Wito Wangu kama Mratibu wa Muziki katika Kigingi
Majukumu
Bwana ana shukrani kwa utayari wako wa kuhudumu katika Kanisa Lake. Hapa chini ni muhtasari wa majukumu ya wito wako.
Madhumuni ya Muziki katika Kanisa
Muziki mtakatifu unaongeza imani katika Yesu Kristo. Unamwalika Roho na unafundisha mafundisho. Pia unatengeneza hisia za staha, unawaunganisha waumini, na unatoa njia ya kumwabudu Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Bwana alitamka, “Kwani nafsi yangu hufurahia katika nyimbo za moyoni” (Mafundisho na Maagano 25:12). (Ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 19.1.)
Mratibu wa Muziki katika Kigingi
Mratibu wa muziki katika kigingi huwasaidia waumini wa kata kuongeza imani katika na kumwabudu Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo kupitia muziki mtakatifu. Wanashauriana na urais wa kigingi kupanga muziki kwa ajili ya mkutano wa kigingi na matukio mengine. Chaguzi za muziki zinapaswa kuongeza roho ya kuabudu na kufundisha injili kwa nguvu na uwazi. (Ona 19.3:1.) Waratibu wa muziki hutumika kama nyenzo kwa viongozi wa kigingi katika masuala ya muziki (ona 19.5.2).
Muziki kwa ajili ya Mikutano ya Kigingi
“Muziki wenye mwongozo wa kiungu ni sehemu muhimu ya mikutano yetu ya kanisa” (Nyimbo za Dini, Dibaji ya Urais wa Kwanza). Mikutano ya kigingi inajumuisha nyimbo za dini na chaguzi zingine za muziki kutoka kwenye kwaya, waimbaji mmoja mmoja, au vikundi vidogo (ona 19.3.4). Nyimbo za dini au teuzi zingine takatifu za kimuziki zinaweza kutumika kwa ajili ya muziki wa utangulizi na baada ya mkutano, muziki wa kwaya, na wimbo wa mtu mmoja au mawasilisho ya kikundi kidogo. Waratibu wa muziki katika kigingi wanaweza kupendekeza kwaya za kigingi au vigingi vingi kwa ajili ya mikutano au matukio mengine, kama vile matukio ya kijamii (ona 19.3.7.2).
Mafunzo na Nyenzo
Waratibu wa muziki katika kigingi wanapendekeza na kusimamia mafunzo ya muziki katika kigingi kadiri inavyohitajika. Wanatoa mafunzo na msaada kwa waratibu wa muziki katika kata. (Ona 19.6.) Kama hakuna mpiga ala saidizi anayepatikana kwa ajili ya mikutano ya kigingi, ona sehemu ya 19.4.3.2 ya Kitabu cha Maelezo ya Jumla ili kufikia ala saidizi iliyorekodiwa.
Miongozo na Sera
Kwa sera na miongozo ya ziada, kama vile kupata muziki, matumizi ya vifaa vya nyumba ya mikutano kwa ajili ya mazoezi, au kwaya ya jamii, ona sehemu ya 19.7 ya Kitabu cha Maelezo ya Jumla.