Ari Yetu ya Kuishi Injili
Mara zote kutakuwa na “maneno magumu.” Lakini mara zote kutakuwa na chaguo la kuchagua imani kuliko shaka yoyote au kutokuwa na uhakika.
Njia ya ufuasi imejaa baraka—zote “zinazoonekana na zisizoonekana.”1 Lakini kuna nyakati ambapo njia hiyo, bila kujali baraka zipatikanazo, huwa si rahisi au ya kupendeza. Kuwa mfuasi wa Yesu Kristo huhitaji kazi na dhabihu, na wakati mwingine ni vigumu kupata msukumo kuzishika amri na kufanya hizo dhabihu.
Kama kijana mkubwa, labda unaweza kuwa na shughuli nyingi kujaribu kukabiliana na majukumu mapya, kufanya maamuzi ambayo hubadili maisha, na kutafuta ni kwa namna gani njia yako mwenyewe ya ufuasi itaonekana katika maisha yako yote. Juu ya hayo yote, kunaweza kuwa na vitu katika sera au historia ya Kanisa au mafundisho ambayo huvielewi vizuri na unahangaishwa na majaribu, vilevile baraka ambazo bado unazisubiri na maswali kuhusu mpango wa Mungu kwako.
Baadhi yetu tunaweza kujiuliza wakati mwingine kama kuishi injili kuna thamani ya kupata baraka ambazo tumeahidiwa. Tunaweza kubisha kwamba hatuendani katika hilo, na kwamba hiyo ni kazi kubwa sana, au kwamba maswali yanaonekana kuwa mengi kuliko majibu. Lakini kile kinachokuja ni ari. Kwa nini unafanya kile unachofanya na kuishi vile unavyoishi? Kwa nini unaendelea kushika amri, hata kama hakuna yoyote anayekuona ukifanya hivyo?
Bila kujali wewe ni nani na katika hatua ipi ya maisha umefikia, uchaguzi wa kutafuta ari yako kwa kupalilia imani yako katika Mwokozi na injili Yake ni juu yako.
Twende kwa Nani?
Kutafuta na kutunza ari ya kuishi injili ni changamoto ngumu na ya kipekee katika siku yetu. Hata wakati Mwokozi alipokuwa duniani, watu bado walikuwa na wakati mgumu kuelewa na kutii kanuni alizofundisha. Baadhi ya wanafunzi wake walikuwa wakisikiliza wakati Akielezea dhana iliyoonekana kuwaudhi—nafasi Yake kama “mkate wa uzima” (ona Yohana 6:35–58). Walijibu kwa wasiwasi, wakisema, “Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia?” (Yohana 6:60).
Mwokozi, akiona kwamba walikuwa na wakati mgumu kuamini au kukubali fundisho hili, aliuliza, “Je! Neno hili linawakwaza?” (Yohana 6:61). Badala ya kuweka imani yao mbele ya shaka zao, wengi wa Wanafunzi Wake “wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena” (Yohana 6:66).
Lakini wakati Kristo alipowauliza wanafunzi Wake waliobaki kama na wao wangefanya vivyo hivyo “kutoandamana Naye” Petro alitoa jibu pekee ambalo kweli ndilo la kutoa : “Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele” (Yohana 6:67–68).
Chanzo cha Ari Yetu
Petro alijua chanzo cha ari yake. Ilikuja katika moyo wa kwa nini tunafanya kile tunachofanya katika injili: ushuhuda wetu na imani katika Yesu Kristo. “Na sisi tunaamini na tunajua” Petro alitamka “kwamba wewe ndiye yule Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai” (Yohana 6:69; msisitizo umeongezwa). Kwa kupata ushawishi thabiti sawa na huo juu ya Yesu Kristo, utakatifu Wake, na kazi Yake, sisi pia tunaweza kupata ari ya kuendelea kuishi injili—hata kama itaonekana kuwa vigumu, hata kama hakuna yoyote atakeyetambua, na hata kama hatuna uhakika wa kama tunataka kufanya hivyo.
Mara zote kutakuwa na “maneno magumu.” Lakini mara zote kutakuwa na chaguo la kuchagua imani kuliko shaka yoyote au kutokuwa na uhakika. Kama Mzee L. Whitney Clayton wa Urais wa Sabini alivyosema “Uchaguzi wa kuamini ni uchaguzi muhimu zaidi ambao tunaweza kuufanya.”2
Kwa hiyo tunafanya nini tunapojikuta kwenye upande mwingine wa mojawapo ya hayo “maneno magumu”?
