Historia ya Kanisa
Kitu Ambacho Kilikuwa na Maana


Kitu Ambacho Kilikuwa na Maana

Charles Osinde, mhudumu wa afya kutoka Kampala, na mke wake, Mary Jean Akello, walisafiri kwenda Scotland mwaka 1989, ambapo wote wawili walimaliza kozi katika mafunzo ya kompyuta. Wakiwa huko, Charles na Mary Jean walikutana na wamisionari Watakatifu wa Siku za Mwisho. Charles alipokuwa akisoma Kitabu cha Mormoni, aligundua “kitu ambacho hakuweza kukipata mahali pengine popote” na punde akabatizwa.

Mary Jean, kwa upande mwingine, alipambana zaidi na uamuzi wa kubatizwa. Wamisionari walipoendelea kujaribu kukutana naye, alianza kupanga miadi na kutafuta sababu za kuwa mbali na nyumbani katika muda walioupanga.

Jioni moja, dhoruba ya theluji ilianza muda mfupi tu kabla ya miadi waliyopanga. Akiwa na uhakika kwamba wamisionari wasingekuwa na ujasiri wa kuikabili dhoruba ile, Mary Jean alibaki nyumbani. Alipokuwa amekaa akitazama ile theluji ikianguka nje ya dirisha la nyumba yake, alishangaa kuona watu wawili wakipambana kutafuta njia yao katika ile dhoruba. Jioni ile, aliikubali nakala ya Kitabu cha Mormoni. Kote huko Scotland na baada ya yeye na Charles kurudi Uganda, Mary Jean kwa bidii alisoma Biblia na Kitabu cha Mormoni na kulinganisha jumbe za kila kimoja.

Kabla ya kuondoka Scotland, Charles aliomba orodha ya Watakatifu wa Siku za Mwisho wote walio nchini Uganda na akapokea majina na anwani za watu saba. Wakati Charles na Mary Jean waliporudi Kampala mnamo Juni 1990, Charles alianza kuwatafuta watu wale walioko kwenye ile orodha na kufanya huduma katika nyumba yake. Kitambo kidogo akaungana na Guy na Peggy Denton, Wamarekani Watakatifu wa Siku za Mwisho waliokuwa wakifanya kazi nchini Uganda. Charles na Mary Jean waliwaalika akina Denton na watoto wao sita nyumbani kwao kwa ajili ya mikutano ya kila wiki.

Wakati huo, Mary Jean aliendelea kusoma Kitabu cha Mormoni. Mary Jean, ambaye daima amekuwa mpenzi wa dini, amekuwa akiwafundisha watoto wake hadithi za Biblia tangu walipokuwa bado wadogo sana. Punde alianza kujumuisha hadithi za Kitabu cha Mormoni kwenye masomo haya. Watoto wake walitambua, na walifurahia kujifunza katika madarasa haya madogo ya Watoto yaliyofanyika kila wiki pamoja na ongezeko la idadi ya Watakatifu na marafiki waliopenda kuja katika nyumba yao. Watoto pia walitambua badiliko la wazi kwa Charles. Ingawa yeye daima amekuwa mkarimu, baada ya ubatizo wake amekuwa msikivu zaidi na kuanza kushiriki katika mafunzo ya jioni ya Biblia na kuiongoza familia katika sala.

Deborah, binti wa Mary Jean, yeye hasa alivutiwa na mabadiliko aliyoyaona. Wamisionari walipowasili nchini, Deborah mwenye umri wa miaka 10 alisikiliza masomo ya wamisionari na kwa shauku aliukubali mwaliko wa kubatizwa. “Nilikuwa nikisoma Kitabu cha Mormoni katika darasa langu la Watoto,” Deborah anakumbuka. “Kila kitu kilikuwa na maana kwangu.” Deborah alibatizwa Februari 2, 1991; Mary Jean alibatizwa baadaye mwezi huo.

Mnamo Machi 3, tawi liliundwa huko Kampala. Tawi, ambalo lilifanya ibada ya ubatizo mara kwa mara, likakua kuizidi nafasi ndogo katika nyumba ya Charles na Mary Jean, na mipango punde ikafanywa ya kukutana katika shule ya eneo hilo. Ilipofika 1993, Kanisa liliongezeka kwa kuwa na matawi kadhaa huko Kampala na Jinja, likiwa na mamia kadhaa ya waumini.

Chapisha