Nabii Wetu: Thomas S. Monson
Ibada ya MEK kwa Vijana Wazima • Mei 5 2013 • Chuo Kikuu cha Brigham Young--Idaho
“We Thank Thee, O God, for a Prophet.” (Hymns, no. 19). Wimbo huu ni mmojawapo wa sifa bainifu ya Kanisa. Sisi twakushukuru Mungu kwa ajili ya Nabii wa kutuongoza katika siku hizi za mwisho.
Kwamba Mungu ametupa nabii ni jambo la kimsingi katika imani na dhana ya Watakatifu wa Siku za Mwisho kila mahali. Tunajua kuwa Mungu yu hai na anatupenda. Tunajua kuwa alimtuma Mwana Wake, Yesu Kristo, kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu, na tunajua kuwa ametupatia nabii.
Wale walioishi katika siku za kwanza za Kanisa walihisi shukrani ya kina kuwa waliishi nyakati za Nabii Joseph Smith. Jumbe na shuhuda za Urejesho kwa mara nyingi zilikuwa ni tukio la moja kwa moja kwa Watakatifu wa kwanza.
Mambo ya ajabu yalitendeka katika miaka ambayo Brigham Young aliongoza Kanisa la Bwana. Watakatifu walikuja Magharibi na kuanza maisha katika kitovu cha Milima ya Rocky ambapo Kanisa lilisitawi. Wale walioishi wakati huo waliihesabu kuwa baraka kuu kwamba waliishi katika nyakati za nabii Brigham Young.
Kielelezo hiki hiki kiliendelea Bwana alipopeana wanaume wakuu na wa kuheshimika kuongoza mambo ya Kanisa Lake. Wazazi na babu zangu waliongea kwa taadhima kuu na upendo kuhusu nabii wa siku zao---Rais Heber J. Grant.
Kwani Dada Walker na mimi, na kwa wengi wa wazazi na babu zenu, tulipenda mfano mkuu na mafundisho ya ajabu ya nabii David O. McKay. Alifwatwa na warithi wake: Joseph Fielding Smith, Harold B. Lee, Spencer W. Kimball, Ezra Taft Benson, na Howard W. Hunter. Kila mwanaume alitayarishwa vyema kuongoza Kanisa kwa muda ulioamuliwa na Bwana Mwenyewe. Kila mmoja wao alipendwa na kuidhinishwa na washiriki wa Kanisa.
Wengi wenu mlio hapa jioni hii mtakumbuka kwa furaha uongozi mkuu wa Rais Gordon B. Hinckley. Ni baraka kuu kuishi wakati wa nyakati zake kama Rais wa Kanisa.
Miaka mitano iliyopita Bwana alimuita Rais Hinckley nyumbani na Thomas S. Monson akawa Rais wa Kanisa---nabii wa Bwana duniani hivi leo. Ewe, ni baraka kuu jinsi gani kwako na mimi kuishi katika siku hii njema ambapo tunaongozwa na nabii mkuu kama huyo.
Hili ni Kanisa la Bwana. Yeye hupanga maisha ya Mitume hawa wakuu, na Yeye huwaweka katika nyadhifa za kuongoza Kanisa Lake. Ni ukweli kuwa mojawapo wa sifa bainifu ya Kanisa la Bwana ni kuwa Yeye ana mitume na manabii duniani hivi leo.
Mtume Paulo alielezea kama kuwa Kanisa lina, “mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni” (Waefeso 2:20). Hivyo ndivyo lilikuwa na hivyo ndivyo lilivyo. Kanisa la Bwana linabainishwa kwa kuwa na mitume na manabii, naye Yesu Kristo Mwenyewe akiwa jiwe kuu la pembeni. Kila Rais wa Kanisa ameshuhudia kuwa Yesu Kristo ndiye kichwa cha Kanisa hili.
Hakuna utukuzi sadfa, hakuna makosa, na hakuna mapambano. Inapokuja kwa urithi katika Urais wa Kanisa la Bwana, Bwana ndiye anaongoza, na kwa kweli matakwa Yake hutendeka.
Ninawashuhudia kuwa ni matakwa ya Bwana kwamba tunaongozwa leo na Rais Thomas S. Monson, ambaye ni nabii wa Bwana duniani leo.
Kama nabii wa Agano la Kale Yeremia alivyotufunza kuhusu manabii, tunajua hii kuwa kweli kwa Rais Monson. Maandiko yanasema, “Kabla sijakuumba katika tumbo nilikujua, na kabla hujatoka tumboni, nilikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa” (Yeremia1:5).
Ninataka kuwazungumzia hivi leo kuhusu maisha na utumishi wa Rais Thomas S. Monson, Rais wa 16 wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Mnamo mwaka wa mwisho wa maisha ya Rais Hinckley, aliniteuwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Hekalu, na Rais Monson amenitunukia kwa kuniruhusu kubaki katika kazi hii. Zaidi ya miaka sita iliyopita, nimekuwa na baraka kuu na isiyosahaulika ya kusaidia Rais Thomas S. Monson na washauri wake juu ya masuala ya hekalu. Nimeshaketi kando yake Rais Monson akinipa ushauri mwingi na maelekezo kuhusu mahekalu na masuala ya hekalu duniani kote. Amenialika kuandamana naye katika ibada za kuweka wakfu mahekalu, uchimbuzi wa ardhi, na kutembelea maeneo yanayotazamiwa kujengwa hekalu. Nimekuwa na baraka ya kusafiri pamoja naye duniani kote, katika maeneo ya mbali kama vile Kyiv, Ukraine, na Cebu, nchini Ufilipino, na maeneo mengine ya kusisimua, kama vile Roma, Italia.
Anapotembea duniani kote, nimebarikiwa kuwa hapo kushuhudia upendo wake mkubwa kwa ajili ya watu---si tu washiriki wa Kanisa, lakini watu wote. Nimeshuhudia upendo wake wa kina na urafiki, huruma yake ya Kikristo na wororo, hasa kwa watoto, wazee, na wagonjwa. Mara nyingi nikimtazama Rais Monson, nimepata hisia: “Hivyo ndivyo Mwokozi angetenda. Hivyo ndivyo Mwokozi angetendea watu.”
