari zimesambaa kuhusu madarasa haya ya dini wakuu wengi zaidi wa shule hizi za umma wanatuma mialiko kwa Kanisa kufikiria pia kupanga madarasa sawa na hayo kwenye shule zao husika. Ni dhahiri kwamba kadiri wanavyosoma maandiko na kujifunza kuhusu Yesu Kristo na dhabihu yake ya upatanisho, watakuwa na hamu ya kutengeneza nafasi ndani ya mioyo yao ili kwamba Roho wa Bwana aweze kufanya makao kwao.

Kama vile Mzee Boyd K. Packer alivyofundisha, “kujifunza mafundisho ya injili kutabadili tabia haraka zaidi kuliko jinsi kujifunza tabia kutakavyobadili. … Hiyo ndiyo sababu tunasisitiza kwa nguvu ujifunzaji wa mafundisho ya injili.”1

Kipindi cha wiki ya mwisho ya mwezi Juni 2023, zaidi ya vijana 300 kutoka Misheni ya Tanzania Dar es Salaam walishiriki kwenye tukio la KNV [Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana] ambalo lilifanyika kwa mara ya kwanza nchini Tanzania. Kwa siku tano walishiriki kwenye ibada fupi zenye uvuvio, madarasa na shughuli, ambazo ziliwasaidia waimarishe imani yao katika Yesu Kristo na kujifunza jinsi ya “kumsikiliza Yeye.”

Mzee Thierry K. Mutombo, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Eneo la Afrika ya Kati, alizungumza na vijana wakati wa ibada fupi yenye uvuvio ambayo ilisisitiza kutumia uwezekano wao mtakatifu ili kukidhi changamoto zao ambazo zinaongezeka kwa kasi.

Vijana kadhaa ambao si wa imani yetu walihudhuria tukio la KNV. Wote walipata taarifa kutoka kwa rafiki zao au ndugu zao ambao ni waumini wa Kanisa. Kila mmoja wao alitoa shukrani kwa kanuni walizojifunza wakati wa KNV.

Mmoja wa vijana hawa alitoa umaizi wa kupendeza wakati aliposema, “Sikujua kama kuna njia sahihi ya kudansi mpaka pale tulipofundishwa na viongozi waliokuwa wakisimamia muda wa kudansi.” Kwa kushiriki na wengine uzoefu wao chanya katika injili, vijana wetu walikuwa wakifanya kile ambacho manabii na mitume wetu waliwahi kukiita “kanuni zinazoeleweka kwa urahisi zilizofundishwa kwa kila mmoja wetu tangu utotoni—za kupenda, kushiriki na kualika.”2

Kadiri Kanisa linavyoendelea kusisitiza mafundisho ya vijana kuhusu mafundisho ya injili katika shule za umma na vilevile kuwaalika kwenye mikutano na matukio kwa ajili ya vijana kama vile KNV, itawasaidia waimarishe imani yao katika Yesu Kristo na hatimaye itawasaidia katika kuepuka tabia zisizo na maadili na kuwa nguvu ya nyongeza katika kutengeneza viongozi wa baadaye, taifa imara na familia imara.

Tanbihi

  1. Mzee Boyd K. Packer, “Little Children,” Ensign, Novemba 1986.

  2. Gary E. Stevenson, “Penda, Shiriki, Alika”, Liahona, Mei 2022, 85.