2018
Njia 5 Unazoweza Kumsaidia Askofu Wako Akusaidie
Oktoba 2018


Njia 5 Unazoweza Kumsaidia Askofu Wako Akusaidie

Hufanya kadiri awezavyo, lakini wakati mwingine huitaji msaada.

young adult talking with bishop

Hukusalimia kwa kukushika mkono kwa nguvu kila mara mnapokutana, hukaa katika sehemu yake maalum kwenye jukwaa wakati wa mkutano wa sakramenti, na hujitolea sana muda wake kukuhudumia wewe pamoja na Bwana.

Yeye ni askofu wako: kiongozi wa ukuhani aliyeitwa na Mungu kusimamia kata yako. Orodha yake ya mambo ya kufanya kamwe haiko wazi, hushauri waumini katika ofisi yake hata baada ya kuwa na siku ndefu ya kazi, na huzunguka katika nyumba ya mkutano baada ya ibada kuisha ili kutimiza majukumu yake yote.

Askofu wako anaweza kuonekana kama ana nguvu zisizo na mwisho, lakini kuongoza kata nzima kunaweza kuchosha! Hujitahidi kufanya kadiri awezavyo, lakini wakati mwingine huitaji msaada. Hizi ni njia tano unazoweza kumsaidia askofu wako akusaidie.

  1. Muombee. Wito wa askofu unaweza kuwa jaribu katika mipaka ya akili yake, roho, na nguvu za kimwili. Anahitaji nguvu ambayo ni Mungu pekee anaweza kutoa lakini inayoweza kuja kwa sababu ya imani yako na sala (ona Yakobo 5:16).

  2. Kuwa na imani katika ofisi yake. Ulimkubali kama askofu wako, lakini imani yako si lazima kuwa katika mtu; iko katika ofisi au wito wa askofu na katika Mungu aliyemuita na kumkubali. Unawezaje kuonyesha imani yako? Kuwa tayari kutimiza wito wako na majukumu. Wakati unapokutana na askofu wako, nenda ukiwa umejiandaa—sali, funga ikiwezekana, na vaa mavazi ya kusitiri mwili kuonyesha heshima yako kwa Bwana. Chukulia ushauri wake kwa umakini. Yeye humwakilisha Bwana.

  3. Mjue. Fanya juhudi ya kumjua. Muulize kuhusu maisha yake, chimbuko lake, na uzoefu wake. Mfanye ajue kamba unathamini huduma yake na kwamba una imani katika uwezo wake wa kutimiza wito wake. (Ona 1 Wathesalonike 5:12–13.)

  4. Usimchoshe. Askofu wako hutaka kukusaidia, lakini kama una tatizo linaloweza kushughulikiwa na walimu wako wa nyumbani, mmoja wa washauri wa askofu, au rais wa akidi ya wazee au Muungano wa Usaidizi wa akina Mama, nenda kwao kwanza. Wito wao upo kwa kusudi! Wako pale kukusaidia wewe na pia kumpa nafasi askofu wako kuzingatia kwenye mambo ambayo yeye pekee anaweza kufanya.

  5. Mchukulie kama mwanadamu. Wakati inaweza kuonekana kwamba askofu wako aliumbwa kwa ajili ya wito wake, bado si mkamilifu. Huwa na shaka juu yake mwenyewe, na hufanya makosa. Lakini kiukweli anakupenda na hufanya kila awezalo kwa ajili ya wito wake. Kuwa muwazi kwake. Kadiri anavyozidi kukujua wewe na hali yako, ndivyo zaidi ataweza kukusaidia.