Nimeshuhudia shauku yake isiyokoma, motisha yake na kujitolea, furaha yake maishani, na nia yake ya kina ya kumtumikia Bwana na kufanya kama vile Mwokozi angetaka afanye. Yeye hachoki kamwe kufanya kazi ya Bwana.
Katika Maagano na Mafundisho, sehemu ya 52, mstari wa 14, Bwana alisema, “Nitatoa …. kwenu utaratibu katika mambo yote, ili msidanganyike.”
Nayapenda maandiko haya, kwa kuwa yanafundisha kwamba Bwana atatoa mfano kwa ajili yangu na kunionyesha jinsi ya kufanya mambo, jinsi ya kutenda, jinsi ya kuishi. Lakini si kunihusu mimi hasa. Ni juu ya kila mmoja wetu. Bwana hakika hutuonyesha njia. Yeye hutoa mifano katika maisha ya kila moja wetu ili kutuonyesha jinsi ya kuishi.
Naamini mmojawapo wa mifano muhimu katika maisha yetu ni maisha ya nabii anayeongoza na kuelekeza Kanisa la Bwana katika siku zetu. Kama nilivyoeleza awali, kwangu mimi kama kijana, mfano ulikuwa Rais David O. McKay. Nilimpenda na kumwidhinisha, nilimwombea, alikagua maneno yake kwa makini, na nilitaka kuwa zaidi kama yeye kwa kiasi kama nilivyoweza kufikiria kwamba ningeweza kuwa.
Ninatumahi kwamba wakati wengi wa wazazi wenu walipokuwa vijana, mfano wao ulikuwa Rais Spencer W. Kimball. Bila shaka, kwa kila mmoja wetu, nia yetu kubwa ni kuunda maisha yetu kama ya Mwokozi---kumfuata, kuishi amri zake, na kuwa kwa kiasi kama Yeye kadiri tunavyoweza kuwa.
Katika 3 Nefi 27:27, Yesu alifundisha: “Mnapaswa kuwa watu wa aina gani? Amina nawaambia, hata vile nilivyo.”
Hilo ndilo lengo letu la msingi---kuwa kama Yeye.
Ikiwa imewekwa kwenye ukuta wa kila ofisi ambayo Rais Monson ametumia tangu aitwe kuwa askofu imekuwa mchoro unaotambulika wa Mwokozi uliyochorwa na Heinrich Hofmann. Ni onyesho nzuri la Mwokozi.
Akizungumzia mchoro huu, Rais Monson alisema: “ Ninaupenda mchoro, ambao nimekuwa nao tangu nilipokuwa askofu wa miaka ishirini na mbili na ambao nimeubeba nami kila nilipotumwa kufanya kazi. Nimejaribu kuunda maisha yangu yawe kama ya Bwana. Nilipokuwa na uamuzi mgumu wa kufanya, nimeitazama picha ile na kujiuliza, “Angefanya nini Yeye? Kisha ninajaribu kukifanya” (katika Heidi S. Swinton, To the Rescue: The Biography of Thomas S. Monson [2010], 135).
Ninajua kuwa Rais Monson hufikiria kuhusu kufuata mfano wa Yesu. Katika wakati mmoja nilikuwa na Rais Monson kwa ajili ya tamasha kabla ya uwekaji wakfu hekalu. Yeye alikuwa amewasili kwa ndege siku hiyo hiyo, na mkutano wa jioni ulipokuwa unaelekea kwisha, nilifikiri Rais Monson angekuwa amechoka, na nilitaka kuhakikisha kuwa alipata kupumzika kwa muda kabla ya matukio ya siku iliyofuata. Wimbo wa kufunga ulipokuwa unaimbwa, nilimkaribia Rais Monson na kusema, “Rais, baada ya sala ya kufunga, tukiondoka nje kupitia mlango wa kando, tunaweza kukurudisha hotelini kwa haraka na unaweza kupumzika kidogo”
Akiniangalia kwa mshangao, aliniambia, “Mzee Walker, Ikiwa Yesu angekuwa hapa, unadhani angeondoka kwa mlango wa kando mkutano ukiisha?”
Sijatoa pendekezo hilo tena. Kama vile Mwokozi angefanya, alitaka kuwa na watu. Hakuwa anajifikiria mwenyewe hata kamwe. Alikuwa akifikiria kuhusu mema ambayo angefanya.
Daima nimehisi kwamba ninaweza kuwa mtu bora zaidi ninapounda maisha yangu kuiga yale ya watu wenye haki ambao Bwana amewaweka katika njia yangu: babu zangu, wazazi wangu, maaskofu wangu, rais wangu wa misheni, na bila shaka, nabii wa Mungu ambaye naweza kumuona na kumsikia na ambaye kwa ajili yake mimi huomba kila siku. Nina hakika kuwa wengi wenu hufanya vivyo hivyo.
Imekuwa baraka kuu maishani mwangu kutaka kuwa zaidi kama Bwana na kutaka kuwa zaidi kama nabii Wake---Rais Thomas S. Monson.
Ningependa kushiriki nanyi baadhi ya maisha na mafundisho ya Rais Monson, na kwa tumaini, ninaposhiriki, utaweza kutambua sifa ambazo utataka kuweka katika maisha yako. Sote tutabarikiwa kwa jinsi tutataka kuunda maisha yetu na kujifunza kutoka nabii wa Bwana.
Kama Nefi, na kama wengi wenu, Thomas S. Monson alizaliwa na wazazi wema. Alizaliwa Jijini Salt Lake mnamo Agosti 21, 1927. Alilelewa katika hali duni. Hakuwahi kujaribu kubadili sifa ya kule alikotoka. Na ucheshi wake wa haya, pamoja na faraja na yule ambaye yeye alikuwa, Rais Monson angesema mara kwa mara kuwa hangehitaji kushughulika na upande gani wa njia ya reli alikotoka---kwa sababu alikulia katikati mwa njia za reli.