1. Fuata mfano wa Petro na wanafunzi wengine waliobakia waaminifu hata pale ambapo ingekuwa rahisi “kuondoka.” Sikiliza ushauri wa manabii, mitume, na viongozi wengine:
“Katika nyakati za hofu au wasiwasi au nyakati za matatizo, simama katika nafasi ambayo umeshaipata. … Shikilia imara kile unachojua tayari na simama kwa uthabiti mpaka uelewa wa ziada utakapokuja.”3
“Piga hatua moja rahisi mbele kwa imani—na kisha nyingine. … Zingatia kwenye kweli [unazoziamini] na acha kweli hizo zijaze mawazo [yako] na moyo. …
“… Anza kwa kweli za msingi za injili.”4
2. Kaa karibu na maandiko na fuata mafundisho yake:
“Kwa sala jifunze na tafakari Kitabu cha Mormoni kila siku.”5
“Mtu akipenda kuyatenda mapenzi yake, atajua habari ya yale mafunzo, kwamba yatoka kwa Mungu, au kama mimi nanena kwa nafsi yangu tu” (Yohana 7:17).
“Kuweni watendaji wa neno na si wasikiaji tu” (Yakobo 1:22).
3. Endelea kushika amri.
“Majibu ya maswali yetu ya dhati yanakuja pale tunapotafuta kwa bidii na tunapoishi amri. … Imani yetu inaweza kufika mbali zaidi ya vikomo vya sababu za sasa.”6
“Unapoendelea kuwa mtiifu, … utapewa elimu na uelewa unaoutafuta.”7
Hatimaye, ari yetu huja kiurahisi katika kile Petro alikisema. Je, tunaamini kwamba Yesu ni Kristo, kwamba anaongoza Kanisa Lake na ana maneno ya uzima wa milele? Je, imani yetu Kwake huzidi “maneno magumu” ambayo tunaweza tusiyaelewe wakati huu?
Zawadi za Kuishi Injili
Tunapoamua kumpenda na kumfuata Mungu na Yesu Kristo na kushika amri hata kama hatuzielewi kikamilifu, zawadi zake hazipimiki. Mwanadamu wa tabia ya asili huuliza “Je, ni faida gani ipo kwa ajili yangu? Mafundisho ya injili hujibu: “Amani katika ulimwengu huu, na uzima wa milele katika ulimwengu ujao”; mahali palipoandaliwa kwa ajili yenu katika makao ya Mungu; Vyote ambavyo Baba wa Mbinguni anavyo; “furaha isiyo na kikomo” (ona M&M 59:23; Etheri 12:34; M&M 84:38; Mosia 2:41); na kama Mzee Dieter F. Uchtdorf wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alivyosema: “Hapa [kanisani] utapata kile ambacho kina thamani kuliko gharama. … Hapa utapata maneno ya uzima wa milele, ahadi za kukombolewa, na njia kuelekea amani na furaha.”8 Kwa kuorodhesha machache tu.
Tunapojitolea nafsi zetu kumfuata Kristo na kutii amri Zake, tunaahidiwa vitu hivi vyote na zaidi. Hii haimaanishi njia mara zote itakuwa rahisi au ya kueleweka, lakini baraka tunazoahidiwa kwa kubakia imara zitaendelea kujifunua katika maisha yetu yote na hata baadaye.
Hata hivyo, hata hizi baraka ziwe za ajabu kiasi gani, hazitakiwi kuwa ari yetu ya msingi ya kuishi injili. Bila kujali ni maswali gani unayo, bila kujali ni fundisho gani hulielewi, imani yako katika Yesu Kristo na upatanisho Wake vitakuwa ni ufunguo wa ari yako kuishi injili, kama ilivyokuwa kwa Petro na wengine.
“Madhumuni yetu na mawazo hatimaye huathiri matendo yetu,” alisema Mzee Uchtdorf. “Ushuhuda wa ukweli wa injili ya urejesho ya Yesu Kristo ni kani ya ari ya juu katika maisha yetu. Bwana mara nyingi alirudia kusisitiza juu ya nguvu ya mawazo mazuri na madhumuni yanayofaa: ‘Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope’ (M&M 6:36).
“Ushuhuda juu ya Yesu Kristo na injili ya urejesho vitatusaidia katika maisha yetu kujifunza kuhusu mpango maalum wa Mungu kwa ajili yetu na kutenda ipasavyo. Hutupatia uhakika wa uhalisia, ukweli na ukarimu wa Mungu, wa mafundisho na Upatanisho wa Yesu Kristo, na wito uliotukuka wa manabii wa siku za mwisho.”9
Kwangu mimi, nitaendelea kujaribu hata kama nitahisi ni vigumu. Nitaendelea kusema sala zangu na kujifunza maandiko. Nitaendelea kuweka bidii kuimarisha ushuhuda wangu juu ya Mwokozi kila siku. Na nitaendelea kujaribu kuishi kama vile ambavyo angetaka niishi na kutegemea maneno Yake na manabii Wake wanaoishi na mitume kunifundisha, nikitegemea kwenye ari ambayo haichipukii tu kutoka kwenye imani yangu na upendo wangu Kwake bali pia kutoka kwenye dhabihu Yake ya milele na upendo Wake wa milele kwangu.