2019
Je, Unaishi Injili Shingo Upande?
Aprili 2019


Je, Unaishi Injili Shingo Upande?

Mitazamo yetu juu ya majukumu ya Kanisa kweli huleta tofauti.

“Ni lazima nifanye?”

Je, umewahi kuwa na fikra hii hapo awali? Imepitia akilini mwangu mara kadhaa. Na nimejifunza kuwa wazo dogo kama hili lisiloonekana kuwa na umuhimu ni kielelezo muhimu cha mtazamo wangu. Kweli, tunaweza kuwafikia na kuwahudumia wengine, tunaweza kukubali na kutetea miito yetu kanisani, na tunaweza kuhudhuria mikutano yetu ya Kanisa. Hata ikifanywa shingo upande, mambo haya yanaweza kuleta tofauti maishani mwetu. Lakini je, yanazuia uwezo wa Mungu wa kukutumia? Yanazuia uwezo wa Mungu wa kukubadili? Kwangu mimi, nadhani yanafanya hivyo.

Wazo hili linanifanya nimfikirie Lamani na Lemueli, walioondoka Yerusalemu, waliorudi kwa ajili ya mabamba, waliosaidia kujenga merikebu, waliofanya mambo mengi ya utiifu—lakini walifanya hivi kwa kinyongo na shingo upande. Hawakukubali uzoefu wao kuwabadilisha kwa wema. Badala yake, mara zote walinung’unika na walikuwa na misimamo mibaya kwa kila hali waliyojikuta nayo. Na baada ya kugundua hilo, kwa kweli sitaki kuwa Lamani au Lemueli.

Chukua muda na ufikirie juu ya sababu ya matendo yako. Je, unawafikia wengine kwa fokasi kwenye baraka zilizowekwa kwa ajili yako? Au unawafikia wengine kwa sababu kwa dhati unataka kushiriki nao nuru na upendo? Je, unafanya yote unayohitajika kwenye wito wako kwa sababu ndicho kinachotarajiwa kutoka kwako? Au unafanya kwa sababu unataka kumhudumia Bwana na wale walio karibu nawe?

Haya ni aina ya maswali ninayojaribu kujiuliza mara kwa mara. Je ninafanya yote niwezayo kuishi kama mfuasi wa kweli wa Kristo na kwa nia ya dhati? Au moyo wangu haumo katika hilo kikamilifu? Ninafikiri Askofu Gerald Caussé, Askofu Msimamizi, alisema vyema zaidi: “Je tunashiriki kikamilifu katika injili, au tunashughulika tu Kanisani? (“Yote ni Kuhusu Watu,” Liahona, Mei 2018, 112).

Kushiriki kikamilifu dhidi ya Kushughulika

Kwangu mimi, ‘ninaposhughulika’ tu Kanisani, kutojali kumeingia akilini mwangu. Kutojali huku kunatokana na mtazamo usio na msisimko au hata kuruhusu majukumu yenye umuhimu mdogo kwenye mpangilio kuingilia yale yenye maana. Kutojali huku kunakuja ninapoketi kwenye mkutano wa sakramenti na kutokuwa makini, ninaposema sala zangu za usiku na akili yangu inaanza kutangatanga kwenye mambo mengine, ninaposoma maandiko yangu kwa haraka bila kuyatafakari, au ninapomfikia mtu ili nipate kusema tu nimefanya hivyo badala ya kujaribu kwa kweli kuwa rafiki yao.

Wakati mwingine ninahisi kuvunjika moyo ninapokuwa sioni maendeleo yoyote maishani mwangu—Ninapoacha kujali na kuwa na “shughuli nyingi” kwenye injili—na hisia hizi zinabaki hadi ninapotambua tatizo ni nini. Wakati mwingine ninarudi nyuma, ninatafakari tena na kujiuliza, “Je, ninaupa wito huu au mtu huyu au sala hii au andiko hili umakini wangu na moyo wangu hivi sasa?”

Baada ya utambuzi huu kunishtua, hapo ndipo mabadiliko hufanyika hasa maishani mwangu. Ninaposali kwa dhati ili kuwaona wengine kama vile Baba wa Mbinguni anavyowaona, ninaposali kwa ajili ya nafasi za kuhudumu, ninaposali kwa ajili ya mwongozo kwenye wito wangu, kwenye kazi yangu, na kwenye maisha yangu ya kila siku, na muhimu zaidi, ninapofanyia kazi msukumo wa kiungu anaonipa, wakati matendo yangu yanapoonyesha hamu yangu ya ndani ya kuwa bora—hapo ndipo ninaposhiriki kikamilifu katika injili. Hapo ndipo ninapohisi badiliko la kweli kwenye mtazamo wangu, ndani ya moyo wangu, na nafsi yangu. Hapo ndipo ninapoona miujiza ikitendeka. Hapo ndipo ninapohisi furaha ya kweli ikiingia maishani mwangu. Hapo ndipo ninapojaribu kwa dhati kubadilika.

Matendo dhidi ya Hisia

Ninafikiri sote tunaweza kutazama nyuma kwa muda mchache katika maisha yetu ambapo matendo yetu yalikuwa adilifu, lakini hisia nyuma yake hazikuwa adilifu sana. Wakati mwingine maisha yanakuwa na shughuli nyingi, wakati mwingine hatuwezi kuwa na furaha kamili katika hali zetu, na wakati mwingine mambo hayafanyiki katika njia tunayoyataka yawe. Sisi si wakamilifu, lakini tukimwomba Baba wa Mbinguni kutusaidia kuweka mioyo yetu ndani ya vitu tunavyoombwa kufanya ambavyo wakati mwingine huchosha au kuchukua muda, tunaweza kujfunza kuvifanya zaidi kwa njia kama ya Kristo.

Ninaweza kufikiria nyakati ambazo nilikubali shingo upande kufanya kazi ya huduma, kisha nikawa na moyo mkunjufu na uliobadilika baada ya uzoefu huo. Au nilipopata wito na kunung’unika kuwa unachukua wakati wangu mwingi, kisha kulia machozi yaliyo ya furaha na huzuni nilipopumzishwa kwa sababu nilitambua kuwa nilikuwa nimejifunza kuupenda.

Tunaweza kushiriki nuru, kutimiza majukumu yetu, na kupokea majibu ya sala zetu kwa njia bora zaidi ikiwa mioyo yetu iko mahali sahihi. Kama tukichukua muda kuchanganua mitazamo yetu na nia zetu zinazohusiana na matendo yetu na kufanya kila kitu kwa “Moyo wa kweli, [na] kusudi halisi” (Moroni 10:4), tutaweza kutambua vyema zaidi mwongozo wa Baba wa Mbinguni, kupata shangwe zaidi, na kuleta tofauti zaidi maishani mwetu na kwenye maisha ya wengine.