Nimefurahishwa daima na jinsi kila mara amezungumzia ujana wake kwa furaha. Nadhani alikuwa kwa kiasi kikubwa kama Nefi. Lamani na Lemueli walikuwa hodari katika kuona matatizo na kuzingatia upande mbaya wa kila kitu, ilionekana hivyo. Nefi, kwa upande mwingine, alikuwa chanya, mwenye matumaini, na shukrani. Aliona mema katika kila kitu kilichokuwa karibu naye. Hivyo ndivyo Tommy Monson alikua---na amekuwa hivyo maisha yake yote!
Alikuwa mwanafunzi mwema, na pengine muhimu zaidi, alikuwa mtoto mzuri. Alionyesha shauku yake ya kufanya vizuri katika huduma ya Bwana alipoitwa kutumikia kama katibu wa jamii ya mashemasi katika kata yake. Karibu miaka 70 baadaye, kama Rais wa Kanisa, aliwazia na kujivunia kidogo juu ya hamu yake ya kufanya kumbukumbu za Jamii yake ya mashemasi kuwa bora iwezekanavyo. Yeye hakuwa na wazo kuhusu “Kwa nini mimi ni katibu na siyo rais wa Jamii?" Yeye alitaka tu kufanya kazi yake vizuri. Alikuwa ameitwa katika nyadhifa katika Kanisa la Bwana, na yeye alitaka kufanya vyema awezavyo. Alitaka kumbukumbu ziwe nadhifu na za utaratibu, hivyo basi alipiga chapa kumbukumbu za jamii yake ya mashemasi. Kama mvulana wa miaka, 12 alikuwa anaweka mfano mzuri kwa ajili yetu.
Kama hii inakustajabisha, mimi sishangai. Ilistaajabisha pia rais wake wa kigingi ambaye, aliposikia kuhusu kazi nzuri ya kijana Tommy, alimteua azungumze katika mkutano wa kigingi---kama katibu wa Jamii ya mashemasi. Je, umewahi kusikia juu ya katibu wa Jamii ya mashemasi akizungumza katika mkutano wa kigingi? Ni mfano gani kwetu sisi sote!
Alimaliza shule ya upili na kujiunga na nevi ya Marekani. Alitumikia nchi yake, na alipokuwa akifanya hivyo, alijiweka kuwa safi na mwema. Alirudi kutoka huduma yake ya kijeshi na kujitahidi kupata elimu bora. Alikuwa mwanafunzi mwema---mfano mwingine mkubwa kwetu sisi sote! (Mfano wa kuwa mwanafunzi mzuri unaweza kuwa muhimu zaidi kwa baadhi yenu kuliko wengine.)
Alifanya miadi na kupendana na msichana mrembo Matakatifu wa Siku za Mwisho aliyeitwa Frances Johnson, na mara baadaye alimuliza amuoe. Walioana katika Hekalu la Salt Lake Oktoba 7, 1948, akiwa na umri wa miaka 21. Je, yeye ni mfano gani kwa sisi wote! (Tena, pengine muhimu zaidi kwa baadhi yenu kuliko kwa wengine.)
Ingawa alikuwa ameoa kwa miezi 18 pekee, na akitia bidii ili kusonga mbele katika kazi mpya, alikubali wito kutoka kwa Bwana kutumikia kama askofu wa kata kubwa iliyokuwa ndani ya mji. Ilikuwa katika kata ambayo alikuwa amekulia. (Fikiria juu ya hayo!) Yeye hakusema, "Wakati si sahihi" au "Mimi ni kijana"; yeye alipokea tu wito, akamwamini Bwana, na kujitupa katika kazi kwa nguvu zote na vipaji ambavyo Bwana alikuwa amempa. Alitaka kuwa bora kabisa katika huduma ya Bwana.
Askofu kijana Monson alikuja kuyapenda maandiko ambayo yanaweza kubariki kila moja ya maisha yetu, kama yalivyobariki maisha yake:
“Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote, wala usizitegemee akili zako mwenyewe.
“Katika njia zako zote mkiri yeye, Naye atayanyosha mapito yako” (Mithali 3:5–6).
Hadi siku ya leo, Rais Monson husema maandiko hayo mara nyingi na huishi maisha yake kwa mujibu wa kile yanachotufundisha. Je, yeye ni mfano gani kwa ajili ya sisi sote! Sote tutafanya vyema ikiwa tutayakumbuka maandiko hayo na kuyafanya kuwa sehemu muhimu ya falsafa yetu ya maisha---jinsi tu alivyofanya Rais Monson.
Kata ya Askofu Monson ilikuwa na zaidi ya washiriki 1,000, ikiwa ni pamoja na wajane 84. Tumebarikiwa katika mkutano mkuu na mazingira mengine kumsikiza mara kwa mara akishiriki baadhi ya uzoefu matamu aliyopitia alipowatunza kina dada hawa ambao walibarikiwa kuwa chini ya utunzaji wake.
Kwangu mimi, kila ninapomsikiza akizungumza juu ya mojawapo wa matukio yale aliyopitia alipokuwa askofu, mimi hutambua, na huwa ya kuvutia sana kwangu, kuwa upendo wake na hisia kwa ajili ya washiriki wa kata yake haikuisha alipoachiliwa kama Askofu. Yeye aliitwa katika urais kigingi akiwa na umri wa miaka 27, lakini hata miaka mingi baadaye (baada ya wito wake kama rais wa misheni na kama Mtume), aliendelea kupenda, kulea, na kujali masilai ya washiriki wakongwe wa kata yake. Kwa hakika yeye hakuwa tu anawapenda na kuwajali kwa sababu ya jukumu alilonalo. Upendo wake na hisia zake kwa ajili yao zilizama kwa kina ndani ya moyo wake na hazingechukuliwa na mabadiliko yoyote ya jukumu.
Kwa hili, Rais Monson ametuonyesha njia. Ni njia bora zaidi; ni njia ya Bwana. Yeye anawapenda wengine na anawajali wengine---kama tu Bwana alivyotufundisha kwamba tunapaswa kuwa. Ni jinsi gani alivyo mfano kwa ajili yetu sote!
