Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Julai 2010
Marafiki Waamiifu
Mojawapo wa heshima kuu ambazo Mwokozi anaweza kupeana ni kutuita “marafiki.” Tunajua kwamba Anawapenda kwa upendo kamili watoto wote wa Baba Yake wa Mbinguni. Ilhali kwa wale ambao wamekuwa waaminifu katika huduma yao pamoja Naye, Yeye anahifadhi cheo hiki maalum. Mnakumbuka maneno kutoka kwa sehemu ya 84 ya Mafundisho na Maagano: “Na tena ninawaambia, marafiki zangu, kwani kuanzia sasa nitawaita ninyi marafiki, ni muhimu kwamba niwape amri hii, ili muweze kuwa kama marafiki zangu katika siku zile wakati nilipokuwa pamoja nao, wakisafiri kuhubiri injili kwa uwezo wangu” (M&M 84:77).
Tunakuwa marafiki Zake tunavyowahudumia wengine kwa ajili Yake. Yeye ndiye mfano kamili wa aina ya rafiki tunayeweza kuwa. Anataka tu kile ambacho ni bora kwa watoto wa Baba Yake wa Mbinguni. Furaha yao ndio furaha Yake. Anahisi huzuni wao kama Wake mwenyewe kwa sababu Amelipa thamana ya dhambi zao zote, akachukua juu yake udhaifu wao wote, akayachukua matatizo yao yote, na kuhisi matakwa yao yote. Dhamira zake ni safi. Hatafuti kutambuliwa kwa kibinafsi lakini kupeana utukufu wote kwa Baba Yake wa Mbinguni. Rafiki kamili, Yesu Kristo, sio mbinafsi katika kupeana furaha kwa wengine.
Kila mmoja wetu ambaye amefanya maagano ya ubatizo ameahidi kufuata mfano Wake wa kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine kama vile Angelifanya (ona Mosia 18:8).
Katika siku chache zijazo mtakuwa na nafasi nyingi ya kuwa rafiki Kwake. Pengine itakuwa unavyotembea kwenye barabara yenye vumbi. Pengine itakuwa unapoketi chini katika gari ya reli. Pengine itakuwa unapotafuta sehemu ya kuketi katika mkusanyiko wa Kanisa. Ikiwa unaangalia, utaona mtu aliyebeba mzigo mzito. Inaweza kuwa mzigo wa huzuni au upweke au kosononeka. Itaweza kuonekana kwako tu ikiwa umeomba ili Roho aweze kukupatia macho ya kuweza kuona katika mioyo na umeahidi kuinua mikono inayoning’inia chini.
Jibu la ombi lako linaweza kuwa uso wa rafiki wa zamani, mmoja ambaye haujamuona kwa miaka lakini ambaye mahitaji yake kwa ghafla yanakuja kwa mawazo na moyo wako na unahisi kama ni yako mwenyewe. Hilo limewahi kunifanyikia. Marafiki wa zamani wamenifikia kutoka mbali na kwa miaka ili kunitia moyo wakati ambapo ni Mungu pekee angewaelezea kuhusu mzigo wangu.
Manabii wa Mungu wanaoishi wametuomba tuwe marafiki waaminifu kwa wale wanaokuja Kanisani kama waongofu na kuelekea kwa uokoaji wa wale waliopotoka. Tunaweza kufanya hivyo, na tutavifanya ikiwa tutamkumbuka Mwokozi kila mara. Wakati tunapofikia kupeana usaidizi na kuinua mzigo, Anafikia pamoja nasi. Atatuelekeza kwa wale wenye mahitaji. Atatubariki ili kuhisi kile wanachohisi. Tunavyojikakamua katika juhudi zetu za kuwahudumia, tutapewa zaidi na zaidi karama ya kuhisi upendo Wake kwao. Hiyo itatupatia ujasiri na nguvu ili kusaidia tena na tena kwa uaminifu.
Na, kwa wakati na katika milele, tutahisi furaha ya kukaribishwa kwa kundi la marafiki Zake waaminifu. Naomba baraka hiyo iwe kwetu sisi sote na kwa wale ambao tutawahudumia.
© 2010 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa Imechapishwa USA Kiingereza kiliidhinishwa: 6/09. Tafsiri iliidhinishwa: 6/09. Tafsiri ya First Presidency Message, July 2010. Swahili. 09367 743