Katika umri wa miaka 31, Monson Rais aliitwa kuwa rais wa misheni ya Kanada, makao yake makuu mjini Toronto, Ontario. Kama vile alivyofanya kama askofu, yeye akarukia mgawo wake, akajitolea kila kitu alichokuwa nacho, na kuamini katika Bwana kwa moyo wake wote. Kila mtu karibu naye anaweza kuona upendo wake kwa Bwana, upendo wake kwa ajili ya mke na watoto wake, upendo wake kwa ajili ya wamisionari na washiriki, na upendo wake kwa ajili ya Kanada, nchi ambako alikuwa ameitwa kutumika. Ushawishi wake kama rais wa misheni ulikuwa wa kushangaza na hadi hivi leo hauwezi kupimwa. Wamisionari wake walimpenda na walitafuta kuishi maisha ambayo yangemfanya rais wao wa misheni kuwa na faraha. Sisi sote tunaweza kujifunza kutoka haya.
Kama tu alivyofanya alipoachiliwa kama askofu, aliendelea kushikilia kwa dhati moyoni mwake hisia zake na mapenzi yake kwa ajili ya wamisionari na Watakatifu ambao walikuwa wamebarikiwa kuja chini ya uwakala wake. Nimekuwa shahidi wa upendo na hisia isiyopunguka ya Rais Monson kwa wamisionari ambao waliohudumu chini yake katika Misheni ya Kanada. Ni mfano kweli!
Ninawajua wamisionari ambao walibarikiwa kuwa na Thoma S. Monson kama rais wao wa misheni wamejaribu kufuata mfano wa huduma ya haki katika ufalme wa Bwana ambao Rais na Dada Monson waliwatolea. Kwa mfano, nashiriki nanyi ukweli wa ajabu kwamba miongoni mwa marais wa hekalu 141 wanaohudumu kwa sasa duniani kote, watano kati yao walikuwa vijana wamisionari ambao walihudumu chini ya Rais Monson katika Misheni ya Kanada.
Maelfu yenu ambao mko pamoja nasi jioni hii ni wamisionari waliorejea. Naomba kuwa kila mmoja wetu tutafuata mfano wa hawa marais watano wa hekalu na kujitahidi kuwa waaminifu na kutembea njia ya huduma ya haki iliyotolewa na marais wetu wa misheni.
Niliguswa hivi juzi kuona picha katika Church News ya Rais Monson akitembelea mtu katika hospitali katikaToronto, Kanada. (ona “Teachings of the Prophet,” Church News, Feb. 3, 2013, 7). Mtu huyu alikuwa amehudumu pamoja na Rais Monson miaka 50 ya awali. Rais Monson hakuwa amemsahau. Miaka mingi na maili nyingi hazikuwa zimemuibia Rais Monson hisia tamu ya upendo na shukrani ambazo huja kwa wale ambao wanamtumikia Bwana pamoja. Natumaini kila mmoja wetu tutafuata mfano wake na tusiwasahau wale ambao wamebariki maisha yetu katika miaka ya awali.
Katika mwaka 1963, akiwa na umri wa miaka 36, Thomas S. Monson alialikwa kwenye ofisi ya Rais David O. McKay, ambaye alikuwa Rais wa Kanisa kwa wakati huo. Ilikuwa ni katika mkutano huo kwamba Rais McKay alimwita kuwa Mtume wa Bwana Yesu Kristo.
Rais Monson ni Mtume wa pekee kuitwa kwa Wale Kumi na Wawili akiwa na umri mdogo hivyo katika miaka 100 iliyopita. Hakika, mkono wa Bwana uliongoza wito wa Mtume huyu kijana, kwa sababu Bwana alijua Thomas S. Monson angeongoza Kanisa katika siku zetu.
Mkutano mkuu wa Oktoba utakuwa mkumbusho wa miaka 50 wa wito la Thomas S. Monson kuwa Mtume. Ni vyema jinsi gani? (Wala tangu Joseph Fielding Smith tumekuwa na Mtume akisherehekea miaka 50 katika Kumi na Wawili.)
Kwa miaka 22 Rais Monson alihudumu kama mshauri wa Marais watatu wa Kanisa: Ezra Taft Benson, Howard W. Hunter, na Gordon B. Hinckley. Mnamo Februari 3, 2008, Thomas S. Monson alitawazwa na kutengwa kama Rais wa Kanisa. Yeye ana washauri wawili wema na wakuu ambao husimama kwa upande wake: Rais Henry B. Eyring na Rais Dieter F. Uchtdorf. Wao ni Makuhani Wakuu Wanaoongoza Kanisa la Bwana duniani leo (ona M & M 107:22).
Huduma ya ajabu ya Rais Monson mara nyingi imeonyeshwa na maelezo “kwenda kuokoa”. Heidi Swinton aliandika wasifu wa ajabu juu ya maisha yake, na aliuta kwa kufaa To the Rescue. Wasifu ulichapishwa mwaka 2010. Kama haujausoma, ninaupendekeza sana kwako. Utabariki maisha yako.
Ujumbe, bila shaka, ni ujumbe ule ule ambao Yesu alitupatia katika Luka: kuwaacha wale 90 na 9, na uende ukamuokoe yule moja (Luka 15:4). Hicho ndicho kiini cha injili ya Yesu Kristo, kuwapenda wenzetu na kufanya tuwezavyo ili kubariki maisha yao. Rais Monson daima amefundisha kanuni hizi, lakini muhimu zaidi, yeye anaishi kwa njia hiyo. Maisha yake yamejaa mifano isiyohesabika ya kujitolea kutembelea, kufariji, au kusaidia wale walio na mahitaji zaidi: wajane, watoto, wagonjwa, wanaotaabika, na wale ambao wana upweke au kuvunjika moyo.
Mtume Yakobo aliandika, "Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele ya Mungu Baba ni hii: Kwenda kuwatazama mayatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa” (Yakobo 1:27).
Hivi ndivyo Rais Monson ameishi maisha yake. Somo kwetu ni kwamba si lazima mtu awe Mtume ili kuishi kwa njia hii. Tunaweza kuishi dini yetu, tunaweza kuwatembelea mayatima na wajane, na tunaweza kujilinda dhidi ya ulimwengu. Tunaweza kumtazamia nabii wetu kuona ni jinsi gani tunavyoweza kufanya hivyo! Tunaweza kujiambia, "Huyo ni aina ya mtu nataka kuwa."
Miaka kadhaa iliyopita, kabla tu ya mkutano mkuu, Rais Monson alifundisha somo lingine la ajabu. Wakati huu lilikuwa kwa Wakuu wenye Mamlaka waliokusanyika, ambao walikuwa wamesafiri kwenda Jiji la Salt Lake, wengi wakija kutoka maeneo ulimwenguni ambapo walikuwa wakihudumu katika Urais wa Maeneo. Ulikuwa ni mkutano muhimu sana. Tulikuwa tumekuja pamoja ili kufundishwa na Urais wa Kwanza na Wale Kumi na Wawili.
Muda wa kuanza mkutano ulipokuwa unawadia, kila mtu alionekana kuwa katika mahudhurio isipokuwa Rais Monson, ambaye alikuwa bado hajafika. Dakika kadhaa kabla ya mkutano kuanza, tuliacha kusalimiana na kuketi kwa heshima tukisikiliza muziki wa utangulizi---tukitarajia kwamba nabii angeingia wakati wowote.
Tulisubiri kwa subira saa 3:00 asubuhi ilipofika na kisha kupita. Mtu akaenda nje kupitia mlango wa upande ---kwa wazi kuangalia na kuona kama msaada wowote ungehitajika. Aliporejea chumbani, tuliambiwa kwamba "Rais Monson ataungana nasi hivi karibuni."
Takribani dakika 15 baada ya mkutano ulipostahili kuanza, Rais Monson aliingia chumbani. Kwa heshima, tulisimama alipokuwa akiingia. Tulifurahia kumuona na kuridhishwa kuwa alionekeana kuwa vyema. Hakukuonekana kuwa kulikuwa na sababu yoyote ya wazi ya kwa nini angechelewa.
Rais Monson alienda moja kwa moja kwenye mimbari na kusema, “Ndugu zangu, poleni kwa kuchelewa, lakini mke wangu alinihitaji asubuhi hii.”
Nilivutiwa kwa kina na kunyenyekezwa. Sikuweza kuacha kufikiria kuhusu maneno ya Rais Monson. Huu ulikwa mkutano muhimu sana. Uongozi mzima wa juu wa Kanisa ulikuwa umekusanyika, lakini Rais Monson akatuwekea sisi sote mfano. Mke wake alimhitaji, naye alichukua muda uliohitajika ili kumhudumia. Ilikuwa ni mahubiri makubwa. Sikumbuki kitu kingine kilichosemwa siku hiyo, lakini ninakumbuka mahubiri hayo: "Mke wangu alinihitaji”
Mahubiri haya yaliimarishwa katika tukio lingine ambapo Rais Monson alisema,“Ninapowasikia waume wakisema wanawapenda wake zao, kisha nataka kuwaambia,” Basi, dhihirisha na jinsi unavyomtendea na jinsi unavyomtumikia.”
Hivyo ndivyo Rais Monson alivyo: Yeye daima hushugulika kwa ajili ya mtu mwingine. Yeye daima anaonyesha wema na huduma kwa wengine.
Si lazima uwe karibu na Rais Monson kwa muda mrefu ili kuhisi upendo wake wa kina na kujitolea kwa kipenzi chake, Dada Frances Monson. Wakati wowote anapozungumza kumhusu, macho yake hung’aa na hupata tabasamu kubwa usoni mwake. Unajua huyu ni mtu ambaye upendo wake kwa mke wake ni mfano kwa kila mmoja wetu. Rais na Dada Monson wametuonyesha mfano wa mwanaume na mwanamke waliotiwa nira katika upendo wao wa Bwana na nia yao ya kumtumikia katika haki.
Nataka kuwa zaidi kama Bwana, lakini pia nataka kuwa zaidi kama nabii Wake.
Ikiwa unashangaa ni nini Rais Monson angetaka kwa kila mmoja wenu, labda ushiriki wa tukio lifuatalo utakusaidia kujua:
Novemba iliyopita hekalu zuri la Boise Idaho lilikuwa tayari kwa kuwekwa wakfu upya baada ya kufungwa kwa miezi 18 ili kulipamba na kuliboresha upya hekalu. Baada ya miaka matumizi ya ajabu ya miaka 30 na Watakatifu waaminifu katika sehemu ya Idaho na maeneo ya jirani, hekalu lilihitaji sana kukarabatiwa. Baada ya kukamilika, kama ilivyokuwa mila kusherehekea tukio la ibada ya kuweka wakfu tena hekalu, vijana wa wilaya ya hekalu walialikwa kuonyesha sherehe kuu za utamaduni. Ilikuwa jioni ya kuimba na kucheza na kuonyesha imani yao na shukrani kwa ajili ya hekalu.
Nilikuwa nimeketi karibu na Rais Monson tulipokuwa tunatazama maonyesho ya ajabu ya vigingi mbali mbali. Mojawapo wa wimbo wa ngoma ulikuwa na kundi lililopendeza la wasichana. Rais Monson alipokuwa akifurahia onyesho, alinikaribia na kushiriki hisia ya moyo wake. Alisema, "Matumaini yangu yangekuwa kwa ajili ya kila mmoja wao kuwa na ndoa ya hekaluni. Nataka sana kila mmoja wao awe na baraka hiyo---kuolewa katika hekalu.”
Niliwaza: "Je, si hii ni vyema. Nabii wa Mungu yuko hapa akishuhudia sherehe hii ya vijana wa wimbo na ngoma, na kwake inahusiana kwa wazi na hekalu ambalo atakuwa akiweka wakfu asubuhi itakayofuata. Matumaini yake yalikuwa kwa ajili ya kila mmoja wao kuwa na ndoa hekaluni.” Ilikuwa hio ndiyo hamu ya nabii kwa ajili yetu, na ndivyo ilivyo,, basi kila mmoja wetu anapaswa kutaka hayo kwa ajili yao wenyewe, na inapaswa kuwa lengo muhimu sana katika maisha ya kila mmoja wetu
Napenda kushiriki nanyi tukio lingine:
Rais Monson, Rais Eyring, na Mzee Quentin L. Cook wa Jamii ya Kumi na Wawili walisafiri hadi Laie, Hawaii, kuwekwa wakfu upya hekalu la ajabu mnamo Novemba ya 2010. Usiku kabla ya ibada ya kuwekwa wakfu hekalu, tulikusanyika katika Cannon Center kwenye kampasi ya chuo kikuu cha BYU-Hawaii kwa ajili ya sherehe ya kitamaduni. Ratiba ilikuwa nzuri. Kupitia wimbo, ngoma, na maelezo, vijana wa wilaya ya hekalu walisimulia hadithi ya historia ya Kanisa kule Hawaii. Walisema kuhusu wamisionari na waongofu wa awali. Wasimulia hadithi ya ajabu Joseph F. Smith ambaye angekuwa nabii wa siku za usoni akiitwa kutumikia misheni Hawaii mwaka 1854, alipokuwa na umri wa miaka 15 peke yake. Kijana Joseph F. Smith alirejea kutoka misheni yake ya miaka mitatu tu kabla ya siku yake ya kuzaliwa ya umri wa miaka 19. (Na mlidhani mabadiliko ya umri ya hivi karibuni ya 18 yalikuwa ya ajabu, ni kweli?)
Sherehe za kitamaduni ziliendelea vijana wakisimulia ukuaji wa Kanisa kati ya watu wa Polynesia na wakasema jinsi Rais Joseph F. Smith alirejea Hawaii zaidi ya miaka 50 baadaye na kama Rais wa Kanisa akaweka wakfu eneo na kuchimba ardhi kwa ajili ya ujenzi wa Hekalu la Laie Hawaii.
Sherehe za kitamaduni zilikuwa za ajabu, na Rais Monson aliipenda kila sehemu yake. Alifurahia onyesho lililokuwa na ngoma maarufu ya Vita Kuu vya Dunia vya II “Boogie Woogie Bugle Boy,” kwa kuwa ilimkumbusha siku zake katika Jeshi la Wanamaji la Marekani. Ngoma zingine zililenga ngoma mbali mbali za watu wa kisiwa hicho.
Ngoma moja ilioshirikisha ngoma ya kupendeza ya hula ilichezwa. Mmoja wa wasichana aliyeshiriki katika ngoma hii alikuwa kwenye kiti cha magurudumu. Alikuwa mrembo sana, na hata kama hakuwa na matumizi ya miguu yake, alicheza densi vizuri. Rais Monson alimuonyesha kwangu na kutoa maoni juu ya jinsi alivyopendeza na alivyocheza densi vizuri .
Ratiba ilipokamilika, kila mtu alikuwa na furaha kuhusu maonyesho mazuri yaliyotolewa.Tulipotoka ukumbini, wachezaji wote walirudi sakafuni, ikiwa ni pamoja na wachezaji wa hula. Rais Monson hakufuata njia iliyopangwa ya kuondoka lakini alikwenda moja kwa moja sakafuni ili kutoa shukrani zake kwa vijana, na hasa alikwenda moja kwa moja kwa msichana mrembo aliyekuwa kwenye kiti cha gurudumu ili kumpongeza na kumwonyesha upendo wake kwake.
Hata katikati ya sherehe na umati mkubwa wa watu, Rais Monson tena alionyesha upendo msafi wa Mwokozi. Alimwendea yule moja. Aliinama na kumbusu juu ya paji la uso wake. Niliwaza: "Je, hii si ni ajabu. Mara nyingine tena nabii wa Mungu anatuonyesha jinsi ya kuwajali wale walio karibu nasi, jinsi ya kuwa wema na wenye upendo, na jinsi ya kuhamasisha na kuinua "Niliwaza:" Hivi ndivyo Yesu angetenda. Hivi ndivyo Mwokozi angetaka tutende moja kwa mwengine. "
Ninaupenda wimbo wa Msingi ambao unayosema, "Najaribu kuwa kama Yesu,” (“I’m Trying to Be Like Jesus,” Children's Songbook, 78). Na ningependa kuongeza kuwa, "Na ninajaribu kuwa kama nabii Wake."
Ningependa kupendekeza njia tano tunaweza kufuata mfano wa Nabii Monson:
Kwanza, tunaweza kuwa na mtazamo mzuri, na tunaweza kuwa na furaha.
Katika Lulu ya Thamani Kuu, Mtume Joseph Smith aelezewa akiwa na uso wa furaha (ona Joseph Smith-Historia 1:28). Hiyo pia inamweleza Rais Monson. Yeye kweli ana uso wa furaha.
Katika wakati mmoja Rais Monson alisema: "Tunaweza …. kuchagua kuwa na mtazamo mzuri Hatuwezi kuelekeza upepo, lakini tunaweza kurekebisha matanga. Kwa maneno mengine, tunaweza kuchagua kuwa na furaha na mtazamo mzuri, bila kujali kinachokuja njiani mwetu (“Messages of Inspiration from President Monson,” Church News, Sept. 2, 2012, 2).
Siku moja nilikuwa ninasubiri nje ya chumba cha mkutano cha Urais wa Kwanza. Nilikuwa nimealikwa pale ili kuhudhuria mkutano wa kujadili maswala ya hekalu. Niliketi nje ya chumba cha mkutano nikiwa kimya, peke yangu. Nilidhani Urais wa Kwanza ulikuwa tayari unakutana na kwamba ningealikwa kujiunga nao katika dakika chache. Nilipokuwa nimeketi pale, ningeweza kusikia mtu akitembea chini ya ukumbi akipiga mbinja. Nikawaza kimoyo: "Kunaye asiyeelewa itifaki sahihi. Huwezi kwenda ukitembea ukipiga mbinja nje ya ofisi ya Rais wa Kanisa.” Muda fupi baadaye aliyekuwa akipiga mbinja alitembea kwenye kona---ilikuwa ni Rais Monson. Alikuwa na furaha, na alikuwa na mtazamo mzuri. Alinisalimia kwa furaha na kusema, "Nadhani tutaweza kuanza mkutano baada ya dakika kadhaa.” Hata na uzito wa Kanisa lote juu ya mabega yake, yeye ni mfano wa furaha na daima huwa na mtazamo mzuri. Tunapaswa kuwa hivyo.
Pili, tunaweza kuwa na huruma na upendo kwa watoto, jinsi Rais Monson alivyo.
Yesu alizungumza mara nyingi juu ya watoto. Nabii wake, Rais Monson, huzungumza mara nyingi juu ya watoto pia, na nimeona hasa kwenye ibada za kuweka wakfu hekalu jinsi anavyowapenda watoto na, kwa mfano wake, anatufundisha jinsi ya kuwatendea watoto. Katika kila ibada ya kuweka wakfu yeye huwazingatia watoto. Yeye hupenda kuwajumuisha katika sherehe ya jiwe la msingi na daima huwaalika wachache miongoni mwao kuweka saruji kidogo kwenye jiwe la msingi ili kushiriki katika ukamilishi wa kimfano wa hekalu. Yeye huifanya kuwa jambo la furaha kwao. Yeye huifanya kuwa jambo la kukumbuka kwao. Yeye daima uwa na tabasamu kubwa kwa ajili yao. Yeye huwahimiza na kuwapongeza. Ni jambo la ajabu kutazama.
Salamu zake za upendo mara kwa mara hujumuisha salamu za kupiga viganja hewani, kutetemesha masikio, na himizo kuhudumu misheni na kuoa katika hekalu. Yeye kweli anafurahia maisha---na je vivyo hatupaswi sote.
Miaka michache iliyopita, Rais Monson alikuwa amepangiwa kuweka wakfu Hekalu la Oquirrh Mountain siku ya kuzaliwa kwake. Alipowasili katika hekalu na kukaribia mlango wa mbele wa hekalu, kundi la vijana lilikuwa limekusanyika. Walijua kwa wazi ilikuwa siku ya kuzaliwa ya Rais Monson, walipoanza kumimbia “Happy Birthday.” Aliipenda. Alisimama na kuwatazama akiwa na tabasamu kubwa usoni mwake. Hata akaanza kuelekeza mkono wake, ni kama alikuwa anawaongoza kuimba. Mwishoni wakaongeza usemi “Na mengi zaidi.” Rais Monson aliipenda hivyo pia, aliniambia, “ Hiyo ni sehemu ninayoipenda zaidi ya yote”
Watoto na vijana wa Kanisa wanampenda, na ninadhani ni kwa sababu hawana shaka kwamba yeye anawapenda! Yesu aliwapenda watoto wadogo, na nabii wake anawapenda watoto wadogo. Huu ni mfano mzuri kwa kila mmoja wetu!
Tatu, tunaweza kufuata ushawishi wa Roho, kama Rais Monson.
Kujitolea kwa Rais Monson kwa Bwana na ahadi yake ya kufuata ushawishi wa Roho ilielezwa vizuri na nabii mwenyewe kwa maneno haya, “matukio ya furaha kabisa ninayojua maishani ni kuhisi ushawishi na kuutenda, na baadaye kugundua kuwa ilikuwa ni timizo la maombi ya mtu au mahitaji ya mtu. Na mimi daima nataka Bwana ajue kwamba kama akihitaji kijana wa kumfanyia kazi, Tom Monson atamfanyia kazi hiyo." (On the Lord’s Errand [DVD, 2008]). Huo ni mfano ambao kila mmoja wetu anapaswa kufuata.
Nne, tunaweza kupenda hekalu, kama Rais Monson anavyolipenda hekalu.
Rais Monson atajulikana katika historia kama mmoja wa wajenzi wakubwa wa hekalu katika historia ya Kanisa. Tangu awe Rais wa Kanisa mnamo Februari 2008, ameendeleza kazi kubwa ya kujenga mahekalu. Baadhi ya mahekalu ambayo ametangaza yamekuwa miongoni mwa yale ya kihistoria: "Asubuhi hii ninafurahi kutangaza mahekalu matano ambayo ardhi imenunuliwa na ambayo, katika miezi na miaka ijayo, yatajengwa katika maeneo yafuatayo: Calgary, Alberta, Canada; Córdoba, Argentina; eneo kuu la Kansas City; Philadelphia, Pennsylvania, na Roma, Italia "(Thomas S. Monson, “Welcome to Conference,” Ensign au Liahona, Nov. 2008, 6).
Katika miaka mitano ambayo amekuwa nabii, Rais Monson ametangaza mipango ya kujenga mahekalu 33 mapya. Mwezi uliopita tu katika mkutano mkuu wa Aprili, alitangaza mipango ya ya mahekalu mawili mapya: Moja katika Mji wa Cedar, Utah, na lingine katika Rio de Janeiro, Brazil.
Pamoja na uwekaji wakfu wa Hekalu la Tegucigalpa Honduras mnamo Machi, sasa tunayo mahekalu 141 katika Kanisa, na mengine 29 yakiwa yanajengwa hivi sasa ama yako katika hatua ya kupanga. Huu ni wakati mkuu wa ujenzi wa hekalu na ibada ya hekalu katika Kanisa la Bwana. Nimemsikia Rais Monson akiwaambia vijana ambao ni wadogo sana kuingia hekaluni waende na waguse ukuta wa hekalu na kisha "waache hekalu liwaguse."
Rais Monson amesema, “Sote tuishi maisha ya kustahili, na kwa mikono safi na mioyo safi, ili hekalu liguse maisha yetu na familia zetu.” (“Blessings of the Temple,” Ensign, Oct. 2010, 19).
Akaongeza ahadi hii ya ajabu: "Tunapopenda hekalu, tunapogusa hekalu, na tunapohudhuria hekalu, maisha yetu yataonyesha imani yetu. Tunapokuja kwenye nyumba hizi takatifu za Mungu, tunapokumbuka maagano ambayo tunafanya, tutaweza kuhimili majaribio yote na kushinda majaribu ya kila aina" ” (Be Your Best Self [1979], 56; mkazo umeongezwa ).
Hebu tufuate mfano ambao nabii ametuwekea katika kupenda hekalu.
Tano, tunaweza kuwa wema, kuwa wapole, na kuwapenda wengine, kama Rais Monson anavyofanya.
Rais Monson ni mfano mzuri wa kuwapenda watu wengine. Huduma yake nzima imejawa na ziara nyumbani; kuweka mikono yake juu ya vichwa na kutoa baraka, na kupiga simu zisizotarajiwa ili kufariji na kutia moyo; kutuma barua za kutia moyo, pongezi na za faraja, shukrani; matembezi hospitalini na katika vituo vya huduma, na kupata muda wa kwenda kwa mazishi na matazamo licha ya ratiba iliyojaa sana.
Nilitaja awali wajane 84 kutoka kwa kata ya Rais Monson wakati alipokuwa askofu. Kwa miongo iliyofuata huduma yake kama askofu, katika dhihirisho la ajabu la kujitolea, pamoja na matokeo ya maombi yao mengi, Rais Monson aliweza kuhudhuria mazishi ya kila mmoja wao. Hebu fikiria kuhusu hilo.
Kama vile Mwokozi angelifanya, Thomas Monson ameenda kote akitenda mema, akiwabariki na na kuwapenda wengine kama kwamba hiyo imekuwa msukumo wa kutenda katika maisha yake. Sote tunaweza kujifunza kutokana na haya sisi tunapotafuta kufuata nyayo zake.
Mfano wa ajabu wa wema wa Rais Monson ulitokea mwaka jana. Hekalu la kupendeza la Jiji la Brigham Utah lilipokaribia kukamilika, nilikutana na Urais wa Kwanza ili kujadili mipango ya ibada ya kuliweka wakfu hekalu. Jiji la Brigham likiwa ni umbali wa saa moja tu kaskazini mwa Jiji la Salt Lake, ingekuwa rahisi kwake Rais Monson kusafiri huko kwa ajili ya ibada ya kuweka wakfu. Badala yake, Rais Monson alisema, “ Jiji la Brigham ni mji wa kuzaliwa wa Rais Boyd K. Packer, Mtume huyu mkuu ambaye ameketi kando yangu kwa miaka mingi katika Wale Kumi na Wawili. Nataka awe na furaha na baraka ya kuweka wakfu hekalu katika mji wake. Nitakaa mbali, na nitampa jukumu Rais Packer kuweka wakfu Hekalu la Jiji la Brigham. Nataka iwe siku yake. "
Ilikuwa ni siku ya ajabu kwa Rais Packer na kwa Dada Packer, ambaye pia alilelewa Jijini Brigham. Niliguswa sana na ishara ya wema na ukarimu wa Rais Monson kwa Mtume mwenzake. Sote tunaweza kuwa hivyo. Tunaweza kushiriki na kuwa na huruma na kutojifikiria wenyewe sana---lakini kufikiri zaidi ya wale walio karibu nasi.
Naupenda wimbo wa watoto “Follow the Prophet.” Una aya tisa za ajabu, lakini nina wakati tu wa kusoma fungu la mwisho:
Sasa tuna ulimwengu ambapo watu wamekanganywa.
Kama huamini hilo, nenda utazame habari.
Tunaweza kupata mwelekeo njiani mwetu,
Tukiwasikia manabii---kufuata wanachosema.
… … … … … … … … … .
Fuata nabii, usipotee
… … … … … … … … … .
Fuata nabii; yeye anajua njia.
(Children’s Songbook, 111)
Rais Monson kweli anajua njia. Njia sahihi ni njia ya Bwana. "Njia iliyo sawa ni kuamini katika Kristo" (2 Nefi 25:29).
Rais Monson ametufundisha njia ya kuishi maisha yetu na ujumbe wake wa ajabu na wakushawishi katika mkutano mkuu. Yeye ametufundisha jinsi ya kuwa wafuasi wa Yesu Kristo. Yeye ametufundisha kwa mfano wake wa kibinafsi wa ajabu na mzuri. Kweli Bwana ametupa mfano katika mambo yote. Mmoja wa mfano tunaopaswa kujitahidi kufuata ni ule wa nabii wetu mpendwa.
Nashuhudia kwamba kuna Mungu mbinguni ambaye anatujua na anatupenda. Yeye ametupa nabii kutuongoza, kutufundisha, na kutuelekeza katika siku hizi za mwisho. Nashuhudia kwamba Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu na Mwokozi wa dunia hii. Mimi naamini Bwana anatutarajia sisi kumpenda nabii, kumkubali, na kufuata mfano wake.
Sisi tunakushukuru, Ewe Mungu, kwa ajili ya nabii. Tunakushukuru kwa ajili ya nabii huyu. Ninaihesabu kama baraka kubwa kuishi katika siku Thomas S. Monson alikuwa nabii wa Bwana. Tunapomfuata nabii na kujaribu kuwa zaidi kama yeye, hakika tutafanikiwa katika kuwa wafuasi waaminifu zaidi wa Bwana Yesu Kristo.
Imekuwa ni heshima kuwazungumzia ninyi jioni hii, na ninaomba Bwana atawabariki kila mmoja wenu kwa wingi, nikishuhudia kuwa hii ni kazi ya Bwana, katika jina la Yesu Kristo, amina.
© 2013 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Kiingereza kiliidhinishwa: 9/12. Tafsiri ilihinishwa: 9/12. Tafrisi ya Our Prophet: Thomas S. Monson. Language. PD50046139 743